Mbeya: Kisa cha watoto kutoroshwa, baadhi ya wazazi wakiri kuridhia watoto wakafanye kazi za Majumbani

dope bwoi

JF-Expert Member
Feb 25, 2009
234
591
Siku mbili baada ya Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, kuwarejesha watoto 11, waliokuwa wanadaiwa kuwa walitoroshwa na kuuzwa kwa wafugaji wilayani Mbarali, ili watumike kuchunga mifugo, baadhi ya wazazi wa watoto hao wameibuka na kudai waliridhia watoto wao kwenda kufanya kazi hiyo.

=====

Septemba 7, mwaka huu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Ulrich Matei, akizungumza na wandishi wa habari hizi, alisema Jeshi hilo liliwakamata watu wawili kwa tuhuma za kuwaiba watoto hao 11, kutoka katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo na kwenda kuwauza kwa wafugaji.

Aliwataja watu hao kuwa ni Daniel Julius (21), mkazi wa Nsonga na Kamungu Julius (30), mkazi wa Rwimba, ambao walikamatwa na jeshi hilo katika Kijiji cha Mahango, wilayani Mbarali wakiwa wamewauza watoto hao kwa wafugaji.

Kamanda Matei alisema walikuwa wanauzwa kwa gharama ya Sh. 25,000 na 30,000 na wenye umri kati ya miaka 10 na 14.

Kamanda Matei alisema kati ya watoto 11, wawili walikuwa wameshatambuliwa na kuchukuliwa na wazazi wao na akawataka wananchi kwenda kuwatambua wengine na kuwachukua.

Juzi Nipashe lilipiga kambi katika Kituo cha Polisi Kati jijini Mbeya, ili kujua hatima ya watoto hao na kushuhudia wote waliokuwa wamebakia wakikabidhiwa kwa ndugu zao na Jeshi la Polisi kwa maandishi.

Mmoja wa wazazi wa watoto hao, Kaputila Mwakalobo, mkazi wa Kata ya Swaya katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, alisema aliridhia mtoto wake kwenda kuchunga mifugo kwa wafugaji wilayani Mbarali, kwa sababu alikuwa mdokozi na amemsababishia hasara.

Alisema waliokuwa wanamhitaji mtoto wake huyo walikubaliana naye kuwa watakuwa wanamlipa mtoto Sh. 100,000 kwa mwaka na mpaka anachukuliwa na polisi alikuwa hajamaliza wiki moja.

“Wakati anaondoka mimi sikuwapo na niliporejea nilikuta ameshaondoka, sikuwa na wasiwasi kwa sababu nilikuwa najua alikokuwa ameenda, ila juzi nikiwa nyumbani nilipigiwa simu kwamba mtoto wangu yupo huku polisi nije nimchukuwe,” alisema Mwakalobo.
Alisema kutokana na maelezo aliyopewa na Polisi baada ya kumrejesha mtoto huyo, hataruhusu apelekwe tena kwenye shughuli hizo.

Naye Japhet Charles ambaye ni kaka wa mmoja wa watoto hao, alisema mdogo wake baada ya kuhitimu darasa la saba alikuwa hana kazi ya kufanya na waliamua kuridhia apelekwe kuchunga mifugo, ili ajipatie kipato.

Alisema familia walikuwa wanajua kuwapeleka watoto kwenda kuajiriwa ni kosa, lakini kutokana na tatizo la kiuchumi waliamua kukubali mdogo wake aende kufanya kazi hiyo.

Alisema alichukuliwa tangu mwaka 2020 na muda wote huo alikuwa anafanya kazi ya kuchunga ng’ombe na wao kama familia waliwahi kwenda kupafahamu alipokuwa anafanya kazi.

“Sisi mdogo wetu tulikubaliana kwamba atakuwa analipwa Sh. 200,000 kwa mwaka, kwa sasa tunarudi naye nyumbani, ili tuanze kufuatilia malipo yake kwa muda, ambao amefanya kazi,” alisema Japhet.

Kwa upande wake Bahati Jonas, ambaye pia ni kaka wa mmoja wa watoto hao alisema awali mdogo wake alichukuliwa kwa lengo la kwenda kufanyakazi kwenye mashine, lakini baada ya kushindwa ndipo walipompeleka kwenye kibarua cha kuchunga mifugo.

Alisema awali mdogo wake huyo alitoroka, lakini baada ya kufika Mbarali alitoa taarifa, lakini kila wakitaka kuwasiliana naye zaidi akawa hapatikani kwenye simu mpaka alipoletwa na Jeshi la Polisi.

Chanzo: Nipashe

PIA, SOMA: - Mbeya: Watatu wakamatwa kwa kufanya Biashara ya kusafirisha Watoto wakafanye kazi za Majumbani
 
Wazazi wao wapigwe viboko kumi na kenda hadharani, iwe fundisho eboo!

Hawa hawana tofauti na wale wanaoozesha mabinti wadogo. Washitakiwe

Everyday is Saturday............................... :cool:
 
Back
Top Bottom