Hili arosto sio la Ulimwengu huu aisee
Sent using
Jamii Forums mobile app
NYEMO CHILONGANI
MAUAJI YALIYOJAA UTATA
Sehemu ya Kumi na Tano.
Todd Lewis, muigizaji aliyekuwa na jina kubwa duniani alikuwa akitoka katika Uwanja wa Kikapu wa Stapple Center kuangalia mechi ambayo iliwakutanisha wenyewe, La Lakers ikiongozwa na Shaq O’ Neil ambayo ilikuwa ikipambana na Chicago Bulls.
Alikuwa ameamua kusafiri kutoka jijini New York mpaka Los Angeles kwa ajili ya kuangalia mechi hiyo. Alipenda mchezo wa kikapu na hakutaka kabisa kukosa mchezo huo ambao ulikuwa ukizikutanisha timu kongwe, kali ambazo zilikuwa na nguvu mno katika kipindi hicho.
Nje ya uwanja huo, watu wengi walikuwa wakimsubiri, alikuwa na jina kubwa, ukiachana na mastaa wengi wa mchezo wa kikapu, pia siku hiyo Todd alikuwa gumzo kubwa, ndani ya uwanja huo, watu wengi walitaka kupiga naye picha, pale alipokuwa amekaa, watu walimsogelea na kuanza kujifotoa picha kadhaa na mpaka mchezo huo unamalizika, kulikuwa na watu wengi waliopata nafasi ya kupiga naye picha.
Wengine hawakuridhika, hata walipokuwa wakitoka, bado mashabiki walikmfuata Todd, walitaka kupiga naye picha huku wengine wakitaka kusainiwa vitabu vyao.
Hayo yalikuwa maisha ya usupastaa, walimheshimu kwa kuwa aliifanya kazi yake ipasavyo, wengi walipenda kutazama filamu zake, kwa kifupi, Todd aliwavutia watu wengi mno.
Alipomaliza kuwasainia watu vitabu vyao na hata kupiga nao picha, kama kawaida akaifuata gari yake ya kifahari, Ferrari nyekundu na kisha kuingia, kilichofuata ni kuanza safari ya kuelekea hotelini kabla ya kurudi New York alipokuwa akiishi siku inayofuata.
Akaliwasha gari hilo na kuondoka mahali hapo. Moyo wake ulijisikia faraja, hakuamini kwamba mwisho wa siku angekuwa na umaarufu mkubwa kama aliokuwa nao katika kipindi hicho.
Katika kipindi cha nyuma alipokuwa akianza, mambo yalikuwa magumu mno, alipambana usiku na mchana lakini mwisho wa siku, alifanikiwa kuwa kama alivyokuwa, hakukuwa na kitu kingine kilichokuwa kikiendelea zaidi ya kukusanya fedha na kuwa nazo zaidi ya zile alizokuwa nazo.
Wakati safari ikiendelea na kuyakuta makutano ya Barabara za St. Barnaba na Morovian ambayo ilikuwa ikienda mpaka katika Mtaa wa Butterfly uliokuwa umbali kama wa kilometa tatu, akashtuka baada ya kuona gari moja likija kwa kasi nyumba yake, lilikwenda mbele yake kwa mwendo wa kasi na kisha kusimama kwa katikati ya barabara, tena kiubavuubavu.
Kama haukuwa umakini wake mkubwa, basi angeweza kuligonga gari hilo. Kwa ustadi mkubwa, Todd akafunga breki na kisha kusimama, alibaki akihema kwa nguvu, mbele yake ilionekana ajali kubwa ambayo pasipo kutumia uwezo wake basi angeweza kuligonga gari hilo.
Huku akijiuliza ni kitu gani kinaendelea, wanaume wawili wakateremka kutoka kwenye ile gari na kuanza kuelekea kule alipokuwa. Hakujua watu hao walikuwa wakina nani na walihitaji nini kutoka kwake.
Mahali hapohakukuwa na magari, ilikuwa usiku sana na magari hayakuwa yakipita mara kwa mara, hasa katika barabara hiyo ya magari yaendayo kasi. Akashindwa kuliwasha gari lake, watu wale walikwenda kwa kasi mpaka pale lilipokuwa gari lake, wakamwambia afungue mlango vinginevyo wangempiga risasi humohumo.
Hakuwa na jinsi, hakutaka kupinga, kitu cha kwanza kabisa, akashusha kioo cha mbele cha mlango wa upande mwingine, mwanaume mmoja akaingia na kumwamuru aendeshe mpaka sehemu waliyotaka wao waelekee.
“Naomba uniache, kama unataka gari chukua,” alisema Todd huku akitetemeka.
“Unadhani sisi tunataka gari?” aliuliza mwanaume huyo huku akiwa na bastola mkononi mwake.
“Hata kama unataka kiasi chochote cha fedha, nitakupa, naomba uniache...” alisema Todd, tayari machozi yakaanza kububujika mashavuni mwake.
Mwanaume yule mwingine akapita upande wa pili, akaufungua mlango na kumshusha Todd kisha kumpeleka katika gari lao walilokuja nalo huku yule mwingine akiachwa katika gari lile kwa ajili ya kuondoka nalo.
Kila kitu kilichokuwa kikifanyika mahali hapo, kilifanyika kwa haraka sana, tukio zima lilichukua sekunde arobaini na tano tu, tayari wakaondoka huku wakiwa na Todd ndani ya gari.
“Naombeni mniacheee...” alisema Todd.
“Hutakiwi kupiga kelele...” alisema mwanaume mmoja huku akimnyooshea bastola.
“Nimefanya nini? Naombeni msiniue..” alisema Todd.
“Kwani kila anayeuawa kuna baya amelifanya? Hakuna kitu kama hicho, kuwa mpole,” alisema mwanaume huyo.
Baada ya hapo, hawakutaka kuongea kitu chochote kile, wakaondoka naye huku garini wakiwa kimya, kwani hata Todd naye aliyetaka kuzungumza maneno mengi aeleweke na hivyo kuachwa, aliambiwa akae kimya kwani suala la kumuua lisingeweza kuzuilika hata kidogo.
Walikwenda mpaka katika barabara nyingine ya Queen Elizabeth I ambayo ilikuwa ikienda moja kwa moja mpaka kwenye jumba la makumbusho ya Lincoln, hawakufika huko, wakakata kulia na kisha kuchukua barabara nyingine ambayo iliwapeleka mpaka katika sehemu ambayo haikuwa na watu, giza lilitawala, gari likasimamishwa mahali hapo.
“Naomba mnisamehe....”
“Halafu?”
“Niondoke, nitawalipa kiasi cha fedha chochote mnacholkitaka....”
“Halafu?”
“Naomba mnisamehe...”
Hawakutaka kupoteza muda, saa zao zilionyeshwa kwamba tayari ilikuwa ni saa nane za usiku hivyo walitakiwa wafanye haraka, wamuue na kisha kuendelea na mambo yao.
Walichokifanya ni kumkaba kooni, tena kwa nguvu kuhakikisha anakufa na kisha kufanya kile walichoambiwa kukifanya. Mwanaume mmoja mwenye nguvu ndiye aliyetumika kumuua Todd ndani ya gari hilo.
Dracula hakutaka kwenda katika lile gari kwani aliamini kwamba vijana wale wangefanya kama jinsi alivyowapa maagizo, kweli wakafanya. Kilichofuata baada ya kuhakikisha kwamba Todd amekufa ni kumchoma sindano iliyokuwa na madawa aina ya cocaine, walipomaliza, wakachukua nailo zenye unyevuunyevu ambazo kwa kutumia utaalamu wao waliweza kuweka alama za vidole za Benjamin na kisha kuziweka katika shingo ya Todd na sehemu nyingine za mwili.
“Vipi?”
“Tayari!”
“Mbebeni mkamuweke ndani ya gari lake, pia wekeni na hizi fedha,” aliagiza Dracula huku akiwapa noti ambazo zilitakiwa kuwekwa ndani ya gari hilo, vijana wale wakafanya kama walivyoagizwa, wakaubeba mwili wa Todd na kisha kuupeleka garini mwake na kuziweka noti zile.
“Tuondokeni!” alisema Dracula baada ya kumaliza kila kitu. Wakaondoka mahali hapo huku kila mmoja akiwa na furaha ya kukamilisha kazi waliyokuwa wamepewa.
****
Hakukuwa na mtu aliyeamini mara baada ya taarifa juu ya kifo cha Todd zilipotolewa katika vyombo mbalimbali vya habari nchini Marekani. Wengi walipigwa na bumbuwazi, kile walichokisikia, hakikuaminika kwao kwamba yule muigizaji, mwenye jina aliyekuwa akivuma sana kipindi hicho, Todd Lewis alikutwa amejidunga madawa ya kulevya kwakujiovadozi.
Watu wakapigiana simu, kila aliyesikia, hakutaka kukubaliana na habari hiyo kwani miongoni mwa watu waliokuwa wakifanya vizuri kipindi hicho, alikuwa huyo Todd, sasa kwa nini afe mapema hivyo? Tena mbaya zaidi alikutwa akiwa amejiovadozi madawa ya kulevya kitu ambacho kiliwachanganya watu wote kwani Todd hakuwa mtumiaji wa madawa hayo hata mara moja.
Wengi wakaenda katika Hospitali ya Calvary kujionea, huko, watu walikuwa wakilia kwani ndipo walipopata taarifa kamili kwamba muigizaji huyo alikutwa ndani ya gari yake ya kifahari ya Ferrari akiwa amejiovadozi madawa ya kulevya.
“Haiwezekani Bwana! Huyu jamaa hakuwa mlevi kabisa,” alisema jamaa mmoja.
“Ndiyo! Hata mimi nimeshangaa sana, yaani Todd awe mlevi wa madawa ya kulevya! Haiwezekani hata kidogo,” alisikika jamaa mwingine.
Kila mmoja alikuwa sahihi kabisa, hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa na shaka na Todd kwamba alikuwa mtumiaji wa madawa hayo, taarifa hizo zikaendelea kusambaa kila kona mpaka ndani ya saa moja tu, dunia nzima ilijua nini kilitokea nchini Marekani.
Hofu zikaanza kutanda, taarifa zilizosema kwamba ndani ya gari la marehemu kulikutwa noti za fedha kutoka nchi mbalimbali ziliwashtua sana kwani hata siku ambayo Carter alikutwa akiwa amekufa ndani ya chumba cha hoteli, fedha kama hizo zilikutwa kitu kilichowafanya watu kuona cha kawaida ila baada ya fedha hizo kukutwa ndani ya gari hilo, wakagundua kwamba inawezekana hizo fedha zilibeba ujumbe fulani.
“Kama huyu Benjamin ndiye aliyemuua Carter, basi inawezekana akawa amemuua na Todd pia,” alisema jamaa mmoja wakati alipokuwa supamaketi, katika sehemu ya kuuzia magazeti na majarida mbalimbali.
“Inawezekana kabisa...hebu tuwasikilizie polisi tuone watasemaje,” alisema jamaa mwingine.
Hilo ndilo lililokuwa vichwani mwa watu wengi, kila aliyesikia namna gari hilo lilivyokutwa, alikuwa na uhakika kwamba muuaji alikuwa yuleyule, kijana wa chuo mwenye akili nyingi, Benjamin Saunders.
Hilo ndilo lililotokea, baada ya siku mbili, taarifa zikatolewa kwamba alama za vidole vya Benjamin vilikuta katika mwili wa Todd, yaani kabla ya kumchoma sindano, alimkaba kooni na kumuua na ndipo alipofanya mambo mengine likiwepo lile la kumchoma sindano ya madawa ya kulevya ili ionekane kwamba alikuwa amejiovadozi.
Hakukuwa na mtu aliyejua sababu ya Benjamin kuwaua watu maarufu, wengi waliuliza, kwenye mitandao wakatoa maoni yao lakini hakukuwa na mtu aliyefahamu lolote lile juu ya sababu ya Benjamin kuwaua watu maarufu na kisha kuacha noti za fedha mbalimbali karibu na miili yao.
“Ila kwa nini anawaua watu maarufu?’ aliuliza mwanamke mmoja.
“Hata mimi sifahamu! Kwanza nashangaa...”
“Halafu nasikia huyu Benjamin mwenyewe ana akili sana darasani.”
“Hata mimi nimesikia hivyohivyo na watu walipokwenda, wakakuta kweli ana akili sana, inawezekana ndiyo ikawa sababu ya kuwasumbua polisi na wananchi kumtia nguvuni,” alisema jamaa mmoja.
Bado watu walitakiwa kumtafuta Benjamin lakini hakukuwa na yeyote aliyempata, kiasi kikubwa cha fedha zaidi ya dola milioni ishirini na tano ambazo zilikuwa ni zaidi ya bilioni hamsini kilitolewa lakini bado majibu yalikuwa yaleyale kwamba mitaani hakuonekana kabisa.
Maofisa wa FBI walikuwa na kazi kubwa, hakukuwa na aliyeamini kwamba mpaka muda huo Benjamin hakuwa amepatikana. Taarifa zilizopelekwa katika meza ya mkuu wa kitengo chao zilisema kwamba walitakiwa kupewa muda zaidi kwani inawezekana kulikuwa na mtu hatari ambaye alikuwa akimlinda Benjamin ili asiingie katika mikono yao.
“Kwa hiyo tumeshindwa?” aliuliza mkuu wa FBI, Bwana Connery Gibson.
“Hapana!”
“Sasa mbona hapatikani?”
“Ngoja tuendelee nadhani kuna kipindi tutampata tu.”
Hakukuwa na muda mwingine wa kupoteza, kama kusubiri, walisubiri kwa kipindi kirefu lakini hakukuwa na mafanikio yoyote yale, kuna kipindi walijiona kama kushindwa hivyo walitakiwa kuwasiliana na Shirika la Kijasusi la FBI ili wawasaidie kwani huyu Benjamin, japokuwa walijua kwamba hakuwa polisi au mtu yeyote mwenye uwezo wowote wa kijeshi lakini alikuwa mgumu mno kupatikana.
Walichokifanya ni kujiongeza tu, wakawagawa vijana wao katika miji mingine kama Los Angeles, Miami, Texas na sehemu nyingine ili kuhakikisha Benjamin anapatikana haraka iwezekanavyo.
“Nadhani hatotushinda tena, si ndiyo?”
“Tutegemee hilo mkuu!”
****
Harry alichanganyikiwa, hakuamini kile alichokuwa amekiona kwamba muigizaji maarufu duniani kwa kipindi hicho, Todd Lewis aliuawa ndani ya gari lake huku wauaji hao wakitaka kuionyeshea dunia kwamba alijiovadozi madawa ya kulevya kitu ambacho hakikuwa kweli kabisa.
Kilichomchanganya zaidi ni alama za vidole zilizopatikana ndani ya gari lile na hata katika mwili wa Todd ambazo zilionyesha kwamba ni Benjamin ndiye aliyefanya mauaji hayo.
Hapo ndipo alipoamini kwamba Benjamin hakuhusika katika mauaji, kulikuwa na watu wengine waliokuwa wakiyafanya huku wakiweka alama za vidole vyake katika kila tukio walilolifanya.
Alimwangalia Benjamin mara mbilimbili, hakuamini kilichokuwa kimetokea, alimuonea huruma sana kwamba inawezekana vipi mtu auwe na kisha kuweka alama za vidole vyake? Alimuuliza Benjamin lakini mwanaume huyo alimwambia ukweli kwamba hakujua kitu chochote kile.
“Sifahamu!” alisema Benjamin.
“Kuna kitu unajua!”
“Harry! Sifahamu chochote, huyu mzee Seppy ndiye anahusika, yaani ni lazima dunia ijue kwamba yeye ndiye anahusika, vinginevyo, nitahukumiwa kwa mauaji ambayo sikuyafanya,” alisema Benjamin.
“Tutatoa vipi taarifa polisi? Watakukamata!”
Huo ndiyo ulikuwa mtihani mwingine, hawakujua ni kitu gani walitakiwa kufanya, hawakuwa na ushahidi wa kutosha hivyo kama wangekosea sehemu moja basi lingekuwa tatizo kubwa kwao, walitakiwa kujipanga ili hata kama watakwenda kutoa taarifa polisi basi kusiwe na tatizo lolote lile.
David ndiye alikuwa na ushahidi kamili lakini bado kulikuwa na kitu kimoja kilichokuwa kikiwatatiza, kila mauaji yalipotokea, kulikuwa na fedha zilizokuwa zikiachwa, zile fedha zilimaanisha nini? Kila walichojiuliza, walikosa jibu.
“Sijui zinamaanisha nini, ila kama nikipewa muda, nitaweza kufahamu tu, kuna kitu,” alisema Benjamin huku akionekana kama mtu aliyekuwa akijifikiria sana.
“Hili ndilo la msingi, sidhani kama hata FBI watakuwa wanajua maana, huu utakuwa ni ujumbe, ujumbe gani sasa? Hebu tuhangaike mpaka tufahamu,” alisema Harry.
Wote wakakubaliana na kuingia kazini kuhakikisha wanajua kwanza maana ya zile fedha za noti zilizokuwa zikiwekwa katika mauaji yaliyokuwa yakitokea.
Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumamosi