NYEMO CHILONGANI
MAUAJI YALIYOJAA UTATA
Sehemu ya Saba
.Walichukua dakika arobaini na tano mpaka kumaliza. Mercy alikuwa hoi, hakuamini kama angeweza kukutana na mwanaume anayeweza kufanya mapenzi kama ilivyokuwa kwa Benjamin.
Hapohapo wakaanza kuvaa nguo zao na kisha kubaki wakiangaliana tu. Hakukuwa na mtu aliyesema chochote kile zaidi ya kusogeleana na kukumbatiana tu.
“Ninakupenda...” alisema Benjamin.
“Nakupenda pia.”
Benjamin hakutaka kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kuondoka kurudi chumbani kwake huku tayari akiwa na kadi ile mfukoni mwake, alipofika, akaingia chumbani na kutulia.
Mpango aliokuwa nao ilikuwa ni lazima akalale chumbani kwa Carter usiku huohuo ili iwe rahisi kwake kukamilisha mpango wake. Muda ulizidi kwenda mbele, kuna kipindi alihisi kwamba angeweza kuchelewa, hivyo akaamka, akachukua kitambaa kilichokuwa na dawa za usingizi na kisha kutoka mule huku mfukoni akiwa na bomba la sindano.
Kwenye korido, hakukuwa na kamera za CCTV hivyo ilikuwa ni rahisi kwake kuingia humo ndani. Akachukua kadi yake na kuipachika katika kimashine kidogo, zikawaka taa nyekundu kwa zamu kisha kubadilika na kuwa za kijani, mlango ukafunguka.
Akaingia chumbani mule, hakikuonekana kuwa tofauti na chumba chake, vyote vilikuwa vya bei kubwa, alibaki akizungukazunguka mule, aliporidhika, akakifuata kitandani, kwa sababu kilikuwa na uvungu mkubwa kidog uliomuwezesha kupenya japo kwa tabu, akaingia humu huku akiwa na bomba la sindano na kitambaa ambacho alikiwekea dawa za usingizi.
“Ngoja nisubiri...Mungu, sifanyi hivi kwa kupenda, nimelazimishwa kwa ajili ya mpenzi wangu,” alisema Benjamin kwa sauti ndogo huku akivaa glovu mikono mwake.
Hakulala hata kidogo, alikuwa macho huku akiendelea kumsubiri Carter ambaye aliamini hakuwa mbali mpaka kufika mahali hapo. Huko uvunguni, alizima simu yake, hakutaka kufanya kosa lolote lile na kuonekana kabla hajakamilisha mpango wake.
Muda ulizidi kwenda mbele, ilipofika saa kumi alfajiri, akasikia sauti za watu nje, kwa kukadiria zilikuwa kama za watu sita, watu wale wakasogea mpaka mlangoni na kisha kuufungua.
Alikuwa Carter na wapambe wake, wakaingia ndani huku kila mmoja akionekana kuwa na furaha. Muda ulikuwa umekwenda sana na hawakuwa na muda wa kupoteza, Carter akaenda bafuni, akaoga na kisha kurudi chumbani pale.
Wakapiga stori, nyingi walizozipiga hapo zilikuwa ni za kumsifia Carter kwamba alifanya kazi nzuri sana, aliwaonyeshea watu yeye alikuwa nani. Walikaa kwa dakika kadhaa mpaka muda ule ambao wengine wakaenda kulala na yeye kutulia kitandani ambapo baada ya dakika chache, akapitiwa na usingizi.
Hiyo ndiyo ilikuwa nafasi kwa Benjamin kumuua Carter, hakutaka kuchelewa kule uvunguni, harakaharaka akatoka na kisha kumwangalia Carter kitandani pale, alichokifanya ni kuchukua kitambaa kile kilichokuwa na dawa ya usingizi na kisha kumkandamiza Carter kitandani pale huku kitambaa kile kikiwa usoni mwake.
Carter hakukubali, alijitahidi kuhangaika huku na kule ili kujinasua lakini ilishindikana kabisa, alikandamizwa kitandani pale na kadiri alivyovuta pumzi na ndivyo alivyokuwa akiivuta dawa ile na sekunde chache mbele, akatulia kitandani pale.
“Kazi imekwisha...” alisema Benjamin.
Mara baada ya kufanikiwa kumlevya kwa yale madawa yaliyokuwa kwenye kitambaa kile akachukua bomba la sindano aliyokuwa nayo na kisha kumchoma katika mshipa mmoja mkononi mwake ili aweze kumuua kitandani pale.
Alipohakikisha sumu ile imeingia vilivyo mwilini mwake, akachukua fedha ambazo aliambiwa aziweke ikiwepo euro, dola, yen na paundi kisha kuanza kufanya mikakati ya kutoka ndani ya chumba kile.
Hakukuwa na shida kwenye kutoka, akaufungua mlango ule na kutoka. Hakutaka kuingia chumbani kwake, akaelekea katika chumba kile cha kufanyia usafi kwa kufua mashuka na nguo kisha akaitupa ile kadi chini, pembenipembeni na kisha kurudia chumbani kwake, akavuta shuka na kutulia.
****
“Umenionea kadi yangu?” aliuliza msichana Mercy huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Kadi gani?”
“Ya milango!”
“Hapana! Kwani wewe uliiweka wapi?”
“Niliiweka kwenye huu mkoba.”
“Sasa iko wapi?”
“Ndiyo siioni.”
“Umeangalia vizuri?”
“Ndiyo! Hakuna!”
Mercy alichanganyikiwa, alikumbuka vilivyo kwamba aliiweka kadi ndani ya mkoba wake, lakini katika kipindi hicho alipokuwa akiitafuta, hakuwa akiiona. Akaondoka mahali hapo na kwenda sehemu zote alizopita lakini huko hakuona kitu.
Mercy alizidi kuchanganyikiwa, hakukumbuka kama aliuacha mkoba ule sehemu yoyote ile, mtu pekee na wa mwisho kumjia kichwani mwake alikuwa Benjamin.
“Inawezekana anajua...”
Alichokifanya Mercy ni kumpigia simu ya mezani chumbani kwake, kitu kilichomshtua ni kwamba simu iliita lakini haikupatikana. Mercy hakutaka kukata tamaa, aliendelea kupiga zaidi na zaidi lakini majibu wala hayakubadilika, bado simu ile haikupokelewa kitu kilichomtia wasiwasi mwingi.
“Au ameshaondoka?” alijiuliza.
Akaondoka na kuelekea mapokezini na kumuuliza dada aliyekuwepo hapo, hakuwa Rose, yeye aliondoka na kumuacha msichana mwingine, akamuuliza kama mteja aliyepanga chumba namba tisini na mbili alikuwa ameondoka.
“Hapana! Bado yupo,” alijibu msichana huyo.
“Mbona nampigia simu simpati?”
“Sijui! Inawezekana amelala, ila hapa inaonyesha yupo, hajaondoka,” aliongeza msichana huyo.
Mercy hakutaka kusubiri, alichokifanya ni kwenda wenyewe mpaka katika chumba kile, alipoufikia mlango, akaanza kugonga kwa nguvu, aligonga zaidi na zaidi lakini mpango wala haukufunguliwa kitu kilichoendelea kumpa maswali mengi.
“Mmh! Mbona naanza kuwa na wasiwasi...” alisema msichana huyo, akahisi akichoka, kilichobaki mbele yake kilikuwa ni kufukuzwa kazi tu, hakukuwa na kitu kingine zaidi ya hicho kwani kupoteza kadi, tena ile masta kabisa lilikuwa kosa kubwa mno.
Akaondoka na kuelekea nyumbani kwake, hakuwa na raha, alipanga siku inayofuata kuwa asubuhiasubuhi kuzungumza na Benjamin kwani bado moyo wake ulimwambia kwamba mwanaume huyo aliiona ile kadi aliyokuwa akiitafuta.
***
Asubuhiasubuhi msichana Mercy akafika hotelini hapo, bado akili yake haikuwa sawa hata kidogo, alikuwa na mawazo mengi, kadi ambayo aliipoteza usiku uliopita ilimchanganya mno.
Alipofika hotelini, hata kabla ya kufanya kitu chochote ilikuwa ni kwenda katika chumba cha Benjamin ili aonane naye na kumuuliza kuhusu kadi hiyo. Alipofika, akagonga mlango ambapo baada ya sekunde kadhaa, mlango ukafunguliwa, mwanaume aliyesimama mbele yake alikuwa Benjamin.
“Kumbe wewe...karibu mpenzi,” alisema Benjamin huku akimkaribisha msichana huyo huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.
“Ahsante! Nimekuja kukuuliza kitu,” alisema msichana huyo.
“Kitu gani?”
“Nilipoteza kadi jana!”
“Kadi gani?”
Alijifanya kutokufahamu chochote kile, hata macho yake yalionyesha kabisa kwamba hakujua kilichokuwa kikiendelea. Mercy akaanza kumwambia kuhusu kadi ile ambayo aliipoteza katika mazingira ya kutatanisha huku muda wote huo akionekana kuwa na majonzi tele usoni mwake.
“Pole sana, ila umeangalia vizuri kwenye kile chumba?” aliuliza Benjamin.
“Nimeangalia kila kona.”
“Umetoa nguo zote na kuangalia vizuri?”
“Ndiyo!”
“Mmh! Sasa iweje isionekane?” aliuliza Benjamin.
“Ndiyo nashangaa!”
Alichokifanya Benjamin ni kumwambia waende kwenye kile chumba cha kufanyia usafi, alikuwa na uhakika kwamba kadi ile ilikuwa mule kwani alfajiri ya siku hiyo aliirudisha na kurudi chumbani kwake.
Mercy alikuwa na uhakika kwamba kadi hiyo haikuwepo huko, aliangalia kila kona, alitoa nguo zote na kuzirudisha lakini hakufanikiwa kuiona kadi hiyo. Benjamin alipomaliza kujiandaa, wakaelekea katika chumba hicho na kuanza kuitafuta kadi hiyo.
Kwanza Benjamin hakutaka waende kwenye ule upande alioiweka kadi ile, alimwambia Mercy waende kwenye upande mwingine kitu ambacho kikafanyika kikamilifu. Walipokosa na ndipo walipokwenda kwenye ule upande uliokuwa na kadi, kweli wakaikuta.
“Ni hii hapa,” alisema Mercy huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.
“Wewe si ulisema umeikosa?”
“Ndiyo! Nilitafuta sana, nafikiri huku sikuja,” alisema msichana huyo.
Wakabaki wakiangalia tu, tayari miili yao ikaanza kuwasiliana mahali hapo, walikuwa wawili tu kama jana na kila mtu alionekana kumtamani mwenzake. Wakiwa wanaangalia kama mbuzi, wakaanza kusikia mlango mmoja huko nje ukigongwa, uligongwa huku sauti za watu zikisikika mahali hapo.
Kwanza wakashtuka, haikuwa kawaida kabisa, wakatoka chumbani humo na kwenda kwenye korido, marafiki zake Carter walikuwa katika mlango wa chumba alichochukua Carter na kuanza kugonga huku wakitaka wafunguliwe.
“Jamani, si jana amechelewa kulala, ataweza kuamka muda huu?” aliuliza Mercy huku akionekana kuwashangaa.
“Hatuna muda, tunatakiwa kuondoka sasa hivi,” alijibu jamaa mmoja.
Alichokifanya Mercy ni kwenda mapokezini ambapo huko akaanza kupiga simu ya mezani ndani ya kile chumba cha Carter, alipiga simu, iliita na kuita lakini haiupokelewa.
Hilohilo ndilo lililotokea kwa Benjamin usiku wa jana, hata naye alipojaribu kupigiwa simu hakuipokea. Wote wakaanza kushikwa na wasiwasi, wafanyakazi wa hoteli hiyo hawakutulia, wakaanza kupandisha juu mpaka kwenye korido iliyokuwa na chumba kile na kuanza kugonga.
Wakati huo Benjamin alikuwa chumbani kwake, alifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea, hakutaka kutoka nje, alitaka kuona kitu gani kingeendelea.
Mara akasikia mlango ukianzakupigwa, watu hao waligonga na kugonga, mlango haukufunguliwa na hivyo kuanza kuuvunja. Ilikuwa kazi kubwa, mlango ulikuwa imara sana, walifanya hivyo kwa zaidi ya dakika nne, mlango ukafunguka na kuingia ndani.
Picha waliyoiona, hakukuwa na mtu yeyote aliyeiamini, Carter alikuwa juu ya kitanda chake, sindano iliyokuwa na madawa ilikuwa katika mkono wake, tena ikiwa imechoma katika mshipa wake, kwa jinsi picha ilivyoonekana ilionyesha kabisa kwamba mtu huyo alikuwa amejidunga madawa ya kulevya.
“What the *** is this?” (Ndiyo nini hiki?) aliuliza jamaa mmoja huku akionekana kushtuka.
Wakamsogelea kitandani pale, wanawake waliomuona Carter wakaanza kupiga kelele, waliokuwa wamelala katika vyumba vyao wakaamka na kwenda chumbani humo kushuhudia ni kitu gani kilikuwa kimetokea.
Mbali na mwili huo, pembeni yake kulikuwa na fedha za noti, dola, yeni, euro na paundi. Hilo wala halikuwafanya kuhisi chochote kile kwani kwa mtu kama Carter, kuwa na fedha mbalimbali lilikuwa jambo la kawaida sana.
“Was he cocaine addicted?” (Alikuwa mtumiaji wa madawa ya kulevya?) aliuliza jamaa mmoja huku akimwangalia Carter pale kitandani.
Marafiki zake walibaki wakiashangaa, hawakuamini kile kilichokuwa kikiendelea, rafiki yao wa muda mrefu, Carter eti alikuwa mtumiaji wa madawa ya kulevya.
Hawakutaka kuamini hilo, pale kitandani alipokuwa, alikuwa kimya kabisa na hata mapigo yake ya moyo hayakuwa yakidunda hali iliyoonyesha kwamba alikuwa amekufa.
Walichokifanya ni kupiga simu polisi ambapo baada ya dakika ishirini walikuwa mahali hapo. Moja kwa moja wakaenda mpaka katika chumba hicho huku wakiwataka watu wote watoke nje na wao kufanya kazi yao.
Tayari mpiga picha wa polisi pamoja na mchoraji walifika mahali hapo na kuanza kuuangalia mwili wa Carter, alionekana kutumia kiasi kikubwa cha madawa mpaka kufariki pale kitandani.
Si marafiki zake walioshangaa tu bali hata polisi wenyewe nao walishangaa. Walimfahamu Carter, alikuwa mmoja wa wanamuziki wadogo ambao walitumika hata na kampuni mbalimbali kutokomeza utumiaji wa madawa ya kulevya, sasa iweje mtu huyo leo afe kwa kuzidisha utumiaji wa madawa hayo? Kila walichojiuliza, walikosa jibu.
Stori juu ya kifo chake zikaanza kusambazwa kwa kasi, hakukuwa na mtu aliyeamini kwamba mwanamuziki aliyekuwa na jina kubwa, Carter alikuwa amefariki dunia tena kwa kujidunga madawa ya kulevya kwa kiasi kikubwa.
Kila mtu aliyesikia taarifa hizo alibaki akishangaa, wengi wakajiuliza na mwisho wa siku kuja na majibu kwamba Carter alifanya siri utumiaji wa madawa ya kulevya.
Ulikuwa msiba mkubwa, kijana huyo, mwanamuziki huyo alikuwa na jina kuubwa, alikuwa kipenzi cha watuu wengi kitendo cha kusikia kwamba alikuwa amekufa ndani ya chumba hicho, hakika yalikuwa majonzi makubwa mno kwa kila mtu.
Taarifa hizo ziliendelea kuwekwa katika mitandao ya kijamii, kila aliyeziona, hakuamini, ndani ya saa moja tu, dunia nzima ilijua kile kilichokuwa kimetokea nchini Marekani huko Miami.
Watu walilia sana, wengine walijiuliza maswali mengi juu ya sababu iliyomfanya Carter kutumia madawa ya kulevya kwa kiwango kikubwa hicho mpaka kufa ndani ya chumba hicho.
Kila mtu alilaumu, wengine wakamuonea huruma. Mpaka mwili wake unaingizwa katika Hospitali ya St. Martin Luther King, tayari watu wengi walikusanyika hospitalini hapo, walitaka kusikia kile kilichokuwa kikiendelea, walitaka kuamini kama kweli msanii huyo alikufa baada ya kutumia madawa ya kulevya kupita kiasi.
***
“Nimefanya mlichotaka nikifanye, naomba mmuachie mpenzi wangu,” alisema Benjamin, alikuwa akizungumza na mtu fulani katika simu.
“Sawa! Tumeona, umefanya kazi nzuri sana...” ilisikika sauti upande wa pili.
“Kwa hiyo?”
“Kuhusu?”
“Mpenzi wangu! Si tayari nimekwishafanya kazi yenu, muachieni sasa,” alisema Benjamin.
Alikuwa akizungumza na mwanaume wa upande wa pili, alikuwa akimpa taarifa kwamba kazi aliyokuwa amepewa tayari ilikuwa imefanyika na hivyo alitaka mpenzi wake aachiwe huru kama yalivyokuwa makubaliano yao kabla.
Kwanza mwanaume huyo alikataa, kwa jinsi ilivyoonekana, alitaka kumuongezea kazi nyingine, ila alipotaka kufanya hivyo, aliona haikuwa sahihi kwani makubaliano ambayo waliwekeana mwanzo yalikuwa ni kumuua Carter na hakukuwa na jingine.
Walichokifanya huko walipokuwa ni kumfunga kitambaa cheusi Vivian na kumpakiza ndani ya gari, wakaanza kuondoka naye huku waliomsindikiza wakiwa wanaume wawili, waliokuwa na miili iliyojazia.
Njiani, Vivian alikuwa akilia, moyoni mwake aliumia mno, hakujua sababu iliyomfanya kutekwa na watu hao, kila alipouliza, hakupewa jibu bali aliambiwa asubiri mpaka atakapokutana na mpenzi wake.
Safari hiyo iliendelea mpaka walipofika katika kituo cha mafuta cha Total ambapo hapo ndipo walipomkabidhi Benjamin msichana Vivian ambaye hakuonekana kuwa sawa kabisa, kila wakati alikuwa akilia tu.
“Wamekufanya nini? Wamekupiga?” aliuliza Carter.
“Hapana! Kwa nini wamefanya hivi?” aliuliza Vivian.
“Sijajua! Acha tuondoke,” alisema Benjamin huku akionekana kutokujiamini.
“Benjamin, bosi amesema uchukue hii simu,” alisema mwanaume huyo huku akimpa simu aina ya iPhone 7.
“Ya nini?” aliuliza Benjamin huku akiichukua simu hiyo.
“Kama zawadi yako!”
“Nashukuru!” alisema Benjamin na kisha kumrudishia mwanaume huyo kwani alihisi kwamba simu hiyo ilikuwa na kifaa cha GPS ambacho kingemfanya kuonekana kila alipokuwa.
“Basi hakuna tatizo!”
Hawakutaka kubaki mahali hapo, walichokifanya ni kuingia ndani ya gari na kuanza kuondoka mahali hapo. Alichokifikiria Benjamin ni kuondoka na mpenzi wake kwenda mbali kabisa kujificha, hakutaka kuonekana kwani kile alichokuwa amekifanya chumbani kwa Carter, alikuwa na uhakika kwamba watu hao wangemtafuta na kumuua tu.
Walipofika katika apartment waliyokuwa wakiishi, Benjamin akamwambia Vivian wachukue kila kitu chao na kuondoka mahali hapo, kweli wakafanya hivyo.
“Ila kwa nini?” aliuliza Vivian.
“Wewe tuondoke, watatutafuta hawa.”
“Kisa?”
“Nimewachezea mchezo!”
“Mchezo gani?”
“Usijali, nitakwambia nini kilitokea,” alisema Benjamin huku akiendesha gari kwa kasi ya ajabu, alikuwa katika barabara ya St. Johnson ya magari yaendayo kasi kwa zaidi ya 180, ilikuwa ni lazima waondoke na kuelekea Alexandria, mji uliokuwa pembeni mwa jiji hilo la Washington DC.
Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumamosi.