SoC02 Matumizi ya mbinu mbadala za ufundishaji ili kuifanya elimu iendane na mazingira halisi ya taifa

Stories of Change - 2022 Competition
Jun 27, 2020
6
3
Utangulizi;

Tangu taifa letu lipate uhuru mnamo tarehe 9 Desemba, 1961 kumekuwepo na hatua kadha wa kadha za kuufanya mfumo wetu wa elimu uendane na mazingira yetu ya hapa nchini na kuendana na falsafa ya Afrika kwa ujumla. Hata hivyo, kumekuwa na changamoto na ukwamishaji wa makusudi kabisa wa hatua na juhudi hizo. Matokeo yake bado tumeendelea kuwa na mfumo wa elimu ambayo msingi wake bado ni kukariri. Makala hii inaangazia mambo anuwai kuhusiana na mfumo wetu wa elimu kwa kuanza na vipindi vitatu tofauti vya mfumo wetu wa elimu, changamoto ambazo bado zinaukumba mfumo wetu wa elimu pamoja na kuangazia kwa undani kabisa kuhusu mbinu mbalimbali zinazoweza kutumika katika taasisi hizi za kielimu ili kuifanya elimu yetu kuwa bora na kupendwa na wanafunzi wakati wa kujifunza.


Vipindi vya mfumo wetu wa elimu;

Elimu ya Tanzania imepitia vipindi vitatu tofauti na kila kipindi kilikuwa na nduni zake bainifu ambazo zinatofautisha kipindi hicho na vipindi vingine. Vipindi hivyo tunaweza kuviangalia kwa ufupi sana kama ifuatavyo;

i) Kabla ya ukoloni; elimu hii ilikuwa ikitolewa kuendana na mazingira husika. Jamii za kilimo zilifundishwa kuhusu kilimo na jamii za uvuvi zilifundishwa kuhusu masuala ya uvuvi. Elimu ya kila jamii iliendana na falsafa ya jamii husika. Baadhi ya mbinu zilizotumika kufundishia wakati huu ilikuwa ni kama vile mafunzo kwa vitendo (shambani, baharini au ziwani, porini kwenye mawindo n. k), kupitia nyimbo, hadithi, misemo, nahau, kupitia miiko mbalimbali kama vile ibada za mizimu, pamoja na kupitia jando na unyago.

ii) Wakati wa ukoloni; elimu iliyotolewa kipindi hiki ililenga kuimarisha misingi ya kikoloni na kuonyesha ukuu wa mtu mweupe. Falsafa na misingi ya ufundishaji ililenga kumtukuza mkoloni. Lengo kuu ilikuwa ni kupata waafrika wachache ambao wangeweza kuwasaidia wakoloni katika shughuli zao za kiutawala. Hapa ndiyo tulipata majumbe, maliwali na viongozi wengine wa ngazi za chini.

iii) Baada ya ukoloni; kuanzia kipindi cha uhuru mpaka sasa taifa letu bado linapambana kuifanya elimu yetu kuendana na utaifa wetu. Ni ukweli usiopingika kwamba bado athari za elimu ya kikoloni zinajitokeza hata sasa. Tangu kipindi hiki elimu yetu imepitia mabadiliko kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya mitaala.

Mifano ya mitaala ambayo taifa letu limewahi kuipitia ni pamoja na;
a) Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995
b) Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya mwaka 1996
c) Sera ya Taifa ya Elimu ya Juu ya mwaka 1999
d) Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014

Changamoto jumuishi zinazoikumba sekta ya Elimu na Mafunzo nchini mpaka sasa.

Hata hivyo, bado kumekuwepo na changamoto lukuki zinazoikumba elimu yetu. Changamoto hizo ni pamoja na;

i) Kukosekana kwa mfumo nyumbufu unaoruhusu elimu na mafunzo kupatikana na kutambulika kwa njia mbalimbali mbadala.

ii) Kuwepo kwa elimu na mafunzo yenye viwango vya ubora visivyotambulika kitaifa, kikanda na kimataifa.

iii) Kutokuwa na mfumo wa ajira unaowezesha upatikanaji wa wataalamu wa kada mbalimbali wanaohitajika katika sekta ya elimu na mafunzo nchini.

iv) Changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa, sayansi na teknolojia yanayotokea kila siku hivyo kuathiri ufanisi wa utoaji wa elimu katika taasisi mbalimbali za kielimu nchini.

Mbinu mbadala za kuifanya elimu yetu iendane na mazingira halisi ya taifa letu;

i) Matumizi ya vielelezo; matumizi ya vielelezo mbalimbali husaidia kufanikisha dhima ya uelewa wa somo husika kirahisi kwa wanafunzi wote wanapokuwa wanajifunza. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wanafunzi tunatofautiana wakati wa kujifunza na hata tofauti zetu pia huweza kutofautiana. Vielelezo hivyo vinaweza kuwa picha, ramani, chati, grafu, video pamoja na lugha za alama. Mbinu hii huwasaidia wanafunzi wenye uwezo wa kuelewa kupitia uoni kuelewa Zaidi na hata wanapoulizwa wanaweza kueleza zaidi kupitia namna walivyoona siyo walivyoambiwa.

ii) Matumizi ya visikizi; baadhi ya wanafunzi hujifunza vema zaidi zinapotumika mbinu za visikizi ambavyo ni tofauti na sauti ya mkufunzi (mwalimu) ambayo mara nyingi wanakuwa wameizoea. Hapa mkufunzi anaweza kutumia mbinu mbalimbali kama vile matumizi ya hotuba au mihadhara iliyorekodiwa, muziki au nyimbo, vitabu vya sauti na aina nyingine za vinasa sauti.

iii) Matumizi ya uandishi au usomaji; wanafunzi wengi hasa katika ngazi za chini za elimu wanapendelea Zaidi kusoma maandishi ambayo yanakuwa yameandikwa na mwalimu au mtu mwingine. Hawa huamini na kuelewa zaidi wakisoma au kunakili kilichoandikwa. Hivyo, mkufunzi anaweza kulisaidia kundi la watu fulani wenye ugumu wa uelewa kwa kuandika kitu hicho. Mwalimu pia anaweza kuwapatia wanafunzi kazi za kuandika ili waongeze uwezo wa kuelewa kutokana na walichojifunza.

iv) Mbinu za ushirikishwaji; uwezo wa kushiriki kwenye ujifunzaji kwa njia ya kushiriki huwasaidia sana wanafunzi kujifunza zaidi. Wanafunzi wanaweza kushirikishwa kwa kugawanywa kwenye makundi madogomadogo na kupewa nafasi ya kuwasilisha kile walichojadili kwenye makundi yao. Wanafunzi wanaweza kukumbuka na kuelewa zaidi kutu ambacho kimetolewa ufafanuzi na wao au ndugu zao. Kwa mfano, juma akiuliza swali likajibiwa na Asha, Juma anaweza kuelewa zaidi kwa sababu atakumbuka kwamba swali lake lilijibiwa na Asha. Wakati mwingine mwalimu hatakiwi kuwa wa kwanza kujibu kila kinachoulizwa. Anashauriwa kuwashirikisha wanafunzi wengine kwanza.

v) Matumizi ya simulizi; mwalimu au mkufunzi anaweza kusimulia jambo lenye kusisimua, kugusa hisia na kuwa funzo kwa wanafunzi lakini jambo au simulizi hiyo lazima iendane na somo husika. Mbinu hii ni muhimu sana kwa sababu inawasaidia wanafunzi kuvuta hisia na uwepo katika somo husika. Hebu angalia watu wanavyofuatilia sauti za hotuba mbalimbali za watu mashuhuri. Sauti hizo zikihusu simulizi ndiyo inakuwa zaidi.

vi) Michezo mbalimbali; matumizi ya michezo hasa kwa watoto wa ngazi za chini za elimu yanasaidia sana watoto kumpenda mwalimu na kulipenda somo kwa ujumla. Binafsi, kuna masomo kadhaa ambayo niliyapenda kwa sababu niliwapenda walimu waliokuwa wakifundisha masomo hayo. Ubunifu wa walimu hao ulisaidia sana kunihamasisha na hatimaye nikajikuta nimeyapenda masomo hayo.

vii) Mbinu ya majadiliano; mwalimu au mkufunzi unashauriwa kuwapatia nafasi wanafunzi wako ili wapate nafasi ya kujadiliana wao kwa wao kabla hujaja kutoa maamuzi jumuishi. Mbinu hii huwaongezea wanafunzi ujasiri wa kushiriki kwa kuchangia mawazo yao wawapo darasani. Unaweza kuwagawa kwenye makundi ya watu watano watano ili wajadiliane.

Hitimisho; msingi mkuu wa mbinu hizi upo kwenye ushirikishwaji kati ya mwalimu na mwanafunzi. Aidha, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla wanayonafasi kubwa sana katika kufanikisha suala la ujifunzaji kwa wanafunzi. Hali hii itasaidia kwa namna moja ama nyingine kuifanya elimu iendane na mazingira yetu.
 
Back
Top Bottom