Matokeo ya Kidato cha nne 2012: Mataifa mawili katika nchi moja! - Zitto

Neiwa

JF-Expert Member
Feb 17, 2012
728
633
Kila Mtanzania sasa anajadili matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012 yaliyotangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi mwanzoni mwa wiki hii. Matokeo hayo yanaonyesha kwamba zaidi ya asilimia 90 ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne walipata daraja la nne na daraja la sifuri. Dara la Sifuri limebeba asilimia 60 ya matokeo yote. Taifa limepata mtikisiko mkubwa kuona vijana wake wakiwa wamefeli kwa kiwango hiki.

Hata hivyo hii sio mara ya kwanza kupata matokeo ya namna hii. Ukiangalia matokeo ya kidato cha nne kuanzia mwaka 2009 utaona kuwa kila mwaka wanafunzi wanaofeli wanaongezeka. Mwaka 2011, wanafunzi 302,000 sawa na asilimia 89 ya wahitimu wote wa kidato cha nne walipata daraja la nne na sifuri.

Mwaka 2010 wanafunzi 310,000 ambao ni asilimia 90 ya wahitimu walipata madaraja hayo ya chini kabisa na mwaka 2009 jumla ya wanafunzi 195,000 sawa na asilimia 78 ya wahitimu wote walipata madaraja ya sifuri na daraja la nne. Kila mwaka matokeo yakitangazwa kuna kuwa na mjadala wa wiki moja au mbili, wabunge tunapiga kelele kidogo kisha tunasahau kabisa suala hili mpaka matokeo mengine.

Hivi tumewahi kujiuliza hawa vijana wanaoishia kidato cha nne wanakwenda wapi? Wanafanya nini? Hii nguvu kazi kubwa ya Taifa inapotelea wapi?

Ni vema ifahamike kwamba Tanzania ni Taifa la vijana na watoto. Kwa mujibu wa taarifa za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, hivi Tanzania ina jumla ya vijana 38 milioni wa chini ya umri wa miaka 35 , hii ni sawa na idadi ya watu waliokuwepo Tanzania mwaka 2003. Asilimia 78 ya Watanzania wapo chini ya umri wa miaka 35 na nusu ya Watanzania wapo chini ya umri wa miaka 17. Kwa takwimu hizi ni dhahiri kwamba suala moja kubwa kuliko yote linalohusu Watanzania ni Elimu. Suala moja kubwa linaloweza kujenga au kubomoa Taifa hili ni Elimu. Suala moja kubwa linaloweza kuepuka matabaka katika nchi ni Elimu. Tena Elimu Bora, na BURE.

Kuna nadharia inaitwa ‘gawio la idadi ya watu’ na ‘bomu la idadi ya watu’. Nadharia hizi zatumika kuelezea namna mataifa yanaweza kufaidika au kupata hasara kutokana na kuwepo kwa nguvu kazi kubwa ambayo ama inatumika kwa faida ya nchi hiyo kwa kufanya kazi na kuongeza uzalishaji ama inatumika kwa kwa kukaa tu kwenye vijiwe na kupiga soga.

Taifa ambalo linaandaa vijana wake kwa maarifa na stadi za kazi huvuna gawio (demograpich dividend). Mataifa yaliyofaidika na hali hii ni kama India, Uchina na Ujapani ambapo nyakati wana vijana wengi sana kuliko wazee vijana hawa walipewa ujuzi mkubwa na stadi za maisha na hivyo kuongeza uzalishaji mali kwa Taifa. Watu ndio mtaji mkuu wa Taifa lolote lile duniani. Taifa ambalo haliandai vijana wake kupata elimu huingia kwenye mgogoro mkubwa maana kundi la vijana wasio na kazi na wasio na maarifa yeyote ni sawa sawa na bomu.

Tanzania tuna chaguzi katika masuala haya mawili, ama tuvune gawio la kuwa na vijana wengi sana kwa kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika Elimu au tusubiri bomu lilipuke. Kwa matokeo haya ya kidato cha nne kwa miaka minne iliyopita, ni dhahiri tumeamua kulipikiwa na bomu.

Tunajua chanzo cha matokeo haya. Watoto hawasomi wala kujifunza shuleni. Hasa watoto wa vijijini ambapo hakuna walimu wala vitabu. Tumejenga mataifa mawili ndani ya nchi moja, Taifa la masikini na wana shule zao, wanapata masifuri kila siku. Taifa la walalaheri wana shule zao na wanapata madaraja ya juu. Hawa ndio watakaoenda vyuoni na wenye elimu wataendelea kutawala. Suluhisho ni moja tu, kuamua kwa dhati kabisa kuwekeza kwenye elimu kwa kuhakikisha kuna walimu wa kutosha, walimu wanalipwa vizuri na kuishi kwenye mazingira mazuri. Iwe na marufuku wenye kufeli ndio wafanye kazi ya ualimu.

Ni lazima kuhakikisha kuwa kunakuwa na vitabu vya kutosha kwenye mashule. Serikali ihakikishe kwamba inaingia makubaliano na wachapishaji wa vitabu wa ndani na kutoa vitabu vinavyojenga Taifa kwa kutoa maarifa ya uhakika kwa watoto. Ieleweke kwamba shughuli ya uchapishaji wa vitabu ni ajira tosha iwapo tutawezesha wachapishaji wa ndani kutoa vitabu vingi zaidi na vyenye ubora.

Matokeo ya mwaka huu ya kidato cha nne yanatuambia jambo moja kubwa sana, kwamba sisi ni Taifa linalokufa. Tuweke siasa pembeni na kahakikisha kwamba kunakuwa na uwajibikaji kwa viongozi kutokana na matokeo ya namna ya hii ya vijana wetu. Tusione tabu kubadilisha mawaziri wa Elimu kila mwaka kwa kuwafukuza kutokana na matokeo ya mitihani ya watoto wetu. Hii itafanya Waziri ajue umuhimu wa elimu anayoisimamia. Tukate mzizi wa fitina, elimu ni suala la uwajibikaji. Makala zijazo tutaona hatua za kuchukua ili kuhakikisha hawa watoto zaidi ya 300,000 waliofeli tunawafanya nini.



Source: Kiongozi - Februari 22, 2013
 
ili tujue kwa nini watoto wanafeli, kwanza ni kuitoa ccm madarakani, maana wao hawana uchungu wa watoto wanavyofeli
 
hebu muulize Kikwete yule mtoto wake wa DIV 4 yuko VETA inawezekana hata wa div wanatakiwa wapokewe form V
 
Raiss dhaifu hawezi kuteua mawazili wachapakazi,subiri 2015,dr wa ukweli na cdm tutaikomboa elimu
 
Rais dhaifu hawezi kuteua mawaziri wachapakazi,subiri 2015,dr wa ukweli na cdm tutaikomboa elimu
 
Rais dhaifu, CCM dhaifu, wanafunzi dhaifu, matokeo dhaifu na tunaelekea kwenye Tanzania dhaifu. Miaka ijayo itabidi nafasi za kazi ziwe za experts wa nje kwani kutakuwa na watanzania dhaifu. Nawasilisha. Tuache siasa tuangalie tutakuwa wapi baada ya miaka 20 hadi 60 ijayo
 
Magamba wakiendelea kutawala nchi hii taifa litaangamia. Wao wanawaza kupata 10% katika mikataba ya uchimbaji wa mafuta,gesi na madini tu.
 
Swali, swali, nasema tena swali, Baba asiyekula nyumbani atawajibika vipi kuboresha lishe ya watoto na familia yake wakati yeye hataki kabisa kugusa au kukiona hata hicho chakula kinachopikwa na kuliwa nyumbani mwake???? Swali, swali, nauliza swali jingine, hivi watoto wenu nyie wabunge, mawaziri, ma-afisa wa serikali wanasoma wapi, katika hizo shule mnazosema mmejenga nyingi au wapi??? swali, swali jingine tafadhali, hivi kwa nini isiwe amri au sheria kali pengine ikawa agizo la kikatiba kwamba mtumishi yeyote wa umma ni marufuku kusomesha mtoto wake shule za private na akitaka kufanya hivyo aachie utumishi wa uma hasa hasa kama anahusika au ana dhamana ya maendeleo ya sekta ya elimu, hili linaweza kuangaliwa hata kwenye mambo ya Afya ambapo viongozi kila kukicha wako nje kutibiwa halafu wanasema eti wana mikakati ya kuboresha afya.....???!!!!!!

Swali langu jamani sina jibu ebu nipeni mwenye kujua majibu yake.....

...........................................................
Matokeo ya mwaka huu ya kidato cha nne yanatuambia jambo moja kubwa sana, kwamba sisi ni Taifa linalokufa. Tuweke siasa pembeni na kahakikisha kwamba kunakuwa na uwajibikaji kwa viongozi kutokana na matokeo ya namna ya hii ya vijana wetu. Tusione tabu kubadilisha mawaziri wa Elimu kila mwaka kwa kuwafukuza kutokana na matokeo ya mitihani ya watoto wetu. Hii itafanya Waziri ajue umuhimu wa elimu anayoisimamia. Tukate mzizi wa fitina, elimu ni suala la uwajibikaji. Makala zijazo tutaona hatua za kuchukua ili kuhakikisha hawa watoto zaidi ya 300,000 waliofeli tunawafanya nini.



Source: Kiongozi - Februari 22, 2013
 
nahisi kama tunampigia mbuzi gitaa acheze kwa sababu kelele zetu Kawambwa jana anatuambia tusiilaumu serikali wala kelele za yeye kuwajibika kwa kufeli kwa watoto wetu ni kelele na majungu ya kisiasa juu yake.
 
Katika hili ondoeni siasa tutafakari njia sahihi ya kuliondoa hili tatizo, kama kusoma ktk shule nzuri kila mzaz mwenye uwezo anafanya hvyo na watamshangaa kama atamua kumpeleka mwanae ktk shule isiyokidhi, mfano mh mbowe wanae wanasoma wp? Ye ni kiongoz wa chama kinachopigania elimu bora kwanini hawaja mfano wa kuwapeleka wanae shule ya kata then kwakuwa anauwezo aisaidie hyo shule kiuchum ili ipate vitabu,maabara na vinginevyo ili iwe mfano kwa taifa,mana atakuwa amelisaidia pia.tukae tuangalie tunachoweza kufata kama taifa siyo kuilaumu serikali pekee
 
hapana bobovic ni lazima tujue sasa ni kwanini afu tukiwatoe tujue tunafanyeje!
ikiwa mafaili yote wanayo wao, Mitaala wanayo wao tukiwaomba watuonyeshe hawataki lakini wanasema ipo,sasa utayaonaje hayo mafaili ili ujue utaanzia wapi, hivyo ni kuwatoa kwanza kama tulivyofanya kwa wakoloni
 
nahisi kama tunampigia mbuzi gitaa acheze kwa sababu kelele zetu Kawambwa jana anatuambia tusiilaumu serikali wala kelele za yeye kuwajibika kwa kufeli kwa watoto wetu ni kelele na majungu ya kisiasa juu yake.
mimi naisifu sana serikali kwa watoto kufeli na Waziri asijiuzulu ili mwakani tufikie asilimia 70,au tupunguze iwe asilimi 55 lakini watakaoingia sekondari wengi wawe awajui kusoma na kuandika
 
okay sir! ila rejea takwimu zako na mfululizo wake, kama vile kuna "error"
 
Back
Top Bottom