Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 20,935
- 30,280
MARA YANGU YA KWANZA KUMTIA MACHONI IDDI SIMBA 1980s
Ilikuwa miaka ya 1980 tuko nyumbani kwa marehemu Bi. Mruguru bint Mussa, mama yake Ally Sykes Mtaa wa Lindi.
Pametokea msiba Bi. Mariamu, shangazi yake Bwana Ally Sykes amefariki.
Watu wamejazana mtaa umefungwa wanasubiri muda wa mazishi.
Bwana Ally mwenyewe kakaa jamvini kazungukwa na jamaa zake wa Gerezani, wamekukuja kuungananae katika msiba wa shangazi yake.
Watu ni wengi sana.
Bwana Ally yeye mwenyewe ni mzishi sasa leo limemfika ndugu zake wamemwitika kwa wingi sana, wamekuja kumzika.
Bwana Ally kuniona ananita nende nikakae nae mbele.
Basi nanyanyuka pale nyuma nilipokuwa kwa unyonge maana umma mzima unaniangalia watu wanajiuliza huyu anaeitwa mbele pale ana umuhimu gani?
Katika lile jamvi alokuwa Bwana Ally ni “nani aliye nani katika mji wa Dar es Salaam,” Waingereza wanasema “Who is Who,” wenyewe watoto wa Gerezani na Dar es Salaam wametanda.
Iddi Simba alikuwa amekaa jirani ya Ally Sykes.
Amevaa nguo zilizomkaa vyema kapendenza na miwani yake.
Sasa Bwana Ally anawanadia watu, “Nyie mnamjua huyu? Mtoto wa Said pale Kipata mwandishi hodari sana…”
Utambulisho umekwisha nakaa pembeni Ally Sykes na Zuberi Mtemvu wanashambuliana kwa maneno.
Bwana Ally kalalamika kuhusu hali ya nchi mambo hayendi vyema.
Zuberi Mtemvu kadakia anawashahidisha watu, “Jamani mnasikia Ally analalamika ati mambo hayendi sawa…”
Mtemvu anaangua kicheko cha kejeli huku akitingisha kichwa.
Watu sasa weshakuwa hadhir wanasubiri Mtemvu atasema kitu gani?
“Huyu Ally na marehemu kaka yake Abdul (Mungu amrehemu) walikuwa wanashirikiana na Nyerere kukipiga vita chama changu kife, leo Ally huyu huyu keshageuka ati nchi imeharibika…”
Wasikizaji wanacheka wengine wanamuunga mkono Bwana Ally wengine Zuberi Mtemvu.
Bwana Ally hakubali kushindwa anarudisha kombora, “Ala kumbe Congress bado mko hadi leo nilidhania tulishakumalizeni.”
Vicheko.
Mzee mmoja kwa mbali anaita, “Ally sikiza bwana, Congress tupo sana. Congress ni mwamba usiovunjika.”
Vicheko vinaendelea.
Hii “Congress ni mwamba usiovunjika,” ni maneno yaliyokuwa katika nyimbo ya Congress wakati wa harakati za kudai uhuru.
Watu wametulia Bwana Ally akafahamu kuwa Mtemvu alikuwa hamjui Iddi Simba na pale akawatambulisha.
Nilishangaa sana vipi miamba hii yote ya Gerezani isifahamiane.
Hapo nami ndipo nikamfahamu Iddi Simba ingawa jina lake lilikuwa maarufu katika vyombo vya habari kila inapotajwa East African Development Bank iliyokuwa na makao makuu yake Kampala Uganda.
Kuanzia hapo Mzee Iddi Simba kila tutakapokutana atakuwa na la kunieleza.
Mzee Iddi Simba alikuwa na kawaida kila akimaliza kusali Dhuhr Msikiti wa Manyema hatoki atakenda kukaa nyuma ya msikiti na jamaa zake watamfuata pale.
Nami hii ndiyo ilikuwa fursa yangu ya kusalimiananae kila nikiswali Msikiti wa Manyema na hapo utamkuta kakaa na rafiki yake kipenzi Muharam Kocha.
Napenda kuhitimisha kwa kueleza kisa kimoja.
Anur Suleiman alipata kuwa Mkuu wa Mkoa Mwanza katika miaka ya 1970/80.
Huyu bwana alikuwa anajenga msikiti sikumbuki kama ni kwao Bukoba au Mwanza.
Akaleta vitabu vya risiti kwa ajili ya kuchangisha nami nikapewa kimoja nichangishe hapa Dar es Salaam.
Basi siku hiyo nikamkuta Mzee Iddi Simba kakaa kwa Daddy huyu alikuwa fundi cherehani maarufu Kariakoo karibu na Saigon ya zamani, Mtaa wa Sikukuu.
Katika maisha yangu hadi hii leo sijawahi kuchangisha kitu chochote nikapata fedha nyingi kama nilizopata katika mchango huu kiasi hata yule aliyenipa kitabu kile alipigwa na butwaa.
Nikamfuata Mzee Iddi Simba kakaa pale kwenye benchi na vijana wa Saigon mtu akikwambia ukubwa wa mtu huyu na hadhi yake utakataa utajiuliza pale anafanya nini?
Mzee Iddi Simba akanisikiliza kisha akabaki kimya hakunambia chochote nami nikaondoka.
Nilidhani hakutaka kunipa mchango.
Baadae kidogo akanifanyia ishara nimfuate.
Fedha alizonipa kama mchango wake wa msikiti zilinishtua na naamini wale waliokuwa wakitaka kuchanga wanataka kwanza waangalie nani na nani washachanga bila shaka mchango ule uliwatia motisha angalau na wao watoe kingi wamkaribie Iddi Simba.
Allah amfanyie wepesi mzee wetu safari yake na amsamehe.
Amin.
PICHA: Mzee Iddi Simba na Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu katika futari ya Saigon mwaka wa 2010