Mapooza ni nini na yanaepukwa vipi

Mapooza ni nini na yanaepukwa vipi

john achila mukumwa

Senior Member
Joined
Jan 4, 2024
Posts
138
Reaction score
275
Mapooza ni nini na yanaepukwa vipi

Mapooza ni vitu au mambo yo yote yasiyoweza kuzalisha chochote, au kufikia kilele chake cha kutoa matunda kamili.

Neno mapooza limetokana na neno kupooza. Kwa mfano, tunaposema mtu amepooza mkono, maana yake ni kwamba anao mkono lakini hana uwezo wa kufanya kazi ya mkono, yaani unakuwa kama vile umekufa, lakini upo.


Nazi zote zinazotoka katika mti wa mnazi, si zote zinafaa kama kiungo, bali nyingine ni koroma. Hizo koroma ndiyo mapooza yenyewe, japo kwa nje zinaonekana ni nazi.

Kwenye biblia, neno hilo la mapooza tunalisoma katika vifungu mbalimbali.

Kifungu katika 2Wafalme 2
19 “Watu wa mjini wakamwambia Elisha, Angalia, twakusihi, mahali pa mji huu ni pazuri, kama bwana wangu aonavyo; lakini maji yake hayafai, na nchi huzaa mapooza.
20 Akasema, Nileteeni chombo kipya, mtie chumvi ndani yake. Wakamletea.
21 Akatoka akaenda mpaka chemchemi ya maji, akatupa ile chumvi humo ndani, akasema, Bwana asema hivi, Nimeyaponya maji haya; hakutatoka huko tena kufa wala kuzaa mapooza.
22 Hivyo yale maji yakapona hata leo, sawasawa na neno la Elisha alilolinena".

Maana yake ni kwamba yale maji waliyokuwa wanakunywa au kuyatumia kwa mimea yalikuwa si mazuri, yanazaa mapooza, yaani vitu vyake havistawi au kuleta matunda. Mimba za wanawake zilikuwa zinatoka. Mboga mboga zilizokuwa zinanyweshewa zilikuwa hazikui ipasavyo. Wala miti haikuivisha matunda yake.

Hivyo, Elisha alipoagizwa na Mungu kutia chumvi katika yale maji, wakati ule ule yakaponywa. Hivyo kukawa hakuzaliwi mapooza tena katika ile nchi.

Je, mapooza yapo hadi sasa?
Jibu ni ndiyo. Kwa mfano, wewe ni mwanamke, halafu kila unaposhika mimba, kabla hujajifungua inatoka. Huenda kuna mapooza nyuma yake.

Au unafanya shughuli fulani, ambayo kwa muda mrefu sana, haijakuletea mafanikio yo yote, hayo pia ni mapooza.

Au unalihangaikia jambo lolote lile jema, lakini kwa muda mrefu, unaona kama kuna dalili njema zinaonekana, lakini mwishoni linakufa. Ujue pia mapooza yapo hapo.

Una karama ya muda mrefu, lakini haina matunda yoyote katika ufalme wa Mungu.

SULUHISHO NI NINI?
Ili kuepukana na mapooza, yapo mambo mawili makuu ya kufanya.

1. KUTIWA CHUMVI
Kama vile Elisha, alivyoagizwa akatie chumvi ndani ya yale maji yaliyozaa mapooza, vivyo hivyo na wewe.

Huna budi kukubali kutiwa chumvi ili mapooza yaondoke ndani yako.

Hapa hatuzungumzii chumvi ya upako, tunazungumzia Neno la Mungu.

Mungu alimuagiza Elisha atie chumvi siyo kwamba alikuwa anatuonyesha kuwa kuna upako ndani ya chumvi, bali alikuwa anatoa taswira ya kufahamu chumvi ni nini katika ulimwengu wa roho, na sisi tunatiwaje chumvi.

Bwana Yesu alisema, katika Marko 9:
47 “Na jicho lako likikukosesha, ling’oe, ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum;
48 ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.
49 Kwa sababu kila mtu atatiwa chumvi kwa moto”.

Tafakari vema, jiulize, kwa nini baada ya kutoa maagizo makali kama hayo, mwishoni akamalizia kwa kusema, kila mtu atatiwa chumvi kwa moto.

Maana yake ni kuwa ili utiwe chumvi, huwezi kuepuka moto.
Ili maisha yako yaponywe, huwezi kuepuka kukata baadhi ya viungo vyako vinavyokukosea (Marko 9:47)

VIUNGO VYA KUKATA NI VIPI?

Marafiki wabaya

Watu wengi wana marafiki ambao, wamekuwa vyanzo vibaya vya kufikia maono yao. Wakikaa nao ni matusi, mashauri mabaya, kutenda dhambi, nk. Achana nao. Wakimbie. Ndiyo itauma kuwaacha, lakini ndivyo chumvi inavyoponya.
Kazi mbaya
Wapo watu ambao hawawezi kuishi bila kufanya biashara haramu, kuhonga, halafu muda huo huo anataka Yesu amsaidie, katika kazi hiyo hiyo. Kamwe huwezi kufanikiwa.
Hiyo ndiyo njia ya kwanza yenye matokeo. Kataa kwa nguvu zako zote, watu/vitu/mambo ambayo yanakufanya usiwe safi mbele za Mungu.
Kwa lugha nyepesi, ni kwamba unapaswa uokoke kwa kumaanisha kabisa kumfuata Yesu Kristo. Hakikisha umejitwika msalaba wako. Hii ndiyo njia kuu ya kuondoa mapooza yoyote ndani yako.

2. MAOMBI YA UPONYAJI NA KUKATAA ROHO ZA MAPOOZA
Katika maombi ya uponyaji, kwa imani, Yesu atakufungua, wewe ambaye, tayari umeshampokea Yesu na kumfuata, au yule ambaye ameahidi kufanya hivyo.


Katika maombi, elekeza mawazo yako palipo na mapooza, yaani tatizo linalokusibu. Inaweza kuwa ni kuhusu ndoa, kupata mtoto, kupata kazi, kupata mafanikio kwenye biashara, nk.

Kuzaa mapooza huanzia rohoni. Unaweza kupambana kubadilisha kazi, biashara, na watu, bila mafanikio. Maana ni jambo la kiroho. Ni roho ya kishetani inayosababisha vitu kufa kabla ya wakati wake.

Tatizo ni kuwa watu wengi wanakuwa na roho ya mapooza hata kwenye maombi.

Mtu anapanga aombee jambo kwa siku kadhaa. Anaomba nusu anaacha. Anaanza kuombea jambo lingine, nalo anaacha, anarukia lingine.

Jiambie kabisa, leo nimeamua kushambulia kila chanzo cha roho cha kuzaa mapooza kwenye maisha yangu, katika Jina la Yesu. Roho yo yote iliyopandwa kwenye maisha yangu naifuta, kwa Jina la Yesu. Ewe roho ya kuzaa mapooza nakung’oa, kwa Jina la Yesu.

Yapo mapooza ambayo watu wameyasia ili baadaye yaote maishani mwa watu. Inabidi kuomba Mungu akupe uwezo wa kuzing’oa roho za mapooza maishani.
Dhamiria kutoka moyoni kuwa unakataa kupata na kupoteza kwa Jina la Yesu.

Ninakataa hasara kwenye maisha yangu.
Nakataa kupata kazi na kufukuzwa.
Nakataa roho ya mauti, Nakataa roho ya mapooza.
Nakataa kunyang'anywa kile nilicho nacho, kwa Damu ya Yesu
Chochote kilichopandwa ndani yangu ili nipooze nakikataa kwa Jina la Yesu.

Sema na kila upepo wa kiroho unaopeperusha miujiza na baraka zangu, ng’ooka, kwa jina la Yesu.
Wengine ndoa ilikaribia tu kufungwa, inapeperuka. Akikaribia tu kupata kazi, anapata kikwazo.
Ewe upepo wa kisulisuli uliotumwa ili upukutishe mayai ndani ya tumbo langu nizae watoto wanakufa, leo nakufyeka kwa Jina la Yesu, rudi ulipotoka.
Kila upepo wa kichawi uliotumwa upukutishe msaada wangu na watu wa kunisaidia, leo nakuagiza kwa Jina la Yesu, simama.
Mganga yeyote wa kienyeji, uliyetumwa kupukutisha furaha yangu, leo nakushinda kwa Jina la Yesu.
Yeye alaye, nakung’oa kwa Jina la Yesu.
Mapooza ya kazi, mapooza ya mahusiano, mapooza ya furaha yangu, ng’ooka kwa Jina la Yesu.

Kwa kuhitimisha, mapooza ni vitu au mambo yo yote yasiyoweza kuzalisha chochote, au kufikia kilele chake cha kutoa matunda kamili.

Katika suluhisho dhidi ya mapooza, kuna mambo makuu mawili.
Kwanza ni kutiwa chumvi. Na pili ni maombi ya uponyaji na kukataa roho za mapooza.
 
Back
Top Bottom