SoC03 Mambo yanayochochea utawala bora na uwajibikaji katika nyanja mbalimbali

Stories of Change - 2023 Competition

Loveness Barnabas

New Member
Mar 23, 2023
2
2
Utawala bora na uwajibikaji; Ni mamlaka na haki ya kuongoza kwa kufuata taratibu za kikatiba, na kujitoa katika kufanya mambo yote yaliyo majukumu anayotakiwa kufanya kiongozi au mtu yeyote aliye na dhamana katika eneo husika. Uwazi, usawa, Uhuru wa vyombo vya habari pamoja na uwajibikaji ni miongoni mwa misingi muhimu ya utawala bora. Maendeleo ya nchi yoyote hutegemea kwa kiasi kikubwa uimara wa utawala bora sambamba na uwajibikaji.Dhima ya utawala bora na uwajibikaji ipo katika nyanja mbalimabli, mfano; siasa, michezo, kilimo, elimu pamoja na masuala ya haki na sheria.Kwa upande wa nchi Kama Tanzania yapo mambo mengi ambavyo kimsingi yanaweza kuwa chachu ya utawala bora na uwajibikaji katika sekta zote.
Baadhi ya mambo ambayo yanaweza kuchochea uwepo wa utawala bora na uwajibikaji ni haya yafuatayo;

Katiba bora; Huu ni muundo wa Sheria na taratibu zinazoongoza kikundi cha watu au nchi katika utekelezaji bora wa majukumu mbalimbali. Endapo Sheria na taratibu za nchi zikiwa imara na madhubuti, Kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa utawala ulio bora na wa sheria pamoja na uwajibikaji.Pale ambapo viongozi katika nyanja mbalimbali watajitoa kikamilifu katika kutimiza wajibu zao kwa kufuata nini katiba inasema na mapendekezo ya watu anaowaongoza.

Uzalendo; Hii ni hali ya mwananchi kuithamini nchi yake na kuwa tayari kufanya mambo kwa haki na uwazi.Uzalendo ni msingi mkuu wa utawala bora na uwajibikaji, hii ni kwasababu mtu au kiongozi ambaye ni mzalendo huwa tayari kuwajibika na kujitoa bila kujibakiza kwaajili ya watu wake. Kiongozi huwa tayari kuruhusu na kupigania maendeleo ya watu wake pasi na ukabila, rushwa, upendeleo wala udini.

Kuwa na elimu ya kutosha inayohusiana na masuala ya kiutawala; Hususani kwa viongozi ambao hupewa dhamana ya kuongoza nchi, ni muhimu watu hawa wawe na elimu ya kutosha kuhusiana na mambo ya utawala ulio bora sambamba na uwajibikaji. Kimsingi kiongozi/mtu yeyote anapoandaliwa kuwa mtawala kwa kupatiwa elimu inayohusiana na utawala, atakuwa na nafasi kubwa ya kufanya mabadiliko chanya kisiasa, kielimu, kijamii na kiuchumi. Mabadiliko hayo yatatokea endapo mtu huyo atakuwa tayari kuitumia vema elimu aliyonayo kuhusu utawala pale anapokwenda kuongoza au kuwajibika.

Demokrasia; Huu ni Uhuru wa wananchi kushiriki katika kuamua masuala ya kisiasa, kijamii, kisheria na kiuchumi. Uwepo wa demokrasia ya moja kwa moja kwa wananchi inasaidia uimarishwaji wa uwajibikaji Kati ya watu, pamoja na kuchangia mawazo bora ya kimaendeleo kwa uongozi uliopo.Haifai kwa kiongozi kuamua mambo bila kuwashirikisha wale anaowaongoza, hii ni kinyume na misingi ya utawala bora. Pasi na ushirikiano kati ya kiongozi na watu wake hupelekea kukosekana kwa umoja katika utekelezaji wa majukumu, mwishowe kuzorota kwa maendeleo katika sekta zote.

Uwazi na uadilifu; Hali ya ushirikishwaji wa wananchi au watu katika shughuli zote za kiutawala inachangia uwepo wa utawala bora na uwajibikaji. Kiongozi anatakiwa kuwa mfano wa kuigwa katika jamii kutokana na muonekano wake pamoja na tabia zake ambazo zinasadifu uadilifu katika maisha yake binafsi na yale ya kiutawala. Uwazi na uadilifu ni chimbuko la utawala bora na uwajibikaji bila shuruti kwa sekta za elimu, kilimo, biashara na nyinginezo.

Kutoa motisha katika sekta mbalimbali; Kiasili binadamu wote hufanya vema zaidi katika shughuli fulani pale wanapopata motisha(msukumo mzuri). Ubora wa utawala na uwajibikaji unaweza kuchochewa kwa asilimia kubwa na uwepo wa motisha katika sekta husika. Mfano; Upandishwaji wa madaraja kwa wafanyakazi kwa wakati husika, posho kwa wafanyakazi katika semina au kazi zilizo nje ya ajira husika, kuwathamini wakulima kwa kupanga bei nzuri za mazao, kupunguza tozo zinazowaumiza wafanyabiashara wadogo n.k.Mambo hayo hupelekea wananchi kuona thamani yao na kujituma katika kulijenga taifa pamoja na maisha yao wenyewe kiuchumi, kisiasa na kijamii. Kuwajibika kwa wananchi kunakotokana na kuridhika kwa yale wanayofanyiwa na viongozi wao kunawapa viongozi urahisi katika kuongoza kwao hivyo kupelekea kuimarika kwa utawala.

Utatuzi wa kero au migogoro kwa wakati husika; Mtu yeyote mwenye dhamana ya kuongoza katika eneo fulani anatakiwa kuwa na ufanisi wa hali ya juu hasa katika kushirikiana na watu wake kutatua kero au migogoro inayojitokeza katika eneo husika.Hii inasaidia kuendelea kwa utekelezaji wa majukumu ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa muda muafaka. Uwepo wa kero au migogoro kwa kipindi kirefu pasi na kupatiwa ufumbuzi unachangia uwajibikaji hafifu wa wananchi katika sekta husika na kuzorota kwa mfumo wa utawala bora.Mfano mzuri katika nchi yetu ya Tanzania, kwa kipindi kirefu kumekuwa na migogoro kati ya wakulima na wafugaji katika maeneo ya wilaya za Mvomero, Kiteto na maeneo mengineyo yenye muingiliano wa wakulima na wafugaji. Hii inasababishwa na kukosekana kwa utawala bora, ambapo chanzo chake ni uwepo wa viongozi wasio na hekima na busara ya kutosha na ujuzi hafifu wa mambo ya kiutawala. Hivyo hupelekea kushindwa kutatua kero zinazowakumba wananchi wao. Ili utawala uzidi kuwa bora na watu kuwajibika ipasavyo, ni lazima viongozi wajifunze kutatua kero na migogoro inayotokea katika maeneo yao kwa wakati husika, wakiongozwa na hekima na busara.

Hitimisho; Ipo misingi mingi ya utawala bora na uwajibikaji ambayo Kama ikifuatwa na watu wote, mabadiliko makubwa yatatokea.Kati ya yote msingi mkuu ni kuwa na hofu ya Mungu, kwakuwa yeyote mwenye hofu ya Mungu daima hutenda mambo kwa haki na kuwajibika vema bila uvunjifu wa sheria na taratibu.Uwazi, uadilifu, utawala wa sheria, ufanisi na usawa vyote huimarisha utawala bora na uwajibikaji ambapo msingi wake ni hofu ya Mungu.
 
Back
Top Bottom