Mbunge amtetea Chenge kuwa hajawahi kuvunja nyumba ya mtu
Na Mwandishi Wetu, Dodoma,
MBUNGE wa Buchosa, Samwel Chitalilo ameibuka bungeni na kumtetea aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge kuwa si mwizi kwa kuwa hajawahi kuvunja nyumba ya mtu.
Mbunge huyo alisema hayo jana bungeni wakati akichangia katika hotuba ya Waziri Mkuu, kuwa Chenge si mwizi na hajawahi kuvunja nyumba ya mtu ili kuiba hivyo aachwe bila kusakamwa.
Chenge alijiuzulu baada ya kudaiwa kuweka kiasi kikubwa cha fedha huko Kisiwa cha Jersey ambazo alikiri kwamba ni zake, lakini hazihusiani na ununuzi wa rada.
Mbunge huyo alisema kwamba, alizingaliza benki ambazo zimekuwa na tabia ya kutoa siri za wateja kuacha kufanya hivyo.
Sambamba na kumkingia kifua Chenge, mbunge huyo pia alidai kuwa ni jambo la kushangaza kuona kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakimzungumza vibaya Rais wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa wakimhusisha na masuala ya ukiukwaji wa maadili.
Vilevile, Mbunge huyo alipongeza juhudi za aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ambaye
alijuzulu kutokana na sakata la Richmond, akidai kuwa kuwajibika kwake kulikuwa ni
kwa kisiasa.
Hata hivyo, wakati akiendelea na mchango akidai kuwa tabia ya wabunge kuingiza ushirikina na kutuhumiana kwa uchawi haifai, kwa sababu wataanza kutajana ovyo, Spika wa Bunge, Samwel Sitta aliingilia kati na kumtaka mbunge huyo kurudi kwenye hoja na kumuangaliza kuwa angalizo kuwa kila mbunge ana uhuru wa kuongea katika jumba hilo.
Aliporejeshwa katika hoja, Mbunge huyo aliamua kuikalia kooni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akidai kuwa imekuwa ikiwaonea wafanyabiashara kwa kuwabambikia kodi zaidi, hususani katika bidhaa zinazonunuliwa kutoka nje ya nchi.
Alisema kuwa wataalam wa TRA, wanajikita katika bei wanazoziona katika mtandao wa
kompyuta na kusahau kuwa biashara hufanywa ikitegemea nguvu ya mapatano.
Mbunge huyo alishauri kuwa katika wakati huu,Tanzania inapaswa kuepuka kuchanganya
masuala ya uchumi na siasa.
www.mwananchi.co.tz