SEHEMU YA PILI
SEHEMU YA PILI
Nikarejea hadi pale nilipokuwa nimesimama mwanzo, nikaanza kukitafuta kile kifurushi alichokiacha pale lakini sikukiona, nilihaha sana na kujiuliza nini kimemsibu yule kijana.
Na ni kitu gani alikuwa ameniachia katika fundo lile la nguo??
Lazima kilikuwa kitu cha msingi maana alionyesha kusihi sana.
Swali gumu jingine likawa, yule bwana amejuaje kama nitakuwa stendi asubuhi ile hadi aniletee ujumbe ule.
Nikiwa bado katika mtihani mgumu, mara basi nililotakiwa kusafiri nalo likapiga honi kuashiria kuwa dakika yoyote ile linaondoka.
Ule utata ambao huwa naujenga kwa wahusika katika simulizi sasa ukajijenga katika nafsi yangu na sikujua nautatua vipi?
Katiba basi tayari begi langu lilikuwa kule, sikukipata kifundo nilichoachiwa na mtu niliyeamini kuwa ni Anti Ezekiel.
Na ubaya mwingine sikujua hata kitu kilichokuwa kinamsibu Ezekiel.
Nikayakumbuka maneno yake usiku uliopita “nitakufa …lakini….IPO SIKU YAO NA WENYEWE”
Hakumalizia, na sikujua alitaka kusema nini.
Kwanini afe na hao wenyewe ni kina nani??
Nafsi yangu haikubariki wazo lolote kati ya hayo matatu yaliyokuwa yakinihangaisha kwa wakati ule. Ni kama nilikuwa mbumbumbu wa sekunde kadhaa.
Ufahamu ulinirejea baada ya kumuona mtoto mdogo akiwa na mfanowe kile kifundo mikononi mwake akirandaranda maeneo ya pale stendi, nilimwendea mbio mara akageuka na aliponiona akaanza kutimua mbio, sijui ni kipi alikiona kwangu hadi akaanza kutimua mbio kiasi kile, nilitamani sana atambue kuwa sikuwa na ubaya wowote bali nilihitaji kile kifundo, lakini angeanza vipi kunielewa iwapo watoto wadogo wasiokuwa na makazi maalumu maisha yao ni kama kivuli tu hawaishi kukimbia siku zote, na ningejuaje huenda alinifananisha na mgambo wa jiji ambaye husafisha mazingira hadi watoto wasiokuwa na makazi.
Niliendelea kutimua mbio hadi akafikia lile geti la kutokea nje ambalo magari huytumikia kupita pale, kwa sababu yeye alikuwa mbele alifanikiwa kupenya lakini mimi nikiwa mtu mzima nilizuiliwa, hakuna mtu aliyeruhusiwa kupita pale pasipo na sababu za msingi, nilijitahidi kumweleza yule bwana kuwa nina haja sana na mtoto yule lakini hakuonekana kukaribia kunielewa, akaniomba nimpe tiketi yangu ambayo itaonyesha kuwa nilikuwa ni abiria kweli lakini hata ile tiketi sikuwa nayo kwani niliiacha katika begi langu lililokuwa ndani ya gari.
Kitendo cha kurejea ndani ya basi kufuata tiketi kingekuwa cha kizembe tena kisichostahimilika na kile kifundo nisichokijua kingepotea hivihivi mbele ya macho yangu na kila kukicha ningeendelea kuteseka pasi na kujua ni ujumbe gani ulikuwa katika kifundo.
“Naomba nipite yule mtoto ameniibia!!!!” nilidanganya ili yule jamaa aweze kunielewa lakini aliendelea kuweka ngumu. Hasira zikanipanda na kuamua kufanya maamuzi, nikamsukuma kando kwa nguvu, akajikwaa na kupiga mweleka huko. Hapo sasa nikapenya kwa kasi, nyuma nikasikia filimbi ikipigwa, sikujali nilichohitaji ni kile kifundo, kwani kwa kukipata kile basi ningeweza kuituliza nafsi yangu.
Niliangaza huku na kule pasi na mafanikio ya kumwona yule mtoto, nilijaribu kuwaulizia watu juu ya mtoto yule lakini hakuna aliyejishughulisha nami, nd’o kwanza kulikuwa kunakucha na kila mtu alikuwa akijipanga kuikabili siku ile.
Sikukata tamaa, niliendelea kuangaza huku na kule, nilijitahidi sana kukumbuka kuwa mtoto yule hakuwa na nywele kichwani na alikuwa na kaptula iliyopasuka pajani, sikuwa nikiijua sura yake.
Nikajificha mahali na kuendelea kufuatilia nyendop za watu mbalimbali, baada ya dakika zipatazo kumi nikafanikiwa kumuona mtoto yule, mkononi hakuwa na kile kifundo lakini alikuwa ni yeye.
Nikamnyemelea na kufanikiwa kumkamata, nilimuuliza maswali kadhaa, akakiri kukiokota kifundo kile na alikitupa mahali, niliongozana naye hadi mahali alipodhani amekitupa.
Tukafanikiwa kukipata, nikampataia pesa ambayo angeweza kunywa chai na kula chakula cha mchana siku hiyo, nikakishindilia mfukoni, na hapo nikachukua pikipiki na hima nikamuamuru dereva alifukuzie gari ambalo lilikuwa na begi langu na tayari lilitoka stendi.
Wakati tunakubaliana bei na dereva mara niliguswa bega, ni kama alivyonigusa Ezekiel. Nikageuka upesi nikidhani ni Ezekiel tena, lakini sasa sikukutana na sura ya mtu bali ngumi kali katika shavu langu.
“We mpumbavu umejifanya mjuaji kunikimbia sivyo.” Alikoroma kipande cha mtu ambaye nilimsukuma kule getini ili niweze kukimbilia kile kifundo alichokuwanacho yule mtoto.
Wakati nataka kujitetea nikamuona yule jamaa akijiandaa kunirushia ngumi nyingine, nikajihami na kuruka kando.
Mwendesha pikipiki akaona isiwe tabu, akawasha pikipiki yake na kutoweka mbali.
Akaniachia kizaazaa kinikumbe peke yangu.
Amakweli mchuma janga hula na wa kwao!!
Kipande cha mtu kikiwa na hasira, kikanikaba mkono wangu kwa uimara wa hali ya juu. Akaanza kunivuta kuelekea anapotaka yeye.
Nikatambua kuwa nikifanya uzembe tu hata lile begi katika gari litapotea, huyu kipande cha mtu lazima angenifikisha katika chombo cha dola na hapo ndipo mlolongo ungeanza, mbaya zaidi hata kitambulisho changu cha kazi sikuwa nacho tena. Vyote vilikuwa katika begi langu.
Akili yangu ikanituma kufanya tukio la mwisho ambalo litaniweka huru, yule kipande akiwa ameridhika jinsi alivyonikwida nami nilijilainisha na kisha ghafla nikamfyatua mtama, mguu wake wa kushoto ukakutana na ule wa kuume, akaniachia kisha akayumba na kuanguka chini tena.
Nikatimua na kufanikiwa kuvuka upande wa pili wa barabara, nikakuta pikipiki nyingine, nikakwea na kutoa maelekezo kama yale niliyotoa awali kwa yule aliyenikimbia baada ya kupata msala.
Tukatoweka!!
Baada ya dakika thelathini nilikuwa nahema juu juu nikiwa ndani ya basi siti ileile, yaliyotokea yote yalikuwa kama ndoto.
Sikuamini kama nimefanikisha mambo yote kwa wakati na sasa nilikuwa katika safari yangu kana kwamba hakuna kilichotokea.
Bahati nzuri nilikuwa siti ya dirishani hivyo upepo ulipunga vyema na kunirejeshea amani pamoja na usawa katika akili yangu ambayo kidogo ilikuwa imeanza kuvurugika.
Hapo sasa nilijipekua mahali ambapo nilihifadhi kile kifundo, nilipanga nikifungue mwisho wa safari lakini kihoro kikanisukuma kukifungua kabla hata safari ya kuikaribia
Morogoro haijakaribia.
Nilifungua kwa makini na tahadhari ya hali ya juu huku nikijitahidi nisiiingie katika taharuki kwa kitu ambacho nilikuwa sijakiona bado.
Kifundo kikawa wazi hatimaye na ndanmi yake kulikuwa na funguo moja ambayo ilikuwa na kutu sana. Haikuonekana kama ilifungua mahali fulani katika siku za karibuni na wala haikuonyesha kama hata siku za usoni itakuwa na manufaa kwa kufungua mahali. Ama la hapo pa kufunguliwa na penyewe pana kutu na pamechakaa kwa kiasi kikubwa.
Funguo ya nini hii? Nilijiuliza huku nikifadhaika na kujiona kuwa nilihangaika na kukaribia kuiokosa safari yangu kwa sababu ya kitu kisichokuwa na mantiki.
Nikakifunga kile kifundo na kisha nikakiweka katika mfuko wa suruali yangu!!
Na hapo nikamkumbuka Ezekiel, hali niliyomshuhudia akiwa nayo maeneo ya Ubungo na hali niliyomshuhudia usiku mmoja kabla baada ya vurugu kumkumba nami nikamwokoa.
Alikuwa katika muonekano wa tofauti sana hasahasa asubuhi hiyo, alikuwa muoga na alitembea kikakamavu na ni kama alikuwa akiongozwa na watu!! Kisha akatoweka.
Akatoweka na asionekane tena!! Ufunguo ule mmoja ni wa nini? Na kwanini alinipa mimi?
Maswali haya yalinisumbua sana.
Simu yangu iliita na mlio wake ukayakatisha mawazo yangu yasiyokuwa na dalili ya kufika kikomo.
Ni namba kutoka ofisini kwetu, nikaipokea na kupewa taarifa kuwa semina iliyotakiwa kufanyika mjini Singida imesogezwa mbele kwa siku mbili kutokana na sababu ambazo nitaelezwa baada ya kufika Singida. Aliyenipigia simu akanieleza kuwa nitapewa posho ya kutosha kuniweka mjini pale hadi siku ya semina.
Simu hii ikanipa mwongozo mwingine, kama Singida hakuna semina kwa siku hiyo basi ningeweza kurejea jijini Dar na kama kuna lolote kuhusiana na Ezekiel na ule ufunguo basi nitaling’amua.
Katika maisha yangu hakuna kitu nilikuwa sipendi kama kubaki na majibu nusunusu!!!
Nilishuka Chalinze na kuchukua usafiri wa kurejea jijini Dar. Bahati nzuri nikapata basi linaloenda Kariakoo moja kwa moja.
Nikakwea, na baadaye tulikuwa tunapita Ubungo, nikatabasamu na kukumbuka balaa nililozusha asubuhi ile.
****
Niliujua ukorofi wa mama Eva ambaye ni mke wangu japo si wa ndoa. Hivyo nilimjulisha kuwa narejea jijini Dar baada ya dharula hiyo.
Nilifika nyumbani na kulitua begi langu kisha nikiwa na ule ufunguo uliochakaa nilienda nyumbani kwa Ezekiel ili kama kuna lolote niweze kutambua na nijue maana ya ufunguo ule uliochakaa tena wenye kutu. Nilishukuru kuwa muda ule nafika nyumbani mama Eva alikuwa ametoka kwenda sokoni maana sikuliona kapu ambalo huwa anabebea mazagazaga mbalimbali.
Upesi nikatoweka, safari hii sikumpa taarifa kuwa nimefika na kuondoka kwani nilitarajia kurejea upesi.
Katika safari yangu kwa Ezekiel nilitarajia kukuta lolote lile ambalo lingeweza kunipa mwanga iwapo kuna tukio limemsibu Ezekiel, lakini hapakuwa na lolote la kushangaza kila mmoja alikuwa katika harakati zake.
Chumba cha Ezekiel kilikuwa kimefungwa, nilijaribu kugonga hodi japo kwa ushahidi tu lakini hapakuwa na majibu.
Ili kuingia ndani ya nyumba ile nilihitaji kuwa na funguo!!
Kutaja neno ufunguo nikakumbuka kitu!
Ni hapo nikaukumbuka ule ufunguo wenye kutu. Nikajipekua na kuibuka na kile kifundo nikakifungua upesi na kuibuka na funguo wenye kutu. Japo sikuwa naamini sana kama yaweza kuwa kweli nililazimika kujiaminisha. Nikatazama kushoto na kulia hakuna hata mtu mmoja aliyejishughulisha na mimi, nikajikoholesha kama yupo ambaye atasema nami bado hakujitokeza mtu yeyote.
Naam!! Ufunguo ukakifungua kitasa, nikaingia ndani.
Sasa mbona una kutu huu funguo?? Nilijiuliza huku roho ya kipekuzi ikiniandama, na ni hii roho ilinituma mara kwa mara kufanya upekuzi mara kwa mara. Hata katika ofisi niliyoajiriwa walinitambua kwa tabia hii isiyokera bali kuwashangaza.
Mara nikakizoea kile chumba, nikaangaza huku na kule sikuona mabadiliko yoyote yale, nikajiuliza kama niliota kuonana na Ezekiel ama tulionana kweli.
Kama hatukuonana ule funguo ningeutoa wapi? Macho yangu yakavutika na karatasi iliyokuwa mezani, ilikuwa imeandikwa kwa wino mweusi mwandiko wa kuyumbayumba, bila shaka mwandishi aliandika huku akiwa na haraka sana.
“CHUMBANI USIACHE…PEKUA HATARI OKOA” maandishi yalisomeka vile, mapigo yangu ya moyo yakaenda mbiombio, nikaukumbuka mdomo wa Ezekiel kule Ubungo ulikuwa unachezacheza ukisema maneno haya kwa kurudia na sikuweza kutambua lolote lile.
Roho ya kidadisi ikazidi kunitawala, nikajiingiza kwa tahadhari kubwa katika chumba cha Ezekiel. Nilipoufikia mlango na wenyewe ulikuwa na tatizo lilelile, haukufunguka hadi ule ufunguo wenye kutu ulipoutekenya!
“Vitasa vinafanana ama…..” nilijiuliza huku nikiufungua vyema mlango.
Chumba kilikuwa kikubwa lakini hakikusheheni vitu vingi sana, kabati la nguo na meza ya kujirembea ya wanawake.
Meza ile ya kisasa ilikuwa na mtoto wa meza, na juu ulikuwa na vipodozi tele, haraka nikauendea mtoto wa meza, nikauvuta na hapo nikakutana na makaratasi mengi yakiwa yameandikwa mambo ambayo sikuyaelewa, nikayatwaa yote na kuyajaza katika mfuko mmoja mweusi, nikapapasa huku na kule sikukutana na kitu kingine ambacho niliona kina maana kwangu.
Katika hayo makaratasi kuna yaliyokuwa yameandikwa na mengine hayakuandikwa chochote.
Nikabeba, wakati nataka kutoka nje nikakumbuka karatasi ile ilinisihi kupekua zaidi tena ilisema nisiache.
Nikaishughulisha akili yangu, nikapekua zaidi na zaidi, mwisho kabisa nikatoa mashuka kitandani.
Hapa ndipo nilipokutana na jambo la kushangaza na kushtua kuliko yote ambayo hadi kipindi hicho cha utu uzima wangu macho yangu yaliwahi kushuhudia.
Sura haikuwa ngeni na ilifanana kabisa na ile niliyoonana nayo asubuhi ya siku hiyohiyo maeneo ya Ubungo!!
Sura ya Ezekiel!!
Alikuwa ametulia tuli kitandani, bora angekuwa anasema neno lolote ama anatabasamu.
Haukuhitaji utaalamu wa kidaktari kutambua kuwa mwanadamu yule alikwishapoteza uhai siku nyingi sana, na alikuwa ameanza kuharibika. Ezekiel hakuwa mweupe tena, ngozi yake ilikuwa nyeusi, alikuwa uchi mnyama.
Kifurushi cha makaratasi kikanitoka mkononi, lakini nilikumbuka kuuzuia mkojo uliotaka kunitoka. Miguu ilikuwa inatetemeka na jasho jembamba lilinitoka.
Ezekiel aliyenipa funguo, Ezekiel sasa ameozea kitandani!!!
Tofauti ya masaa matatu tu!!
Hapana!!
Nikaanza kurudi kinyumenyume na hapo nikajikwaa kwenye kile kifurushi na nikakumbuka kukiokota, ujasiri ukakaa kando, nikashindwa hata kumfunika Ezekiel pale kitandani.
Mara mlango wa Ezekiel ukagongwa!!!
Sikujibu chochote kile!! Mara sauti ya kike ikaita jina lake.
Hofu ikazidi kutanda, yule ni nani anayemtafuta Ezekiel, na je anamtafuta Ezekiel aliye hai ama huyu anayeozea kitandani!!
Maswali yakawa lukuki huku nikiwa sina majibu, na sauti kutoka nje ikazidi kuita.