Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu hadi Julai 1, 2025 kwa ajili ya kusubiri Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kupitia jalada la kesi hiyo ili kuona kama iende Mahakama Kuu au hapana.
Hatua hiyo inatokana na Upande wa Mashtaka kuomba ahirisho mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Franko Kiswaga ambapo Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga alisema jalada la kesi hiyo lipo kwa DPP analipitia kisha atatoa taarifa kuhusu upelelezi ulipofikia na kama kesi hiyo iende Mahakama Kuu au hapana.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Kiswaga ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 1, 2025 ambapo kesi hiyo iliitishwa leo kwa ajili ya kutajwa.
Lissu anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3, 2025 ndani ya Jiji la Dar es salaam kuwa siku hiyo kwa nia ya uchochezi aliushawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.
Juni 2, 2025, upande wa mashtaka uliieleza Mahakama kuwa jalada la upelelezi lilikuwa limeshawasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), lakini baada ya DPP kulipitia alibainisha kuwa kuna jambo ambalo bado lilikuwa halijakaa sawa hivyo alilirejesha tena kwa wapelelezi kufanyia kazi eneo hilo.
Kutokana na taarifa hiyo, kiongozi wa Jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga aliomba Mahakama itoe ahirisho mpaka tarehe nyingine.