Athuman Yengayenga aliyefunga ndoa na wake watatu hivi karibuni mjini Mpanda ameingia matatani baada ya kushindwa kukamilisha kandarasi ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa shule ya msingi Mnyagala wilayani Tanganyika.
Yengayenga ni kati ya watu wawili waliochukua kandarasi ya ujenzi wa vyumba 6 vya madarasa na matundu 10 ya vyoo katika shule hiyo, ambapo yeye anajenga vyumba vitatu vya madarasa.
Akizungumza na Mwananchi katika ziara ya Katibu Tawala Mkoa wa Katavi Hassan Rugwa, wakati wa ukaguzi miradi ya BOOST wilayani Tanganyika, Yengayenga amesema alipata tenda hiyo kupitia jina la Majaliwa Lusambo.
"Maandalizi ya harusi yangu yamesababisha mradi kutokamilika kwa wakati, niliweka mtu wa kusimamia lakini vifaa vilichelewa kufika site, msimamizi badala ya kutoa taarifa kwa maandishi yeye alitoa kwa mdomo,” amesema na kuongeza;
"Mimi hakunishirikisha, kitu ambacho kilisababisha pia wahusika kutotilia manani, najenga vyumba vitatu na kila kimoja kinagharimu Sh2.4 milioni, nimelipwa nusu yake na zimenisaidia kwenye harusi," amesema.