KIKOSI cha Simba jana kimeanza mazoezi Dubai kwa ajili ya kambi ya wiki moja kujiandaa na mechi za Ligi Kuu Bara na ile ya kimataifa, huku kocha mkuu mpya, Roberto Oliveira 'Robertinho' akisema anafahamu kila kitu kuhusu Yanga na kutamba hana presha nao kabisa.
Akizungumza na Mwanaspoti mara baada ya kurejea kutoka Zanzibar, kocha huyo Mbrazili alifichua analijua soka la Tanzania na amekuwa akilifuatilia kwa ukaribu tangu akizinoa Rayon Sports ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya na Vipers ya Uganda, hivyo anajua kila kitu kuhusu wapinzani na wataji wa jadi wa klabu aliyojiunga nayo, yaani Yanga.
Robertinho alisema anafahamu kuna ushindani mkubwa kwa michuano ya ndani ikiwemo upinzani wa timu yake ya sasa Simba dhidi ya Yanga kila zinapokutana na hata upinzani wa timu nyingine na kwamba alishajiandaa mapema kukabiliana nao hata kabla ya kuja kujiunga Msimbazi.
Kocha huyo mwenye falsafa za kujilinda na kushambulia kwa pamoja mwanzo mwisho, alisema kwa bahati nzuri Yanga anaifahamu hata kabla ya kuja Simba na aliwahi kuifunga mara kadhaa alipokutana nao tangu akiwa Rayon Sports ya Rwanda na hata msimu huu waliitungua kwenye kilele cha Tamasha la Wiki ya Mwananchi lililofanyika Agosti 6 mwaka jana.
"Naamini kuwepo wangu hapa nchini, unaifanya nitafahamu zaidi vitu vingi mbali ya wapinzani wetu Yanga, kwani imani yangu Simba itakuwa bora zaidi dhidi yao ikiwemo kupata matokeo bora kwa mechi zinakuja na hata kwenye ushindani dhidi ya wapinzani wengine," alisema Robertinho