Wakati dirisha la maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2022/2023 likiwa wazi kwa muda wa siku 70 kuanzia Julai 19 hadi Septemba 30 mwaka huu, Serikali imetangaza Tume ya Watu watatu kuchunguza utoaji wa mikopo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Tume hiyo itaongozwa na Prof Allan Mushi ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro, Idd Makame kutoka Zanzibar na Dkt Martin Chegeni ambao wote kwa pamoja ni Wataalamu wa mifumo waliobobea katika sayansi ya Kompyuta na Takwimu.
Tume hiyo itachunguza uhalali katika utoaji wa mikopo kwa Wanafunzi wa elimu ya juu kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2017/2018 mpaka 2021/2022 ili kubaini kama kulikuwa na upendeleo kwa Watu wasiokuwa na sifa.
Waziri Mkenda amesema kuwa Tume hiyo itapitia malalamiko ya Wanafunzi mbalimbali nchini ambao wamekuwa wakiyatoa kuhusu upendeleo wa utoaji mikopo kwa kupata mikopo kwa Wanafunzi wenye sifa huku wale wasiokuwa na sifa stahiki wakikosa mikopo hiyo.
“Na kwenye hili tunakaribisha Watu watoe taarifa kwasababu kama kuna Mtoto wa Mkenda uliyesoma nae utakuwa unamjua Baba yake ni nani na uwezo wake, halafu wewe unaona Mtu huyo amepewa mkopo toa taarifa”