“Sisi Viongozi, Wanachama na Wafuasi wa Vyama vya Upinzani tuliishi kwa mateso sana ndani ya miaka mitano na nusu iliyopita, tukifilisiwa mali na kufungiwa akaunti zetu……. Ndugu Freeman Mbowe akiwa ni kielelezo cha hili”
“Tulipigwa risasi zaidi ya 30 na mpaka leo hakuna hata uchunguzi dhidi ya vitendo hivyo vya kinyama, Ndugu Tundu Lissu ni kielelezo cha hili, tulibambikiwa kesi na kuhukumiwa Mahakamani (Mimi na mamia ya Viongozi wenzangu wa kisiasa ni kielelezo cha hili)”
“Mamia ya Wanachama wetu wakipata vilema vya kudumu kwa vipigo (humu kwenye Kamati Kuu tunao kina Jussa na Mazrui), unaweza kusema bila kupepesa maneno kuwa Wapinzani walitendewa ugaidi mkubwa mno na vyombo vya Dola”
“Kesi ya Ugaidi dhidi ya Mbowe ni jambo linalokumbusha machungu makubwa sana ya awamu iliyopita, Watu waliofungua mashtaka hayo hawamkomoi Mbowe wala hawatuvunji moyo wa kupambania Tanzania yenye usawa wa kisiasa na kuheshimu utofauti wetu wa mawazo, wanalichelewesha tu Taifa letu kupata Umoja na Maendeleo ya Kiuchumi, wanataka turudi kulekule ambapo hatupaswi kurudi”
“Wito wangu na Viongozi wenzangu kwa ndugu Rais Samia ni kuingilia kati na kumaliza jambo hili la kisiasa kwa njia za kisiasa, Rais asikubali jambo hili, awazuie Wasaidizi wake wanaotaka tuendelee kuishi kama ilivyokuwa ndani ya miaka mitano na nusu iliyopita, tunajua anao uwezo huo, tunajua akitaka anaweza kulizuia jambo hili, tunajua yeye hataki tuendelee kuishi kigaidi” ——— asema Zitto Kabwe leo akiwa Zanzibar.