Tafasiri Unavyoweza: Ujinga Ni Kutosema
Najua kabisa naandika ikiwa ni mwanzo wa mapumziko ya mwisho wa wiki. Kawaida sana huwa sipendi kuandika mambo magumu na ya kufikirisha sana maana hata nami ninahitaji, kama ulivyo wewe, mapumziko ya kurudisha kilichopotea na nilichokosa kwa siku tano za kazi. Ninaandika magumu leo kwa sababu tu ya kuwepo kwa nia ya kufumba jamii mdomo, isiongee, isihoji na wala isiwe na maoni tofauti na wenye kukasimiwa madaraka. Taifa sio viongozi na kwa kuwa taifa letu tumeamua kuwaamini wachache kuongoza basi haimaanishi kuwa wao wanao uwezo wa kufikiria na kutuamulia wanachotaka wao binafsi au taasisi wanazoziongoza. Hii ni kwa sababu si wote wenye maslahi timamu kwa taifa, wengine ni kutaka kujineemesha wenyewe na tunaliona sana hili kwa sasa.
Bunge halifanyi kazi yake, linakutana kutegemea huruma za dola ambayo nayo inatoa masharti mengi tu ili bunge na mahakama ziendelee kuilamba miguu dola. Upo ushahidi wa maneno na vitendo vya wakuu wa taasisi hizi mbili wakijipendekeza vilivyo kwa taasisi dola ambayo kiongozi wake anatamani kuwa kila kitu, awe IGP, awe rais wa Znz awe kamishna wa kodi awe mkuu wa bandari, awe mpiga ngoma, awe 'stedishoo' na lolote unaloweza kutaja.
Bunge butu, bunge kibogoyo, bunge linalowafanya wabunge waingie na 'power bank' kwa sababu hakuna kinachojadiliwa cha maana na hivyo bora mbunge aendelee kucheza game au kutizama mitandao wakati wa mijadala ya bunge. Bunge linaloamua kupeleka taarifa yake ya uchunguzi kwa serikali bila kwanza kuijadili. Ukiwa unadhani ninaandika hisia basi jipe muda wa kufuatilia majukumu ya bunge na uangalie kinachofanyika sasa, tafasiri unavyoweza.
Bunge linaloongozwa na baadhi ya viongozi wanaowakilisha wapiga kura wajinga, ndiyo wapiga kura wajinga ambao hawajui thamani ya kura waliyoipiga, wanapiga kwa mazoea na hivyo kuendelea kuaminin wanachoambiwa na nambunge hata kama ni cha uongo ilmradi tu walikula wali nyama na kilo ya chumvi wakati wa kampeni za uchaguzi.
Ukikaa kimya bila kuongelea udhalimu na unyang'anyi unaofanywa na bunge hili la sasa usijedhani uko salama na ukaendelea kukenua meno kwa viongozi wasiotaka kusikia maoni mengine na hasa wasiyoyapenda. Hakuna mnafiki anayekufa mara mbili. Uwe na mapumziko mema.
Tukutane wiki lijalo.