MOJA ya kosa kubwa watakalolirudia viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015, ni kukubali mtego wa kuwapokea na kuwapatia uongozi wafuasi wa CCM waliobwagwa kwenye uchaguzi wa ndani unaoendelea.
Nasema hilo ni kosa kubwa na natabiri mapema kuwa yatakayowafika watajuta akini wakati huo haitakuwa na faida tena kwao maana watakuwa wamepigwa mweleka tayari.
Ni kweli kila mtu ana haki ya kujiunga na chama chochote wakati wowote anaoona unafaa lakini kwa wanachama hawa wa CCM wanaongojea kwanza kukosa ushindi ndani ya chama chao ndipo watafute hifadhi CHADEMA, hawafai.
CHADEMA wanatambua ninachokisema kuwa kwenye uchaguzi mkuu wa 2010 katika maeneo mengi walifanya makosa makubwa kama hayo kwa kuwapokea wana-CCM waliojeruhiwa kwenye uchaguzi wa ndani kisha wao wakawapokea na kuwapa nafasi ya kugombea udiwani na ubunge na matokeo yake wameyaona.
Leo wako baadhi ya watu hao ndani ya CHADEMA wameshinda ubunge na udiwani lakini matendo yao ni ya kutaka kukiyumbisha chama kwani hawana cha kupoteza. Wanajua mkakati wao ukifanikiwa CHADEMA ikapasuka watapongezwa na CCM kwa kupewa vyeo hata serikalini.
Uchaguzi ndani ya CCM unaendelea na tayari vigogo wenye majina makubwa wameangukia pua, sasa wanahaha kurejesha heshima zao kwenye taswira ya kisiasa. Hawa eti wanataka kuhamia CHADEMA. Hivi kweli wana nia ya dhati?
Kwangu nasema hapana. Hawa si wanasiasa wenye mapenzi mema na Taifa wala CHADEMA,bali kiu yao ni madaraka. Hivyo iko siku hata ndani ya CHADEMA wakishindwa watakimbia tena.
Kwangu mimi mwanasiasa makini na mkomavu ni yule anayekubali kuwa wako watu wengine ndani ya chama chake wanafaa kuongoza kama yeye. Hivyo hata akishindwa kwenye uchaguzi hatakimbia ila atazidi kujipanga kwa uchaguzi mwingine.
CHADEMA kwa sasa ndilo tumaini pekee la Watanzania wapenda mageuzi.
Hiki ndicho chama pekee mbadala kimeweza kuikabili CCM na hivyo kinastahili kupewa dola lakini kamwe kisikubali kutegwa kupokea majeruhi wa CCM na kudanganyika kuwapa uongozi.
Anayeipenda CHADEMA na kutaka kuleta mageuzi hapaswi kungoja mpaka chama chake kimfukuze au ashindwe uchaguzi, isipokuwa anapaswa kuamua mapema kwa hiari yake na kjiunga na makamanda wapambanaji.
Hawa wanaotaka kukimbilia leo kwa sababu tu wamenyimwa uongozi CCM ni wabinafsi, wasio na uvumulivu, wepesi wa kuhadaika. Kama CHADEMA itainia mkenge wao ikawaona wa maana na kuwachukua basi tujipe muda mfupi nayo itakuwa imegawanyika mapande kama CCM.p
Kama wafuasi hawa wanahama CCM kwa vile makundi yao ya kusaka urais 2015 hayajashinda, ina maana hata ndani ya CHADEMA watakwenda kutengeneza makundi hayo hayo.
Chonde chonde tuachane nao na hata wakiingia tuwaone kama wanachama na kawaida.
Wako wana-CHADEMA wamepifia chama tangu kinaanzishwa hadi leo hawajapata madaraka makubwa, sasa kwanini wakimbilie kuwachukua walioshindikana CCM na kuwapachika madaraka pasipo kujihoji endapo wametumwa kukisambaratisha chama?
Kwa mwaka 2005 CHADEMA tunaweza kuwatetea kuwa walilazimika kuokoteza kila mtu hata wakawapokea wale waliotemwa CCM na kuwasimamisha wagombee lakini majibu waliyapata mapema kwani wako waliopewa fedha wakajitoa na kurejea CCM na wengine wakafanya kila aina ya hadaa na mwishowe CHADEMA ikala mweleka.
Tangu mwaka huo hadi leo, CHADEMA imefanya oparesheni za kila aina mijini na vijijini, imejiongezea mtaji wa wafuasi wenye sifa za kuwania nafasi zozote zitakazotakiwa, hivyo hawa ndiyo wanapaswa kupewa kipaumbele badala ya kukimbilia kupokea wale wenye sura mbili.
Kama itabidi kuwapokea wafuasi hao walioangushwa ndani ya CCM, dawa ya CHADEMA inapaswa kuwa laini kwamba wabakie wanachama wa kawaidi ila wakirogwa kuwapa vyeo wakafika juu na kuzisoma siri zao hakika kutakuwa na kilio cha kusaga meno.
Mifano iko mingi sana ya watu wa aina hii ambao mwaka 2005 walinyimwa uteuzi CCM wakakimbilia CHADEMA na kupewa nafasi kugombea ila waliposhindwa wakarejea tena CCM. Sasa hawa tunawaitaje kama si 'wasaka madaraka'?
Wanasiasa wetu wanapaswa kujifunza jambo moja kubwa kwamba nje ya madaraka kuna maisha. Hivyo kushinda ama kushindwa katika uchaguzi ni jambo la kawaida lisilowalazimu kuhama vyama kwa vile hawakuchaguliwa.
Orodha ya wana-CCM walihama kwenda upinzani ni ndefu sana tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, lakini watu hawa ebu tujiulize wengi wao wako wapi? Si hawa walipewa fedha na kuahidiwa madaraka ndani ya CCM na serikalini wakakimbia upinzani. Sasa hawa wanaotaka kuja CHADEMA baada ya kushindwa uchaguzi wanatofauti gani na hao wengine?
Tafakari!
Chanzo: Tanzania Daima