Alikuwa mcheshi pia, mtu mwenye bashasha na mwenye furaha. Nakumbuka mwaka 2005, wakati wa kampeni za urais na ubunge, CCM walikuwa wameteua kaulimbiu ya kampeni, “ARI MPYA, NGUVU MPYA, KASI MPYA,” na kauli mpya hiyo ikawavutia watu kwa mamia ya maelfu kila mahali.
Chachage aliiangalia kaulimbiu hiyo, akaitathmini pamoja na wale waliokuwa wakiifanyia kampeni, mwisho akaniambia, “Unajua, hii kaulimbiu imebeba utabiri mkubwa. Sikuelewa anachotaka kusema mwalimu wangu, lakini akaniambia, “Angalia jinsi maneno yalivyopangiliwa, halafu soma silabi ya kwanza ya kila msitari” Nilipofuatilia nikasoma:
A RI MPYA
NGU VU MPYA
KA SI MPYA
Kwa kuchukua silabi ya kwanza ya kila msitari nikasoma: “ANGUKA”. Niliporudi kumwangalia nikakuta anacheka kile kicheko chake ambacho wengi walikuwa wanakitambua kama ishara ya utundu wa kisomi wa Profesa Chachage.
Siwezi kujua ni nini kilichokuwa kimemfanya aone kwamba katika hamasa yote ya mwaka 2005 kulikuwa na anguko lililokuwa linatuvizia, lakini hatimaye tulilishuhudia anguko hilo kubwa, si tu kwa wale waliobuni kaulimbiu hiyo bali na kwa hao walionufaika kutokana na hadaa ya ujumbe uliobebwa na kaulimbiu hiyo