Simulizi : Nilivyotolewa Kafara Kwa Sababu ya Utajiri
Mtunzi Juma Hiza
Sehemu ya 01.
Nilizaliwa Julai 27, 1982 katika hospitali ya Bombo mkoani Tanga, nikiwa mtoto wa pekee katika familia ya wazazi wangu.
Maisha yangu baada ya kuzaliwa, sikuyafahamu, lakini nilipoanza kuwa na akili, sikuhitaji kutumia akili nyingi kujua kuwa niliishi maisha ya ufukara sana.
Hilo lilishereheshwa na chumba kimoja tulichokuwa tukiishi na wazazi wangu pale Nguvumali. Lakini pia kazi ya baba yangu ya kukodisha baiskeli nayo ilikuwa ushahidi tosha wa maisha magumu niliyoishi na wazazi wangu.
Pamoja na ufukara huo, nikiwa nalala chumba kimoja na wazazi wangu, mimi nikilala kweny kochi kubwa na wao wakilala kitandani, nilikuwa nina ndoto kubwa ya kuwakomboa wazazi wangu katika maisha hayo magumu yanayonuka dhiki tupu.
_____________
Nilikuwa nina ndoto ambayo niliamini sana, njia pekee ya kuupata utajiri ilikuwa ni elimu tu!
Nakumbuka sana mwalimu wangu wa darasa la tatu, alikuwa kila anapoingia darasani kwetu asubuhi kufundisha somo la hisabati, alisisitiza “Elimu ndiyo ufunguo wa maisha”.
Niliamini sana kauli yake na niliamua kuitumia kwa nguvu zote nikiamini kwamba ndiyo njia pekee itakayonisaidia.
Nikaanza kusoma kwa bidii. Sikujali ufukara wa wazazi wangu, nikasoma kwa bidii sana. Kuanzia wakati huo, nilikuwa nashika nafasi ya kwanza katika kila muhula mpaka nilipofika darasa la saba.
___________
Ni kati ya siku ambazo haziwezi kufutika akilini mwangu. Siku ambayo nilijiuliza kama baba yangu ni mchawi.
Ilikuwa lazima nijiulize swali hilo gumu kichwani kwani mambo niliyomuona baba yangu akiyafanya alikuwa mazito sana.
Ilikuwa ni siku ya Alhamisi, nikiwa ndiyo nimetoka shuleni, begi langu mgongoni, njaa kali ikiwa inaniuma sana.
Nilipofika niliingia ndani bila kubisha hodi, nilifanya hivyo nikiwa nina uhakika kwamba baba yangu hawezi kuwa ndani muda huo. Kwa kawaida, muda huo baba huwa kijiweni kwake anapowasubiria abiria wa kuwakodishia baiskeli.
I