Kurzweil
JF-Expert Member
- May 25, 2011
- 6,622
- 8,410
Mahakama ya Juu nchini Urusi imekubali ombi la serikali kuorodhesha kanisa la Mashahidi wa Yehova, kwa Kiingereza Jehovah's Witnesses, kama kudi la kidini lililoharamishwa, na kuliorodhesha kuwa kundi lenye msimamo mkali.
Wizara ya haki nchini humo ilisema kundi hilo lilikuwa limesambaza nyaraka zilizokuwa na ujumbe wa kuchochea chuki dhidi ya makundi mengine.
Mawakili waliokuwa wanatetea kundi hilo wamekanusha madai hayo na wamesema watakata rufaa.
Kundi hilo la kidini lina waumini 175,000 nchini urusi, taifa ambalo wafuasi wa madhehebu hayo waliteswa na kudhulumiwa wakati wa utawala wa Josef Stalin.
Inakadiriwa kwamba kuna watu milioni nane kote duniani ambao ni waumini wa madhehebu hayo ya Kikristo, yanayofahamika sana kwa kampeni zake za kwenda nyumba kwa nyumba kutafuta waumini wapya.
Wafuasi wa kundi hilo la kidini wanasema hatua ya kuharamisha kundi hilo ina maana kwamba shughuli zake pia ni haramu kisheria.
Wizara ya haki iliiomba mahakama kufunga makao makuu ya kitaifa ya kundi hilo la kidini karibu na mji wa St Petersburg, mashirika ya habari ya Urusi yalisema, pamoja na kupiga marufuku baadhi ya vitabu vyenye msimamo mkali vinavyochapishwa na kundi hilo.
Moja ya vijitabu vilivyosambazwa na kundi hilo nchini Urusi vilimnukuu mwandishi mashuhuri wa vitabu Leo Tolstoy akieleza imani kuu ya kanisa la Orthodox la Urusi kama ushirikina na uchawi.
maafisa wamelituhumu kundi hilo la kidini kwa kuharibu familia, kupanda mbegu za chuki na kuhatarisha maisha.
mashahidi wa Yehova wanasema tuhuma hizo si za kweli.
Msemaji wa kundi hilo aliambia shirika la habari la AFP kwamba alishangazwa sana na uamuzi huo.
"Sikutarajia kwamba hilo linaweza kutokea katika Urusi ya sasa, ambapo katiba inawahakikishia raia uhuru wa kuabudu," alisema Yaroslav Sivulsky.
Kundi la Mashahidi wa yehova lilianzishwa nchini Marekani karne ya 19.
Huwa wanafasiri Biblia moja kwa moja na miongoni mwa mengine waumini wake hawaruhusiwi kutoa au kupokea damu.
Huwa hawatazamwi na makanisa mengine makuu ya zamani ya Kikristo kama madhehemu makuu.
Wakati wa utawala wa Joseph Stalin katika Muungano wa Usovieti, kundi hilo lilipigiwa marufuku na maelfu ya waumini wake wakapelekwa Siberia kuteswa. makundi mengine ya kidini yalihangaishwa na serikali pia.
Muungano wa Usovieti ulipoporomoka, dini za Kikristo zilifufuka Urusi na marufuku dhidi ya Mashahidi wa yehova ikaondolewa mwaka 1991.
Lakini msimamo wa serikali dhidi ya kundi hilo la kidini ulianza kuwa mkali tena na mwaka 2004 lilituhumiwa kwa kuwaandikisha watoto kuwa waumini na pia kuwazuia waumini kupokea usaidizi wa kimatibabu.
Chanzo: BBC Swahili