Makindi, yote uliyoyaandika ni UONGO MTUPU, umeyaandika bila chembe ya haya. Hata hivyo, naheshimu uhuru wako wa kujieleza. Umefika mahali unaandika kuwa nilitoa msimamo kuwa ni kwa nini nitampigia kura JK! Kama una ushahidi wa hilo uweke hapa hadharani, ukishindwa useme tu samahani kama una chembe za uungwana.
Niliyoyaandika ni maoni yangu. Niliandika nikijua nachochea mjadala na si wote watakaokubaliana nami. Ni kawaida, mie mpenzi wa Simba, kuna hata Simba wenzangu wanaonichukia.
Mwaka juzi kulikuwa na sakata la mchezaji Athumani Iddi kufungiwa na TFF kucheza soka kwa vile Simba hawakumpa kibali cha uhamisho. Simba walisema wako tayari kumwona Athumani Idi akiuza ndimu kuliko kumruhusu kurudi Yanga. Niliandika makala kwenye gazeti la Sayari kumtetea Athumani Iddi. Niliweka bayana kuwa, kuwa nilikuwa mpenzi wa Simba lakini kwa lile nilisimama upande wa Athumani Iddi.
Siku ile nilipigiwa simu nyingi na kutumiwa sms za WanaSimba wenzangu wenye hasira. Ikafika hata mmoja wa viongozi wa Simba alinipigia na kuniambia; " Maggid wewe si Simba mwenzetu, ni kondoo uliyevaa ngozi ya Simba!"
Na juzi usiku nimeshambuliwa vikali na Redio Imaan ya Morogoro. Nimeambiwa maneno mengi ikiwamo kuwa mimi mnafiki, mchochezi , na kuwa natumiwa kupambana na Waislamu. Kisa? Niliandika kwenye Raia Mwema kuwa redio hiyo inachochea uhasama kati ya Wakristo na Waislamu!
Tatizo langu ni kuandika mawazo yangu kwa uhuru. Ndio maana naamini, kuwa kuna CHADEMA wanonichukia, lakini kuna wanaonipenda pia. Hivyo hivyo kwa CCM, CUF, Waislamu, Wakristo na wengineo. Lakini naamini pia, kwa jinsi nilivyo, wote hao wanaweza pia kuniheshimu. Ni matumaini yangu.