Miaka ya 1980+ ilikuwa kama fasheni hivi, kwa vijana/watoto wa kiume Mbeya mjini kuwafuga ndege hawa.
Binafsi, kuna rafiki yangu mmoja tulikuwa darasa moja pale Azimio shule ya msingi, yeye akiishi Jacaranda, nami maeneo ya REJIKO, aliniuzia wawili, dume na jike. Sasa, ilikuwa, ukiwapata wakubwa wanaoruka, basi unawatoa manyoya yale marefu kwenye mabawa yao ili wasiruke, kabla hawajazoea makazi mapya. Wengine walikuwa wanatumia njia katiri ya kuwatengua mabawa, na wataanza kuruka baada ya kupona.
Sasa, njiwa wangu, walipoanza kuokota majani yakiwa ni maandalizi ya kutaga, jike akakanyagwa na gari na kufa. Akabaki dume peke yake. Sasa hili dume, lilikuwa lina tabia ya kutoka pale home, na kwenda mbali nisikokujua. Baada ya siku chache, akaja na jike, alikompata, hataaa sijui.
Baada ya siku chache, hilo jike likataga mayai mawili. Baadaye nikapata vifaranga. Kabla hawajaanza kuruka vizuri, wakataga tena. Sasa, kimbembe kilichoniudhi, na kuchukia kuwafuga hao ndege, ni tabia iliyokuwa nayo hilo dume. Pamoja na kuwa nilijenga mabanda mengi, lakini watoto wake wakianza kuruka vizuri tu, alikuwa anaondoka nao, na kuwaacha huko huko. Kwa hiyo muda mrefu, nilikuwa nina vifaranga tu, wakikua, wanahamishwa.
Nikaona huo ni ujinga, walipokaribia kuanza kutaga, nikawachinja, vifaranga nikawauza, kwani walishaanza kula wenyewe.
Wakati ule, tulikuwa tunaambiwa kuwa, kuna matunda fulani hivi, yana umbo kama chungwa hivi, ukiyaning'iniza kwenye banda, hawatoroki/hawahami. Lakini waapii. Pia, tulikuwa tunaambiwa kuwa, kikitokea kilio/msiba hapo nyumbani, basi tupia ushanga kwenye mabanda, ili wasiondoke. Kwa sababu hakikutokea kilio wakati ninafuga hao ndege, hivyo sina uhakika.
Lakini, ukiwa na hao ndege wengi, na wakiwa na rangi tofauti tofauti, ni burudani tosha kuwaangalia!