Madhara ya ufisadi ni haya

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
Umaskini wa kupindukia wa kipato (ufukara) unaowasumbua wananchi wengi vijijini na mijini hapa nchini,wanawake na wanaume, huenda usipatiwe ufumbuzi wa kudumu kwa kutumia ushindani wa sera za vyama wa vyama vya siasa na ubora wa uongozi kama tatizo la ufisadi ambalo linalitikisa taifa letu hivi sasa, halitang’olewa na mizizi yake.

Ufisadi na rushwa ni adui namba moja wa haki ya wananchi katika kudai uwajibikaji wa viongozi kwa sababu vitendo hivyo viovu vinaharibu kabisa dhana nzima ya uadilifu katika uongozi na hivyo kuhatarisha maendeleo ya uchumi, amani, mshikamano na umoja wa kitaifa.

Kwa vile ufisadi ni tatizo linalohusiana moja kwa moja na uongozi wa nchi, na kwa vile uongozi wa nchi yetu unatokana na siasa za vyama, dawa ya kukomesha ufisadi itapatikana endapo tu wanasiasa wataweka pembeni maslahi yao binafsi na ya vyama vyao na kujali zaidi maslahi ya taifa. Waswahili husema ni rahisi kuziba ufa kuliko kujenga ukuta. Au ni heri nusu shari kuliko shari kamili.

Ni viongozi, makada na wanachama wangapi wa vyama vya siasa ambao wanafahamu kuwa katika zama hizi za utandawazi vyama vyao vinaweza kutekwa kirahisi na mafisadi na hivyo chama kujikuta kinakuwa mawakala wa mafisadi wenye lengo la kuiba na kuhamisha utajiri wa nchi yetu kwenda kutajirisha nchi nyingine?

Je wapo viongozi wa vyama vya siasa hapa nchini ambao wakichungulia ndani ya mioyo yao wanabaini kabisa kwamba wanao upendo usiotiliwa shaka kwa nchi yetu na watu wake? Ni wangapi watakuwa tayari kujitoa mhanga hata kama kwa kufanya hivyo watakuwa wamepoteza maslahi yao binafsi na/au ya vyama vyao ili kuliokoa taifa lisiendelee kuharibika kutokana na athari mbaya za ufisadi?

Ni viongozi wangapi wa kisiasa ambao wako tayari kujitoa mhanga kuona kuwa demokrasia ya vyama vingi vya siasa inaimarika na kustawi vizuri nchini ili vyama hivyo viweze kuwa chimbuko la kuibua fikra mpya, sera mpya na mipango mipya ambayo itachochea kasi ya maendeleo endelevu ya kiuchumi kwa wananchi wengi mijini na vijijini ambao leo hii wanaishi maisha ya ufukara wakati nchi yetu ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika na duniani zenye utajiri mkubwa wa mali asili?

Kila kiongozi, kada na mwanachama wa vyama vya siasa (DP, TLP, CCM, UDP, CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na vingine vyote) nchini akitafakari maswali haya bila unafiki, kisha akayafanyia kazi bila woga majibu yanayotoka kwenye moyo wake, muda si mrefu ufisadi unaweza kuwa jambo la historia a hivyo janga linaloinyemelea nchi kutokana na ufisadi kuzimwa.

Ufisadi kimsingi ni wasilisho au ainisho la wananchi hapa nchini kwetu kuhusu vitendo vya rushwa, wizi, ukwapuaji au udanganyifu mkubwa wa kupindukia wa fedha na mali za umma unaofanywa na kikundi kidogo cha watu (mtandao) kinachohusisha baadhi ya viongozi wa serikali na baadhi ya wafanya biashara wakubwa.

Kimsingi ufisadi hufanywa kwa ajili ya wahusika kujinufaisha binafsi kiuchumi na kuwawezesha kubaki madarakani kwa gharama yoyote ile hata kama kwa kufanya hivyo kutaathiri kwa kiwango kikubwa uwezo, heshima, kiwango na thamani ya uongozi katika mfumo wa demokrasia inayopaswa kuwa chachu ya maendeleo endelevu kwa wananchi na taifa lao.

Neno ufisadi lilianza kutumika rasmi hapa nchini baada ya mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mwembeyanga, Temeke jijini Dar es Salaam mwaka 2007 ambapo viongozi kadhaa waandamizi serikalini wa awamu hii na awamu awamu iliyopita walitajwa hadharani (list of shame) kwamba wamehusika na vitendo vya ufisadi vilivyochangia kulifukarisha taifa letu ikiwa ni pamoja na wizi wa shilingi bilioni 133 kutoka akaunti ya madeni ya nje (EPA) katika benki kuu (BOT).

Hadi sasa wananchi wanaendelea kuwatilia shaka viongozi waliotajwa katika tuhuma hizo kuhusu uadilifu wao kama viongozi kwa sababu hakuna hata mmoja alishakwenda mahakamani kukanusha tuhuma hizo.

Hatari ya viongozi waliotuhumiwa kwa ufisadi kutowajibika kutokana na tuhuma hizo ni nini? Taifa limeanza kushuhudia kasi ya ajabu ya kushamiri kwa vitendo viovu nchini jambo linaloashiria kuwa makundi mengine ya watu nje na ndani ya serikali yanafanya mambo maovu kadha wa kadha bila woga pengine kutokana na kuidharau serikali kwa vile baadhi ya viongozi walioko madarakani wametuhumiwa hadharani kwa kuhusika na ufisadi lakini hawajawajibika au kuwajibishwa na mamlaka.

Maovu ambayo yameshamiri kwa kasi kubwa hapa nchini katika miaka ya hivi karibuni ni pamoja na wimbi la matumizi mabaya/wizi wa fedha za serikali, ajali nyingi za kizembe, biashara ya viungo vya binadamu, udanganyifu na wizi wa mitihani, matukio mengi ya mauaji ya kikatili, watu taaluma kukimbilia siasa, wanasiasa kuchochoe migogoro ya kidini na kuingizwa nchini bidhaa feki ikiwa ni pamoja na chakula na madawa ya bianamu.

Kadhalika kumezuka mitandao mingi ya watu kujipatia fedha haramu, wanyonge kuporwa mali zao hasa ardhi kwa kisingizio cha uwekezaji, rasilimali za nchi kuporwa kiholela kama madini, samaki, magogo napembe za ndovu na wanyonge kukosa haki mbele ya vyombo vya sheria.

Mengine ni rushwa za kutisha kutawala katika chaguzi, migomo ya wafanyakazi, ongezeko la vifo vya wananchi maskini vinavyoweza kuzuilika, wanataaluma kudhalililishwa, viongozi kuzomewa na wananchi, viongozi kuwa wababe na kutoona aibu juu ya makosa wanayofanya na mambo mengine ya aina hiyo yanayolitia aibu taifa.

Ufisadi unapokuwa ni sehemu kubwa ya utamaduni kwa taifa ni jambo la hatari kubwa sana. Hii ni kwa sababu rushwa, wizi na udanganyifu wa kutisha havitaishia kufanywa na watu wenye mamlaka serikalini peke yake, bali vitendo hivyo husambaa na kujengeka kama tabia ya wanajamii kwa sababu mienendo, vitendo na tabia za watawala huigwa kirahisi na watawaliwa.

Je ni nini chanzo cha kushamiri kwa ufisadi nchini? Tanzania ni moja ya nchi za Kiafrika ambazo baada ya kupata uhuru wake ziliweka utaratibu wa kupata viongozi wake wa kuongoza taifa kwa kutumia mfumo wa chama kimoja cha siasa. Wakati huo chama kilikuwa kinaweka misingi thabiti ya uongozi ili kuhakikisha kuwa anayependekezwa na chama kugombea uongozi ni mtu mwadilifu anayeweka maslahi ya taifa mbele.

Lakini kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 1990, kutokana na mabadiliko duniani, nchi hizi zililazimika kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa ili kwenda sambamba na mfumo wa uchumu wa utandawazi ambao chanzo chake ni kuanza kuanguka kwa mfumo wa ubepari duniani. Mfumo wa ubebari ni mfumo wa unyonyaji ambao hutajirisha watu wachache na kuwaacha wengi wakiwa fukara.

Katika siasa za vyama vingi, kunakuwepo na ushindani mkubwa katika suala zima la kupata madaraka ya kuongoza nchi. Ushindani siyo tu unakuwa baina ya vyama, bali pia ndani ya vyama kunakuwa na ushindani unaohusisha makundi/mitandao yanayotafuta kwa udi na uvumba kushika madaraka ya nchi.

Katika ushindani wa kupata madaraka na au fursa ya kuchuma utajiri, hata ndani ya chama inawezekana watu (raia au wageni au wote wawili kwa kushirikiana) wenye malengo hayo wakatumia fedha safi na chafu kufikia malengo yao.

Kimsingi ufisadi huwa unaikumba nchi endapo chama tawala kwa wakati husika, hasa kama viongozi, makada na wanachama wake wanajali zaidi maslahi yao binafsi na ya chama chao kuliko maslahi ya taifa lao.

Lakini zaidi ufisadi kirahisi huikumba nchi kama nchi hiyo haijaweka itikadi/misingi rasmi na imara ya taifa ambayo kila chama kinapoingia madarakani kitalazimika kuifuata kwa maslahi ya nchi. Hivyo baadhi ya watu wenye fedha nyingi na malengo binafsi ya kiuchumi na /au kisiasa, hujenga mahusiano makubwa na vyama vikubwa hasa chama tawala na uhusiano huo hushamiri kutokana na hitaji la chama kupata ufadhili kwa ajili ya kushinda uchaguzi.

Kutokana na kutaka kung’ang’ania madaraka ya uongozi wa nchi kwa ajili ya maslahi binafsi zaidi, chama hicho tawala kinaweza kuamua kufanya kila linalowezekana, liwe jema au baya, ili mradi kishinde uchaguzi.

Kinaweza kufanya hivyo kwa kutoa propaganda za kuhadaa umma kwa kutumia hoja mfilisi kwamba vyama shindani (upinzani) hasa vyenye nguvu kwa wakati husika kwamba havina sera, au vina udini, ukabila, urangi, ujinsia utabaka na mambo mengine ya aina hiyo ili mradi lengo kuhalalisha ushindi lifanikiwe.

Wakiona wana ushindani mkubwa utakaohatarisha ushindi wao na wenyewe hawana fedha za kutosha kwa ajili ya mikakati ya ushindi, wanaweza kufanya mbinu za kupata fedha zaidi kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi walioko madarakani wakati husika kufanya mambo machafu.

Wanaweza kupata fedha wanazohitaji kwa ajili ya kupata ushindi kwa kuiba/kukwapua kutoka taasisi za serikali kama kwenye mabenki au miradi mikubwa ya umma yenye fedha nyingi.

Vile vile wanaweza hata wakatafuta watu ambao watapewa zabuni feki za serikali ambazo watalipwa fedha nyingi kwa makubaliano kwamba watamega fungu kubwa la fedha zitakazochotwa kifisadi kukisaidia chama kushinda uchaguzi.

Isitoshe inapokuwa ni utamaduni chama tawala kushinda uchaguzi kwa gharama yoyote ile, fedha za kutengeneza ushindi zinaweza zikawekwa kimkakati katika bajeti ya serikali au zikapatikana kutokana na mikataba mibovu na dhalili ya uwekezaji. Kwa mfano mwekezaji anaweza kumilikishwa mali yenye thamani ya fedha nyingi lakini anapewa mkataba ambao serikali itapata manufaa kidogo tu mradi mwekezaji huyo akisaidie chama kushinda chaguzi.

Fedha za kutafuta ushindi zinaweza kutafutwa kwa njia njingine chafu pia ikiwa ni pamoja na kuunda mitandao ya ujambazi ambayo inaweza kuendesha wizi wa kutisha katika shughuli za wananchi kwa mfano wizi kwenye maduka makubwa ya bidhaa, maduka yanayoendesha biashara ya fedha, (Bureau De Change), vituo vya mafuta, migahawa na baa, kuvamia maofisi siku za kulipa mishahara na kwingineko kokote zinakoweza kupatikana fedha.

Chama cha siasa kikishafikishwa hapo, kimsingi kinakuwa ni chama cha mafisadi au wakala wa mafisadi kwa kujua au kutokujua. Hivyo dola (serikali, bunge na mahakama) yake kwa vyovyote itakuwa imetekwa na mafisadi. Kwa hiyo dola hiyo penda isipende itakuwa inatekeleza matakwa ya mafisadi waliowezesha chama kupata ushindi.

Hii ndiyo sababu chama husika kikishapata ushindi, waliosaidia ushindi kupatikana wanakuwa wanalindwa kikamilifu ili malengo yao yatimie. Katika hali hii wanaoingia madarakani wanakosa wanakosa nguvu na ujasiri wa kufanya lolote hata kama wale waliosaidia watakuwa wanatenda mambo ya kutia taifa dosari kubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Kibaya zaidi kama fedha za kuwezesha kushinda uchaguzi zitakuwa zimepatikana kifisadi, na ikatokea siri ya ufisadi huo ikavuja, basi kazi kubwa waliopata madaraka kutokana na uchaguzi huo inakuwa ni kubuni mikakati mbali mbali na kwa gharama yoyote kuhakikisha ufisadi huo unafunikwa

Hali ya chama tawala husika kuogopa kushindwa uchaguzi au kuumbuka kwa ufisadi inaweza kusababisha chaguzi zitakazofuata kugubikwa na ufisadi mkubwa zaidi tena wa kutisha na ambao pengine haitakuwa rahisi kufichuliwa kutokana na ukweli kwamba uzoefu wa kufanya ufisadi kwa ajili ya kushinda uchaguzi utakuwa unajengeka na kuimarika kutoka uchaguzi mmoja hadi mwingine.

Ikiwa lengo kuu la chama cha siasa ni kushinda uchaguzi, shughuli kubwa siku zote itakuwa ni kutafuta mbinu za kupata ushindi hata kama ni kwa ufisadi au kufanya chochote kile kichafu au kisafi, labda makundi makumba yenye uchungu na hatma ya nchi yawe jasiri na kukimama imara bila kugawanyika kuhakikisha waliohusika/chama husika kinawajibishwa kabla sumu hiyo haijasambaa na kuigwa na vyama vingine vikubwa ambavyo vinaweza kushinda chaguzi zinazofuata.

Ni kwa sababu ya ukweli huu ndiyo maana hata kama baadhi ya wale waliosaidiwa kuingia madarakani watakuwa na nia njema ya kutaka kuwatosa waliowasaidia, hawatathubutu kufanya hivyo kutokana na hofu kwamba mipango ya kushinda chaguzi zinaofuata itavurugika na hivyo kukiweka chama katika hatari ya kushindwa.

Ili kuhakikisha kushindwa hakutokei, uhakika wa fedha za kuwezesha chama kishinde ukishakuwepo, kitakachofanyika ni kutumia fedha hizo kupata ushindi hasa kwa kucheza na saikolojia na mahitaji ya msingi(chakula, vinywaji, mavazi na hata kiroho) ya wapiga kura hasa wasiojua kinachoendelea na madhara yake kwa ustawi wa demokrasia, amani na maendeleo yao binafsi na ya taifa lao.

Hii inawezekana kwa kuweka mkakati mahususi ikiwa ni pamoja na kuhonga wananchi fedha, mavazi, chakula au vitu vingine vidogo vidogo kukidhi mahitaji ya fukara, kununua shahada za wapiga kura ili wasiweze kupiga kura, kuwatisha wananchi kwa kutumia vyombo vya dola, kuunda vikundi vya kihalifu kuwashambulia, kuwafilisi na kuwatisha watu watakaoonekana kuunga mkono vyama vingine.

Kama mambo ni magumu zaidi wanaweza kununua baadhi ya maafisa wa tume ya uchaguzi ili majina ya wapiga kura yavurugwe wapiga kura hasa kwenye maeneo yenye upinzani mkubwa wasiweze kupiga kura kabisa au kwa wakati uliopangwa.

Vile vile sheria za nchi hasa zinazohusu uchaguzi kwa wakati husika hata kama ni nzuri kiasi gani, wanaweza kucheza nazo kwa ajili ya kuwezesha ushindi.

Kwa mfano, sheria inaweza kuwa inatoa fursa kwamba mgombea Urais au mgombea Mwenza wa Urais akifariki dunia kabla ya uchaguzi, uchaguzi huo utahairishwa ili chama hicho kiweze kutafuta mgombea mwingine.

Sheria hii inawezekana kuonekana ni nzuri, lakini hebu fikiria, wagombea Urais wanaweza kuwa ni wengi baadhi kutoka vyama vikubwa na wengine kutoka vyama vidogo sana ambavyo kwa wakati husika havina uwezo kisiasa kushinda hata udiwani lakini vimesimamisha mgombea wa Urais iwe ni kwa vyama husika vyenyewe kutaka kutumia demokrasia iliyopo au ni kwa kushinikizwa na mafisadi kwa malengo mahususi la kuwezesha chama kilicholengwa kusaidiwa kupata ushindi kiweze kushinda.

Sheria hiyo nzuri inaweza kutumiwa na watu wenye malengo mabaya ya kuweka madarakani watu ambao watalinda maslahi yao zaidi kwa sababu wenye malengo mabaya wanaweza kuhonga mwanasiasa ambaye wanajua yuko taabani kiafya agombee kwa lengo la kutumia fursa hiyo kutekeleza mikakati ya ushindi.

Kwa vile ukwapuaji wa mali za umma kwa malengo ya kiuchumi na kupata madaraka ni kitu ambacho ni kichafu kwa jamii yoyote, na kwa vile wanaoumizwa na ufisadi ni wananchi fukara mijini na vijijini, wanawake na wanaume, vijana na wazee, siri ya ufisadi ikivuja wahusika wanachofanya ni kuhakikisha kuwa kila sauti ambayo inaweza kuinuka na kudai uwajibikaji dhidi ya uovu huo inazimwa.

Inaweza kufanyika kwa kupenyeza mamluki kwenye vyama shindani vya siasa ili kutengeneza migogoro au kusababisha mazingira ambayo baadhi ya vyama hivyo navyo vinajitumbukiza katika mambo yatakayovipunfguzia sifa mbele ya umma au mambo ambayo yatawanyang’anya ujasiri wa kudai uwajibikaji wa waliotumia ufisadi kushinda uchaguzi.

Mbinu nyingine ya kuzima uwajibikaji dhidi ya ufisadi ni kwa wanataaluma kwa wanahabari kutishwa ili waogope kufanya kazi yao kikamilifu ili kushinikiza uwajibikaji wa watawala wa wakati husika kuhusiana na ufisadi. Pia wakati mwingine baadhi yao hasa wahariri na wanahabari makini na pengine hata wamiliki wao wanaweza kununuliwa kwa kujua au kutokujua njama hizo mradi tu wasiweze kutumia fursa na taaluma zao kukomesha ufisadi.

Wengine wanaoweza kununuliwa na mafisadi au mawakala wake ili kuzima uwajibikaji kwenye ufisadi ni viongozi wa vyama vya wanataaluma kwa mfano wanasheria/mawakili, vyama vya wahadhiri vyuo vikuu, vyama vya wanafunzi, vyama vya wafanyakazi, taasisi za dini, mitandao ya mashirika yasiyo ya kiserikali na wasanii mashuhuri na wanamuziki.

Mambo mbali mbali yanaweza kufanyika kisiasa kuhakikisha kuwa makundi hayo yanapata ganzi/kigugumizi au kuona kuwa hakuna ufisadi au ufisadi ni sehemu ya maisha na hivyo hakuna umuhimu wa wao kushiriki kudai uwajibikaji dhidi ya vyama vya siasa vinavyokumbatia ufisadi ili watu binafsi na vyama hivyo vinufaike kisiasa.

Kwa mfano wanasiasa wenye malengo binafsi wanaweza kutengeneza jambo ambalo litazusha mjajala unaoleta mgawanyiko na pengine chuki katika ya makundi katika jamii husika kutokana na imani za dini, mila na desturi, kijinsia na/au ukabila.

Lengo ni wenye uchu wa madaraka kubaki madarakani na wenye maslahi ya kiuchumi waweze kuendelea kuchuma. Lakini kamwe hawatathubutu kuzusha jambo litakalozua mjadala katika tatizo la mzingi ambalo ni siasa kutumika kutengeneza matajiri wa kupindukia na huku wananchi wengi wakiwa ni maskini wa kutisha.

Vile vile wabunge jasiri kutoka chama tawala husika ambao watathubutu kutaka vinara wa ufisadi katika chama chao au serikalini wawajibishwe, wanaweza kufanyiwa vitimbi na vitisho pamoja na kusukiwa mikakati ya kuhakikisha kuwa wanashindwa katika chaguzi zinazofuata.

Kadhalika watu waadilifu hasa wazee, vigogo, viongozi wastaafu na makada kwenye chama kilichosaidiwa kuingia madarakani kwa fedha za ufisadi nao pia wanaweza kufanyiwa vitimbi mbali mbali ili washindwe kufurutika kuwajibisha uwajibikaji kwenye chama chao.

Wanaweza kufanyiwa mambo yatakayowajengea hofu kuhusu hatma yao wenyewe na/au hatma za familia zao hasa kisiasa na kiuchumi. Kwa mfano wanaweza kutengenezewa tuhuma za kupika ili na wenyewe waonekane mbele ya jamii kuwa ni watuhumiwa wa ufisadi.

Lakini zaidi wazee, viongozi na makada wadilifu katika chama wanaweza kushindwa kutoa sauti zao dhidi ya ufisadi hasa endapo mfumo utakuwa umewawezesha kunufaika kiuchumi kutokana na chama chao kuwa madarakani.

Baadhi wanaweza kuwa wana kampuni ambazo ni mawakala wa kukusanya ushuru ambapo sehemu kubwa ya fedha zinazokusanywa zitanufaisha wakala na serikali inaambulia fedha kidogo sana. Katika hali hii hawataweza kuwa na sauti ya kukemea ufisadi katika chama wala serikali kwa sababu na wenyewe wanaweza kuonekana mbele ya jamii kuwa ni watu wanaoinyonya serikali na hivyo kufukarisha wananchi.

Zaidi ya hayo, kwa sababu ufisadi una tabia ya kuwajengea wahusika jeuri ya kifisadi kutokana na nguvu ya madaraka na nguvu ya fedha, hata kama zipo sauti nyingi zinazodai uwajibikaji, wahusika wanaweza kuzipuuza sauti hizo na kuamua kuziba masikio kwa sababu liwe liwalo wanakuwa na uhakika wa chama chao kushinda chaguzi zijazo. Hivyo kwao kuogopa wananchi au kuwatumikia kikamilifu si jambo la lazima wala lenye umuhimu.

Ikifikia hapo wa demokrasia ya vyama vingi inakuwa haina maana yoyote katika kuharakisha maendeleo ya nchi sababu wanaoshika madaraka wanapata madaraka hayo kutokana na jinsi walivyo karibu na waliowezesha chama husika kushinda uchaguzi na siyo uwezo wao katika kubuni mbinu za kuisaidia taifa kusonga mbele.

Kibaya zaidi, vyama vingine vya siasa vikishabaini kuwa chama tawala ni king’ang’anizi wa madaraka na tena kinafanya ufisadi kupata ushindi, navyo ikifika mahali vikaishiwa uzalendo vinaweza kulazimika kuiga mbinu hizo chafu au pengine chafu zaidi na zenye maumivu makubwa zaidi kwa taifa na hivyo demokrasia kuzima kabisa sauti za wananchi maskini zisisikike na kufanyiwa kazi na watawala ili waondokane na ufukara.

Kitakachofuata katika hali hiyo ya kila chama chenye nguvu kutafuta ushindi kwa mbinu za kifisadi ni nchi kutumbukia katika machafuko. Machafuko kutokea katika nchi kutokana na chama tawala kutafuta ushindi kwa namna yoyote ile kumeshajidhihirisha katika nchi kadhaa za Afrika ikiwepo nchi jirani ya Kenya na pia Zimbabwe.

Je kwa hali ilivyo sasa nchini kwetu kuhusu ufisadi, kweli tutaweza kusalimisha taifa letu lisiingie katika mgogoro wa kugombea madaraka? Kama tutakubali kurudi nyuma au kuyumbishwa ili tupuuze au kuogopa kusimama kidete kushinikiza uwajibikaji katika ufisadi, je kuna yeyote miongoni mwetu ambaye hataguswa kwa namna moja au nyingine amani ikichafuka nchini kwetu?

Kwa hiyo, kama sote hatutaki ufisadi uhatarishe demokrasia ya vyama vingi, amani, mshikamano na maendeleo ya taifa letu, ni vema makundi yote muhimu katika jamii yajitoe mhanga kushinikiza uwajibikaji dhidi ya tuhuma za ufisadi zinazoikabili nchi hivi sasa ili hatua madhubuti zichukuliwe kuhakikisha kuwa wanaotaka kupeleka taifa kubaya hawaogopwi na wanawajibishwa..

Lakini zaidi ni vema wale wote wanaotumia ufisadi kung’ng’ania madaraka wakubali kuwa sehemu ya mabadiliko ya kidemokrasia yanayotokana na mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini. Vinginevyo wasipobadilika na ikatokea sauti za wananchi zikashinda ufisadi, wanaweza kujikuta mabadiliko yenyewe yakiwalazimisha nao wabadilike na ikifikia hapo wanaweza wakawa katika hatari ya kufedheheka. Tukiamua Watanzania, tutashinda adui ufisadi kwa manufaa ya taifa zima.
MUNGU IBARIKI TANZANIA. ( Tuwasiliane 0754 464368 email –ananilea_n...@yahoo.com)
 
Post yako ni ndefu sana nimesoma first and last paragraph tu. Lakini je wananchi tunachangiaje kwenye hili tatizo?
 
wananchi mbona inaeleweka si ndio tunaowachagua hao mafisadi kwenye majimbo yetu ya uchaguzi!
Post yako ni ndefu sana nimesoma first and last paragraph tu. Lakini je wananchi tunachangiaje kwenye hili tatizo?
 
Back
Top Bottom