Kwanza nianze kwa kukupongeza kwa dhati kabisa RC. Makonda.
Wewe ni shujaa wa leo na kesho. Umeruka dhambi ya unafiki na kuwa mkweli.
Vitabu vya dini vinakataza sana unafiki. Na wewe umeonekana ama kwa hakika hupendi unafiki.
Umeweka mbele maslahi ya watanzania na Umeonyesha utiifu wako kwa nchi yako na kwa Rais wetu ambaye ama kwa hakika amekua akikerwa na uovu unaofanywa ndani ya Taifa hili.
Ama kwa hakika kila mmoja ameona nguvu ya wauza madawa waliyonayo kila kona na idara ya nchi hii. Siamini kwamba bunge liliamua kuacha shughuli zake na kuamua kujadili kauli yako ya kupingana na Mbunge mmoja tu bila nguvu kutoka mahali pengine.
Pia tumeona jinsi wabunge wetu walivyoungana kudhoofisha juhudi zako za kupambana na uuzwaji wa dawa za kulevya nchini pamoja na kwamba wamejipambanua kuwa wanapinga mbinu inayotumika.
Kwa mwenye akili anajua wazi kuwa kupinga mbinu uliyotumia ni kupinga vita yenyewe.
Vita ni vita tu : Hakuna vita isiyo na madhara. Huwezi kuanzisha vita halafu unaogopa madhara ya vita hiyo. Hapo una maanisha vita iachwe. Hao wanaopinga madhara ya kuwataja watumiaji eti ni kuwadhalilisha wanasahau kuwa ndio hao hao siku zote polisi inapokamata kimya kimya wamekua wakipiga kelele kuwa wanawaonea na kukamata watu ovyo bila sababu na kuwabambikia bangi /madawa ya kulevya.
Polisi wakiwaachia hao hao wanalalamika kuwa polisi wanakula rushwa na kuwaachia watuhumiwa wa madawa ya kulevya. Leo hii imani yao kwa jeshi la polisi inatoka wapi kama sio mbinu ya kupinga na kukwamisha zoezi hili la kupambana na hii biashara haramu?
Kwa nini Bunge halikuunda tume au kamati maalum ili kufanya uchunguzi wa kina kwa waliotuhumiwa na ikiwezekana kuchunguza mali za wale askari waliohusishwa na kuwasaidia wauza unga kukwepa mkono wa dola na ikiwezekana kupitia vielelezo alivyonavyo Mh. Makonda ili kubaini ukweli au uongo wa Makonda ndipo watoe mapendekezo?
Ukiangalia kwa umakini maazimio ya Bunge yanawabeba zaidi waliotuhumiwa kuliko RC Makonda ambaye anaonekana wazi kuwa ana taarifa za kutosha juu ya hao aliowatuhumu.
Ukiona mtu anasimama adharani kudili na magenge ya watumiaji wa madawa ya kulevya ujue huyo mtu amejitoa muhanga.
Naamini RC Makonda umejitoa muhanga kuokoa watoto wetu na kizazi kijacho.
RC Makonda Historia itakusoma kama shujaa na wanaokaa na kujifanya kuwa wanakutafutia utaratibu wa kisiasa wa kupambana na madawa ya kulevya watahukumiwa na majina yao hayatakumbukwa kamwe.
Hivi kama usingejitokeza adharani na kusema wazi na kuwataja kwa uwazi kuwa kuna askari wanaoshirikiana na wauza unga na wanatoa siri na kuvuruga zoezi la kukamata hao wauza unga ni nani angesema.?
Je , hizo tuhumu hao wapinzani wako ndio mara ya kwanza kuzisikia?
Nani ambaye hajui kuwa kuna ubabaishaji na kuharibiwa kwa vielelezo mara kwa mara na madawa yanageuzwa kuwa chumvi? Matokeo yake wakamataji wanaonekana ni wajinga na hawajui wajibu wao?
Je hao wapinzani wako siku zote walikua wapi kuhakikisha wanatunga sheria bora za kuwapa mazingira bora zaidi wakamataji na namna bora zaidi ya kuhifadhi na kuyagundua madawa ya kulevya badala ya kutegemea ofisi moja tu ya mkemia mkuu wa serikali peke yake ambayo haina maabara mikoani?
Hivi nani hajui kuwa vita dhidi ya madawa ya kulevya inahitaji utashi wa kisiasa zaidi kuliko sheria na vyombo vya dola peke yake? Ni askari gani ataweza kwenda kumkamata bilionea na kumweka ndani kwa madawa ya kulevya ?Na ni bilionea gani atakubali kuwekwa ndani kwa tuhuma ya madawa ya kulevya bila kutoa mabilioni na kuwahonga wote waliomkamata kisha kuwa yeye ndio rafiki yao na mtu muhimu kwao?
Ni nani atakayeweza kukataa hongo ya bilioni moja ili amwachie mtuhumiwa wa madawa kama hakuna nguvu kubwa ya kisiasa inayotamka kwa wazi kuwa sasa basi? Akikataa kupokea hiyo rushwa ujue anakua ni adui namba moja na hakuna mtu wa kumtetea! Akikataa mkamataji basi atachukua mpelelezi! Akikataa mpelelezi basi atachukua kule kwa mkemia na Madawa yatageuka chumvi.
Ni lazima wanasiasa na wabunge wote waungane na Jeshi la polisi kwa wazi ili wauzaji nao waone hawana wa kumtegemea kwani kila jicho liko nyuma yao.
Hata magaidi huwa yanatajwa hadharani na kwa wazi ili kila mtu ayatafute na kuyakamata. Usipowataja wauzaji na watumiaji basi watazagaa mitaani na kupewa heshima kumbe ndio wanaotumaliza.
Kwa hili RC Makonda usirudi nyuma kamwe.
MAPENDEKEZO YANGU KWAKO SHUJAA WA SASA NA SIKU ZIJAZO RC MAKONDA:
(1) Muombe Mh. Rais aunde tume maalum ili kuwachunguza kwa kina wale wote waliotajwa ili kuweka uwazi zaidi na hatimaye wajipime wenyewe kama wanaacha au wanaishia kwenye mikono ya sheria.
>Tume hiyo iundwe na watu makini na waadilifu sana wakiwemo Majaji, viongozi wa dini ,askari waadilifu na wastaafu kama Akina Nzowa , Tosi,Mwamunyange,shehe mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Alhaji Mussa, watu wa haki za binadamu,baadhi ya waandishi mashuhuri, wafanyabiashara waadilifu, madaktari waadilifu kwenye upande wa phamasia, madaktari mahiri kutoka ndani na nje ya nchi na wataalam wa madawa ya kulevya kutoka ndani na nje ya nchi.
(2) Wachaguliwe madaktari wa serikali na wa binafsi na wakemia kutoka ndani na nje ya nchi ili kila aliyetuhumiwa achukuliwe DAMU na kuipelekwa kwenye maabara za ndani na za nje ili kulinganisha matokeo ya vipimo vya damu husika.
Hatutaki mtu aonewe wala atafute huruma kwa yale aliyotenda. Mbinu za kisayansi za kuwapima damu kama wanavyopimwa wachezaji huko nje zitumike. Ili tuwajue
(3) Tangaza dau na zawadi kwa mtu atakayefanikisha kukamatwa kwa madawa ya kulevya kuanzia sasa.
(4) Hakikisha unatoa ushirikiano kwa vyombo vingine vya sheria akiwemo pia waziri wa Sheria ili sheria ya mihadarati ifanyiwe marekebisho ili watumiaji wamadawa wabainike na kuadhibiwa pia kwa kupitia vipimo vya damu ili kuondoa dhana ya kubambikiwa kesi.
Iwe kama ilivyo kwa madereva ambao wanapimwa kupitia pumzi zao au vipimo vya damu na wanapewa adhabu.
(5) Hakikisha ndani ya mkoa wako maabara za mkemia mkuu wa serikali zinafunguliwa kwenye Hospitali za Temeke ,Mwananyamala na Mnazi mmoja ili kupunguza urasimu uliopo kwenye ofisi moja tu ya mkemia jambo linalochelewesha na kuharibu upelelezi wa makosa ya mihadarati ikiwemo bangi.
Hii ni vita takatifu uliyoianzisha na :-
Mungu yupo nawe.
Mh. Rais yupo nawe.
IGP yupo nawe.
Kamanda Siro yupo nawe.
Waziri wa mambo ya ndani yupo nawe.
Usirudi nyuma mpaka wajisalimishe wote.