Madai ya Rushwa za Ngono Yasitumike Kukandamiza Wengine

DidYouKnow

Senior Member
Joined
Jul 28, 2019
Messages
160
Points
500

DidYouKnow

Senior Member
Joined Jul 28, 2019
160 500
Moderator naomba andiko langu lijitegemee, lisiunganishwe na nyuzi kadhaa zilizoandikwa humu kuhusiana na Rushwa za ngono kwa sababu maudhui yake ni tofauti kabisa.

Hivi karibuni kumekuwa na taarifa nyingi zinazoandikwa kuhusiana na rushwa za ngono au manyanyaso ya kingono yanayofanywa zaidi na wanaume dhidi ya wanawake. Matukio haya mara nyingi taarifa zake zinatolewa na wanawake wenyewe, ila kuna wakati yanatolewa na watu wanaodai kuwa na uhusiano wa karibu na hawa wanawake. Taarifa hizi husaidia kuwakamata watu wenye tabia hizi mbaya, lakini shida ni pale taarifa kama hizi zinapotolewa kwenye mitandao ya kijamii huku mwandishi akificha utambulisho wake lakini akitoa majina ya mtu anayedai ni mnyanyasaji wa kingono. Mitandao kama Jamiiforums imekuwa mstari wa mbele kupambana na matatizo kama haya, lakini pia ikijisahau kumsitiri mtuhumiwa ambaye ana haki zake pia. Ni kanuni ya kisheria ambayo mtu huchukuliwa kuwa hana hatia hadi kuthibitika kuwa na hatia. Hii pia ni haki ya kimataifa ya binadamu chini ya Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu, Kifungu cha 11.

Kama nilivyosema hapo juu, utoaji wa taarifa hizi hufanya kusiwe na haki pande zote (mlalamikaji na mlalamikiwa), kwa sababu upande mmoja unapewa manufaa ya kuaminika huku upande unaotuhumiwa ukikosa haki hiyo. Bahati mbaya zaidi kila kinachoandikwa kwenye mitandao ya kijamii huaminika zaidi; na watu wengi hupenda kusikia taarifa mbaya, kwani taarifa nzuri huwa si habari tena. Laana lukuki huwafuata watuhumiwa hata kabla hatujajua ukweli wowote.

Mara nyingi sisi kama jamii tumekuwa tukitoa hukumu kwa taarifa ambazo hata sisi wenyewe hatujajua ukweli wake au mamlaka husika hazijathibitisha ukweli wake, ila kwa sababu taarifa hizi zimeandikwa kwenye mitandao basi sisi wasomaji huamini kila kilichoandikwa kuwa ni kweli. Lakini tukumbuke mtu yeyote yule anaweza akaandika lolote kuhusu Fulani ili kutimiza lengo lake, na kwa hakika huyo Fulani atapata shida sana kujisafisha. Utaamini huu msemo mashuhuri usemao Usiamini kila kitu unachokiona au kusoma kwenye mitandao ya kijamii, pale mtu wako wa karibu au wewe mwenyewe atakaposingiziwa na wewe ukafahamu ukweli halisi.

Nina bahati mbaya (si kumbukumbu nzuri) ya kuwa karibu na mmoja wa waathirika wa tuhuma za rushwa za ngono kipindi fulani nikiwa ninafanya kazi taasisi moja iliyokuwa jijini Dar es Salaam. Kila kitu kilichoongelewa kuhusu huyo mtu, na jinsi anavyogawa kazi kwa kutoa rushwa ya ngono havikuwa na chembe ya ukweli, lakini mtu mmoja tu ambaye ama alisikia au alihisi au alikuwa anataka kumharibia huyu Rafiki akaamua kutunga uongo kufanikisha lengo lake. Watu walikuwa wakitoa taarifa nyingi sana kuhusu huyu mtu kama vile wanamfahamu, lakini zote zilikuwa ni tuhuma zisizokuwa hata na chembe ya ukweli. Bahati mbaya sana, lengo la mleta tuhuma lilifanikiwa, kwani Rafiki yangu alipoteza mke na watoto, akaanza kunywa pombe kupita kiasi na mwisho wake haukuwa mzuri, kwani alikufa kwa unywaji mkubwa wa pombe.

Malalamiko ya manyanyaso kijinsia au kingono yasiyothibitishwa au kuaminika yanamwondolea haki mlalamikiwa na mara nyingi huharibu career za mlalamikiwa. Malalamiko ya uongo ya manyanyayo ya kingono na yanaoyofanana na hayo yamekuwa yakiongezeka kila mwaka hata katika idara kubwa za mataifa ya nje kama Pentagon, Marekani.

Mfano mzuri wa udhalimu wanazofanyiwa baadhi ya wanaume na wanawake kwa kudaiwa kuwanyanyasa kingono wanawake ni Generali wa Jeshi la Anga la Marekani, John Hyten, alipoteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya ushauri wa kijeshi (Joint Chiefs of Staff). John Hyten alilalamikiwa na Kanali Kathryn Spletstoser kwamba alimnyanyasa kingono. Lakini uchunguzi wa ndani uliofanywa na kikosi maalum (OSI) uligundua madai yote yaliyotolewa dhidi ya John Hyten hayakuwa na ukweli. Jambo hili kama lingekuwa ni kweli, lingefuta ndoto na hata kazi yake na asingepata cheo alichonacho sasa.

Mhariri mwandamizi wa jarida The Federalist, ameripoti kwamba wachunguzi 53 wa OSI walihoji watu 63 na walifanya ukaguzi wa uchunguzi wa maelfu ya barua pepe, rekodi za kusafiri na nyaraka zingine. Uchunguzi uliokithiri haukupata ushahidi wa kuunga mkono kitu chochote ambacho Kanali Spletstoser alikuwa ameshtaki, lakini wachunguzi walithibitisha kuwa Kanali Spletstoser alikuwa na historia ya kutengeneza mazingira magumu ya kazi yaliyojaa magombano na kupunguza utenda kazi kwa wasaidizi wake na kuweka madai yasiyokuwa na ukweli dhidi ya wasimamizi.

Uchunguni uliripoti kwamba mashuhuda kadhaa waliwaambia wachunguzi kuwa hawajawahi kuona Gen. Hyten akimtendea tendo baya au pasipo kufuata taaluma Col. Spletstoser. Badala yake, mashuhuda walizua maswali juu ya tabia yake ya ajabu wakati mwingine na kulipiza kisasi dhidi ya Hyten aliyemwondolea majukumu Spletstoser kwa sababu ya utendaji kazi wake usioridhisha.

Wakati Hyten anahojiwa na seneti ya Marekani ili kupitishwa kuwa Makamu Mwenyekiti, Seneta Martha McSally ambaye anajitambulisha kuwa naye ni muathirika wa shambulio la kingono, alisema yeye mwenyewe alipitia kazi ya uchunguzi iliyofanywa na OSI dhidi ya jenerali General Hyten na kuthibitisha “hana hatia na tuhuma hizi”. Pia Meja jenerali Heidi Brown ambaye ni mstaafu pia alihakiki na kuidhinisha taarifa ya uchunguzi huu maalum na akaandika kwenye jarida la Wall Street Journal, “Lazima kuwe na adhabu ya kumwingiza mtu asiye na hatia na familia yake kupitia mateso kama haya.”

Nchini Marekani, katika mwaka 2009, iliripotiwa kwamba tukio moja katika manne yanayohusisha unyanyasaji wa kingono yaliamuliwa kuwa hayana ukweli kwa kukosa vielelezo vya kutosha au madai kutokuwa ya msingi.

Kati ya mwaka wa fedha 2009 hadi 2018, taarifa za uongo za matukio ya kingono nchini Marekani ziliongezeka toka asilimia 13 hadi 28. Ukweli kwamba matukio matatu katika manne ni ya ukweli na yanapaswa kupewa adhabu yasitutoe kwenye ukweli kwamba mtu mmoja asiye na hatia katika matukio manne yaliyotolewa taarifa atashitakiwa kwa uongo. Hii ni kwa mujibu wa Takwimu za Marekani, sijui kwa Tanzania.

Malalamiko ya unyanyasaji wa kingono yanapaswa yafanywe kwa uchunguzi makini na toshelevu. Lakini bila kujali nani katuhumiwa, wale ambao wanatajwa kwa madai ya uwongo wanaharibiwa maisha yao na familia zao na hasa pale kila mtu anapowahukumu bila kujua ukweli na taasisi zinazohusika kuwachunguza zikashindwa kuwasafisha. Hii ni changamoto kwa viongozi kwamba ni lazima wahakikishe taasisi zinazosimamia kutafuta haki kwa mshtaki na mshtakiwa zina weledi wa kutosha.

Linda Fairstein, mkuu wa zamani wa kitengo cha uhalifu wa kingono katika ofisi ya Mwanasheria wa Wilaya ya Manhattan huko Marekani, alitoa maoni yake juu ya uzoefu wake na madai yasiyokuwa na msingi ya ubakaji:

“Baada ya kufanya kazi katika uwanda huu kwa miongo kadhaa, nimeona jambo hili kuwa chungu sana kushuhudia. Wanaume wasio na hatia wanakamatwa na hata kufungwa gerezani kwa sababu ya madai ya uwongo. . . uwongo huu huathiri ukweli wa matukio halisi ya ubakaji waliyotendewa baadhi ya watu.”

Wachunguzi waliofunzwa maridadi wanatambua njia rahisi za kutambua ukweli wa tuhuma kama hizi ambazo ni muhimu katika kutathmini ukweli wa malalamiko. Hakuna njia moja sahihi zaidi, lakini mchanganyiko wa mambo yasiyo ya kawaida utaonyesha uwezekano wa malalamiko ya uwongo. Kwa maneno ya jumla, kwa mfano:

 • Malalamiko ya kweli kawaida hutolewa haraka; ya uwongo mara nyingi hucheleweshwa kwa wiki au miezi.
 • Mlalamikaji hatoi habari za uongo namna alivyoomba au kupata msaada wa karibu au kutoa taarifa kwenye mamlaka husika.
 • Mlalamikaji hawezi akawa ni muathirika wa matukio zaidi ya moja yanayofanywa na watu tofauti sehemu moja ile ile, labda mlalamikaji awe ni mtumwa wa kingono aliye utumwani.
 • Mara nyingi madai ya uwongo huwa hayana ukweli juu ya maumbile ya shambulio, aina za vitendo vya ngono, kiwango cha kupinga, na hata mahali ambapo shambulio hilo limetokea.
 • Mashtaka ya uwongo kawaida hayana ushahidi unaodhibitisha vurugu; mfano ishara za vurugu katika eneo la uhalifu, uharibifu wa mavazi sanjari na mapambano (damu).
 • Walalamikaji wenye shida ya kihemko (emotional or psychological) wakati mwingine huweka ripoti za uwongo ambazo zinanakili makosa ya zamani.
 • Waathirika wa kweli kawaida huripoti maelezo yasiyofurahisha bila kukasirika wanapoulizwa kudhibitisha kilichotokea.
 • Mlalamikaji kutounganisha historia za matukio ya mlalamikiwa ili kuzifanya zifanane na tukio lake
 • Muathirika hawezi toa taarifa zinazochanganya n.k
Kila madai huwa ni tofauti, na muonekane wake mara nyingi hudanganya. Viashiria fulani vinapaswa kuchunguzwa ili kutenganisha madai ya kweli na ya uongo. Mara nyingi madai ya uongo husababishwa na:
 • Wivu au kulipiza kisasi - mifano kama kugombania madaraka, matatizo ya uchumba, kuingiliana katika mahusiano, ufaulu hafifu darasani, ni wivu tu, n.k. Maneno na muonekano wa sura wa mdai vinaweza kushawishi kutokea kwa tukio lakini vikadanganya.
 • Kupenda umaarufu - Mtumishi wa Fox News Tucker Carlson alikabiliwa na shida hii mnamo 2001. Mwanamke ambaye alikuwa hajawahi kukutana naye alidai kuwa alimdhalilisha kwenye mgahawa mmoja huko Kentucky, Marekani na kumnyanyasa kingono. Kwa siku kadhaa Tucker alikosa usingizi na akalipa zaidi ya pesa za kitanzania million 30 kama ada ya kisheria, baadaye, mshtakiwa alifuta mashtaka.
 • Kuepuka lawama – Hii hutokea sana miongoni mwa watumishi na wanafunzi. Mfano mtumishi anayekumbana na msimamizi mkali na wakawa na migongano ya hapa na pale ataingiza tuhuma za ngono dhidi ya msimamizi, pia mwanafunzi baada ya kutofanya vizuri darasani hutafuta visingizio vya rushwa za ngono kwake yeye mwenyewe au kwa watu ambao wamefaulu zaidi kama ndio chanzo cha kutofanya vizuri.
 • Siasa na Itikadi mbalimbali – Hii hutokea pale kundi moja linapotaka kushinda kundi la pili.
Ili kuepuka utoaji haki usio sawa kwa pande zote, ni vyema kanuni za jumla kama zifuatazo zikatumika katika maswala ya unyanyasaji wa kijinsia:
 • Viongozi wanapaswa kuzuia kujenga hisia au maoni hasi mapema kabla ya kufanya uchunguzi bali kutengeneza mazingira ya uchunguzi wa haki, hata kufikia mashahidi au Ushahidi haraka.
 • Ili kufanikisha mchakato na kutoa haki, mshtaki na mshtakiwa wanapaswa kupewa miongozo au ushauri wa kisheria yenye usawa na kusiwepo kuingiliwa na serikali au wanasiasa.
 • Watu wanaoripoti unyanyasaji wa kingono wanapaswa kuheshimiwa na kulindwa na matukio ya kulipiza kisasi, lakini pia watu wanaowasilisha mashtaka ya uwongo kwa nia ovu pia ni lazima wawajibike pakubwa kama kufukuzwa kazi na kulipa faini kubwa.
 • Kutumika kwa madawati ya manyanyaso ya kijinsia yaliyopo vituo vya polisi.

Chanzo cha Habari: Kwa msaada wa vyombo vya habari za Kimataifa
 

Forum statistics

Threads 1,390,026
Members 528,081
Posts 34,041,309
Top