๐๐๐ฎ๐น๐ฎ ๐๐๐บ๐ฝ๐๐ฟ, ๐ ๐ฎ๐น๐ฎ๐๐๐ถ๐ฎ โ Jua lilikuwa bado halijapanda sana asubuhi ya tarehe 23 Agosti 2001, lakini katika kona ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kuala Lumpur kulikuwa na shughuli nyingi zikiendelea.
Moja ya shughuli hizo ni ndege kubwa aina ya Boeing 747-300 ya shirika la ndege la Saudi Arabian, yenye usajili HZ-AIO, ambapo ilikuwa imekamilisha matengenezo na majaribio ya injini.
Ndege hiyo ilikuwa imepangwa kubeba abiria 319 kwenye safari ya kuelekea Jeddah, Saudi Arabia.
Mafundi 06 walipanda ndani. Hapakuwa na abiria, hapakuwa na wahudumu wa ndege. Kazi yao ilikuwa rahisi tu, kuiongoza ndege hiyo kutoka karakana hadi lango la abiria.
Walianza kuisogeza polepole kwa kutumia injini mbili tu, namba 2 na namba 3. Kila kitu kilionekana sawa, hadi walipofika kwenye kona ya kuelekea njia nyingine.
Ndipo kosa dogo lakini la gharama kubwa lilipotokea. Katika haraka zao za siku hiyo walikuwa wamesahau kuwasha pampu za dharura za mfumo wa haidroliki.
Bila pampu hizo, mfumo mzima wa haidroliki unapoteza nguvu. Breki hazikushika na usukani wa gurudumu la mbele ulikataa.
Ndege hiyo kubwa badala ya kupinda, iliendelea mbele moja kwa moja kama ilivyoamrishwa na injini hizo mbili zilizowashwa na mafundi hao.
Mafundi ndani walijaribu kila njia, wakakanyaga breki, wakageuza usukani, lakini 747 ile haikusikia kitu.
Sekunde chache baadaye, ndege ilitoka nje ya njia ya lami na kwa kishindo kikali pua yake ilizama ndani ya mfereji mkubwa wa zege wa maji ya mvua.
Kelele zilisikika uwanja mzima.
Sehemu ya mbele ya chumba cha marubani ilipasuka na kubonyezeka vibaya.
Lakini bahati nzuri, mafundi wote sita walitoka hai, wakiwa na mshtuko tu, hawakuumia vibaya.
Ndege yenyewe, iliyokuwa na miaka 16, haikuwa na bahati.
Wahandisi wa ndege walipoangalia uharibifu huo walitikisa vichwa.
Gharama ya kuitengeneza ilikuwa kubwa kuliko thamani yake. Kwa hivyo, Boeing 747-300 hiyo iliandikwa rasmi โimeharibika kabisa, haifaiโ na safari yake ya mwisho ikaishia kwenye mfereji wa Kuala Lumpur.