Majira ya joto mnamo mwaka 1983, ndege ya Air Canada (Flight 143) aina ya Boeing 767 ilikaribia kuanguka kutoka angani kwa sababu ya kosa dogo la kihesabu.
Canada ilikuwa imebadilika kutumia mfumo wa metriki na hii Boeing 767 ilikuwa ndege ya kwanza kutumia kipimo cha kilogramu badala ya paundi katika ujazaji mafuta.
Mmoja wa wafanyakazi wa chini alikosea kubadilisha hesabu wakati wa kujaza mafuta baada ya kutumia kipimo cha paundi badala ya kilogramu hivyo ndege kupaa ikiwa na mafuta nusu tu ya yale yaliyohitajika kwa safari.
Ikiwa Nusu ya safari angani injini zikaanza kukosa mafuta na kuzima.
Ndege hiyo ya tani 100 ikageuka kuwa moja ya ndege kubwa isiyo na injini kuwahi kuelea angani (Giant Heavy Glider).
Bahati nzuri, Nahodha, "Captain" Robert Pearson alikuwa rubani mzuri wa ndege ndogo zisizo na injini (Glider) hivyo kutumia mbinu za ndege hiyo ndogo kuteremsha Boeing 767 kwa zaidi ya maili 72 bila injini.
Pearson alilenga uwanja wa kijeshi uliotelekezwa huko Gimli, Manitoba lakini kwa bahati mbaya ni kwamba, siku hiyo ilikuwa 'Family Day' na uwanja huo uligeuzwa kuwa uwanja wa michezo ya watoto na mbio za vigari.
Hata hivyo Pearson aliteremsha dubwasha hilo zito lisilo na Honi kimya kimya na kwa hesabu kubwa akitumia ujanja tofauti tofauti unaotumika kurusha ndege ya 'glider', kuelekea kwenye uwanja huo.
Kwa bahati nzuri baadhi ya watu waliweza kuona ndege hiyo iliteremka kuelekea walipo kimya kimya na kuanza kutawanyika pembeni.
Mara baada ya kutua gurudumu la mbele likavunjika na ndege ikateleza kwenye njia ikizalisha moshi na cheche.
Kwa bahati nzuri mwishowe ikaishia mita chache tu kutoka kwenye umati ulipojikusanya na kwa miujiza hakuna mtu aliyejeruhiwa vibaya.
Tukio hilo lilibaki katika historia kama "Gimli Glider" na video za tukio hilo zinapatikana mtandaoni kwa jina hilo.