Maana ya Usimulizi

Kasomi

JF-Expert Member
Sep 3, 2014
11,036
20,337
Maana ya Usimulizi

Ni dhana inayoelezea utoaji wa habari au hadithi kwa kutumia mdomo au maandishi.

Pia usimulizi huweza kuwa wa matukio mbalimbali kwa kuzingatia ufasaha wa Kiswahili yaani kiimbo, matamshi, sarufi na matumizi ya lugha

Aina za Usimulizi

(a)Usimulizi wa hadithi

(b)Usimulizi wa habari



Usimulizi wa Hadithi

Ni masimulizi yenye lugha ya mjazo(nathari) na mtiririko wake huwa sahihi na rahisi, mara nyingi masimulizi huwa mafupi.

Kuna sifa zinatambulisha utambaji wa hadithi jukwaani, sifa hizo tunaposoma hatuwezi kupata kitabuni, sifa hizo ni Sauti ya utambaji ambayo husikika moja kwa moja na utambaji wa matukio kwenye jukwaa.



MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA HADITHI



Kujua muundo wa hadithi –Hadithi huwa ina sehemu tatu Mwanzo, Kati na Mwisho

Mwanzo

Mwanzo wa hadithi hupaswa kuwaandaa wasikilizaji ili waweze kuwa tayari kusikia kile kinachotaka kusimuliwa.

Kwa mfano

Msimuliaji: Hadithi hadithi!

Wasikilizaji: Hadithi njoo uwongo njoo utamu kolea

Msimuliaji: Hapo zamani za kale

Wasikilizaji: Enheeeee(Wakiitikia)

Kati

Hadithi zote huelezwa kwa kifupi na kufuata mambo muhimu kwa maelezo ya moja kwa moja

Kwa mfano: Kuzaliwa….kukua…..kuoa.

Mwisho

Katika sehemu hii ya hadithi mara nyingi huonyesha mwisho wa kisa, kwa mfano kufa, kufanikiwa au kuharibikiwa. Mara nyingi huhitimishwa na maneno kama vile…….Na hadithi yangu ikaishia hapo.



Kisa kinachosimuliwa kinapaswa kuendana na maisha ya jamii husika



Kisa kinachosimuliwa kinapaswa kuendana na wakati.



Msimuliaji wa hadithi anapaswa kutumia lugha fasaha na matamshi sahihi ili wasikilizaji wapate kuelewa.



Mtumiaji atumie wahusika wanaoeleweka kwa wasikilizaji wake, Kwa mfano wahusika wanaweza kuwa wanyama kama vile sungura, fisi au twiga, Pia wanyama wanapaswa kupewa uhusika kulingana na matendo yao, kwa mfano sungura anawakilisha ujanja, simba anawakilisha ubabe na pundamilia anawakilisha uzuri



Msimuliaji anapaswa kutumia lugha ya picha ili aweze kuwavutia wasikilizaji wake, Kwa mfano; Simba alimtazama sungura kwa dharau…. Swala alikuwa anatembea kwa maringo…..simba aliponguruma ardhi yote ilitetemeka



Msimulizi pia anapaswa kutumia vitendo vya maigizo ili kuongeza uhai na msisimko katika hadithi inayosimuliwa, kwa mfano;sehemu ya hasira msimuliaji anapaswa kukunja sura ili kuonyesha hasira.



Msimuliaji pia anapaswa kupangilia matukio katika mtiririko unaofaa kuanzia mwanzo, kati na mwisho



SIFA ZA HADITHI SIMULIZI

Huhifadhiwa kwa kichwa na kutolewa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya masimulizi

Hadithi simulizi mara nyingi hutumia wakati uliopita. Kwa mfano Hapo zamani za kale au zama zile za mabibi na mababu

Hadithi simulizi huwa fupi na zenye kueleweka.

Hadithi simulizi hutumia wahusika kama vile wanyama pia huweza kutumia wanadamu.



DHIMA ZA HADITHI SIMULIZI

Huelimisha jamii, Husaidia jamii kuelewa mambo mbalimbali yaliyopo katika jamii yao

Kujenga jamii kwa kutoa maelezo m,balimbali kutoka kwenye hadithi

Hadithi husistiza ushirikiano katika jamii

Hadithi hurithisha busara toka kizazi kimoja kwenda kingine

Hadithi huburudisha jamii.



USIMULIZI WA HABARI

Ni maneno yanayotolewa na mtu au kundi la watu kuhusu jambo Fulani lililotokea au litakalotokea. Mara nyingi msimulizi wa habari huwa ni yule aliyeona tukio kwa mara ya kwanza au kusikia tukio likisimuliwa toka kwa mtu aliyeona kwa mara ya kwanza.



MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA USIMULIZI WA HABARI

Kutumia sauti inayosikika; sauti hutumiwa ili msikilizaji aweze kusikia na kuelewa vizuri kile kilichokusudiwa, Pia sauti huweka msistizo pale panapostahiki na kupambanua kauli.



Mpangilio mzuri wa mawazo; Huwezesha wasikilizaji kuelewa mtiririko wa habari au mawazo yanayotolewa



Kutumia lugha fasaha, msimuliaji anapaswa kumjua vizuri msikilizaji wake, wakati anaosimulia na mahali ili aweze kutumia maneno sahihi kulingana na wasikilizaji wake



Ni vizuri habari ikawa fupi ili isiwachoshe wasikilizaji.



Ni vizuri msimulizi kuwa na uhakika way ale anayoyasimulia, kwa kawaida kila habari huwa na ushahidi wa yale yanayosimuliwa.
 
Back
Top Bottom