*Kuthibitisha leo tuhuma za Baraza la Mawaziri
Na Grace Michael, Dodoma
MBUNGE wa Jimbo la Kigoma Kaskazini Bw. Zitto Kabwe, leo anawasilisha maelezo yake kuthibitisha kauli aliyoitoa bungeni akituhumu Baraza la Mawaziri kutoa maamuzi yanayotokana na ushawishi watu wenye nia ya kuua mashirika ya umma.
Tuhuma hizo alizitoa bungeni wiki iliyopita wakati akichangia azimio la kuongeza muda wa uhai wa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC).
Kutokana na tuhuma hizo, Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda alimpa muda wa siku saba ambazo zinamalizika leo, kuthibitisha kauli yake.
Akizungumza na Majira jana, Bw. Zitto alisema leo atawasilisha taarifa hiyo kwa Spika Makinda kama alivyoagizwa.
Katika mjadala huo, Bw. Zitto alipingana moja kwa moja na azimio hilo ambalo lilitaka kuongezwa muda wa miaka mitatu kwa CHC ambapo yeye alishauri liongezwe muda wa kutosha ili kukamilisha majukumu yake.
Hoja nyingine iliyomfanya apinge na kushikilia tuhuma hiyo kwa mawaziri, alisema kuwa maamuzi yaliyofikishwa bungeni yanatofautiana na makubaliano yaliyofikiwa katika Kamati ya Uchumi na Fedha.
Bw. Zitto aliwataka wabunge kukataa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kwa kuwa yametokana na kurubuniwa na watu wenye lengo la kuua CHC kwa ajili ya maslahi yao binafsi.
Alisema kuwa CHC ni chombo kinachoangalia mali za umma na mashirika, lakini pia kuna kesi mbalimbali za watu ambao wanadaiwa na mashirika, hivyo kwa kutoa muda wa mfupi ni kutaka kuua shirika hilo.
Shughuli zinazofanywa na CHC ambazo mpaka sasa hazijakamilika ni pamoja na urekebishaji wa TRL baada ya kampuni ya Rites kuondoka, kushughulikia uuzaji wa hisa za serikali NBC (T) Ltd, uhakiki wa mashirika yaliyobinafsishwa, urekebishaji wa mashirika 34 yaliyobaki na kukamilisha ufilisi wa mashirika ya umma 24 yaliyobaki, ukusanyaji wa madeni ya iliyokuwa NBC yenye thamani ya sh. bilioni 15.8 na urekebishaji wa kampuni ya TTCL baada ya hatua ya awali ya ubinafsishaji kushindikana na mwekezaji wa Airtel kuonesha nia ya kutoka katika ubia.