Asema kujiuzulu kwake kulimuumiza
na Kulwa Karedia
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyemaliza muda wake, Samuel Sitta, amesema alishtushwa na kuumizwa na uamuzi wa ghafla wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu.
Sitta alitoa kauli hiyo jana baada ya kutakiwa na gazeti hili kueleza ni jambo gani ambalo hatalisahau tangu alipoingia bungeni mwaka 2005 akiwa Spika wa Bunge.
Moja ya mambo ambayo sitayasahau katika maisha ya uspika wangu ni kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, unajua ni mchapa kazi, alishtua wengi ambao hawakuuamini uamuzi ule, alisema Sitta.
Kauli ya Sitta imekuja siku moja tu baada ya Lowassa kujitokeza hadharani na kueleza sababu ya yeye kuchukua uamuzi huo.
Akihojiwa na kituo cha Shirika la Habari Tanzania (TBC1) juzi usiku, alisema hulka yake ya kuwa tayari kuchukua maamuzi magumu pasipo kuhofia matokeo mabya ndiyo iliyomsukuma kushughulikia kwa ujasiri tatizo la mgawo wa umeme na sakata la Richmond, ambalo lilisababisha ajiuzulu.
Akizungumza na Tanzania Daima katika mahojiano maalumu kwa njia ya simu kutoka jimboni mwake, Urambo Mashariki, mkoani Tabora jana, Spika Sitta alisema siku hiyo hakuamini macho yake baada ya kuona Lowassa akilitangazia Bunge na taifa kuhusu uamuzi wake huo wa kuachia ngazi.
Nakwambia tangu nimekuwa Spika wa Bunge mwaka 2005, nimepitia mambo mengi mno, lakini kubwa zaidi ambalo siwezi kulisahau ni siku ile aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alipochukua uamuzi wa kutangaza kujiuzulu wadhifa wake, nilipatwa na mshangao, nilishtuka na sikuamini, alisema Spika Sitta.
Lowassa alilazimika kujiuzulu wadhifa huo baada ya kuhusishwa na tuhuma za rushwa katika Kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond mwaka 2007.
Spika Sitta alisema yeye aliamini kabisa katika kipindi hicho baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, sanjari na mtangulizi wake katika wizara hiyo, Dk. Ibrahim Msabaha, kungetosha serikali kuwajibika.
Mimi siku ile nilipoona wale wadogo (mawaziri), wamewajibika, nilielewa wazi kwamba imetosha, lakini baada ya siku kadhaa zilizofuata, mheshimiwa Lowassa naye akajiuzulu, kwa kweli, niliona ni maamuzi magumu aliyochukua,
sikujisikia raha kabisa
kwa vile mimi nafsi yangu huwa haimtakii mtu mabaya, alisema Spika Sitta.
Alipoulizwa mbali na tukio hilo, anakumbuka mambo gani mazito zaidi, Spika Sitta alisema ni mijadala motomoto iliyokuwa ikiwasilishwa na wabunge iliyosababisha akabiliane na changamoto nyingi.
Unajua pale bungeni kila mbunge anastahili yake ya kuongea au kuuliza swali, wakati mwingine anaweza kuanza kwa methali
hapo unatakiwa kuwa makini kweli kuwasilikiza, nawashukuru wote kwa michango yao motomoto, alisema Spika Sitta.
Alisema hata baada ya Mizengo Pinda kuteuliwa kushika wadhifa wake, waliendelea kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku bila tatizo.
Baada ya Mheshimiwa Rais kumteua Mizengo Pinda, tumeweza kushirikiana vizuri katika utekelezaji wa majukumu yetu bila tatizo, haya ni mafanikio makubwa, alisema Spika Sitta.
Kuhusu hali ya kisiasa jimboni mwake, Urambo Mashariki, Sitta alisema ni nzuri na ana matumaini ya kutetea kiti chake bila wasiwasi.
Hivi sasa niko jimboni nasubiri kesho (leo), kuchukua fomu ya kuwania kiti cha ubunge
hali ya kisiasa ni nzuri, naamini nitatetea kiti changu vizuri, tumuombe Mungu, alisema Spika Sitta.
Alisema hadi jana amesikia kuna wagombea wengine watano waliotangaza nia na leo wanatarajia kuchukua fomu ili kupambana naye kwenye kinyanganyiro hicho. Nasikia kuna wagombea wengine watano, lakini hawaonekani hapa, nitakutana nao huko huko, alisema Spika Sitta. Kufuatia kujiuzulu kwa Lowassa, mawaziri wengine, Naziri Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha nao waliachia ngazi, baada ya kuhusishwa na tuhuma za Kampuni ya Richmond.
juu