Lowassa si muumini wa ‘Janteloven’, anatufaa urais?

Komando Kipensi

JF-Expert Member
Jun 8, 2014
334
59
Niseme tu hapa kwamba walioisoma riwaya ya mwaka 1966 ya hayati Chinua Achebe ya A Man of the People (Mtu wa Watu), watanielewa nikisema hapa kwamba si kila mtu wa watu ni mtu wa watu kweli!

Watanielewa nikisema ya kwamba, kati ya hao wanaoitwa ‘watu wa watu' wapo pia ‘watu wa watu' wa sampuli ya Mh. Nanga kama ilivyosimuliwa na Chinua Achebe katika riwaya yake hiyo ya A Man of the People.

Niende mbali zaidi kwa kusema ya kwamba, hata hao waandishi wa habari waliofurahishwa na matokeo hayo ya utafiti wa Twaweza kuhusu Lowassa miongoni mwao wapo wa aina ya James wa gazeti la Daily Chronicle; kama ilivyosimuliwa na Achebe katika riwaya yake hiyo.

Labda niwe muwazi zaidi kwa kusema kwamba, binafsi, mpaka sasa sijakutana na wafuasi wa Lowassa, wakiwemo waandishi wenzangu, ambao wanamshabikia kiongozi huyo kwa sababu ya kuvutiwa na vision yake (kama anayo) ya namna ya kuikomboa nchi hii.

Kwa hakika, wengi niliokutana nao wala hata hawajui mtu wao huyo (Lowassa) anaelemea mrengo gani katika siasa za duniani hii – kulia au kushoto, kati kushoto au kati kulia.

Wao hilo haliwasumbui. Wanachojali tu ni mtu wao huyo (Lowassa) aingie Ikulu ili nao wanufaike kwa kuteuliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi kama vile u-DC, u-RC, ujumbe wa bodi za mashirika ya umma, ubunge wa kuteuliwa, ubalozi, ukatibu mkuu wa CCM nk!

Hisia zangu ni kwamba hata kwa wagombea urais wengine ndani ya CCM- hali ni hiyo hiyo. Yaani wanazungukwa na wafuasi na wapambe ambao hawajali kujua sera zao, vision zao, mirengo yao ya kisiasa nk; bali wanachojali ni kukamata tu Ikulu na kuanza kugawiana vyeo na njia za ulaji!

Wala hakuna wanaojali kuhoji kama wagombea urais wao hao wana mkakati wowote mpya unaotekelezeka wa namna ya kulitokomeza tatizo kuu linaloitafuna Tanzania ya sasa, na ambalo sasa limekuwa kansa sugu- - tatizo la kukithiri kwa ufisadi na mmonyoko wa maadili.

Huko nyuma nilishawahi kusema kwamba, hata mtu akiniamsha usingizini saa nane usiku na kuniuliza ni tatizo gani moja kuu linaloiangamiza Tanzania yetu kwa sasa, nitamjibu kuwa ni ufisadi na kuporomoka kwa maadili.

IPTL – ufisadi, ununuzi vipaza sauti bungeni – ufisadi, biashara meno ya tembo – ufisadi, ugawaji vitalu vya uwindaji – ufisadi, ujenzi maabara – ufisadi, uuzaji UDA na mashirika mengine ya umma – ufisadi, zabuni za halmashauri – ufisadi, uchimbaji madini – ufisadi, vyeo, chaguzi na nyadhifa – ufisadi, manunuzi ya umma – ufisadi, utoaji ajira – ufisadi, huduma za jamii kama elimu na afya – ufisadi, utoaji haki mahakamani – ufisadi, ujenzi wa barabara – ufisadi, utoaji ardhi za vijiji kwa wawekezaji - ufisadi; yaani ni ufisadi, ufisadi, ufisadi! Hata dini siku hizi ni ufisadi mtupu! Ninaposema ufisadi ni tatizo kuu la Tanzania kwa hivi sasa maana yangu ndiyo hiyo.

Ni kweli kuwa tuna matatizo mengi – kuanzia ya ukosefu wa ajira, elimu duni, kilimo duni, huduma duni za afya, miundombinu duni, ukosefu wa maji safi na salama kwa watu wetu, demokrasia changa, utawala dhaifu, nk, lakini, kwa mtazamo wangu, bado tatizo kuu linabaki kuwa ni ufisadi – kuporomoka kwa maadili.

Naamini hivyo kwa sababu, juhudi zote zinazofanyika na zitakazofanyika baadaye kutatua matatizo ya ukosefu wa ajira, elimu duni, kilimo duni, huduma duni za afya, miundombinu duni nk, zinakwazwa na zitakwazwa na kutamalaki kwa ufisadi katika kila nyanja ya maisha yetu.

Huo ndiyo ukweli. Kwa hiyo, adui wetu mkuu wa zama hizi ni ufisadi.

Na ndiyo maana, binafsi, nampima Lowassa kwa kigezo hicho, na sio wingi wa shule za sekondari za kata ambazo alisimamia kujengwa wakati akiwa waziri mkuu!

Kwangu mimi, tuhuma za ufisadi aliohusishwa nao katika kashfa ile ya Richmond ambayo kwayo alilazimika kujiuzulu uwaziri mkuu nazipa nafasi kubwa katika kumpima kama anafaa kuwa rais wetu mpya ajaye kuliko kuangalia idadi ya shule za sekondari za kata alizosimamia kujengwa nchini.

Hata kama nitaiweka tuhuma hiyo ya Richmond pembeni, na kujiuliza iwapo katika maisha yake yote ya kisiasa na nafasi alizoshika aliwahi kuibeba ajenda ya vita dhidi ya ufisadi, napata kigugumizi kutoa jibu la ‘ndiyo'.

Yaani sikumbuki ni lini Lowassa amewahi kukemea ufisadi nchini! Na kama miujiza itatokea na CCM kumteua awe mgombea urais wake, nitashangaa kama kwenye mikutano ya kampeni ataibeba ajenda ya vita dhidi ya ufisadi! Atathubutu?

And yet, ufisadi na kutoweka kwa maadili ndiyo tatizo kuu linaloitafuna nchi yetu kwa sasa. Kwa maneno mengine ni kwamba, bila kuchukua kwa makusudi hatua za kujenga utamaduni wa kuuchukia ufisadi sawa na ule wa Janteloven wa nchi za Scandnavia, hatutafika popote kimaendeleo.

Hatutafika popote kimaendeleo hata kama tutampata rais ‘mchapakazi' kama Lowassa mwenye uwezo wa ajabu wa kusimamia ujenzi wa sekondari mbili mpya kila mwezi katika kila wilaya nchini! Kama si muumini wa Janteloven, hatufai.

Dk. Kitila Mkumbo katika chambuzi zake za hivi karibuni, kwenye gazeti hili, kuhusu wasaka urais aliandika ya kuwa Lowassa ni mchapakazi lakini mwenye nakisi ya uadilifu!

Kama kweli Lowassa ni mchapakazi wa kiwango cha hali ya juu, ni jambo lenye ubishi linalojadilika. Lisilo na ubishi, hata hivyo, ni ukweli kwamba Lowassa ana nakisi kwenye kipimo cha uadilifu – labda kama kashfa ya Richmond au ile ya kusimamia uuzaji wa mali za AICC haina maana yoyote kwa anayebisha.

Na kama ana nakisi katika kipimo cha uadilifu (rejea vuguvugu lile la CCM la kumvua gamba yeye, Rostam na Chenge), huhitaji kuwa msomi wa elimu ya kurusha maroketi kujua kwamba Lowassa na Janteloven ni mbali kwa mbali – angalau mpaka sasa.

Ndiyo maana sitachoka kusema ya kuwa, kama atachaguliwa mwaka 2015 kuwa rais mpya wa Tanzania, kamwe hatawezi kuupiga vita ufisadi na kujenga nchini mwetu utamaduni wa ki-Janteloven kwa sababu si muumini wa utamaduni huo.

Na bila kuujenga utamaduni huo nchini na kuukomesha ufisadi uliotamalaki kila kona ya maisha yetu, siioni nchi yetu hii ikijinasua kutoka kwenye dimbwi la umasikini ilikozama, na wala siioni haki ikitendeka kwa wanyonge na masikini.

Janteloven ni nini? Janteloven ni utamaduni wa kuuchukia ufisadi. Utamaduni huo asili yake ni Denmark. Wenyewe wanauita utamaduni huo The Jante Law au kwa ki-Denishi "Janteloven".

Ni Janteloven hiyo ambayo kwa miaka kadhaa sasa imeifanya Denmark ishike nafasi ya kwanza katika nchi 10 bora duniani ambazo ufisadi ni wa kiwango cha chini mno, kwa mujibu wa vigezo vya Transparency International (TI); yaani Corruption Perception Index.

Sheria ya Jante au Janteloven (ki-Denishi) au Jantelagen (ki-Swedish) ni sheria ambayo haikuandikwa popote ambayo asili yake ni kitabu cha mtunzi wa kale wa Denmark aliyeitwa Aksel Sandemose.

Mwaka 1933 Sandemose aliandika kitabu cha riwaya kinachoitwa A Fugitive Crosses His Tracks (En Flyktning krysser sitt spor) ambacho kimezisaidia nchi za Scandnavia hadi leo kuuchukia ufisadi.

Riwaya hiyo ya Sandemose inahusu maisha ya jamii katika kijiji kinachoitwa Jante ambako walijiwekea utamaduni wa kuheshimu kanuni 10 ambazo kwa pamoja zinaunda hicho kinachoitwa The Jante Law.

Kimsingi, kanuni hizo zinazounda The Jante Law zinazungumzia saikolojia ya kuuchukia ubinafsi; saikolojia ya kuuchukulia utajiri uliopatikana kwa njia zisizo halali kuwa hauna maana (un-worthy) na si sahihi na haukubaliki (in-appropriate).

Katika riwaya hiyo, wakazi wa Jante waliovunja sheria ya Jante (ambayo kama nilivyosema, haikuandikwa popote) walitiliwa shaka na kuchukiwa. Mathalan; kama raia wa Jante aliweza kujenga jumba kubwa ghafla, alitiliwa shaka na inapobainika kwamba alilijenga kwa njia za dhuluma za aina yoyote, alichukiwa na jamii nzima.

Kwanza unatiliwa shaka, na ikibainika ni kweli mafanikio yako ni ya kifisadi, unachukiwa na jamii nzima. Mambo mawili yalikuwa muhimu kwa raia wa Jante inapotokea mtu akapata mafanikio ya haraka – kwanza shaka (suspicion) na kisha chuki (hostility).

Ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba Sheria ya Jante (kama ilivyo katika riwaya ya Sandemose), ilisaidia kujenga utamaduni wa kuuchukia ufisadi katika nchi ya Denmark miaka nenda rudi, na ndiyo maana haishangazi ripoti za TI zinaionyesha Denmark kuwa ni nchi yenye kiwango cha chini mno cha ufisadi duniani.

Leo hii, nikitafakari kuhusu Tanzania yetu, na jinsi tulivyozama katika ufisadi kuanzia kwenye siasa hadi kwenye miradi ya maendeleo nchini, kuanzia majumbani kwetu tunakoishi hadi kwenye nyumba zetu za ibada, nashindwa kuamini kwamba ipo siku nasi Tanzania tutaitwa "Nchi Iliyoendelea" (A Developed Nation).

Na ni kwa sababu ya kiu hiyo ya kutaka kuiona siku moja nchi yetu ikiitwa "A Developed Nation" sitamuunga mkono hata mara moja mgombea urais mwenye virusi vya kukumbatia ufisadi na mafisadi!

Daima nitawaunga mkono wagombea urais wanaonipa matumaini ya kuwa watasimamia nchini mwetu ujenzi wa saikolojia ya kuuchukia ufisadi (Janteloven).

Nasema hivyo, kwa sababu, kama nilivyoeleza mwanzo, -hilo ndilo tatizo mama linalotukwaza na litakalotukwaza na kuturudisha nyuma katika mipango yote mizuri ya maendeleo itakayopangwa baadaye.

Nihitimishe kwa kusema kwamba hata hao wagombea wengine wa CCM wanaochuana kwa karibu na Lowassa; yaani kina Membe, Pinda, Sumaye, Makamba, Wassira, Magufuli, Sitta nk, simuoni hata mmoja ambaye ni muumini kikwelikweli wa Janteloven. Simuoni hata mmoja anayemkaribia japo kidogo Mwalimu Nyerere au Sokoine au Thomas Sankara wa kule Burkina Faso kabla wana wa shetani hawajamuua.

Hakuna hata mmoja. Na hapo ndipo ninapokubaliana tena na mwalimu wangu wa somo la uraia, Profesa Kitila Mkumbo ya kwamba, waadilifu ndani ya mduara wa sasa wa CCM wa wataka urais, hawapo.

Na kwamba kama CCM watataka kutumia kigezo cha uadilifu kumpata mgombea urais wake kwenye uchaguzi wa mwakani, basi hawana budi ‘watoke nje ya boksi' kumpata mwana CCM MWADILIFU na muumini wa Janteloven ambaye hayumo katika mduara wa sasa wa utawala, na asiye na chembe ya kashfa ya ufisadi – hata ya kusingiziwa tu!

Naamini watu wa namna hiyo bado CCM inao. Kumbuka: Si kila ‘mtu wa watu' ni ‘mtu wa watu'. Tunao pia kina Mh. Nanga wa riwaya ya A Man of the People ya Chinua Achebe ndani ya nchi yetu.

Najua wapo wajinga watakaofikiri kuwa ninayaandika haya kwa kuwa labda najiona kuwa mimi ni mtu mwadilifu. La hasha. Wengi wetu ni waathirika wa namna moja au nyingine ya huu mmomomyoko wa maadili ninaouzungumzia; nami pia nikiwemo.

Ninachomaanisha, hata hivyo, ni kwamba tulioathirika tukae pembeni tusigombee uongozi wa juu wa umma, na badala yake tuwaachie waadilifu; maana hao wanaweza kutufikisha mahali pazuri katika safari hii ndefu na ngumu ya kushamirisha utamaduni wa Janteloven katika nchi yetu.

Chanzo: Raia Mwema
 
mtanunuliwa sana mwaka huu wandishi wengi hasa wasiojitambua kama huyu.
 
mtanunuliwa sana mwaka huu wandishi wengi hasa wasiojitambua kama huyu.
Mkuu, wenyewe waandishi na wamiliki wa vyombo vya habari wanasema kuwa huu ndo wakati wa mavuno. Wengine wanaulilia UDC
 
Mkuu, wenyewe waandishi na wamiliki wa vyombo vya habari wanasema kuwa huu ndo wakati wa mavuno. Wengine wanaulilia UDC
Kazi ipo, nimeshangaa sana kuona eti hata Mwandishi wa habari wa Tanzania Daima(mali ya mwenyekiti wa CHADEMA) anampamba LOWASSA
 
Back
Top Bottom