“Muda wa kuona Wagonjwa umekwisha, Wagonjwa wanataka Kupumzika” Aliingilia kati Maongezi hayo Mmoja kati ya Wale Madaktari Wawili waliokuwa wakimsukuma Martin kutoka Nje. Baada ya Kusikia Kauli hiyo, Wanafunzi wote walimuaga Angela na kuanza kutoka nje ya ICU.
***************
Nje ya ICU, Wanafunzi Walionekana wakitawanyika kila mmoja akielekea kwenye Geti Kuu la Hospitali hiyo, Walitembea kwa Makundi wakipita Gereza, Kituo Kikuu cha Polisi na Soko Kuu la Mkoa wa Iringa, wakielekea Stendi Kuu ya Daladala Ya Miyomboni kwa ajili ya Kurudi Chuoni.
Katika Msafara huo, Martin, Restuta na Master P waliongozana na kupanda Daladala Moja. Njia Nzima mpaka wanafika Chuoni, Martin alikuwa ni mwenye Mawazo sana. Walivyofika, Martin na Master P Walipitiliza Moja kwa Moja mpaka Chumbani kwao.
Martin alijitupa Kitandani kwa ajili ya Kupumzika huku Kichwani mwake akitafakari kila Kitu Kilichotokea.
Mawazo yake yalimpeleka Moja wa Moja mpaka Chumba cha ICU na Kumuona Angela akiwa kwenye Maumivu Makali amelala Juu ya Kitanda cha Hospitali. Aliendelea kujilaumu kufanya Mpango wa Kuonana na Maria kuwa Siri. Lakini zaidi Nafsi yake ilimlaumu Maria kwa Kufanya fujo.
Alijiona Mkosaji kwa kushindwa kumsaidia Angela Usiku wa Jana. Cha zaidi kilichomsumbua Martin ni kutaka Kujua ni nani aliyemwambia Angela kuwa alikuwa Uwanjani na Maria. Akiwa bado katika Dibwi zito la Mawazo, Hatimaye Usingizi ulimpitia.
Kwa Upande wa Restuta ilikuwa ni tofauti, Alivyofika hakwenda Bwenini kwanza, alipitiliza Moja kwa Moja kwenye Mgahawa wa Samaria uliopo Chuoni hapo, kwa ajili ya kuonana na Rafiki yake Maria ambaye alikuwa akimsubiri hapo Muda Mrefu kwa shauku ya kutaka kujua kilichoendelea Hospitali.
Maria alionekana kutokujali wala kuwa na hofu kwa kilichotokea, Kila akikumbuka Maumivu aliyopata yeye kwa Miaka yote kwa Kukosa Upendo wa Baba Yake, aliona Angela alistahili Maumivu tena zaidi ya yale.
Kwa wakati huo Kichwani mwake aliwaza Vitu viwili tu, Baba Yake Mch. Moses endapo angejua Kilichotokea na Pia Aliwaza Namna ya kuwa Karibu tena na Martin. Alijua kuwa Martin hakupendezwa na Kilichotokea Hivyo aliwaza Mikakati ya Kurudi tena Kwake. Kwa hivyo alipanga kutumia Ugomvi huo kati ya Martin na Angela kujisogeza zaidi kwa Martin.
Restuta alivyofika pale alimkuta Maria akiwa amekaa peke yake kwenye Meza Yenye Viti Vinne akinywa Juice, Maria alipomuona Restuta, alisimama na Kumkumbatia rafiki yake huyo kwa nguvu.
“Pole Mama” Alisema Restuta huku akimpapasa Maria Mgongoni.
“Nishapoa” Alijibu Maria.
Wote wawili walikaa na Restuta kufungua Maongezi kwa kuanza kwa kumuelezea hali ya Mgonjwa na hatimaye kumhadithia Kila kitu kilichotokea Hospitalini, alimuelezea Dokta alivyosema Wote Wanaruhusiwa kwenda Kumuona mgonjwa Isipokuwa Martin na Maria, Alimuelezea kuhusu Zawadi ya Maua Aliyopewa Master P Apeleke na kukataliwa.
Alimuelezea Jinsi Martin alivyofungua Mlango wa ICU kwa Nguvu na Jinsi Madaktari walivyomzuia na kumuachia baada ya Angela kusema aachiwe. Kwa Kifupi, Restuta alimuelezea Maria kila kitu kilichotokea Hospitali Siku hiyo mpaka Jinsi Angela alivyokataa Kumsamehe Martin.
“Kwa hiyo Angela aliwaambia Madaktari kuwa Mimi na Martin tusiruhusiwe kwenda Kumuona” Aliuliza Maria.
“Itakuwa Hivyo” Alijibu Restuta.
“Angejua kuwa Sina hata Mpango wa Kwenda Kumuona wala asingejisumbua Kutaja Jina langu kwa Hao Madaktari”
“Ndiyo Hivyo Shoga”
“Ila Ahsante kwa Kila Kitu Rest, najua nimekuchosha sana” Alisema Maria.
“Usijali Shoga, Kilichonifurahisha zaidi ni kuona Jana haukuniangusha hata Kidogo”
“Usiniambie kuwa Nilifanya Kila Kitu kama tulivyopanga”
“Sasa Je, Shoga wewe ni Muigizaji Mzuri Kumbe, Maana sio kwa macho yale uliyokuwa ukiniangalia bado kidogo tu Nicheke”
“Shoga angu we acha tu kumbe Waigizaji wana Kazi”. Wote Wawili walicheka.
“Wanakazi tena si Kidogo ila hakikisha unamaliza Mpango wetu wa Mwisho wa kukutana na Martin na kumuomba Msamaha kwa Kilichotokea ” Alisema Restuta.
“Siwezi Kusahau Shoga” Alisema Maria
****************
Ndani ya Jiji la Dar es Salaam Justine alionekana kufurahia maisha yake mapya. Aliendelea Kuosha Vioo Vya mbele vya Magari yaliyosimama katika Mataa ya Ubungo, Taratibu aliendelea Kujifunza Maisha ya Watu wa Mjini. Na muda wa Mapumziko akiwa na Sule, aliweza kutembelea maeneo ya Karibu kama Ubongo River Side, Kituo cha Daladala Cha Mawasiliano na Sinza Kijiweni.
Katika Siku hizo Chache Justine aligundua kuwa Buda Kazi yake haikuwa tu Kukusanya Ushuru bali alikuwa na Biashara nyengine aliyofanya kwa Siri Kubwa.
Muda mwingi Buda alionekana akiwa amesimama pembeni ya Barabara, kuna Gari Binafsi za watu zilifika kwa muda tofauti tofauti na kusimama Karibu yake, Buda aliingia ndani, kuna kitu alifanya kisha alishuka Nje ya Gari na kusimama tena kusubiri Gari nyengine ifike.
Kwa Siku zilifika pale Gari zaidi ya Ishirini na Zote Buda aliingia ndani na kushuka. Alishuka Muda mfupi baada ya kumaliza kuzungumza na watu hao.
Ukweli Justine hakugundua Buda alifanya Biashara gani na hao watu waliokuwa wakimfuata pale kila Siku na Magari yao. Isipokuwa alichogundua ni kwamba Magari yote yaliyofika pale, kwenye Vioo yaliwekwa Tinted na hakuna hata Gari Moja ambalo Dereva alithubutu hata kushusha Kioo. Hivyo Justine hakuweza kuona sura hata ya Mtu Mmoja kati ya waliofika pale kuonana na Buda.
Alitamani kujua Biashara aliyofanya Buda kwani ilionekana kumuingizia Pesa Nyingi na ndiyo maana aliweza kumudu kupanga Chumba eneo la Magomeni tofauti na Vijana wengi wa pale ambao kuna wengine walikosa hata Pesa ya kula.
Alikuwa na Shauku ya kufahamu lakini aliona ni mapema sana kuanza kumuuliza Maswali kama hayo. Justine aligundua pia Buda alionekana kuwa ni Mtu Muhimu sana kwa watu hao sababu baadhi ya Watu walivyofika na kumkosa, waliondoka na kurudi tena Baadae bila kuchoka.
Katika Gari zote zilizofika eneo hilo, Justine aliikariri Range Rover Moja Nyeusi ambayo ilionekana kufika hapo Asubuhi na Jioni Kila Siku. Na Kitu kingine kilichofanya aikariri kwa urahisi Gari hiyo ni Muda Mwingi aliotumia Buda kila Alipoingia ndani ya Gari hiyo tofauti na Muda aliotumia kwenye Magari mengine yaliyofika hapo.
Kama ilivyokawaida, Giza lilipoanza kuingia Vijana wote walikusanyika na Kila mmoja kumpatia Buku Buda kisha walianza safari ya kuelekea Kilima Hewa Pub. Justine alikuwa na hamu kubwa ya Kuonana na Patra Usiku huo. Na hayo ndiyo yalikuwa Maisha yao.
*************
Siku iliyofuata Asubuhi na Mapema, kabla ya Muda wa kwenda Darasani kufika, Akiwa bado amelala Kitandani, Martin aliamshwa na Sauti ya Maria. Maria alivyomaliza Kujiandaa kwa ajili ya kwenda Darasani aliona apitie kwanza moja kwa moja Bwenini kwa Martin. Alipitiliza mpaka kwenye chumba cha Martin, alivyogonga Mlango na kuona kimya aliingia ndani na kumkuta Martin akiwa bado amelala. Alimkuta Martin akiwa peke yake Chumbani, Taratibu alikaa pembeni yake na kumuamsha.
“Martin” Aliita Maria kwa Sauti ya Upole huku akimtingisha Bega lake la Kulia.
“Maria umefata nini tena” Aliuliza Martin alivyofumbua macho na kumuona Maria.
“Amka,Kuna Kitu Nataka kuongea na wewe”
“Kitu gani kama ni kuhusu kilichotokea Juzi sipo tayari kwa sasa nataka kupumzika” Aliuliza Martin kwa sauti ya Uchovu.
“Nimekuja kuomba Msamaha”
“Anaestahili kuombwa Msamaha ni Angela sio Mimi”
“Angela nitazungumza nae lakini nimeona nizungumze na wewe kwanza” Maria aliongea kwa Sauti inayotia huruma.
“Kwa nini ulisema uongo”
“Nilijikuta tu nasema vile, Nisamehe Martin”
“Nataka kujua lengo la kufanya yote yale”
“Ni Hasira tu Martin, Sikutegemea kumuona Angela na Restuta pale kwa hiyo nilishtuka sana nikajikuta nafanya mambo ambayo sikutarajia” Alijitetea Maria.
“Bado sio sababu ya kufanya fujo” Martin alisema huku akiwa anakaa vizuri Kitandani.
“Ukweli ndio huo Martin”
“Wakati Mnarushiana maneno ulisema unamchukia Angela kwa sababu amekusababishia Maumivu katika Maisha yako yote, ulikuwa una maanisha nini??” Aliuliza Martin
“Hakuna Kitu Martin zilikuwa ni Hasira tu”
“Kuna Kitu unanificha”
“Hakuna kitu, kingekuwepo ningekwambia”
“Sawa”
“Sawa umenisamehe? ” Aliuliza tena Maria
“Nikusamehe kwani mimi ndiye uliyenikosea”
“Kwa hiyo hauna hasira na Mimi, tutawasiliana kama kawaida”
“Sina hasira na wewe ila kuwasiliana hapana”
“Kwa nini Martin”
“Sitaki kurudia Kosa”
“Kwani Mtu kuwasiliana na shemeji yake ni makosa jamani”
“Angela akijua atakasirika sana na sitaki kumuudhi tena”
“Atajuaje kwa mfano labda Umwambie tena” Maria alisema na kutabasamu
“Nimwambie tena nini”
“Kama Ulivyomwambia kuwa tulikuwa pale uwanjani”
“Halafu umenikumbusha, Ni nani aliyemwambia Angela kuwa tulikuwa pale”
“Si wewe ndo ulimwambia”
“Nani Mimi, nimwambie Angela ili iweje”
“Martin acha utani wako, nani mwengine wa kumwambia Angela kama sio wewe”
“Sikumwambia Angela”
“Kweli Martin??”
“Ndiyo, Ningefanya hivyo nisingekuuliza”
“Sasa hatakua nani aliyemwambia, Maana mimi nilifikiri wewe baada ya kunitumia Ujumbe wa Kutaka tuonane ukaona umwambie na Angela au kuna mwanafunzi alituona pale akaenda kumwambia Angela”
“Nitamuuliza Angela mwenyewe”
“Sawa, kwa hiyo tutaendelea kuwasiliana”
“Hata Sijui”
“Jiandae Basi twende Darasani” Alisema Maria.
******************
Baada ya Siku Tatu, Angela aliruhusiwa kutoka Hospitali na kurudi Chuoni Kuendelea na Maandalizi ya Mitihani yao ya Mwisho (University Examination) ambayo ilipangwa kufanyika Wiki Inayofuata, akiwa mwenye Afya Njema. Maria Alitumia Bima yake ya Afya kufanya Malipo ya Matibabu yake yote na kuanza utaratibu wa kurudi Chuoni akiwa amesindikizwa na Restuta.
“Asante sana Rest, wewe kwangu ni zaidi ya Rafiki, sijui bila wewe ningefanya nini” Alisema Angela wakati wanatoka Hospitalini.
“Usijali, Ni wajibu wa Marafiki kusaidiana” Alijibu Restuta.
Katika siku zote hizo Tatu, Martin alikwenda Hospitalini kumuangalia bila Mafanikio kwani Madaktari waliendelea kumzuia kuingia kwa madai ya kwamba mgonjwa hakutaka kuonana nae.Ukweli ni kwamba, Angela alikuwa bado ana hasira hivyo hakutaka kuonana na Martin wala Maria.
Kwa Upande wa Maria wala hakujisumbua kutaka kwenda Hospitali kumuona mdogo wake, aliendelea kupata taarifa zote kutoka kwa Restuta ambaye ndiyo Mtu Pekee aliyeruhusiwa kwenda kumuona Angela mara kwa mara.
Wakati wote huo, Mch Moses hakuna alichojua, Angela aliamua kukaa kimya kwa sababu alijua ambacho kingetokea iwapo Mchungaji angepewa taarifa ya tukio hilo. Angela hakutaka kuwa chanzo cha Familia hiyo kugombana. Aliamua kutosema Chochote.
Siku iliyofuata wakiwa wapo katika Ukumbi wa Multi-Purpose wanasoma, Katika Darasa la Wanafunzi zaidi ya 200, lakini Macho ya Martin muda mwingi yalitua kwa Mwanafunzi Mmoja tu kwa wakati huo ambaye ni Angela. Angela hakutaka kukaa karibu na Martin wala Maria, hivyo aliamua kukaa na Restuta, Nyuma Kabisa ya Ukumbi huo.
Licha ya kwamba Mwili wake Martin ulikuwa Darasani lakini Akili yake ilikuwa mbali, kilichomkosesha zaidi furaha ni kutokana na stori zilizoenea Chuoni kwamba Martin kafumaniwa na Shemeji yake. Alitamani angekuwa na uwezo wa kubadilisha mawazo yao lakini hakuweza.
Mwalimu wa Somo la ‘Advanced Public Relations and Advertsing’ Madam Edna Mwaipopo, alivyomaliza kufundisha na wanafunzi kuanza kutoka Nje ya Ukumbi, Martin alisimama na kwenda nyuma kumfuata Angela ambaye alikuwa bado hajanyanyuka kwenye Kiti chake.
“Angela” Martin aliita kwa Sauti ya Chini.
“Unasemaje” Alijibu Maria huku akisimama.
“Naomba Kuongea na wewe”
“Ongea nakusikiliza” Alisema Angela huku akitoka Nje ya Ukumbi akiwa ameambatana na Restuta.
“Sio hapa, naomba kama una muda tutafute sehemu tukae tuongee”
“Sina Muda” Angela alijibu kwa Mkato.
“Najua bado una hasira lakini naomba tukae tuzungumze”
“Wala sina hasira, Nilishakwambia Sitaki kuonana na wewe” Angela alisema hayo huku akipandisha ngazi kuelekea Maktaba ya Chuoni hapo. Restuta alikuwa pembeni, Muda wote alionekana akichati kwenye simu yake.
“Baby usiseme hivyo”
“Nani Baby wako, tena nisikusikie tena ukiniita hivyo” Angela alisema kwa sauti ya Ukali
“Nataka kujua ni nani aliyekwambia kuwa Mimi na Maria tulikuwa pale Uwanjani”
Martin alivyouliza swali hilo, Angela na Restuta walitazamana na Kisha Angela akamgeukia tena Martin.
“Unataka Kumjua ili ufanye nini, kwani alikusingizia haukuwa pale na Maria”
“Hapana nataka tu kumjua”
“Siwezi kukwambia”
“Nisamehe kama nimekosea”
“Nilishakusamehe ila Sitaki kukuona” Angela alijikaza kusema maneno hayo huku moyo wake ukiumia.
“Siwezi kuishi bila Kukuona Angela”
“Usijali Maria atakufundisha kuishi bila Mimi” Alisema Angela na Kisha kuingia ndani ya Maktaba na Restuta, wakimuacha Martin akiwa bado hajamaliza alichotaka kuzungumza.
“Martin” Ghafla Martin akiwa bado yupo pale Nje ya Maktaba alisikia akiitwa na Maria. Kumbe Muda wote Ule wakati Martin na Angela wapo katika Mazungumzo, Maria alikuwa amesimama kwa Mbali akiwasiliana na Restuta, kuhusu kilichokuwa kikiendelea Pale.
“Unasemaje Maria” Martin alimuuliza.
“Twende tukasome Mitihani Inakaribia” Alijifanya kama hajui Kilichotokea.
“Toka Lini tumeanza kujisomea Pamoja” Aliuliza Martin.
“Kwani kuna ubaya tukianza kufanya hivyo leo”
“Maria niache kwanza sipo sawa” Alisema Martin
“Ok ngoja nikuache ukiwa sawa utaniambia” Maria alisema na kuondoka Mahala Pale.
Huo ulikuwa ni Mkakati mwengine kati ya Maria na Restuta, wenye lengo la kumzidishia Hasira Angela. Walijua kuwa endapo Angela angewaona Martin na Maria wakiwa Pamoja tena, lazima hasira zingezidi. Na hilo walifanikiwa, kwani Angela akiwa ndani ya Maktaba, kupitia Madirisha Makubwa ya Vioo vya Maktaba hiyo aliweza kuwaona Martin na Maria wakiongea pale nje. Licha ya kwamba hakuweza kusikia neno hata moja waliloongea lakini kitendo cha kuwaona wakiwa pamoja, Kilimuumiza.
Kufuatia Tukio hilo na Lile lingine, Angela na Martin, hawakuweza kuzungumza tena kwa Upendo na Furaha kama ilivyokuwa zamani. Hasira zilitawala katika Maongezi yao. Kila Martin alivyotaka kuongea nae, Angela alimrushia Maneno Makali.
Angela kila akikumbuka Kilichotokea na maneno mengine mengi aliyoendelea kuambiwa na Restuta, alishindwa kumsamehe Martin na wala hakutaka kumuona tena. Mpaka wanafanya Mitihani yao ya Mwisho ya Kumaliza Chuo na kuondoka Kila Mmoja kurudi Nyumbani, bado Martin na Angela walikuwa hawana Mawasiliano mazuri.
Angela, Maria na Restuta walirudi Dar es Salaam, Martin alirudi Kijijini kwao Kalenga kwa Wazazi wake bila kujua Ni Nani aliyemwambia Angela kuwa alikuwa Uwanjani na Maria. Rafiki yake, Master P alirudi kwao, Naivasha Nchini Kenya.
Hatimaye Kila Mmoja aliendelea na Maisha yake.
STOLEN LOVE