Kuja kutahamaki, Maria alimsukuma Angela hadi akadondoka chini na Kichwa chake kujigonga kwa nguvu kwenye Jiwe lililopo karibu yake na kupoteza fahamu.
“Ameua” Walisema kwa Mshtuko baadhi ya wanafunzi waliokuwepo katika eneo lile, baada ya kuona Angela akitokwa na damu nyingi kichwani.
******************
Kila inapofika Majira ya Jioni mara baada ya kumaliza kazi yao ya kuosha Magari Vijana hao huwa wanajikusanya pamoja na Vijana wengine wanaofanya Biashara ndogo ndogo katika eneo la Ubungo kisha kila Mmoja humpatia Buda Kiasi cha Shilingi Elfu 1 kama Ushuru wa kutumia eneo hilo na huwapatia Risiti.
Ukweli ni kwamba Pesa waliyomlipa Buda sio Ushuru wa Serikali kama Buda alivyowadanganya, hata Risiti alizowapatia ni za kugushi, hazikuwa halali. Pesa waliyompatia iliishia Mifukoni mwake. Kijana yeyote aliyekataa kufanya hivyo Siku ya Pili, Buda kwa Ubabe wake hakumruhusu kuendelea tena kufanya Biashara katika Eneo hilo. Vijana wote walimuogopa Buda.
Wakimaliza Kumpatia Buda Pesa hizo Vijana hao huwa hawakumbuki hata kwenda kusafisha miili yao, wanachofanya ni kuongozana na Buda kuelekea moja kwa moja kwenye Kilabu cha Pombe za kienyeji maarufu maeneo ya Manzese kiitwacho “Kilima Hewa Pub”.
Jioni ya Siku hiyo, Justine alikuwa miongoni mwa vijana hao waliokuwepo ndani ya Kilima Hewa Pub wakinywa Pombe za Kienyeji na Kucheza Muziki. Mkononi akiwa ameshikiria vizuri Mfuko wake wa Sandarusi, Macho yake yalitazama kila Pembe ya Kilabu hicho, macho yake yaliona jinsi Paa la Kilabu hicho lilivyochakaa.
Licha ya Uchakavu wa Banda hilo, lakini Justine alionekana kuvutiwa sana na mazingira hayo, alivutiwa na jinsi watu walivyochangamka katika eneo hilo. Muda mwingi Justine aliutumia kuyasoma mazingira hayo.
“Mama Patra ongeza nyengine” Kwa sauti ya Kilevi alisema Buda huku akimwangalia Justine usoni.
“Leta Pombe Mama Patra”Alidakia Sule.
“Jamani Naleta ” Alisema Mama Patra huku akicheka. Licha ya unene Mkubwa aliokuwa nao Mama Patra lakini alikuwa shapu katika kuwa hudumia wateja wake.
“Fanya Haraka, tupo Bungeni lazima vikao viendelee, unafikiri sisi tumekuja Bungeni kulala, tumekuja kufanya kazi, Lete Vyombo” Alisema Buda aliyeonekana kulewa zaidi kuliko mwenzake na Kisha alimgeukia Justine
“Mdogo wangu kama nilivyokwambia Mchana, usiwe Mnyonge, hapa nyumbani, hata ukitaka Mwanamke unapata,Yule pale anaitwa Mama Patra, shemeji yako ila kama ukitaka kula ruska, wewe tu na roho yako” Alisema Buda huku akiweka sawa Vitabu vyake vya Risiti Mfukoni.
Justine alitabasamu.
“Mama Patra leo tumekuja na Mgeni” Alisema Sule.
“Mgeni karibu, hapa ndo Manzese Kilima Hewa, kwa Mama Patra, Patra mwenyewe Yule pale anahudumia wateja” Alipofika hapo Mama Patra alimtazama Binti yake na kisha akamwita
“Patra ukimaliza kuhudumia wateja njoo umsalimie Mgeni”Alisema Mama Patra huku akiwamiminia Buda na Sule, Pombe aina ya Gongo.
“Pombe yako ya Leo hatari sana”Alisema Buda
“Siku zote Pombe yangu nzuri” Alisema Mama Patra huku akiondoka kuelekea kwenye eneo analohifadhia Pombe zake.
“Ya Leo imezidi Mama Patra” Alidakia Sule.
Haikupita Muda, Patra akawa amefika kwenye meza ile. Licha ya kwamba kulikuwa na Giza kwa mbali lakini waliweza kuonana.
“Mambo Mgeni” Patra alimsalimia Justine
“Poa tu” Alijibu Justine
“Kila siku nakwambia Unatakiwa Kupiga Magoti unapomsalimia Mwanaume” Alidakia Buda.
“Usijali nitapiga Magoti siku nyengine, Mgeni Unaitwa Nani?”
“Naitwa Justine”
“Karibu sana, Mimi naitwa Patra”
“Nimeshakaribia”
Japo walikuwa wamelewa lakini waliweza kuongea mengi. Justine aliwaelezea wenzake historia ya Maisha yake. Aliwaeleza matukio ya Ukweli na Uongo ilimradi kunogesha maongezi. Mara kadhaa rafiki zake walisikika wakicheka.
Kwa Upande wa Buda na Sule hawakusita kumueleza Justine Mpango wao wa muda mrefu wa Kwenda Nchini Africa Kusini baada ya Mwaka Mmoja, kwa lengo la kutafuta Maisha nchini humo. Kwa kuwa Buda ilikuwa sio mara yake ya Kwanza kwenda Afrika Kusini, alikuwa na Rafiki yake huko, walipanga Kufikia kwake. Walimueleza Jinsi walivyochanga Pesa zao kwa ajili ya Kupata nauli na Pasi ya Kusafiria (Passport) kwa Ajili ya Sule.
Ilipotimu saa tisa Usiku, Justine na rafiki zake hao wapya waliondoka Kilima Hewa Pub na kuelekea upande wa Kaskazini, walipita vichochoro viwili vitatu, wakakutana na barabara iendayo moja kwa moja mpaka eneo la Manzese Darajani. Walitembea huku wakipepesuka. Njia nzima, walisikika wakiimba nyimbo walizozijua wenyewe.
Walipofika Kwenye Daraja la Manzese Buda alivuka Barabara na kupanda Daladala iliyompeleka Magomeni alikokuwa anaishi. Sule, Justine na Vijana wengine walianza kupandisha ngazi kuelekea juu ya Daraja.
Justine akiwa juu ya Daraja alitazama vizuri Mandhari ya Jiji, alitazama Magari yaliyokuwa yakipita.
Ilikuwa ni Usiku lakini kwa jinsi watu walivyokuwa wengi barabarani utafikiri kuwa ni Mchana. Daladala zilionekana zikifanya kazi zake kama kawaida. Moyo wake ulifurahi.
Justine alivyoangalia vizuri, alishangaa kuona vijana wengi wamelala juu ya lile Daraja. Aliona jinsi Uchafu ulivyozagaa katika eneo lile, ulioambatana na Harufu Kali ya Mikojo. Hakutaka kuamini kama kuna watu wamegeuza Daraja hilo kuwa Makazi yao.
Wengi waliolala pale walionekana ni watu wasiokuwa na shughuli maalumu ya kuwaingizia kipato, wahuni na Mateja. Ili kujikinga na Baridi la Usiku pamoja na Mbu, Wengi wao walionekana kujifunika Maboksi, wengine Mifuko ya Rambo, Matambala na wengine hawakujifunika kitu na hawakujali.
Wakati akiendelea kushangaa zaidi, na kudhani kuwa hapo Darajani walikuwa wanapita njia, Ghafla aliona wenzake aliopanda nao juu ya Daraja hilo, wakina Sule na wengine wakilala kwenye sakafu ya Daraja hilo.
“Kumbe tumefika” Alijisemea Justine Kimoyo moyo.
“Justine Karibu Mjini Hapa ndiyo Nyumbani Kwetu” Alisema Sule huku akionekana akiingiza mkono wake wa kulia Mfukoni na kutoka ukiwa umeshikilia Pakti ya Pombe maarufu kama Kiroba, akanywa, alipomaliza akachukua kipande chake kirefu cha Gunia kilichotengenezwa kama shuka akajifunika, haikupita muda usingizi ulimpitia.
Justine hakuwa na jinsi zaidi na yeye kulala katika eneo lile, tena bila hata ya kitu cha kujifunika. Alikumbuka alivyotoka Kijijini kwao hakuchukua Shuka.
Alisikia Sauti za Mbu wakiimba nyimbo mbalimbali na kisha walianza kumshambulia. Kelele za Magari yaliyokuwa yakipita chini ya Daraja zilimsumbua, mara kwa mara zilikatisha usingizi wake.Yote hayo yalikuwa mageni kwa Justine, Licha ya ulevi aliokuwa nao Kijijini kwao lakini hakuwai kulala nje nyakati za usiku kama hivi, tena Juu ya Daraja.
Hatimaye usingizi ulimpitia. Na Hivyo ndivyo, Jiji la Dar es Salaam lilivyomkaribisha Justine.
************
Wakati Martin anapanga namna atakavyokutana na Maria Kwenye Uwanja wa Mpira wa Kikapu, wazo lake la kwanza Lilikuwa ni kumtumia Ujumbe wa Maneno kuelezea ombi lake hilo.
Wakati Ujumbe huo wa maneno unaingia kwenye simu, Maria alikuwa na rafiki zake katika Mgahawa mmoja chuoni hapo ujulikanao kwa jina la Samaria.
Baada ya Maria kusoma ujumbe ule hakuamini kama kweli Martin alitaka waonane. Alijua malengo yake ya muda mrefu yanatimia. Ilikuwa ni furaha isiyona na kifani kwake. Aliwasomea Rafiki zake ujumbe ule nao hawakuamini. .
“Shosti Martin anakuitia nini tena” Aliuliza Restuta
“Hata Sijui shoga angu ila nitakwenda kumsikiliza”
“Ndo utumie nafasi vizuri” Alisema Restuta
“Mimi tena” Alisema Maria
“Sio unafika mtoto wa kike macho makavu, Mtoto wa kike sharti macho uyalegeze”
“Haya endelea kunipa maarifa” Alisema Maria
“Halafu Tufanye hivi, ukiwa umeshaonana na Martin niambie ili nimlete Angela tujifanye kama tumekuja kufumania”
“Jamani sitaki vurugu kabisa, nataka tuwe wenyewe wawili tu”
“Vurugu gani? Kwa taarifa yako Angela akiwafumania kwanza hatoamini macho yake, Pili, Wataachana”
“Mnachotaka kufanya sio vizuri” Kwa sauti ya Upole aliingilia kati mazungumzo hayo rafiki yao mwengine aitwaye Maimuna, ambaye muda wote alikuwa kimya akiwasikiliza.
“Huyu nae vipi? Ndo kujifanya Mlokole sana au!” Aliuliza Restuta
“Achana nae hujamzoea tu” Alidakia Maria.
“Basi ndo hivyo shosti,hakikisha Martin unakuwa nae karibu kabisa tena kama utaweza Angela awakute mmekumbatiana kabisa ili roho imuume zaidi”.
Baada ya kumaliza kupata chakula walisimama na kuelekea Bwenini kupanga vizuri mikakati yao ya kumnasa Martin huku wakimwacha Maimuna peke yake Mezani. Hawakujali walisimama na kwa mwendo wa madaha waliondoka zao.
Maria na Restuta walipofika Bwenini waliendeleza mipango yao na hatimaye Muda ulipofika Maria hakufanya makosa, alihakikisha anavaa vizuri na kupendeza kama alivyoshauriwa na rafiki yake, alivalia suruali yake yenye rangi ya blue na Shati lake analolipenda kuliko yote lenye rangi ya damu ya Mzee kisha akajipulizia marashi, akatengeneza nywele zake vizuri akisaidiwa na Restuta, tayari kwa ajili ya kwenda kuonana na Martin.
Ukweli kama ungepata bahati ya kuonana na Maria siku hiyo, usingeweza kujua kama kweli mwanamke huyu alikuwa Mkubwa kiumri kumzidi Angela na Martin, ungeweza kudhani wote wanalingana.
Maria hakutaka siku hiyo ipite bila kuandika historia katika Maisha yake. Maria alipanga kutimiza ndoto yake ya muda mrefu ya Kumchukua Mtu yeyote anayempenda Angela kwa lengo la kulipiza Kisasi. Alipanga kuona Angela anaumia kama yeye alivyoumizwa .
“Usiniangushe” Hayo yalikuwa maneno ya Mwisho ya Restuta wakati anaagana na Maria.
SEHEMU YA TATU
Patricia Kiga Joseph ni Binti Mcheshi na Mpole, aliyelelewa Katika kituo cha Serikali cha kulelea watoto yatima na wenye ulemavu kiitwacho Hope Orphonage Center (HOC) kilichopo Buguruni Kwa Mnyamani.
Uzuri wa asili, macho Makubwa ya Goroli pamoja na vishimo vidogo vidogo vilivyopo mashavuni mwa binti huyu vinamfanya kupendeza zaidi na kusababisha watu wengi kushindwa kuamini kama kweli ni Yatima.
Baba yake Mzazi Patricia aitwaye Kiga Joseph, alifika Nchini Tanzania kutafuta Maisha miaka ya 1990 akitokea Lilongwe nchini Malawi na Baadae kupata Mwanamke wa Kitanzania aitwaye Veronica Ndema, aliyeanzisha nae Maisha kwa kupanga Chumba kimoja eneo la Buguruni, Malapa na Hatimaye kupata watoto wawili Mapacha wa Kike, Mkubwa aliitwa Patra na Mdogo aliitwa Patricia. Watoto hawa Mapacha walifanana sana kiasi cha Watu kushindwa kuwatofautisha kirahisi.
Kabla ya Umauti kumfika, Baba yao alikuwa ni Dereva wa Malori ya Mizigo na kifo chake kilitokana na kushambuliwa kwa risasi na Waasi wa Kikundi cha Allied Democratic Forces (ADF) wakati akielekea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Alishambuliwa na Waasi waliotaka kupora Chakula, Mafuta na Mizigo mingine iliyomo kwenye gari yake katika eneo la Mkoa wa Kivu Kaskazini nchini humo.
Kutokana na Ugumu wa Maisha ulioikumba familia hiyo baada ya Baba Yao kufariki, Dada yake Patra alichukuliwa na kwenda kuishi kwa Mama Yake Mkubwa.
Ugumu huo wa Maisha na Maradhi mbalimbali yaliyomsumbua, Mama Yake Patricia alilazimika kuwa OmbaOmba katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi karibu na Daraja la Sarender ili kuweza kupata Pesa ya Kula na Mwanae.
Wakati akifanya shughuli hiyo ya Kuomba Omba, alikuwa akimuweka Mtoto wake Patricia aliyekuwa na Miaka 8 pembeni ya Barabara sehemu yenye Kivuli na Yeye kuingia Barabarani kuomba Msaada kwa watu walio kwenye Magari.
Mama yake alifariki Miezi Michache baadae toka aanze kazi hiyo, Baada ya Kugongwa na gari wakati akiwa barabarani kuomba Msaada, Kifo chake kilitokea miaka 2 tu baada ya kifo cha mumewe.
Wasamaria Wema walioshuhudia Ajali hiyo, baada ya kugundua kuwa Mtoto aliyekuwa analia pembeni ya barabara kuwa ni wa mama huyo, walimchukua na kumpeleka Kituo Kikuu Cha Polisi Wilaya ya Kinondoni cha OysterBay.
Baada ya Juhudi za kutafuta ndugu zao kushindikana, Mwili wa Mama yake ulizikwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika Makaburi ya Kisutu. Patricia kwa kusaidiwa na Polisi wa OysterBay, alipata nafasi ya kushiriki mazishi ya mama yake. Japo alikuwa Mdogo lakini aliweza kujua kila kitu kilichokuwa kinaendelea pale. Alilia sana mpaka kutia Huruma. Kila aliyemuangalia naye Machozi yalimtoka.
Siku Mbili Baada ya Mazishi, Polisi waliamua Kumpeleka Mtoto huyo katika kituo cha Serikali cha kulelea watoto yatima na wenye Ulemavu kiitwacho Hope Orphonage Center (HOC) kilichopo Buguruni Kwa Mnyamani. Patricia akiwa ndiyo mtoto mdogo kuliko wote kituoni hapo.
Siku zote akiwa Kituoni hapo, kama kuna kitu kiliisumbua Akili yake basi ni kujua Mahali alipo dada yake Patra. Alijua tu kwamba yupo kwa Mama yake Mkubwa lakini hakuwa na kumbumbuku ya kutosha ya kujua Mahali alipokuwa akiishi Mama yake huyo Mkubwa.
Miaka Miwili baadae toka afikishwe kituoni hapo, akiwa tayari na umri wa miaka 10, Mchungaji Tajiri na Maarufu Nchini na Africa, Mch. Moses Kalinga alifika kituoni hapo kwa lengo la kutoa Msaada kwa Watoto Yatima na Walemavu, kwa ajili ya kusheherekea nao pamoja Siku Kuu ya Pasaka.
Alivyofika kituoni hapo alivutiwa sana na Mtoto Patricia ambaye alipewa Jukumu na Walezi wa Kituo hicho la Kuwakaribisha na Kusoma Risara ya Shukrani kwa Wageni.
Licha ya kwamba alikuwa mdogo kuliko watoto wote kituoni Hapo lakini aliweza kusoma vyema Risara iliyoandaliwa na Walezi wa Kituo kwa ajili ya kuwashukuru Wageni mbalimbali waliofika kituoni hapo kutoa Msaada.
Hakika Maneno yaliyomo katika Risara hiyo, yaliwagusa Wageni wengi na kuwatoa machozi, huzuni na simanzi. Sio Mchungaji Moses pekee aliyevutiwa na Uchangamfu wa Mtoto Patricia , kila Mgeni aliyefika Kituoni hapo alivutiwa nae.
Mwezi 1 baadae toka Mchungaji Moses atoke pale Kituoni alianza taratibu za kufanya maombi kituoni hapo kwa ajili ya kumchukua Mtoto huyo na kwenda kuishi nae nyumbani kwake Mikocheni Dar es Salaam, kwa ahadi ya kumpatia malezi bora na Elimu kwa kiwango atakachohitaji. Hatimaye Mch. Moses aliruhusiwa kuondoka na Patricia baada ya kufanikisha taratibu zote kama alivyoagizwa na kituo hicho.
Uwepo wa Patricia nyumbani kwa Mch. Moses uliibua furaha sana. Kwa kifupi Patricia alikuwa na Akili kuliko hata umri wake. Baadaye Mchungaji aliamua kumbadilisha Jina Mtoto huyo na Kumuita Angela Moses Kalinga.
Heshima na Unyenyekevu wake vilimvutia zaidi Mchungaji kuliko hata Mtoto wake Maria ambaye alikuwa Mkorofi na Kiburi.
Mara kwa Mara ndani ya Nyumba hiyo vilisikika vilio kutoka kwa Maria kwa kile alichodai kuwa baba yake anampenda sana mtoto huyo Mgeni kuliko yeye, hadi kufikia hatua Maria kumchukia Mdogo wake huyo. Aliumia kuona upendo aliokuwa akioneshwa na Baba yake zamani kuchukuliwa na Mtoto mwengine.
Kwa upande wa Mke wa Mchungaji, Bi Anna Emmanuel hakufurahishwa na kitendo cha Mchungaji kumleta Mtoto huyo nyumbani hapo. Moyoni mwake hakufurahishwa kwa Madai ya kwamba ameamua kumleta nyumbani kwao Mtoto aliyezaa Nje ya Ndoa yao. Hakutaka kuamini kama Mtoto huyo amechukuliwa kutoka Kituo cha Watoto yatima.
Lakini kilichomuumiza zaidi ni jinsi Mchungaji alivyokuwa akionesha mapenzi ya wazi kwa mtoto huyo na zaidi hakufurahishwa kuona Pesa za familia zikitumika kumuendeleza.
Kwa Kifupi ndani ya Nyumba ya Mchungaji ni kama waligawana Watoto. Alichofanya Mch. Moses, baada ya kugundua kuwa Mke na Mtoto wake, hawajafurahishwa na uwepo wa Patricia ndani ya Nyumba hiyo, ni kumsaidia kwa nguvu na uwezo wake wote katika kuhakikisha anampa elimu. Alihakikisha anamuonesha Upendo kiasi kwamba ni watu wachache sana waliofanikiwa kujua ukweli kuwa Patricia sio Mtoto wake wa Kumzaa.
Mpaka wanakuwa wakubwa Ugomvi kati ya Maria na Patricia au kwa Jina Jingine Angela, haukwisha ndani ya Nyumba ya Mch. Moses. Kila muda walipishana Kimawazo hata kwa hoja zisizo na Msingi.
Maria aliapa kulipiza Kisasi kwa Mdogo wake huyo kwa Kuchukua Upendo wa Baba Yake na kumfanya yeye asipendwe tena kama ilivyokuwa zamani, kabla ya Patricia kuingia ndani ya nyumba hiyo.
Licha ya kwamba Maria alipatiwa hudumu zote muhimu lakini hakuridhika, Kitendo cha Baba Yake kumpenda zaidi Patricia kuliko yeye kilimuumiza.
Alijiapiza kumchukua Mtu yoyote atakayempenda Patricia kama yeye alivyomfanyia. Hakutaka kuona Patricia anakuwa na Amani na furaha na mtu anayempenda. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Martin. Maria alipanga kuhakikisha Patricia au Angela anakosa amani na Mpenzi wake Martin.
**********
Baada ya Taarifa za tukio la Angela kupoteza fahamu kusambaa, wanafunzi wengi walimwonea huruma, ambaye mara baada ya kupoteza fahamu alipelekwa Kituo cha Polisi kwa ajili ya kuchukua PF3 na kisha kukimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Iringa kwa matibabu zaidi.
Alivyofikishwa Hospitali aliingizwa moja kwa moja kwenye Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) na kufungwa Mashine ya Oxygen ili kumsaidia kupumua.
Wakati wote huo wa kupambana kuoa Maisha ya Angela, Martin alikuwa pembeni yake. Hata walivyomfikisha ICU, Martin alikataa kutoka nje ya Chumba hicho, licha ya kuombwa kufanya hivyo mara kadhaa na Madaktari wa Hospitali hiyo. Martin alionekana kama mtu aliyechanganyikiwa. Hakuelewa hatma ya Maisha ya Angela.
Akiwa pembeni ya Kitanda alicholazwa Angela, Ndani ya moyo wake Martin alijiona Mkosaji, alijilaumu kwa kufanya mpango wake wa kukutana na Maria kuwa Siri. Alijiuliza ni nani aliyemwambia Angela kuwa alikuwepo pale Uwanjani na Maria bila Mafanikio.
Martin alimtazama Angela pale kitandani, kwa sauti ya taratibu huku machozi yakimtoka alisema
“Angela najua nimekukosea sana lakini naomba unisamehe kwa yote yaliyotokea sikuwa na maana ya kukuumiza, nakuomba uamke walau useme neno moja tu, maisha yangu hayatakuwa na maana yoyote bila uwepo wako”
Martin ni Kama vile aliongea peke yake tu kwa sababu Angela bado hakuwa na fahamu, alionekana kuwa katika usingizi mzito. Hakuelewa chochote kilichokuwa kikiendelea Duniani.
“Martin tunakuomba utoke nje umwache mgojwa apumzike” Alisema Muuguzi mmoja wa Kike katika chumba hicho.
Martin aligeuka na kumtazama muuguzi huyo huku machozi yakimtoka, hakutaka kuendelea kukaidi amri hiyo, alitoka nje ya Chumba cha wagonjwa Mahututi (ICU).
“Usijali mgojwa wako atapona” Alisema Muuguzi huyo wakati Martin anatoka nje na kufunga Mlango wa Chumba hicho.
Nje ya Chumba hicho, Martin alikuta wanafunzi wamejaa hasa wale waliokuwa wakisoma nao darasa moja. Alikuta wengine wamesimama na wengine wamekaa kwenye mabenchi mbalimbali yaliyopo Hospitalini hapo. Kila mwanafunzi alionekana ni mwenye nyuso ya huzuni. Walivyomuona Martin akitoka nje ya Chumba hicho wote walimfata kutaka kujua kinachoendelea.
“Pole sana Martin, Vipi hali ya Mgonjwa?” Aliuliza Rafiki yake Master P.
“Bado amepoteza fahamu” Alijibu Martin
Mara baada ya Martin kusema hivyo, wanafunzi wote walishikana mikono na kufumba macho yao kwa ajili ya kufanya Maombi ya kumuombea Angela. Aliyeongoza Maombi hayo si Mwingine bali ni Restuta. Maombi hayo yalichukua takribani Dakika10 hadi kumalizika.
Taarifa za Kukamatwa kwa Maria na Kufikisha Kituo Kikuu Cha Polisi cha Mkoa wa Iringa zilipomfikia Mama yake, Bi. Anna Emmanuel kupitia Simu aliyopigiwa na Maria mwenyewe mara baada ya kufikisha Kituoni hapo, muda huo huo Bi. Anna aliomba kuongea na Mkuu wa Kituo hicho aitwaye ACP. Charles Kitwana.
Baada ya kumaliza Mazungumzo yao yaliyochua takribani nusu saa, Mkuu wa Kituo hicho. ACP Kitwana aliamuru Maria aachiwe huru akaendelee na Masomo yake. Kwa Kifupi, Bi Anna alitumia Umaarufu wa Familia yao Kumshawishi Mkuu wa Kituo kumuachia Huru Binti yake na Kumuahidi, kwa kuwa hayo ni Maswala ya Kifamilia Wao kama Wazazi watayashughurikia na Wasingependa kuona mambo hayo yanafika Mbali zaidi kwani yataharibu Taswira ya Kanisa. .
Wakati Bi. Anna anazungumza na Mkuu huyo wa Kituo, Mch Moses hakuwepo Nyumbani na alipanga hata akirudi, hatomfahamisha chochote kilichotokea, alijua kama Mch. Moses angejua tukio hilo kusingekua na Maelewano Mazuri ndani ya Nyumba. Na Hivyo Ndivyo Ilivyokuwa.
*****************
Licha ya kwamba walichelewa kulala, lakini ilikuwa ni Usiku mrefu sana kwa Justine. Ukweli kutokana na Mazingira alivyoyaona pale Manzese Darajani hakulala usingizi wa Pono, muda wote alionekana akiushikiria vyema Mfuko wake wa Sandarusi ili kulinda vilivyomo visiibiwe. Alitamani Asubuhi ifike haraka.
Vumbi, Mbu na harufu kali ya Mikojo ilimfanya Justine kushindwa kulala vizuri. Licha ya kwamba alikuwa amelewa lakini Muda wote alishtushwa na Kelele za Magari yaliyokuwa yakipita chini ya Daraja hilo. Alipowatazama wenzake hakuna aliyeonekana kusumbuliwa na hali hiyo. Walionekana kulala fofofo.
Ilivyofika asubuhi Justine alikuwa wa kwanza kuamka. Alitazama huku na kule hakuona mtu mwengine aliyeamka. Akiwa bado kaushikiria mfuko wake vile vile kama alivyolala, alipoungalia, aligundua kuwa umechanwa kwa pembeni. Alishtuka kidogo na kukaa vizuri ili auchunguze, ndipo alipogundua kuwa ameibiwa Simu yake ya Nokia aliyomuibia Yule Bibi ndani ya Daladala kule Iringa.
“Nimeibiwa saa ngapi wakati sikulala fofofo” Alijiuliza Justine.
Justine alitamani kupiga Kelele za Mwizi lakini alishindwa kwa sababu hakuna aliyemuona akimuibia. Justine hakutaka kuamini kama kweli ameibiwa. Hakuelewa ameibiwa saa ngapi. Kilichomshangaza zaidi ni kuona watu wote waliomzunguka bado walionekana kulala fofofo.
Haikupita muda wenzake waliamka. Baada ya Salamu aliwahadithia kila kitu kuhusu wizi uliotokea. Walimsikitikia na kumtaka siku nyengine kuwa makini. Baada ya maongezi hayo machache walianza kujiandaa kwa safari ya kuelekea Ubungo kwa ajili ya shughuli yao ya kila siku ya kuosha magari.
Siku ya Pili Jijini Dar es Salaam, kwa Justine ilikuwa kama Mwanafunzi ambae yupo Darasani anaendelea kujifunza. Walivyofika eneo lao la Kazi, Justine alikumbuka Maneno aliyoambiwa Jana na Buda kuwa, Kazi ya kuosha magari inahitaji kuchangamka.
Kwa hiyo Kitu cha kwanza kufanya walipofika, Justine alikwenda moja kwa moja Dukani kwa ajili ya kununua vifaa vyake mwenyewe vya kazi. Alivyotoka Dukani alirudi na kukuta baadhi ya wenzake wameanza kuosha magari yaliosimama kwenye foleni na yeye akaungana nao.
Mpaka inafika Jioni ya Siku hiyo, Justine alikuwa ameosha magari mengi zaidi ya wenzie.
Giza lilipoanza kuingia kama kawaida yao, Kila Mmoja alimpatia Buku Buda, kisha walianza safari ya kuelekea Kilima Hewa Pub. Walipofika waliagiza Pombe na kuanza kunywa. Watu walikuwa wengi sana siku hiyo.
Alipoona Wenzake wote wameingia kati na kuanza kucheza Muziki. Justine aliinuka na kwa mwendo wa taratibu alizunguka nyuma ya Banda hilo, alifanya kama anakwenda uelekeo wa eneo Kilipo choo cha Kilabu hicho. Alipoona wenzake hawamwangalii alikata kushoto na kwenda moja kwa moja mpaka sehemu aliyosimama Patra.
“Mambo Patra, tunaweza kuongea ?” Justine alimnong’oneza Patra.
“Sasa hivi?”Aliuliza Patra
“Ndiyo”
“Sawa hakuna shida, napeleka Pombe meza ile halafu nakuja, utakuwa wapi” Aliuliza Patra.
“Utanikuta Nje”
“Sawa”
Muda si Mrefu, Patra alitoka nje kwenda kuonana na Justine. Justine na Patra walitafuta sehemu iliyotulia na yenye Giza kidogo walisimama na kuanza mazungumzo. Justine na Patra walionekana wakiongea kama watu waliofahamiana muda mrefu. Mara kwa mara Patra alisikika akicheka. Kwa kifupi Justine hakuwa na muda wa kupoteza, alitumia nafasi hiyo kuhakikisha anazoeana na Patra.
“ Patra umeolewa?” Katikati ya Mazungumzo yao Justine aliuliza
“Bado sijaolewa, kwa nini umeniuliza ”Alisema Patra
“Basi tu nataka kujua, Mtoto mzuri kama wewe unakosaje Mume”
“Wanaume wa Siku hizi waongo, hakuna hata muoaji”
“Sio wote Patra, wapo wanaume waaminifu”
“Mmoja kati ya Mia”. Wote wawili walisikika wakicheka.
Baada ya Maongezi yao yaliyotawaliwa na vicheko vya hapa na pale, wote wawili walirudi ndani, kila mmoja akitumia mlango wake, Justine hakutaka rafiki zake wajue kuwa alikuwa nje na Patra. Aliwakuta wenzake bado wakiendelea kucheza Muziki. Alienda moja kwa moja kwenye Meza yao, alichukua kinywaji chake na kuanza kunywa kwa mpigo na kisha akaenda kuungana na wenzake kucheza Muziki.
Kama Kawaida ilipotimu saa tisa usiku waliondoka na kuelekea Daraja la Manzese. Walisikika wakipiga Kelele njia nzima. Kuna wakati walionekana Wakiimba Vyimbo na Kupiga Makofi huku Buda akiwa katikati yao akicheza. Walipofika Buda kama Kawaida aliwaaga na kisha akavuka Barabara kuelekea Magomeni.
Wengine walivyofika Juu ya Daraja kila mmoja alielekea sehemu yake na kulala. Tofauti na ilivyokuwa Jana, Leo Justine hakutumia nguvu nyingi kupata Usingizi.
******************
Masaa takribani 12 Toka Angela afikishwe Katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa, Mlango wa Wagonjwa Mahututi( ICU) ulifunguliwa na Daktari alionekana akitoka nje. Baadhi ya Wanafunzi wa Chuo cha Tumaini waliokuwepo pale nje, akiwemo Mpenzi wake Martin, Rafiki yake Restuta na Master P, kwa haraka walisimama na kumfata kwa lengo la kutaka kujua hali ya Mwenzao.
“Dokta Mgonjwa wetu anaendeleaje” Hilo lilikuwa swali la kwanza kutoka kwa Martin kwenda kwa Daktari.
“Anaendelea vizuri na tunamshukuru Mungu kwamba fahamu zake zimerudi” Alisema Daktari.
“Asante Mungu” Walisikika baadhi ya Wanafunzi wakisema hivyo.
“Vipi tunaruhusiwa kumuona??” Aliuliza Restuta
“Ndio mnaruhusiwa kumuona, isipokuwa Martin na Maria Kama Wapo” Alisema Daktari na Kisha Kuendelea “Hiki ni Chumba cha wagonjwa Mahututi kwa hivyo hatuhitaji Kelele” Alivyomaliza kusema hayo, Daktari Alirudi ndani ya ICU.
Dada yake na Angela ambaye ni Maria hakuwepo Hospitalini wakati huo na wala hakujali kwa kumsababishia Mdogo wake Maumivu Makali kiasi hicho, alitegemea kupata taarifa zote juu ya maendeleo ya Mgonjwa kutoka kwa Restuta, ambaye Alimtuma kwenda Hospitalini hapo kwa kazi Maalumu.
Lakini kwa Upande wa Martin aliyekuwepo Hospitalini hapo alishtushwa na Kauli ya Daktari ya kutoruhusiwa kwenda kumuona mpenzi wake Angela.
“Martin Usijali nitaongea nae, kila kitu kitakuwa Sawa” Alisema Restuta kwa sauti ya Taratibu na Kisha Wanafunzi wengine waliokuwepo, walionekana wakianza kuingia ndani ya ICU kwenda kumuona Angela.
Licha ya Kwamba Kulikuwa na Wagonjwa Mahututi Kadhaa ndani ya ICU kwa muda huo, Lakini Walivyofika ndani hawakupata shida kutambua Kitanda alicholala Angela, kwani kilikuwa ni Kitanda cha Mwisho Upande wa Kushoto mwa Chumba hicho, walimkuta Angela akiwa amelala Kitandani ila macho yake yakiangalia Mlangoni kama mtu aliyekuwa akiusubiria Ujio huo.
Mkononi alikuwa amewekwa Dripu ya Maji na Kichwani alionekana kufungwa Bandeji katika ile sehemu iliyopasuka. Kwa kumuangalia tu ilitosha kufahamu ni maumivu kiasi gani aliyokuwa nayo. Alivyowaona wenzie wakiingia na kumzunguka katika Kitanda alicholala, machozi yalianza kumtoka kwa wingi.
“Angela Jikaze Mama Usilie” Alisema Restuta kwa Sauti ya kunong’oneza huku akiwa amemkumbatia pale Kitandani.
“Pole Angela Usijali Utapona” Walisema Baadhi ya Wanafunzi wenzake na kuweka kwenye Droo za Kitanda Chake baadhi ya Vitu walivyokwenda navyo Kama Chakula, Matunda, Juice na Kadi mbalimbali zenye Ujumbe wa kumtakia hapone haraka.
“Ahsanteni sana kwa Zawadi” Angela alisema kwa sauti ya Chini iliyojaa Maumivu huku akijifuta Machozi yaliyokuwa yakiendelea kupenya na kutoka kwenye Kingo za Macho yake.
“Shem Mimi nina Zawadi Maalumu Kutoka kwa Martin” Alisema Master P huku akimkabidhi Zawadi ya Maua. Martin baada ya kuzuiliwa kuingia ICU kumuona Angela alimuomba Rafiki yake Master P amsaidie kufikisha Maua hayo kwa Angela.
“Kamwambie Siwezi Kuyapokea” Alisema Angela.
“Tafadhali Shemeji Usifanye hivyo” Master P alisisitiza.
Ghalfa, Master P akiwa bado anambembeleza Angela kupokea zawadi hiyo, Martin alifungua Mlango wa ICU kwa Nguvu na kuingia ndani, moja kwa moja akielekea kwenye Kitanda Alicholala Angela.
“Martin toka Nje Tafadhali” Walisema Madaktari waliokuwemo ndani ya Chumba kile huku wakimfata Martin kwa Kasi na kumzuia kwa mbele ili asiendelee kwenda kwenye Kitanda alicholala Angela. Kila Mtu aliyekuwemo ICU alishtushwa na Kitendo hicho cha Martin kwani hakuna aliyekitegemea.
“Usitake tutumie nguvu kukutoa nje” Walisema Madaktari wale huku wakimsukuma Martin kuelekea kwenye Mlango wa Chumba hicho.
“Muacheni” Alisema Angela kwa Sauti ya Chini.
Kauli hiyo ya Angela iliwafanya Madaktari wale kumuachia Martin kwenda kumuona. Martin alifika kwenye Kitanda cha Angela akihema na Kumkumbatia Angela huku Machozi yakimtoka kwa Wingi. Kwa Martin kuondoka pale bila kumuona Angela akiwa katika fahamu zake ingekuwa ni Kosa Jingine ambalo hakuwa tayari kulitenda.
Moyo wake ulikubali kosa alilofanya na kumsababishia Mpenzi wake maumivu hayo Makali lakini aliona bado ana nafasi ya kuomba Msamaha kwa kilichotokea.
“Nisamehe Angela” Alisema Martin kwa sauti iliyochanganyika na Kilio huku akiwa bado amemkumbatia Angela.
“Nilishakusamehe Martin ila Sitaki kukuona, Ninapokuona Unanikumbusha Vitu ambavyo Sitaki Kuvikumbuka” Alisema Angela.
“Unajua kuwa Nakupenda na siwezi kukaa bila Kukuona” Alisema Martin kwa Sauti ya Kunong’oneza.
“Nilikuwa najua Mwanzo ila kwa sasa Sijui, Nadhani Dada yangu Maria anakufaha zaidi kuliko Mimi” Alisema Angela huku Machozi yakimtoka
“Muda wa kuona Wagonjwa umekwisha, Wagonjwa wanataka Kupumzika” Aliingilia kati Maongezi hayo Mmoja kati ya Wale Madaktari Wawili waliokuwa wakimsukuma Martin kutoka Nje. Baada ya Kusikia Kauli hiyo, Wanafunzi wote walimuaga Angela na kuanza kutoka nje ya ICU.
**************