Tuwaseme
JF-Expert Member
- Oct 8, 2014
- 645
- 1,188
UTANGULIZI
Mvua ikiwa inaendelea kunyesha, Takribani masaa 12 Toka Angela afikishwe katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa, Mlango wa Wagonjwa Mahututi (ICU) Unafunguliwa na Daktari anaonekana akitoka nje. Baadhi ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini waliokuwepo pale nje, akiwemo Mpenzi wake Martin, Rafiki yake Restuta na Master P, kwa haraka wanasimama na kumfuata kwa lengo la kutaka kujua hali ya Mwenzao.
“Dokta Mgonjwa wetu anaendeleaje” Hilo lilikuwa swali la kwanza kutoka kwa Martin kwenda kwa Daktari.
“Anaendelea vizuri na tunamshukuru Mungu kwamba fahamu zake zimerudi” Alisema Daktari.
“Asante Mungu” Walisikika baadhi ya Wanafunzi wakisema hivyo.
“Vipi tunaruhusiwa kumuona??” Aliuliza Restuta
“Ndio mnaruhusiwa kumuona, isipokuwa Martin na Maria Kama Wapo” Alisema Daktari na Kisha Kuendelea “Hiki ni Chumba cha wagonjwa Mahututi kwa hivyo mtaingia kwa Makundi na hatuhitaji Kelele” Alivyomaliza kusema hayo, Daktari Alirudi ndani ya ICU.
Dada yake na Angela ambaye ni Maria hakuwepo Hospitalini wakati huo na wala hakujali kwa kumsababishia Mdogo wake Maumivu Makali kiasi hicho, alitegemea kupata taarifa zote juu ya maendeleo ya Mgonjwa kutoka kwa Restuta, ambaye Alimtuma kwenda Hospitalini hapo kwa kazi Maalumu.
Lakini kwa Upande wa Martin aliyekuwepo Hospitalini hapo Usiku kucha alishtushwa na Kauli ya Daktari ya kutoruhusiwa kwenda kumuona mpenzi wake Angela.
“Martin Usijali nitaongea nae, kila kitu kitakuwa Sawa” Alisema Restuta kwa sauti ya Taratibu na Kisha Wanafunzi wengine waliokuwepo, walionekana wakianza kuingia ndani ya ICU kwenda kumuona Angela.
Licha ya Kwamba Kulikuwa na Wagonjwa Mahututi Kadhaa ndani ya ICU kwa muda huo, Lakini Walivyofika ndani hawakupata shida kutambua Kitanda alicholala Angela, kwani kilikuwa ni Kitanda cha Mwisho Upande wa Kushoto mwa Chumba hicho, walimkuta Angela akiwa amelala Kitandani ila macho yake yakiangalia Mlangoni kama mtu aliyekuwa akiusubiria Ujio huo.
Mkononi alikuwa amewekwa Dripu ya Maji na Kichwani alionekana kufungwa Bandeji katika ile sehemu iliyopasuka. Kwa kumuangalia tu ilitosha kufahamu ni maumivu kiasi gani alikuwa nayo kwa wakati huo. Alivyowaona wenzie wakiingia na kumzunguka katika Kitanda alicholala, machozi yalianza kumtoka kwa wingi.
“Angela Jikaze Mama Usilie” Alisema Restuta kwa Sauti ya kunong’oneza huku akiwa amemkumbatia pale Kitandani.
“Pole Angela Usijali Utapona” Walisema Baadhi ya Wanafunzi.
“Ahsanteni sana” Angela alisema kwa sauti ya Chini iliyojaa Maumivu huku akijifuta Machozi yaliyokuwa yakiendelea kupenya na kutoka kwenye Kingo za Macho yake.
“Shem Mimi nina Zawadi Yako Kutoka kwa Martin” Alisema Master P huku akimkabidhi Zawadi ya Maua. Martin baada ya kuzuiliwa kuingia ICU kumuona Angela alimuomba Rafiki yake Master P amsaidie kufikisha Maua hayo kwa Angela.
“Kamwambie Siwezi Kuyapokea” Alisema Angela.
“Tafadhali Shemeji Usifanye hivyo” Master P alisisitiza.
Ghalfa, Master P akiwa bado anambembeleza Angela kupokea zawadi hiyo, Martin alifungua Mlango wa ICU na kuingia ndani, moja kwa moja akielekea kwenye Kitanda Alicholala Angela.
“Martin toka Nje Tafadhali” Walisema Madaktari waliokuwemo ndani ya Chumba kile huku wakimfuata Martin kwa Kasi na kumzuia kwa mbele ili asiendelee kwenda kwenye Kitanda alicholala Angela. Kila Mtu aliyekuwemo ICU alishtushwa na Kitendo hicho cha Martin kwani hakuna aliyekitegemea.
“Usitake tutumie nguvu kukutoa nje” Walisema Madaktari wale huku wakimsukuma Martin kuelekea kwenye Mlango wa Chumba hicho.
“Muacheni” Alisema Angela kwa Sauti iliyojaa Maumivu.
Kauli hiyo ya Angela iliwafanya Madaktari wale kumuachia Martin kwenda kumuona. Martin alifika kwenye Kitanda cha Angela akihema na Kumkumbatia Angela huku Machozi yakimtoka kwa Wingi. Kwa Martin kuondoka pale bila kumuona Angela akiwa katika fahamu zake ingekuwa ni Kosa Jingine ambalo hakuwa tayari kulitenda.
Moyo wake ulikubali kosa alilofanya na kumsababishia Mpenzi wake maumivu hayo Makali lakini aliona bado ana nafasi ya kumuomba Msamaha kwa kilichotokea.
“Nisamehe Angela” Alisema Martin kwa sauti iliyochanganyika na Kilio huku akiwa bado amemkumbatia Angela.
“Nilishakusamehe Martin ila Sitaki kukuona, Ninapokuona Unanikumbusha Vitu ambavyo Sitaki Kuvikumbuka” Alisema Angela.
“Unajua kuwa Nakupenda na siwezi kukaa bila Kukuona” Alisema Martin kwa Sauti ya Kunong’oneza.
“Nilikuwa najua Mwanzo ila kwa sasa Sijui, Nadhani Dada yangu Maria anakufaa zaidi kuliko Mimi” Alisema Angela huku Machozi yakimtoka
“Muda wa kuona Wagonjwa umekwisha, Wagonjwa wanataka Kupumzika” Aliingilia kati Maongezi hayo Mmoja kati ya Wale Madaktari Wawili waliokuwa wakimsukuma Martin kutoka Nje. Baada ya Kusikia Kauli hiyo, Wanafunzi wote walimuaga Angela na kuanza kutoka nje ya ICU.
SEHEMU YA KWANZA
Martin Jonathan Chota ni Kijana aliyezaliwa miaka 24 iliyopita katika Kijiji cha Kalenga Mkoani Iringa. Ni Mtoto wa pili na wa Mwisho wa Mzee Jonathan Peter Chota na Bi. Maria Emmanuel Magova. Mtoto wao wa kwanza aliitwa Justine.
Toka akiwa mdogo Martin alikuwa ni kijana mtulivu, msikivu na mnyenyekevu.
Tofauti na watoto wengine wa rika lake, Martin alipenda sana kuimba. Toka akiwa mdogo alidhihirisha uwezo wake wa kuimba. Aliwahi kujiunga na Kwaya ya Kanisani kwao bila kuwashirikisha wazazi wake.
Martin alikuwa ni mwimbaji mdogo kuliko wote katika Kwaya hiyo, lakini watu walivutiwa sana na uimbaji wake. Sauti nzuri, uwezo wake wa kukariri Mashairi na kupiga Gitaa kwa ufasaha vilizidi kumpatia sifa kemkem.
Martin alikuwa tofauti sana na Kaka yake Justine. Justine muda wote alionekana mwenye hasira, mkali, kiburi na mgomvi. Kutokana na vitendo vyake hivyo vya ukatili, watu wengi kijijini hapo walizoea kumuita ‘Nunda’, Jina ambalo lilikuwa maarufu Kijijini Kote.
Justine alifahamika kwa tabia yake ya kupenda kujikweza, ukorofi na ubinafsi. Justine alimchukia mtu yeyote aliyejitokeza kumwonya.
Mara kadhaa alionekana akigombana na wazazi wake juu ya tabia zake hizo lakini hakubadilika. Wazazi wake waliamini tabia zake hizo wenda zilitokana na Justine kuugua sana maradhi ya kichwa, kitaalamu ‘Hemiplegic Migraine Headache’ alipokuwa mdogo kiasi cha wazazi wake kukata tamaa kama mtoto wao angepona.
Martin na Justine walikuwa kama watoto wa wazazi tofauti, walikuwa na tabia zisizoshahabiana. Japo Martin alijitahidi kumheshimu na kumuonesha upendo kaka yake, lakini juhudi zake ziligonga mwamba, Justine hakujali.
Mama yake alijitahidi kumtetea mtoto wake huyu lakini ilifika kipindi alichoshwa na vitendo vyake hasa pale Justine alipokataa kuendelea na masomo ya Kidato cha Tano na Cha Sita licha ya kwamba alifaulu vizuri Mitihani yake ya Kumaliza Kidato cha Nne. Kila siku alikuwa mtu wa matukio na Kila mtu Kijijini Kalenga alimfahamu hivyo.
Pale tabia ya Justine ilipozidi kuwa mbaya zaidi kwa kujihusisha na vitendo viovu kama vile ulevi wa pombe, mihadarati pamoja na kuchanganya wasichana ilipelekea akiwa na umri wa miaka 27 wazazi wake kumfukuza nyumbani.
“Toka nyumbani kwangu nakwambia” Hiyo ilikuwa sauti ya Mzee Jonathan Peter Chota akiongea na Justine siku ambayo Justine alirudi nyumbani akiwa amelewa kupitiliza.
“Haya Maisha tu Mzee” Kwa sauti ya kilevi, akiyumba yumba Justine alimjibu Mzee Jonathan huku akiwa ameshikilia Chupa ya Pombe aina ya ulanzi mkononi.
“Maisha gani kutwa nzima umelewa, mwili mzima unanuka pombe, hukumbuki hata kufanya usafi wa mwili wako, siku ya ngapi leo haujaoga, nakwambia nimechoshwa na tabia zako mbovu, rudi ulikotoka na nisikuone tena nyumbani kwangu” Mzee Jonathan aliendelea kusema huku akimsukuma Justine atoke nje ya uzio wa nyumba yao.
Justine aliyumba yumba mpaka nje pembezoni kidogo mwa ukuta wa nyumba yao akadondoka chini, alijaribu kusimama akashindwa na kuamua kulala hapo. Haikupita muda usingizi Ulimpitia.
*********************
Kwa upande wa Martin katika Maisha yake, alitumia muda wake mwingi kumtumikia mungu. Aliipa Elimu kipaumbele akiamini atafanikiwa, ili siku moja aje kuisaidia familia yake iliyokuwa ikiishi katika lindi la umaskini.
Kitu ambacho kilimfanya Martin kupendwa na watu wa rika zote ni tabia yake njema. Upole, Uzuri wa sura, urefu kiasi na rangi yake ya kahawia ilizidi kuipamba sura yake na kumfanya kuwa kivutio kwa wadada wengi aliokutana nao.
Hata wakati anasoma shahada yake ya Uandishi wa Habari (Bachelor of Arts in Journalism) katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini tawi la Iringa, alisumbuliwa sana na wanafunzi wa kike waliokuwa wakimhitaji kimapenzi.
Barua za kumtaka kimapenzi, Martin alikuwa ameshazizoea hakumbuki hata kama kuna nyingine aliwai hata kuzisoma au kuzijibu, anachokumbuka alitumia muda wake mwingi katika Masomo..
Kati ya Wanafunzi chuoni hapo waliomtaka na kumsumbua Martin Kimapenzi ni Mabinti wawili wa familia moja, Maria & Angela, Mabinti wa Mchungaji Moses Kalinga.
Maria ambaye ni Mkubwa alimpenda sana Martin licha ya kwamba alijua wazi kuwa Martin yupo katika mahusiano ya kimapenzi na Mdogo wake Angela, lakini hakusita kumuonyesha hisia zake za mapenzi Shemeji yake Martin. Wakati wote alitamani kuona Martin akiwa wake japo alitaka kufanya hivyo kwa siri kubwa bila mdogo wake kujua.
Mabinti hawa wa Mchungaji Tajiri na Maarufu Tanzania na Afrika, Mch. Moses Kalinga wa Kanisa la Eagles Revival Outreach Ministry (EROM), Wote wawili wanasoma Kozi moja na Martin.
Baba yao kabla ya kurudi Tanzania, alikuwa akihudumu kama Mchungaji Msaidizi katika Makao Makuu Ya Kanisa Hilo la Eagles Revival Outreach Ministry (EROM) lililopo Johannesburg Nchini Africa Kusini na baadae kurudi Nyumbani Tanzania. Licha ya Kwamba alirudi ili kuwa Mchungaji Mkuu wa Kanisa hilo Tanzania lakini pia aliweza kuanzisha Kampuni ya EMG (Erom Media Group) iliyomiliki Kituo Cha Television Kilichoitwa EROM Tv na EROM FM Radio. Vyombo vyote vya habari vikiwa Jijini Dar es Salaam.
Maria ni binti yake aliyempata baada ya Miaka 10 ya Ndoa yake na Bi. Anna Emmanuel.
Maria alitokea kumpenda sana shemeji yake kiasi cha kushindwa kuzuia hisia zake. Kila walipokutana alitumia muda wake mwingi kumtazama Martin bila kuchoka. Maria aliumia sana alipoona Martin haoneshi kuvutiwa na chochote kutoka kwake.
Maria hakupenda kumwona Martin akiwa karibu na msichana yoyote Chuoni hapo. Alikuwa na wivu kwa shemeji yake pengine kumzidi hata Angela mwenyewe. Maria hakujua kwa nini alimpenda Martin kiasi kile.
Maria alijaribu kutumia kila mbinu ili amnase shemeji yake Kimapenzi, alitumia uwezo wa kifedha waliokuwa nao wazazi wao ili kumpata Martin lakini ilishindikana. Kwa Kifupi, Maria hakuwa tayari kumkosa Martin. Maria aliumia moyo kila alipowaona pamoja Mdogo wake Angela na Martin.
********************
Martin akiwa Chuoni hapo aliendeleza kipaji chake cha kuimba, tofauti na alivyokuwa mdogo, safari hii alikuwa akiimba nyimbo tofauti tofauti, aliimba nyimbo mbalimbali za wasanii maarufu duniani kama wakina Paul McCartney, Boyz II Men, Elvis Presley na wengine wengi. Uwezo wake wa kuimba ulimuongezea umaarufu zaidi.Chuo Kizima walimfahamu Martin kwa Uimbaji wake.
Akiwa Mwaka wa Mwisho wa Masomo yake, Wiki Moja kabla ya kufanya Mitihani yao ya Mwisho Ya kumaliza Chuo (University Examination), Serikali ya wanafunzi chuoni hapo iliandaa Bonanza lililoshirikisha wanafunzi kutoka Kozi mbalimbali. Lengo la Bonanza Lilikuwa ni kujenga Ushirikiano miongoni mwa wanafunzi na Pili, Kuweka miili na akili zao sawa ili kujiandaa na mitihani yao ya Mwisho.
Mashindano hayo yaligawanywa katika Makundi mawili, Kundi la kwanza ni la michezo iliyopangwa kufanyika mchana kama Mpira wa Miguu, Mpira wa Kikapu, Mpira wa Pete, Kukimbiza Kuku, Kukimbia na Gunia na Riadha.
Mashindano ya Kuimba, Kucheza Muziki na Ucheshi (Stand-Up Comedy) yaliwekwa katika Kundi la Pili na kupangwa kufanyika usiku katika Ukumbi Maarufu chuoni hapo wa Multi- Purpose, Ukumbi Maalumu kwa kufanyika matukio mbalimbali yanayotokea chuoni hapo.
Wanafunzi walivyopata habari hiyo kila mmoja alifurahi, Waliokuwa tayari walianza kujiandikisha kushiriki.Kila mmoja alijitamba kufanya vizuri zaidi ya mwenzake.
Wanafunzi Waliisubiria siku ya Mashindano hayo kwa hamu kubwa.
****************
Maria toka mashindano yatangazwe alipita katika kila kona ya Mbao za Matangazo Chuoni hapo kutafuta jina la Martin ili kuona mchezo atakaoshiriki lakini hakubahatika kuliona Jina la Martin mahala popote.
Maria alishindwa kumuuliza Mdogo wake Angela kwa nini hajaona jina la Martin kwenye Mbao za Matangazo, aliamua kwenda kumdadisi rafiki wa karibu na Martin aliyeitwa Peter Matiang’i, alijua kwa jinsi Peter alivyokuwa muongeaji asingeweza kumficha kitu, angeweza kupata majibu ya maswali yake.
Peter ni raia wa Kenya, aliyefika Tanzania kwa ajili ya Masomo, alifahamika Chuo kizima Kwa uongeaji wake. Kutokana na kuwa Mshehereshaji (Mc) katika matukio mbalimbali yaliyokuwa yakifanyika Chuoni hapo, wanafunzi wengi walizoea kumuita “Master P”.
Maria alizunguka maeneo mbalimbali ya Chuoni hapo kumtafuta Master P, alifanikiwa kumkuta katika Kiwanja cha Mpira wa Kikapu akifanya mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na Mashindano. Maria alimsubiri mpaka alivyomaliza mazoezi na kumfata.
“Mambo P” Maria alimsalimia
“Poa tu Maria, kumbe na wewe unapenda Basket Ball” Master P aliongea huku akionekana kunywa Maji.
“Kiasi sio sana” Maria alisema
“Basi kwa sababu umeanza kuja uwanjani ntakufanya uupende mchezo huu, basket ni mchezo mzuri sana” Safarii hii waliongea huku wakionekana kuondoka uwanjani, wakipita nyuma ya Maktaba Kubwa ya Chuoni hapo kuelekea upande yalipo Mabweni ya Kiume. Baada ya maongezi ya hapa na pale, Maria akaona atoe la moyoni.
“Mbona rafiki yako simuoni” Maria aliuliza
“Nani?....Martin” Master P aliuliza.
“Ndio”
“Mbona yupo,nilimwacha amelala bwenini”
“Simuoni akifanya mazoezi kama nyinyi”
“Martin amesema hatoshiriki Mashindano ya Mwaka huu, tumemshawishi tumeshindwa tumeona bora tumwache na maamuzi yake”
“Au anaumwa?” Maria alisema.
“Anaumwa wapi, nikikwambia sababu yenyewe utacheka eti kwa sababu hajalipa ada ya muhula huu ndiyo anasema hawezi kushiriki mashindano, sasa sijui ada ina uhusiano gani na haya Mashindano”
“Master P ada ina uhusiano, ili mtu yoyote aweze kushinda katika shindano lolote anahitaji kuwa na utulivu wa fikra, kama Martin bado hajalipa ada hawezi kuwa na utulivu wa fikra na wenda kweli ndiyo sababu inayomfanya kushindwa kushiriki, atakuwa anafikiria vitu viwili kwa wakati moja”. Aliongea Maria.
Mazungumzo kati ya Master P na Maria yaliendelea mpaka walipofika karibu na Bweni analokaa Master P na Martin lijulikanalo kama German-America, waliagana. “Usisahau kumsalimia Martin”. Hayo ndiyo yalikuwa maneno ya Mwisho ya Maria wakati wanaagana na Master P.
Martin alikuwa miongoni mwa wanafunzi walioshindwa kujiandikisha kushiriki katika Mchezo wowote. Hii ilitokana na ukweli kwamba Martin alikuwa na hofu kubwa ya kushindwa kufanya mitihani yake ya kumaliza Chuo, iliyokuwa inakaribia kutokana na kutolipa Ada. Hali hiyo ilimkosesha raha.
Mara kwa mara aliwapigia simu wazazi wake kuwakumbusha kuhusu Ada, wazazi wake walimjibu bado wanatafuta wakipata watamtumia, majibu ambayo yalimkatisha tamaa zaidi.
Katika Kipindi chote cha Maandalizi ya Mashindano hayo, Martin hakujihusisha na chochote, alikuwa Mnyonge sana. Muda mwingi alitumia kufikiria namna atakavyopata ada ili aweze kufanya mitihani.
******************
Justine mara baada ya kufukuzwa na wazazi wake kijijini kalenga alipanga mikakati ya kwenda Jijini Dar es Salaam, kutafuta maisha. Siku nyingi alikuwa na ndoto ya kufika Mji huo, kutokana na sifa kemkem alizowai kuzisikia kuhusu Mji huo alitamani kufika na aliamini atafanikiwa kupata kazi yoyote itakayo mpatia kipato. Kwa kuwa hakuwa na maelewano mazuri na wazazi wake hata safari yake hiyo alipanga kuwa siri hakutaka mtu yoyote hajue.
Akiwa amekaa pembezoni mwa nyumba yao mara baada ya kuamka na kukumbuka kuwa amefukuzwa nyumbani na wazazi wake, Justine alijipapasa kwenye mifuko ya suruali yake na kukuta amebakiwa na sh 200.
Bila hata ya kujikung’uta vumbi, Justine aliinuka na kwenda ndani ya uzio wa nyumba yao ambako alimkuta baba yake akiwa amepumzika kwenye Mkeka akisoma gazeti.
“Nani amechukua hela yangu” Kwa sauti ya juu Justine alimuuliza baba yake
“Nani achukue hela yako, kwa hela gani hasa uliyokuwa nayo” Mzee Jonathan alimjibu.
“Nauliza tena, nani amechukua hela yangu, nilikuwa na elfu 1 mfukoni siioni”
“Usitupigie kelele hapa, kwanza nilishakwambia sitaki kukuona nyumbani kwangu”
Kwa sauti ya jazba “Halafu we mzee usinichanganye, nimekuuliza hela yangu iko wapi unaniletea habari nyengine” Kisha akamgeukia mama yake ambae muda wote alikuwa kimya akiwatazama “Mama mwambie mume wako tabia ya kufatilia maisha ya watu aache, kuna watu wengine tumepinda, tutakuja kufanya tukio hapa tuwepe lawama, halafu kila siku nasema kama Pombe nakunywa mimi, niacheni, tena nakunywa kwa pesa zangu mwenyewe”
“Justine…..!!” Mama yake aliita na kuendelea “Kama kweli mimi ni mama yako nisikilize ninachotaka kukwambia, mwanangu unakoelekea sasa ni kubaya. Siku hizi umekuwa mlevi kupindukia, hukumbuki hata kula. Hata Mafundisho ya dini…….” Kabla hajamalizia anachotaka kusema, Justine akadakia“Kumbe Bi. Mkubwa na wewe wale wale tu umeshirikiana na mume wako kuniibia hela yangu”
Baada ya majibizano ya muda mrefu na wazazi wake, Justine alichukua uamuzi wa kuondoka nyumbani kwao.
Akiwa bado ana randa randa mitaani, aliwaza namna ya kupata nauli itayomfikisha stendi ya Miyomboni, stendi kuu ya daladala iliyopo Iringa Mjini ambapo angeweza kufika na kujipanga na safari yake ya kuelekea Dar es Salaam siku inayofuata.
********************
Hatimaye, Siku iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa ikawadia, ilikuwa ni Jumamosi iliyosheheni shamra shamra za hapa na pale. Kila mwanafunzi alionekana ni mwenye vyuso ya furaha.
Hali ya hewa ya Baridi ilizidi kuipamba siku hiyo kuwa ya aina yake. Kelele za Mavuvuzela ya hapa na pale yalisikika kutoka kila pembe ya Chuo hicho. Lugha za Kebehi, Vijembe na Kejeli zilitawala. Muda ulipofika, wanafunzi walianza kumiminika viwanjani.
Michezo ilifanyika katika viwanja mbalimbali vilivyopo Chuoni hapo kutegemeana na asili ya mchezo husika. Kundi la kwanza la Michezo liliendelea na kumalizika jioni, wanafunzi walipata nafasi ya kupumzika kwa ajili ya michezo mingine itakayofanyika usiku.
Jioni ya Siku hiyo, ndiyo ilipangwa kufanyika sehemu ya pili ya Mashindano hayo katika Ukumbi wa Multi- Purpose. Muda ulipofika wanafunzi walianza kumiminika kwa wingi katika Ukumbi kwa ajili ya kushuhudia Mashindano yaliyosalia. Vipengele vilivyokuwa vikishindaniwa wakati huu ni Kucheza Muziki, Ucheshi na Kuimba.
Ndani ya Ukumbi, nderemo na vifijo vilisikika. Waliofanya vizuri katika Mashindano ya Mchana walionekana wakishangilia na kuzunguka kila Pembe ya Ukumbi huo, Kelele za Mavuvuzela zilishamiri.
Jukwaa lilipambwa kwa vitambaa vya rangi za kuvutia na maua mbalimbali. Muziki ulipofunguliwa kila mmoja alishangilia na kuingia kati kucheza. Ukweli ilikuwa ni siku ya furaha kwa wanafunzi wengi. Mc wa shughuli hiyo, Master P alipanda Jukwaani na kuanza kuchombeza maneno ya hapa na pale.
“Sema yeaaah”
Kisha Master P aliwatangazia ratiba ya usiku huo kuwa wataanza na kipengele cha Ucheshi, Kucheza Mziki na watamaliza na Waimbaji. Akatumia fursa hiyo kumkaribisha Jukwaani Mlezi wa Wanafunzi (Dean of Students) Chuoni hapo, Rev. Emmanuel Aswile, kwa ajili ya kufungua rasmi Mashindano hayo.
Mashindano yalianza na amsha amsha ya hali ya juu, washiriki wote walionekana kujipanga vizuri.
Ufundi wa kutumia maneno, ucheshi na mbwembwe alizokuwa nazo Mc vilizidi kupendezesha shughuli. Mashindano yaliendelea huku kukiwa hakuna dalili ya Martin kuweza kushiriki.
Maria akiwa ndani ya Ukumbi alizunguka huku na kule kuona labda atamwona Martin lakini hakufanikiwa. Alipepesa macho yake kumtafuta mdogo wake Angela nae pia hakufanikiwa kumuona ndani ya Ukumbi. Kutomuona Martin na Angela katika Ukumbi huo lilikuwa pigo jingine kwake sababu aliamini fika kuwa watakuwa pamoja. Alizungusha Macho kila kona ya ukumbi huo bado hakufanikiwa kuwaona.
Minong’ono ya hapa na pale kuhusu kutoonekana kwa Martin katika Mashindano hayo ilianza kusikika ndani ya Ukumbi. “Leo Martin hayupo?”Watu waliulizana bila Majibu.
******************
Wakati Mashindano yakiendelea ndani ya Ukumbi, Martin alikuwa amekaa na Angela, nje ya Bweni lake wakiongea mambo yao huku akipiga Gitaa na kwa Sauti ya Taratibu akiimba Wimbo aliochaguliwa na Angela Uitwao ‘Do you remember Me’ ulioimbwa na Mwanamuziki wa Kimarekani Mwanadada V. Bozeman. Angela aliupenda sana Wimbo huo.
Kwa kifupi, Martin na Angela pale Nje, walifanya mambo yao mengine kabisa kana kwamba hakuna kilichoendelea Chuoni hapo Usiku huo. Angela aliamua kama Martin hatokwenda ukumbuni basi na yeye hatokwenda pia.
“Huo Wimbo Naupenda sana” Alisema Angela.
“Usijali nitakuimbia Kila utakapohitaji nifanye hivyo” Alisema Martin kisha akasimamisha kupiga Gitaa na kuendelea kusema.
“Hivi unajua Siku za kuendelea kuwepo chuoni zimekwisha, Karibu tunamaliza Chuo” Alisema Martin huku akimwangalia Angela Usoni.
“Siku zinakimbia jamani, ni kama Juzi tu tulipoingia hapa, nakumbuka ulivyokuwa ukiangaika kunipata" Alisema Angela na kuachia tabasamu pana.
Wote wawili walijikuta wakicheka.
“Ni kweli niliangaika sana kukupata mpaka kuna wakati nilitamani kukata tamaa”
“Mwanaume hatakiwi kukataa tamaa, unatakiwa kupambana kumpata mwanamke unayempenda, mwanamke anahitaji kubembelezwa, wakati mwengine mwanamke anakukataa sio kwamba hakupendi bali anataka kupima kiasi cha upendo ulionao kwake”
“Ni kweli lakini Maneno yako yalikuwa makali sana kiasi cha kunikatisha tamaa bado kidogo ningechoka kukubembeleza” Alisema Martin huku akilisimamisha Gitaa lake Pembeni ya Ukuta.
“Nilikuwa nataka kujua uvumilivu wako, unajua kuna wakati katika mahusiano mnapitia mambo mengi ambayo kama wapenzi mtapaswa kuombana msamaha, kusameheana na kuvumiliana, Hata katika maisha ya kawaida kuna wakati mungu anakupitisha katika nyakati ngumu, kama hautakuwa mvumilivu basi unaweza kujikuta unafanya matendo mabaya, uvumilivu ni muhimu katika kufanikisha jambo lolote”
“Ule ulikuwa sio uvumilivu, ilikuwa ni mateso”
“Sio mateso mpenzi wangu, Unajua kuwa wewe ni Mwanaume wangu wa Kwanza, hivyo nilikuwa nataka kujua kama nikikukabidhi moyo wangu utakuwa salama”
“Moyo wako utakuwa salama siku zote za Maisha yetu, halafu nimekumbuka kitu kuna Siku nilikuuliza nini Kirefu cha KJ Kwenye hii Cheni yako” Martin alisema huku akishika Mkufu wa Dhahabu ulioning’inia vizuri kwenye shingo ya Angela.
“Endelea kuwa Mvumilivu kuna Siku nitakwambia Kirefu chake, ila tu fahamu kwamba hizi herufu zina Maana kubwa sana kwangu”
Wakiwa bado wanaendelea kuongea, Ghafla Maria alifika na Kuwakatisha mazungumzo yao.
“Martin Mambo” Maria akiwa ameongozana na Rafiki yao Restuta, alisikika akimsalimia Martin huku akimwangalia usoni mdogo wake Angela.
Maria baada ya juhudi zake za kuwatafuta Ukumbini kushindikana aliona aje kuwaangalia Bwenini.
“Poa Shem, mambo vipi” Martin Alijibu huku akimpa Mkono Maria na rafiki yake.
“Safi tu” Maria aliitikia na kumgeukia Mdogo wake “Angela mbona nakupigia simu haupokei na Martin simu yake haipatikani?”
“Simu yangu nimeiacha kwenye chaja Bwenini na Simu ya Martin imeharibika toka jana ameipeleka kwa fundi ameambiwa kesho asubuhi itakuwa tayari, vipi dada ulikuwa unasemaje?”
“Nilitaka tu kujua uko wapi maana Ukumbini sijakuona na Tulikwenda Mpaka Bwenini kwako haukuwepo”
“Nipo huku dada angu, Martin aliniomba nije kuonana nae”
“Ok…Twendeni Ukumbini basi”
“Natamani kwenda ila sijisikii vizuri shemeji yangu” Martin alidakia na kisha kuendelea “ Wiki nzima hii naumwa ila natumai ukumbini kila kitu kinakwenda sawa” Martin alidanganya bila kujua kwamba Maria anajua sababu iliyomfanya kushindwa kushiriki kwake Mashindano hayo.
“Ok, Pole sana Shem, Umekwenda Hospitali?”
“Alikwenda na kuna dawa alipewa atumie” Angela kwa sauti ya taratibu alimsaidia Martin kudanganya huku akimwangalia Martin usoni na kuachia tabasamu kwa mbali.
“Aya Pole sana basi ngoja sisi tuwaache” Maria aliongea huku akiwapa mikono ya kwa kheri wawili hao na kuondoka mahali pale kuelekea Ukumbini.
*******************
Akiwa ukumbini , Fikra zake zilitawaliwa na Martin, roho yake iliumia sana kuwakuta pale nje pamoja. Alichukia kuona anadanganywa wakati anajua hasa sababu iliyomfanya Martin kushindwa kushiriki Mashindano hayo. Alijitahidi kujizuia chuki yake kwa mdogo wake lakini alishindwa taratibu alianza kumchukia mdogo wake. Aliona Mdogo wake anakuwa kikwazo cha yeye kushindwa kufanikiwa mambo mengi katika maisha yake.
Kiufupi ni mwili wake tu ndiyo uliokuwepo pale Ukumbini lakini fikra zake hazikuwepo kabisa. Fikra zake zilikuwa nje ya Ukumbi, zilimpeleka moja kwa moja mpaka kwenye kule nje, alimwona Martin na Maria pale nje ya Bweni.
Kutokana na Hasira na wivu kuchanganyika, Maria alijikuta anashikwa na kitu Fulani kama Kwikwi kwenye Shingo yake. Alijitahidi kunywa maji lakini ilishindikana, ile hali iliendelea kumtesa. Alijaribu kujizuia asilie lakini kwa mbali machozi yalipenya kwenye Kingo za mboni ya macho yake na kutoka nje. Alichukua Kitambaa na kujifuta Machozi.
Kilichomfanya Maria kulia sio tu upendo wake kwa Martin bali pia aliumia kuona mtu anayekuwa kikwazo cha yeye kutimiza ndoto za kuwa na mwanaume anayempenda ni mdogo wake, Angela.
Alijitahidi kujichanganya na wenzake kwa kuamua kucheza muziki ili hasahau kilichotokea lakini fikra zake hazikumpa ushirikiano bado zilitawaliwa na wivu.
Mashindano yakiwa katika hatua za mwisho, akiwa bado hajasahau kilichotokea dakika 15 zilizopita, Ghalfa Maria alishtushwa na Mlio wa simu yake ya Mkononi, alipoangalia vizuri ulikuwa ni Ujumbe Mfupi wa Maneno.
*******************
“Kaka hapo naomba nauli” Hiyo ilikuwa ni sauti ya Kondakta wa daladala aliyopanda Justine kutoka Kijijini Kalenga kwenda Miyomboni.
“Unapenda kudai nauli mara mbili unafikiri watu tuna pesa za kuokota, nimeshalipa” Justine alisema kwa sauti nzito.
“Haujalipa nauli”
“Jifanye umesahau ukitegemea nitalipa mara mbili, tena nipe chenji yangu kabisa”
“Umetoa Shilingi ngapi”
“Elfu 5”
“Kumbuka vizuri bado haujalipa nauli”
“Nimetoa nauli halafu usinizingue”
“Achana nae anaonekana Mtata huyo” Alidakia Dereva wa Daladala hiyo.
“Dereva acha kuingilia mambo yasio kuhusu” Justine alimjibu Dereva ambae alionekana kuingilia mabishano yao, na kisha akamgeukia Konda “Nipe Chenji yangu, halafu nishushe hapo kwenye tuta”
“Dereva simamisha gari kwanza, nimeibiwa Simu na Pesa zangu” Alisikika Bibi Mmoja ndani ya ile Daladala akilalamika.
******************
Ujumbe Mfupi wa Maneno aliopokea Maria kwenye Simu yake ya Mkononi akiwa Ukumbini, ulionesha kuwa amepokea kiasi cha Pesa kutoka kwa Mama yake, Bi Anna Emmanuel. Kwa mara ya kwanza toka atoke kule Bwenini alitabasamu.
Toka siku aliyofahamu kutoka kwa Master P kuwa Martin hatoshiriki Mashindano hayo kwa kushindwa kulipa Ada ya Muhula huo, Maria alifanya Juhudi za kuwasiliana na Mama Yake ili kuhakikisha anamsaidia Martin kupata Ada. Alifanya Juhudi hizo ili Martin aweze kushiriki Mashindano hayo.
Baada ya Kupokea Pesa hizo, Maria aliona anayo nafasi nyengine ya kuwa karibu na shemeji yake Martin. Alipomshirikisha Restuta kuhusu wazo lake hilo la Kumsaidia Martin ada, Alionekana akimuunga Mkono kwa kuamini kuwa njia hiyo itazidi kumweka karibu na Martin.
Kwa haraka Maria akiwa ameongozana na rafiki Yake walitoka nje ya Ukumbi na kuelekea kwenye moja ya Duka la Wakala kwa ajili ya kutoa Pesa hizo. Walimkuta Mhudumu akijiaanda kufunga Duka.
“Dada samahani nataka kutoa Pesa” Alisema Maria
“Mngechelewa Kidogo tu Mngekuta nimeshafunga” Alisema Mhudumu.
Maria alivyofanikiwa kutoa pesa kwa Wakala, walirudi Ukumbini na Moja kwa moja walikwenda sehemu aliyosimama Master P na kumnong’oneza “Martin yuko wapi”. Maria aliuliza akijifanya kama hajui sehemu alipo Martin. “Nadhani atakuwa Bwenini” alisema Master P. Maria akaendelea “Master P nisaidie kitu, Mzigo huu naomba ukampe Martin, ni Pesa ya Ada, tumia maneno yoyote utakayowezaila usimwambie kama hizi Pesa zimetoka kwangu”. Maria alitaka kufanya siri ili Mdogo wake Angela asijue kinachoendelea.
Baaada ya kusikia maneno hayo kutoka kwa Maria, Master P aliduwaa, Macho ya mshangao yalimtoka. Siku ile wakati wanatoka kwenye Kiwanja cha Mpira wa Kikapu, Master P alijua maongezi yao yaliishia pale. “U cant be serious, Umepata wapi Pesa zote hizi?” Kwa sauti ya Mshangao Master P aliuliza.
“Hayo mengine tutaongea baadae Master P, nenda kwanza kampe hizi Pesa” Maria aliongea huku akimpatia ile Bahasha, kisha akaendelea“Ombi la mwisho, naomba umshawishi Martin aje kuimba, hata wimbo mmoja tu, nitafurahi” Master P aliipokea Bahasha na kwa haraka alitoka nje ya ukumbi kuelekea Bweni la German-America kumfata Martin huku akifikiria Maneno atakayotumia kumshawishi Martin apokee pesa hizo bila kujua kama zimetoka kwa Maria.
“Martin kuna mzigo wako nilitumiwa na Baba yako, amesema ni Pesa za ada halafu alitaka kujua kwa nini haupatikani nikamwambia kuwa simu yako imeharibika” Master P alisema hayo huku akimkabidhi Martin ile Bahasha.
Master P alifikiria kutumia Mbinu hiyo, akijua wazi kuwa kwa kusema hivyo ataweza kupunguza idadi ya Maswali kutoka na urafiki wao wa muda mrefu hadi kufahamiana mpaka nyumbani. Japo Wazazi wa Martin hawakuwai kumtumia ada motto wao kwa utaratibu huo lakini asingeshangaa sana kama wazazi wake wangeweza kufanya hivyo kutoka na Urafiki mzuri uliopo kati yake na Master P.
Taarifa hiyo ya kutumiwa ada na wazazi wake kama alivyoambiwa na Master P, haikumfurahisha tu Martin bali pia iliibua hisia za furaha kwa Angela pia.
Master P hakuchukua muda mwingi Pale, alirudi ukumbini na kumkuta Mshiriki aliyemuacha akiimba akimalizia. Mshiriki huyo alipomaliza kuimba, Master P alipanda Jukwaani na kuchukua Kipaza Sauti na Kusema.
“Mshiriki wetu wa mwisho kutufungia Mashindano yetu ya leo, akiimba wimbo wa “I will make love to you” ulioimbwa na “Boyz II Men” si mwingine bali ni……Martin Jonathan Chota” Ukumbi mzima ulizizima.
Wanafunzi wakiendelea Kushangilia, Martin alionekana akipanda Jukwaani huku akiwa amebebelea Gitaa lake, alianza kuimba na kupiga Gitaa kwa Wakati Mmoja. Kwa Kifupi, Wanafunzi wengi walifurahi kumuona Martin akiimba.
STOLEN LOVE