Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 34,251
- 44,586
NAOMBOLEZA KIFO CHA KAPTENI KOMBA - CHIRIKU ALIYEIMBA
Na. M. M. Mwanakijiji
Taa iliyokuwa inawaka kwa muda mrefu sasa imezimika milele. Taa hii iliwaka na kuangaza katika fani ya sanaa ya uimbaji na iliangaza kwa karibu miaka thelathini na ushee sasa. Iliangaza kwa muda wote na hadi ilipoanza kufifia bado nuru yake ilikuwa inawaangazia wachache. Na wakati ule taa ile ilipokuwa inangara basi ilingara kweli kweli!
Ndege yule aliyekuwa anaimba sana mtini sasa amenyamaza. Chiriku yule aliyeimba na kufundisha, kuhamasisha, kufariji, kukumbusha, kuhamasisha na hata kukorofisha wengine; chiriku yule amenyamaza. Milele. Alipoimba hata wale ambao walikuwa hawajui muziki walijikuta wakitikisa miguu yao mioyo yao ikifuatilia taratibu midundo ya nyimbo zake. Na nyimbo zake zilikuwa maridadi kwelikweli.
Nimesema taa iliyozimika iliwahi kungara; ikafifia na hatimaye imezimika. Naomboleza kifo cha Chiriku wengine walimuita Kinanda si mwingine bali Kapteni John Damian Komba ambaye hadi mauti Ijumaa iliyopita alikuwa pia ni Mbunge wa Mbinga kwa tiketi ya chama tawala Chama cha Mapinduzi. Komba aliwahi kungara bwana!
Alingara
Katika muziki wa kwaya sidhani kama kuna Mtanzania mwingine yeyote ambaye anamfikia Kapteni Komba kwa kudumu kwake katika fani hiyo na umahiri wake wa tungo. Tungo zake zimeacha alama ya kudumu kwenye kumbukumbu ya Watanzania ambao walikuwa wanafuatilia siasa za Tanzania. Hii ni kweli hasa wakati tulipokuwa bado tunapigania Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika.
Komba aliweza kufanya kile ambacho wanasiasa wengi hawakuweza; kulishawishi Taifa na kuwahamasisha vijana. Vijana wengi wa miaka ya themanini mimi mmojawao tulijifunza siasa katika nyimbo za kina Komba; tulielewa maana ya Uzalendo na mapenzi kwa Taifa. Na kila wakati ambapo Taifa lilikuwa linapitia mambo magumu Komba alikuwepo kutuongoza kwa sauti yake.
Nani atasahau maombolezo ya Msiba wa Sokoine aliyekuwa Waziri Mkuu kipenzi cha Watanzania? Nani atasahau hasa wakati ambapo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alikuwa ametangaza kungatuka? Komba akitumia kipaji chake kikubwa alitufanya tuamini kuwa Ali Hassan Mwinyi aliyependekezwa na Mwalimu kushika nafasi badala yake ataweza kulimudu Taifa. Taifa ambalo lilikuwa linapitia mabadiliko makubwa likiwa limepigishwa magoti kutoka katika hali ngumu ya uchumi baada ya Vita na njaa ya miaka ya themanini.
Wimbo wake wa Ali Mwinyi Awamu ya Pili ulivuma na sauti yake imekuwa akiitumia kuwanadi wagombea wa chama chake ngazi ya Urais toka wakati huo. Alitufanya tuamini kuwa madudu yaliyokuwa yameota katika utawala mafisadi wa zama zile yangeweza kuondolewa. Aliimba:
Ali Mwinyi kiongozi wetu, tumpambe maua!
Ali Mwinyi Awamu ya pili, tumpambe maua!
Tumpambe pambe, tumuweke mbele
Tumempa jembe nyundo, afye fyeke
Angoe ngoe, shambe linone kisha tuvune!!
Na wapo walioamini kweli Mwinyi angeweza kusafisha hasa alipokuja na kauli yake ya kufagia na kile kilichoitwa fagio la chuma.
Komba aliimba; aliimba kwenye misiba na aliwashangaza watu kwa uharaka wake wa kutunga nyimbo kiasi kwamba wengine waliamini alikuwa ana nyimbo kwa kila tukio! Fikiria kifo cha Mwalimu Nyerere na jinsi wimbo wa maombolezo ulivyosikika mapema tu baada ya kutangazwa kifo cha Baba wa Taifa. Wasichokijua watu wengi ni kuwa Komba alikuwa ni msanii wa kweli; alijiandaa na kujipanga kwa mambo mambo mbalimbali.
Hata hivyo siri ambayo wengi hawaijui ni kuwa Komba alitumia hazina ya nyimbo za kabila lake; za Kingoni kutengeneza nyimbo nyingi za kwaya yake. Na alifanya kwa namna fulani uimbaji wa Kingoni kujulikana zaidi kuliko bila ya shaka kabila jingine lolote lile. Wangoni kama yalivyo makabila mengine wana tamaduni za kuimba lakini wao wana nyimbo za mavuno, wana nyimbo za kilabuni na wana nyimbo hadi za misiba. Komba alitumia sauti za nyimbo kutoka Kitoto, Lizombe, Chioda n.k kutengeneza nyimbo za kukumbukwa. Alichofanya ni kubadilisha maneno. Lakini pia akiwa mtunzi aliweza kutumia msingi wake wa kuimba kingoni kutengeneza nyimbo nyingine nyingi tu.
Mojawapo ya nyimbo ambazo wengi wanazifahamu sana ni ule wa Nambari wani CCM. NI wimbo wa kingoni ambao una kiitikio cha kukumbukwa kabisa. NI kwa sababu hii Komba alikuwa kipenzi cha wagombea wa Chama cha Mapinduzi.
Wakati huo aliongara alitunga nyimbo za kutukuza Umoja wa Afrika n ahata kusherehekea kwa mfano Uhuru wa Namibia kwa wimbo wake wa Which Way Namibia, The Way To Go ukiwa labda miongoni mwa nyimbo zake chache alizoziimba kwa Kiingereza. Nyimbo nyingi za wakati huo ni lazima zieleweka katika mwanga wa zama hizo chini ya mfumo wa chama kimoja na aliimba akiwa na kikundi cha Jeshi.
Aliimba nyimbo nyingi; za kisiasa, za kijamii n ahata kuhamasisha mabadiliko katika jamii mfano mzuri ni ule wimbo wa Mgeni Kwetu Ameingia au ule wimbo wa Acha Turinge, Kama Siyo Nguvu Zako Mwalimu, Wenyewe kwa Wenyewe Wanagombana, CCM Yabwina, CCM Mbele kwa Mbele ambao aliuimba hivi majuzi na kutukera wengine!
Alingara ndani ya CCM
Mojawapo ambayo nayo ni lazima yakubaliwe kuwa ni kweli ni kwamba inawezekana Komba alikuwa ni sababu ya ushindi wa wagombea wengi wa CCM na labda aliijenga sana CCM mbele ya wananchi kwa nyimbo zake labda kuliko msanii mwingine yeyote. Wasanii wanaotumiwa sasa na CCM kwa mfano wengi hawana umahiri wa kuimba siasa; sidhani hata kama wanafuatilia siasa kivile. Komba alikuwa ni mwanasiasa.
Alisifa chama chake kama wengine wanavyosifia vya kwao; alitukuza chama kilichompa maisha yake na bila ya shaka alijua kuwa mafanikio yake yote yanatokana kwa kiasi kikubwa na kuwa mwaminifu kwa chama chake. Hili tunaweza tusilipende wale ambao si mashabiki wa CCM au wanachama. Tunaweza kuona ni jambo la kukera lakini ndio ukweli. Ukikuta Muislamu anaenda kuswali mara tano kwa siku au ukimsikia Mlokole ananena kwa lugha hakuna cha kushangaza. Huwezi kumlaumu Muislamu kuswali au Mlokole kunena kwa lugha. Au Mkatoliki kila siku asubuhi anawahi kwenda Misa unamshangaa!? Kituko kitakuwa ukimuona Muislamu ananena kwa lugha na Mlokole anaenda kuswali! Hapo patakuwa na maswali. Komba kutetea, kusifia au au kuilinda CCM haijawahi kunishangaza; alifanya kile ambacho wana CCM wa kweli watafanya na wengi wamekuwa wakifanya tayari; kuiweka CCM mbele kwa mujibu wa Katiba ya chama chao.
Alingara na kikundi chake cha TOT na hata kuanzishwa kwa bendi na taarabu na bila ya shaka kuna watu wengi tu ambao na wao maisha yao wanamshukuru Mungu kwa kuwepo kwa Kapteni Komba; kwani kipaji chake kilibeba vipaji vingine navyo vikangara. Wakati ulipofika aliona nay eye aingie kichwa kichwa kwenye siasa na alipoingia alishinda na kuwa Mbunge. Na kama Mbunge tuliona jinsi gani alitukuza CCM. Hata yale malumbano yaliyovuma sana mwaka jana kwenye Bunge la Katiba kuhusiana na Jaji Warioba baadhi yetu tuliona ni katika mwendelezo ule ule wa kuiweka na kukitetea chama chake. Kama wengine wanatetea vyama vyao kwani nini iwe vibaya kwa yeye kutetea chama kilichompa kula yake toka ujana wake?
Ni kwa sababu hiyo basi naamini kumhukumu mtu kwa ukali kwa sababu hatukubaliani naye kisiasa ni mojawapo ya ukosefu mkubwa sana wa hekima. Kushukuru kwamba ati mpinzani wako wa kisiasa kafa ni kutokuwa na maono ya mbali yaliyojaa busara. Wapo ambao bila ya shaka wala kujificha wameshukuru kwa kifo cha Komba wakiamini labda alikuwa kikwazo kikubwa kwa mabadiliko au alikuwa anawakera kwa misiamamo yake Bungeni. Inasikitisha kuwa wapo kweli watu kama hao.
Binafsi siombei wabaya wangu wa kisiasa wafe au wakutwe na mabaya kiasi cha kushindwa kuja kuona mambo ambayo naweza kuyafanya. Natamani waishi maisha marefu waone; waone waliposhindwa wao wengine wanaweza vipi. Natamani waishi maisha marefu ili wapate nafasi ya kuja kukiri ubovu wa sera zao na udhaifu wa uongozi wao. Natamani waishi maisha marefu ili waje kujuta mbele ya safari.
Alikuwepo huko Marekani Gavana wa Jimbo la Alabama kwa jina la George Wallace. Wakati Marekani iko katika vuguvugu la harakati za haki za kiraia (civil rights movement) na wakati Mahakama imeamua kuwa shule zote zitakuwa na haki ya kupokea watu wa rangi zote; hazitobagua tena watu wetu weusi, Gavana Wallace aliapa kuwa hilo halitokuwepo kwenye Jimbo lake. Alipokuwa akiapishwa Januari 14, 1964 aliapata katika kauli yake ambayo inajulikana zaidi kutengana sasa, kutengana kesho, na kutengana milele akimaanisha kuwa jamii za weupe na weusi zitaendelea kutengana katika mambo yao.
Aliishi na akaona mabadiliko; mwaka 1979 alisimama na kuomba radhi kwa misimamo yake ya kibaguzi wa rangi; alikubali kuwa misimao yake na sera zake zilikuwa na makosa. Na alipochaguliwa mara ya tatu kuongoza jimbo la Alabama alionesha mabadiliko kwa kuchagua weusi wengi katika nafasi za uongozi n ahata kuwa na weusi wawili katika Baraza lake la Mawaziri. Aliishi akaona makosa ya sera zake. Miaka ya mwisho ya uhai wake aliwaomba radhi Wamarekani Weusi na alijitahidi kujipatanisha nao. Hakuomba radhi tu bali pia alikana hadharani misimamo yake hiyo.
Ndio sababu nawaombea watawala wetu hawa maisha marefu! Sifurahii kufa kwa binadamu yeyote hasa adui yangu. Adui yangu akifa kabla ya kuona mafanikio yangu miye inanifaa nini? Si bora aishi aje kuona. Na labda aishi zaidi na baadaye ajirudi na anaweza kuwa rafiki yangu?
Maandiko ya Biblia yanasema kuwa Mungu hafurahii kufa kwake mtu mwovu; sasa kama Mungu hafurahii kufa kwa mwenye dhambi mimi ni nani hata nifurahie? Na kama wote sisi ni wenye dhambi kuna furaha gani kwa mwenye dhambi mmoja kufurahia kifo cha mwenye dhambi mwingine isipokuwa kama mtu hana hekima tu? Lakini cha kusikitisha zaidi ni kuwa mtu unaweza kweli kuna na haki ya kufurahia kifo cha mtu mwingine; kama wewe mwenyewe umepata jibu la kuwa hutakufa au unajua utakufa linin a vipi! Kama hujui mbele ya mauti nyenyekea. Lililomkuta, litatukuta na litawakuta watoto wetu pia na litawakuta hata wanaokuja nyuma ya watoto wetu. Hakuna mkwepaji. Nawasihi wale waliofurahia mauti ya Komba, kuweni na hekima kidogo tu. Hakuna cha kufurahia mwanadamu anapokufa; hata kama ni adui kabisa. Tunapotetea uhai hatutetei wa rafiki zetu tu; bali hata wa adui zetu. Utu wa binadamu haujali binadamu huyo ni nani. Ndio maana hasa ya kuwa na utu. Utu unaochagua mtu si utu huo ni kutu hiyo!
Ni kweli kuwa kwa kuamua kutukuza chama chake Komba alipoteza mashabiki wengi wa nyimbo zake; lakini kutokuwa shabiki au mpenzi wa nyimbo zake hakuondoi ukweli wa kukiri kipaji alichokuwa nacho. Ninamshukuru Mungu kwa maisha yake kwani hata mimi leo hii katika mambo ya sanaa hasa ya kwaya na nyimbo nimejifunza mengi kutoka kwake na naweza kusema kuwa bila kuwahi kukutana naye au hata kumuona jukwaani nilipata nafasi ya kujua maana ya kuwa mtunzi na mwimbaji. Na ndio sababu hasa naomboleza.
Walimuita Chiriku. Sasa amenyemaza. Tulipata heshima na bahati ya kushuhudia kipaji hiki pamoja na mapungufu yote ya kibadamu kikingara mbele yetu. Na kipaji alikuwa nacho bwana.
Pumzika kwa Amani Kapteni. Poleni wafiwa, poleni Watanzania, Poleni wana CCM, poleni wasanii wenzangu.
Amina
Last edited by a moderator: