Kwanini ni rahisi kijana asiye na kipato kushawishiwa na makundi mabaya?

Aug 10, 2023
1
2
Global peace Foundation.PNG

Kila mwaka idadi kubwa vijana hapa nchini wanamaliza masomo yao katika ngazi mbalimbali za elimu. Taasisi za elimu kuanzia darasa la saba, kidato cha nne, kidato cha sita, vyuo mbalimbali vya ufundi na vyuo vikuu vinazalisha idadi ya wahitimu kila msimu.

Takwimu za Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) zinaonyesha ongezeko la udahiri wa wanafunzi wa ngazi ya cheti mpaka Uzamivu (PhD) wa taasisi za elimu ya juu 213,829 (2017/17) mpaka kufika 314,643 (2022/23). Hii inatupa picha ya idadi kubwa ya wanafunzi wanaomaliza licha ya kwamba wachache wao wanakatiza masomo. Wahitimu hao wanaondoka wakiwa na matumaini ya maisha bora kwa kupata ajira zenye tija.

Lakini hali halisi ikoje? Pengine, wote tukawa na jibu kwa sababu sisi ni sehemu ya jamii ambayo vijana hawa wapo. Huenda katika familia zetu ama jamii zetu tumeshuhudia vijana hawa wakihangaika kupata walau kibarua cha kujiingizi kipato. Na si ajabu hata kukutana na wahitimu wa vidato na shahada mbalimbali wakiwa katika hekaheka hizi mitaani. Kwa kipindi kati ya mwaka 2015 hadi sasa kumekuwa na wimbi kubwa la vijana wa namna hii. Na mara nyingi Vijana wengi ni wale wanaotoka katika kaya masikini, ambapo mpaka anamaliza masomo kuna gharama kubwa imelipwa na familia. Kutokana na hili kijana anajikuta ana mzigo mkubwa wa matazamio ya wazazi, ndugu na jamaa nyuma yake. Hili huongeza sonona kwa kijana.

Hivyo basi, athari zake ni vijana kujikuta wanajiingiza kwenye vitendo vibaya ili mradi tu maisha yaende wakati akipambana. Lakini wapo wachache wanaoamua kuweka elimu zao pembeni na kufanya kazi ambazo zinaonekana hazina staha. Niliwahi kumuona binti mmoja, mhitimu mmoja wa Chuo Kikuu akiuza mahindi ya kuchoma barabarani. Hili ni jambo la huzuni.

Lakini suluhisho la kudumu ni nini? Pengine tunaweza kujifunza kwa ushauri alitoa hivi karibuni, Mh. Christopher Ngubi, Mkuu wa Wilaya Kilwa ambapo aliwasihi vijana kuwa wasione aibu kuweka usomi pembeni na kutafuta njia mbadala ya maisha.

Kiongozi huyo aligusia kuwa maarifa peke yake hayatoshi hasa katika mazingira yetu bali ujuzi. Kijana badala ya kukumbatia cheti cha shahada yake anaweza kujifunza stadi maalum ambazo zinahitajika mtaani kwa sasa kama ufundi magari, mapishi, ubunifu mashine, kilimo cha kisasa, uvuvi n.k.

Aidha, Mh. Christopher Ngubi alitoa rai kwa taasisi zetu za elimu kubadilisha mfumo wa elimu. "Badala ya kutoa shahada zilizopitwa na wakati tukazanie zaidi elimu ya ufundi. China na nchi kadhaa zinazoendelea zimetoa mfano bora wa njia ya kusaidia makundi ya vijana" aliongeza.

Akizungumzia mikakati ya Wilaya ya Kilwa, Mh. Christopher Ngubi, amesema kutaanzishwa kituo Maalum cha Vijana (ICT Center) ambacho kitahusika na kuratibu mipango ya kusaidia vijana. Kituo hicho kitaanzishwa kwa ushirikiano na Shirika la Global Peace Foundation na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Vijana wataweza kupata taarifa za fursa mbalimbali za biashara, ajira, masomo na mikopo na mengine mengi kupitia kituo hicho.

Aidha kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Mh. Filberto Sanga alitanabaisha kwamba kundi la vijana lina changamoto nyingi. Kundi hili linahangaika kujiandaa na maisha ya sasa na baadae.

Anasema “Kila kijana anatamani kupata maendeleo kwa kasi, wakati huo anashindana na wenzake bila kujali wenzake wanatumia mbinu gani kupata mafanikio. Na yeye anajikuta anatumia njia ambazo hazitakiwi ili afanikiwe haraka. Hata akiambiwa ‘pale kuna madawa ya kulevya, kasafirishe kule utapata utajiri’. Yeye yuko tayari! Akisikia pale kuna vitu vya kuiba, yeye anakwenda anaiba akitengemea atapata utajiri”.

Mheshimiwa Sanga anaendelea “Hata kwenye uvunjifu wa Amani katika mataifa mbalimbali, sehemu kubwa wanaotumika ni makundi ya vijana. Hata hapa kwetu, wahalifu hulenga kutumia vijana”.

Mratibu wa Masuala ya Vijana katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Nassibu Richard Mwaifunga nae kwa upande wake aliongelea kwa undani fursa zinazotolewa na Serikali kusaidia vijana kujiinua kiuchumi. Aligusia nafasi za mikopo ya mtu mmoja mmoja, masomo ndani na nje ya nchi na fursa za kusaidia vijana waliomaliza masomo kupata ujuzi kivitendo.

Mmoja wa vijana washiriki naye anaongeza “Kama umekosa ajira usikae tu. Inabidi vijana tujiongeze kwa kuangalia fursa ambazo zipo. Ili kuweza kuwa na Amani lazima tufanye kazi kwa bidii kujitafutia riziki. Tusiogope kuchukua mikopo bali tuone kuwa kama ni fursa. Kinachotakiwa ni uaminifu tu”. Anaeleza Jane Songalele kutoka Nyasa.

Makala hii imetokana na zoezi la uandaaji mradi wa Dumisha Amani kwa Maendeleo Endelevu unaosimamiwa na Shirika la Global Peace Foudation Tanzania kwa ushirikano na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Ofisi ya Waziri Mkuu unakelezwa katika Mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara.
 
Back
Top Bottom