Kwanini hadi leo Filbert Bayi anatajwa na kuheshimika sana kwenye riadha? Soma hapa

MamaSamia2025

JF-Expert Member
Mar 29, 2012
10,217
22,280
Binafsi nimekuwa nikimfahamu Mzee Bayi toka nikiwa mdogo ila sikuweza kujua kiundani kwamba kwanini hadi leo dunia inamheshimu mno kwenye riadha wakati wapo wanariadha wengi wa enzi zake waliofanya vizuri na hatuwakumbuki.

Serikali yetu inabidi ibadilishe mitaala ili historia za mashujaa wetu zielezewe kiundani badala ya hii ya juu juu kusema Bayi alivunja world record ndo inaishia hapo. Sasa leo nitaelezea jinsi kwanini Mzee Bayi hadi leo anasifika kwa jinsi mimi binafsi ninavyomjua pia kwa msaada wa machapisho mbalimbali. Twende pamoja.

Filbert Bayi Sanka amezaliwa Juni 23, 1953 huko Karatu, Arusha. Ni mwanariadha wa zamani wa Tanzania wa mbio za kati miaka ya 1970 hadi 1980. Pia Mzee Bayi ni mjumbe wa kamati ya ufundi ya chama cha riadha duniani na ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania.

Rekodi mbili za riadha za dunia zilizowekwa na Filbert Bayi zimeorodheshwa katika Makumbusho ya Riadha ya Dunia (Mowa) huko Monaco, Ufaransa yalipo makao makuu ya shirikisho la riadha la dunia

Nje ya riadha Filbert Bayi kawekeza kwenye mambo ya elimu kwa kuanzisha shule za chekechea hadi kidato cha sita huko Kimara Dar es Salaam na Kibaha, Pwani. Shule zake pia zinajihusisha kwa karibu sana na vipaji mbalimbali kuanzia soka, riadha, na vingine. Ni shule yenye Multi-purpose Sports Complex yenye viwango vya olimpiki.

BAYI KAWEKA ALAMA GANI ZISIZOFUTIKA?

Baada ya utambulisho huo mfupi turudi kwenye swali letu la msingi ili tujue Bayi alikuwa mwanamichezo wa aina gani na alama alizoweka hadi leo hii anaheshimika duniani na kusifiwa dunia nzima.

Mafanikio ya Bayi yanatajwa zaidi kwenye zile medali ambazo alivunja rekodi za dunia lakini ieleweke kwamba Mzee Bayi kashinda medali nyingi sana kwenye mashindano mbalimbali aliyoshiriki. Pia tofauti na wanariadha wengi, Filbert Bayi ana medali za mashindano yote makubwa yanayotambulika na shirikisho la riadha la dunia yaani kuanzia mashindano ya taifa, Afrika Mashariki, Africa games, Ubingwa wa dunia, Olimpiki na yale ya jumuiya ya madola. Ndoto za wanariadha wengi ni kushinda medali ya olimpiki... Mzee wetu kakichafua sana huko kwenye olimpiki.

Kilichomfanya Bayi aweze kuwa bingwa kwa miaka mingi ni nidhamu yake ya ndani na nje ya riadha. Filbert Bayi anatajwa kama mwanariadha wa mfano linapokuja suala la nidhamu kwa kazi yake.

Nidhamu yake ilimfanya abaki kwenye ubora wake kwa miaka mingi sana. Kwa msiofahamu ni kwamba Mzee Bayi kabla ya kustaafu kashiriki pia mbio za mita 800, 5000, 10000, 21km (Half marathon) na 42km (Marathon) na sio mbio za 1500m pekee. Inahitaji utulivu wa hali ya juu kuweza kumudu mbio zote hizo kwa takribani miaka 20 (1969 - 1989).

Jambo lingine linalomfanya Bayi awe kwenye kumbukumbu za wengi ni mtindo wake wa kukimbia anapokuwa mashindanoni. Bayi alikuwa tangu kipenga kinapigwa anakaa mbele mwanzo hadi mwisho wa mbio. Yaani anamaliza biashara mapema kabisa. Tazama video.

Mwenyewe anadai alikuwa akifanya hivyo kwasababu hakuwa na mwili mkubwa kulinganisha na wapinzani wake wengi hivyo kuchelewa kuliamsha ingeweza kumgharimu hasa kwenye ile finishing time. Kwahiyo kwa usalama ni kuchomoka tu mapema.

Rekodi ya kwanza ya dunia;

Alama yake kubwa zaidi aliyoiweka ilikuwa kwenye fainali ya mita 1500 katika Michezo ya Jumuiya ya Madola ya 1974 huko Christchurch, New Zealand, aliposhinda medali ya dhahabu mbele ya mwanariadha wa New Zealand John Walker na Mkenya Ben Jipcho. Bayi aliweka rekodi mpya ya dunia ya dakika 3:32:16s, iliyoidhinishwa na IAAF kama 3:32.2s, na Walker akaenda chini ya rekodi ya zamani ya dunia iliyowekwa na Jim Ryun pia.

Hii ina maana mshindi wa kwanza na wa pili walivunja rekodi ya dunia iliyokuwepo... hakika yalikuwa maajabu. Nafasi ya tatu Jipcho, nafasi ya nne Rod Dixon, nafasi ya tano Graham Crouch, namba sita Mike Boit na namba saba mtanzania Suleiman Nyambui.

Pia mtu wa tatu hadi saba nao walivunja rekodi zao binafsi. Kimsingi hiyo fainali ilikuwa ya moto mno. Fainali hiyo imeorodheshwa kama moja ya mbio kubwa zaidi na za kipekee za 1500m za wakati wote.

Upekee mwingine wa hii rekodi ya Bayi kwenye mashindano ya jumuiya ya madola ni kuchukua miaka mingi sana kuvunjwa. Tangu ilipowekwa mwaka 1974 imekuja kuvunjwa mwaka 2022 na mwanariadha wa Australia Oliver Hoare kwa muda wa dakika 3:30:12s huko Birmingham.

Rekodi ya Bayi kwenye jumuiya ya madola imevunjwa baada ya miaka 48. Kumbuka kwenye Commonwealth games kuna wakenya wa kutosha.

Rekodi ya pili ya dunia;

Mnamo 1975, Bayi alivunja rekodi ya dunia iliyowekwa na Jim Ryun ya mbio za maili moja iliyodumu kwa miaka minane kwa muda wa dakika 3:51.0 mjini Kingston, Jamaika tarehe 17 Mei. Rekodi hiyo ilidumu kwa muda mfupi kwani mwanariadha John Walker aliivunja mnamo Agosti 12 ya mwaka huo huo, akitumia 3:49.4 huko Gothenburg. Cha kushangaza kila mwaka wamarekani huikumbuka siku rekodi ya bingwa wao ilivyovunjwa. Wenyewe huwa wanaiita MIRACLE MILE.

Ilitarajiwa ushindani wa Bayi-Walker ungeendelea lakini ilishindikana kwa sababu Tanzania ilisusia Michezo ya Olimpiki ya 1976 huko Montreal, Canada. Hata hivyo, kwa vile Bayi alikuwa akiugua malaria muda mfupi kabla ya Olimpiki, huenda asingeweza kumshinda Walker hata kama kusingekuwa na kususia.

Bayi alishinda medali ya fedha katika mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji kwenye Olimpiki ya 1980 huko Moscow. Alikimbia kwa dakika 8:12.5 nyuma ya Bronisław Malinowski.

Alishinda mbio za mita 1500 kwenye All-Africa games ya 1973, huku Kipchoge Keino akishinda medali ya fedha. Bayi alifanikiwa kutetea taji lake katika Michezo ya All-Africa ya 1978.

Kiukweli Mzee Bayi ni tunu ya taifa na inapaswa historia yake isimuliwe vizuri mashuleni ili kuweza kuwahamasisha vijana kuwa na nidhamu kwa vipaji vyao. Tukiachana na nidhamu yake akiwa kwenye riadha bado Mzee Bayi ni mfano wa kuigwa kwa nidhamu ya kawaida kwasababu kinyume na hivyo asingeweza kuwa kiongozi wa shirikisho la riadha duniani wala kuwa katibu mkuu wa kamati ya olimpiki.

Filbert-bayi.jpg
Filbert-Bayi-world-record-1500m-1974.jpg
Filbert Bayi bado ni jina linaloheshimika hadi kwa makampuni makubwa ya biashara kama PUMA, ADIDAS, NIKE nk. Ni somo tosha kwa vijana wetu wanaofanya upuuzi kwa kujidanganya wanakuza "brand". Mzee wetu hakutumia skendo yoyote kukuza jina.

Kitu pekee Mzee Bayi aligonga mwamba ni siasa hasa za CCM. Mara kadhaa alijaribu kuomba nafasi ya kugombea ubunge Karatu kupitia CCM ila wajumbe wakamtosa. Lakini pia hata kama wajumbe wangempitisha asingeuweza muziki wa Dr Slaa enzi hizo.

Mimi namshukuru sana Mungu kwa kutupa huyu Filbert Bayi. Namshukuru pia Luteni mstaafu wa JWTZ Filbert Bayi kwa maisha yake yaliyojaa mambo mengi mazuri ya kuigwa hasa kwa vijana.

filbert-bayi-1974.jpg
Medal-Ceremony-Mens-1500m-Christchurch-1974.jpg
20220918_214353.jpg
20220918_214337.jpg
 
Mzee alikuwa kweli anajua kukimbiza upepo
Nje ya riadha kwa uchache bayi ni mtu asiye na majivuno shuleni kwake pale wanafunzi wake alitulea kama watoto wake hasa masuala ya misosi 😄
 
ibadilishe mitaala ili historia za mashujaa wetu zielezewe kiundani

Na pia CCM bila kusahau serikali zitambue kuna historia za ushujaa za waTanzania nje ya siasa za CCM.

Kuna mashujaa waliofanya au kutoa mchango ktk michezo mbalimbali, utabibu, kijeshi, waalimu, wafanyabishara n.k n.k Wigo wa mashujaa utanuliwe na tuwaone katika maktaba za taifa, makumbusho ya taifa, wakihojiwa ktk media n.k
 
Na pia CCM bila kusahau serikali zitambue kuna historia za ushujaa za waTanzania nje ya siasa za CCM.

Kuna mashujaa waliofanya au kutoa mchango ktk michezo mbalimbali, utabibu, kijeshi, waalimu, wafanyabishara n.k n.k Wigo wa mashujaa utanuliwe na tuwaone katika maktaba za taifa, makumbusho ya taifa, wakihojiwa ktk media n.k
Kweli kabisa
 
Pamoja na hayo Yote, ila Filbert Bayi ndiye Chanzo Cha Migogoro kwenye Shirikisho la Riadha Tanzania, amezuia Wanariadha wengi wasivunje Rekodi yake Kwa kufanya figisu Mbalimbali, amekula au ameuza foundation ya John Stephen Akhwari Ili yeye aonekane ndiye mwenye sifa zaidi, amejimilikisha Shule ya kibaha ambayo ni Pesa za Olimpiki Solidarity kwa ajili ya kukuza Vipaji vya watanzania. ametafuna pesa Nyingi zinazotolewa na IOC toka aingie madarakani.
 
Hawa ndio watu majina yao yawekwe kwenye kumbukumbu kama Madaraja na vivutio na sio wanaweka majina ambayo baadae mnaanza kuyakataa kwa mabaya yao

Hakuna wa kuwakumbuka?
Mashujaa wetu hao ndio walifanya Tz ikajulikana kimataifa miaka hiyo Dream line ya Bayi hatutaisahau tuliokuwepo miaka hiyo
 
Hawa ndio watu majina yao yawekwe kwenye kumbukumbu kama Madaraja na vivutio na sio wanaweka majina ambayo baadae mnaanza kuyakataa kwa mabaya yao

Hakuna wa kuwakumbuka?
Mashujaa wetu hao ndio walifanya Tz ikajulikana kimataifa miaka hiyo Dream line ya Bayi hatutaisahau tuliokuwepo miaka hiyo
Baada ya hapo , amemsaidia nani kabla na baada ya umaarufu au Uongozi wake?
 
Una akili za kimaskini sana. Badala ya kupambana na wewe ufanikiwe unasubiri Bayi akusaidie? Jiulize wewe hadi kufika hapo umeshawahi kumsaidia nani hata ngazi ya familia yako?
Filbert Bayi ni Mwizi , ni Jambazi na mfujaji wa mali za umma na kuwagandamiza wanariadha wenzake. Endelea kumlamba miguu , mwisho wake umefika.
 
Baada ya hapo , amemsaidia nani kabla na baada ya umaarufu au Uongozi wake?
Kuna barabara iko Hatton Cross lnaitwa Dick Turpin Way alikuwa mwizi balaa mpaka wakaweka kumbukumbu yake

Na sisi wahenga tumeona majina mengi ya watu mashuhuri yakitumika sehemu nyingi

Hata F Bayi kuna shule kama Tatu zinaitwa kwa Jina lake

Na kuna Filbert Bayi Foundation pia ambayo nafikiri hujawahi hata kuisikia
 
Kuna barabara iko Hatton Cross lnaitwa Dick Turpin Way alikuwa mwizi balaa mpaka wakaweka kumbukumbu yake

Na sisi wahenga tumeona majina mengi ya watu mashuhuri yakitumika sehemu nyingi

Hata F Bayi kuna shule kama Tatu zinaitwa kwa Jina lake

Na kuna Filbert Bayi Foundation pia ambayo nafikiri hujawahi hata kuisikia
Mweleweshe huyo
 
Back
Top Bottom