Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,809
- 15,443
Ni vyema kuwa na upendo kama watoto wadogo maana hata sisi kama watu wazima tumezaliwa tukiwa na upendo ila katika makuzi yetu tunanyang'anywa huo upendo na na ndiyo maana tunaishi kwa chuki na visasi tofaui na watoto ambao hugombana lakini punde tu husahau na kucheza pamoja kwa furaha na amani wakiwa wamesahau tofauti zao......
Kuwa na upendo: Ninaposema upendo sina maana ya mapenzi, nina maana pana zaidi. Ili uwe na upendo kamili, zingatia yafuatayo:-
kujipenda- jipende wewe kwanza. kujipenda wewe haina maana ya kuvaa vizuri ingawa ni muhimu, haina maana ya kula vizuri ingawa ni muhimu, au kuoga kila baada ya masaa mawili, ni zaidi ya yote haya. Kujipenda maana yake ni kujikubali wewe kama ulivyo, kujipokea wewe kama ulivyo, kuamini kwamba umekamilika kama ulivyo bila kutaka kujibadili kuwa mtu mwingine, bila kujali elimu uliyonayo, uwezo ulionao, uzuri au ubaya ulionao, umaarufu uliuonao au kasoro zozote ulizonazo. Ni kuamini kwamba wewe ni sawa na mtu mwingine yoyote. Ni kutokujiona kwamba wewe una uwezo kuliko watu wengine (kujipandisha), lakini pia kutokujiona kwamba wewe huna uwezo kama watu wengine (kujishusha). Ukiweza kujipenda, inakuwa rahisi sana kuwapenda watu wengine, lakini ukishindwa kujipenda, ni ndoto kuwapenda watu wengine, hii ni kanuni ya kimaumbile.
kupenda- kupenda maana yake ni kumkubali na kumpokea mtu mwingine kama alivyo na mapungufu yake, na kasoro zake, na umaarufu wake, na uwezo wake bila ya kutaka kumbadilisha awe mtu mwingine au awe kama wewe, ni kumuacha mtu mwingine aendelee kuwa yeye, bila kutaka kumbadilisha awe mtu mwingine. Usijaribu kumbadili mtu mwingine kwani hutaweza. Mtu pekee unayeweza kumbadili hapa duniani na akawa vyovyote unavyotaka ni mmoja tu, mtu huyo ni wewe mwenyewe. Hivyo wewe ukibadilika, na ukafanya yale yanayokufurahisha wewe na wengine, ni rahisi sana watu wengine kubadilika kupitia kwako (matendo yako mema).
kupendwa- maana yake ni watu wengine kukukubali au kukupokea wewe kama ulivyo na mapungufu yako, na kasoro zako, umaarufu wako, umaskini wako, uwezo wako, bila kutaka au kufanya jaribio la kukubadili uwe kama wao au mtu mwingine. Jukumu hili la kupendwa siyo lako, ni la upande wa pili, ni la mtu mwingine. Jambo la kusikitisha ni kwamba kila binadamu anataka kupendwa lakini yeye hajipendi na hayupo tayari kuwapenda watu wengine. Ni mtoto peke yake ndiye anayetaka kupendwa tu bila yeye kuwapenda wengine. Hivyo wale wanaotaka au wanaodai kupendwa ni watoto wadogo, wamekuwa kimwili lakini kiakili ni watoto wa miaka miwili au mitatu. Mtu mzima hahitaji kupendwa, yeye kazi yake na jukumu lake ni kujipenda yeye na kuwapenda watu wengine bila kudai malipo, bila kuchoka. Mungu anawapenda wanadamu kama walivyo pamoja na mapungufu yao yote, hajafika mahali akasema amechoka kukupenda, hivyo na wewe usichoke kupenda hata kama wewe hupendwi. Lakini haijawahi kutokea kwa mtu anayejipenda na kuwapenda watu wengine lakini yeye watu wasimpende, haijawahi, sijawahi kuona, ni lazima atapendwa sana na watu. Ni kama ilivyo kwa Mungu, anapendwa na kila mtu.
upendo- maana yake ni kujipenda+kupenda+kupendwa (soma maelezo hapo juu). Lakini kumbuka kwamba ili upendo ukamilike ni lazima uzungukwe na chuki, upendo bila chuki haufai kuitwa upendo, chuki hukamilisha upendo, huufanya upendo uwe na maana. Mwanamume bila mwanamke hajakamilika, kumbuka kila jambo lina pande mbili, na pande hizi hazipingani, ila zinakamilishana. Kumbuka pia kwamba, bila Ibilisi hakuna Mungu (najua utabisha, lakini kubisha kwako hakutabadili ukweli, ukweli utabaki kuwa ukweli) Kuna watu huwa wanaomba Ibilisi aangamie, nimesikia maombi haya tangu nikiwa mdogo na mpaka leo yanaendelea lakini Ibilisi haangamii, ukweli ni kwamba haitatokea akaangamia, na kama itatokea akaangamia, hata Mungu naye ataangamia au atakosa maana. Watu wanamuabudu Mungu kwa sababu ya Ibilisi, kama ikitokea Ibilisi akaangamia kuna haja gani ya kumwabudu Mungu?