Hakuna ibara ya katiba ya CHADEMA inayoeleza kwamba mavazi ya wanachama ni aina ya nguo ambazo zinajulikana kama kombati.
Nimemsikia kwamba kama kombati zinazidi kuingia bungeni, basi yanaweza kuanza mashindano ya kuvaa kombati, wengine wakaja na ya kijani.
Cha msingi kuangalia ni kwamba je hilo vazi ni la heshima au vipi. Je, hilo linaloitwa kombati linakatazwa na sheria gani za Tanzania. Maana kombati za jeshi zinakatazwa na wanavaa wanajeshi tu.
Kama kuna sheria inakataza vazi kama wanayovaa viongozi wa CHADEMA basi vazi hilo lipigwe marufuku bungeni na atakayevaa afukuzwe.
Kuna mkuu wa mkoa fulani aliyekuwa mwanajeshi huwa tunasimuliwa kuwa aliwahi kufukuzwa bungeni kwa sababu alivaa nguo isiyostaili. Sijui ni kweli au la.
Mwaka 2006, Samwel Sitta alimtoa nje Amina Chifupa kwa sababu alivaa aina fulani ya kofia.
Lakini mavai ni vigumu kusema yanaishia wapi. Julius Nyerere alikuwa haachani na kifimbo, pamoja na kwamba kilitungiwa majina mengi. Keneth Kaunda hakuachana na kitambaa. Leo mtu akiingia bungeni na kitambaa cheupe kwa mawazo kama haya watamfananisha na mpenzi wa Kingi Kiki mwenye ule wimbo wa {Nainua mikono mama, kitamba cheupe, ishara ya mapenzi mama, Yee Shibola}!
Ibara ya 143 (1) ya kanuni za bunge inasema hivi: {Mbunge anayeingia kwenye Ukumbi wa Bunge atawajibika kuvaa mavazi ambayo ni safi na yenye kuhifadhi heshima yake, hadhi ya Bunge na utamaduni wa nchi, kama ilivyoainishwa katika Kanuni hii.}.
Je, cheni za mguuni wanazovaa wabunge wanawake ni utamaduni wa nchi? Na kama si utamaduni wa Tanzani, je huwa zinasemwa kuwa ni utamaduni wa watu wa aina gani hapa duniani?
Kama sababu ya kukataza kombati ni kwa sababu eti wengine watakuja na za kijani, basi hilo haliwezi kuzuilika kwa sababu mtaani kina mama wanavaliana khanga hadi utachoka.
Humohumo bungeni, je, Mwigulu Nchemba haachani na scarf ya CCM. NI ya CCM kwa sababu inavaliwa na Chipukizi wa CCM na ina rangi za bendera ya CCM tofauti na hizo kombati za CHADEMA ambazo hazina rangi ya Chadema.
Wakati mwingine huwa tunatumia maneno kwa kukurupuka. Hivi neno "Kombati" ni nini? Je, lina maana kama hiyo waliyouliza wabunge bungeni jana?
Hapana. Mimi nimefungua dictionary yangu hii {Kamusi Ya Kiswahili Sanifu, ISBN: 9780195732221}. Kwenye ukurasa wa 192, neno Kombati limefafanuliwa hivi:
Kombati=wingi wa ukombati.
Hapa haikutosha maana ilibidi napo nitafute maana ya ukombati ambayo nimeipata kwenye ukurasa wa 431
Ukombati=
1: ufito mdogo utumikao kujengea nyumba ambao hufungwa kiambazani kabla ya kukandika.
2: mti mwembamba mrefu: uwati
Hivyo, hii ni dhahiri kwamba kumbe neno kombati wanaotaka kukataza zile nguo, basi wanajua walikoliokota. Si neno rasmi la kiswahili na waliodai hivyo hawajui kama wale waliosema neno IMPOTENCY ni matusi.
Kwa hiyo, kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili, lile vazi linalovaliw amle bungeni si kombati. Ni vazi tu kama mengine. ni vazi la heshima kwa mujibu wa kanuni za bunge nitakazoziorodhesha baada ya maoni yangu haya. Ni vazi ambalo haliko affiliated na Chama kama scarf ya Mwigulu. Haliko affiliated na Chama kama khanga yoyote au fulana yoyote ya chama chochote.
Hakuna tofauti na kofia aliyokuwa anavaa Adam Sapi Mkwawa akiwa popote na hakuwahi kuzuiwa. Kofia ile alikuwa anaenzi utamaduni wa wahehe.
Kama Chadema wakizuiwa kuvaa haya mavazi ambayo kimakosa wanayaita "kombati", basi kuna hatari kesho yake wakaja na suti za kawaida tu lakini zimeandikwa PEOPLEEEEEEEEES POWEEEEEEEER. Je ndilo wanalotaka huko bungeni?
Nimeandika vya kutosha na nimesema kuwa nitaweka hapa chini kanuni za bunge zinazo-guide mavazi mle ili kila mmoja apime hizo wanazoiita kombati zina kosa gani kwa nchi, kimaadili au kanuni za bunge:
*****************
Ibara 146:
(1) Mbunge anayeingia kwenye Ukumbi wa Bunge atawajibika kuvaa mavazi ambayo ni safi na yenye kuhifadhi heshima yake, hadhi ya Bunge na utamaduni wa nchi, kama ilivyoainishwa katika Kanuni hii.
(2) Vazi Rasmi la Spika na Naibu Spika litakuwa ni joho lenye kuonesha rangi za Bendera ya Taifa, Nembo ya Taifa na baadhi ya mazao makuu nchini, lililoshonwa maalumu kwa ajili hiyo, ambalo litavaliwa juu ya vazi lolote ambalo ni vazi rasmi kwa Wabunge.
(3) Vazi rasmi kwa Wabunge litakuwa lolote kati ya yafuatayo:-
(a) Kwa Wabunge wanawake:-
(i) vazi lolote la heshima yaani ambalo si la kubana mwili, lisiloonesha maungo ambayo kwa mila na desturi za kitanzania hayapaswi kuoneshwa na ni refu kuvuka magotini;
(ii) gauni la kitenge au blauzi inayovaliwa na kitenge au sketi ya rangi yoyote;
(iii) kilemba cha kadri au mtandio;
(iv) suti ya kike; na
(v) vazi linalovaliwa wakati wa eda.
(b) Kwa Wabunge wanaume:-
(i) suti ya Kiafrika au safari ya mikono mirefu au mifupi yenye ukosi au shingo ya mviringo na yenye fulana au bila fulana ndani, ya rangi moja, isiyokuwa na nakshi, pamoja au bila baragashia;
(ii) vazi la kimwambao yaani kanzu rasmi na nadhifu, koti, baraghashia na makubadhi au viatu;
(iii) suti kamili ya kimagharibi ya rangi kadri isiyomeremeta;
(iv) koti aina ya blazer na tai, pamoja na suruali yoyote ya heshima; au
(v) tarbushi na kilemba cha Singasinga, au kilemba chochote kinachovaliwa kwa mujibu wa masharti ya imani au mila.
(4) Vazi Rasmi la Katibu na Wasaidizi wake Bungeni litakuwa kama ifuatavyo:-
(a) Kwa Makatibu wanaume:
(i) suti kamili ya kiafrika au safari, yenye ukosi au shingo ya mviringo na mikono mirefu au mifupi ya rangi nyeusi au bluu; au
(ii) suti kamili ya kimagharibi ya rangi nyeusi au bluu na shati jeupe na tai.
(b) Kwa Makatibu wanawake:
Suti ya rangi nyeusi au ya bluu na shati jeupe na tai.
(c) Makatibu na Wahudumu watavaa mavazi maalumu wakati wa shughuli maalumu za Bunge.
(5) Mpambe wa Bunge na Wasaidizi wake ndani ya Ukumbi wa Bunge watavaa mavazi rasmi ambayo yataamuliwa na Spika.
(6) Spika anaweza kwa sababu maalumu, kumruhusu mtu mwingine anayehusika na shughuli za Bunge kuvaa viatu ambavyo sio rasmi.
(7) Mbunge yeyote anaweza kutoa taarifa Bungeni iwapo Mbunge mwingine ataingia kwenye Ukumbi wa Bunge akiwa na mavazi yasiyoruhusiwa kwa mujibu wa Kanuni hii.
(8) Spika atakaporidhika kuwa Mbunge aliyetolewa taarifa kwa mujibu wa fasili ya (7) ya Kanuni hii hajavaa mavazi rasmi ataamuru Mbunge huyo atoke nje ya Ukumbi wa Bunge.
(9) Mbunge aliyetolewa nje kwa mujibu wa fasili ya (8) ya Kanuni hii hataingia ndani ya Ukumbi wa Bunge hadi pale atakapokuwa amevaa mavazi rasmi.
*****************