Kumalizika kwa ziara ya Qin Gang ni mwanzo mzuri kwa diplomasia ya China barani Afrika kwa mwaka huu

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,036
VCG111417481045.jpg


Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Qin Gang amemaliza ziara yake ya siku tano barani Afrika ilivyomfikisha Ethiopia, Gabon, Angola, Benin, na Misri. Hii ni ziara ya kwanza ya kikazi ya Bw. Qin Gang tangu ateuliwe kuwa waziri wa mambo ya nje wa China, na imefanyika wakati ushirikiano kati ya China na Afrika unaweka rekodi mpya.

Kwa wanaofuatilia mambo ya ushirikiano kati ya China na Afrika bila shaka wanatambua kuwa huu ni mwaka wa 33 mfululizo kwa Waziri wa mambo ya nje wa China kuanza mwaka wa kazi zake kwa ziara ya kikazi barani Afrika. Hii ni desturi inayoonyesha kuwa bara la Afrika linaendelea kuwa kipaumbele kwenye sera ya mambo ya nje ya China.

Tukiangalia mambo kadhaa yaliyofanyika wakati wa ziara ya Bw. Qin Gang, tunachoweza kukiona ni kuwa ziara hiyo imeendelea kuthibitisha nia thabiti ya China ya kuendeleza ushirikiano imara kati yake na nchi za Afrika, bila kujali hali yake inakuwaje au hali ya dunia inakuwa na mabadiliko kiasi gani. Kwa mtazamo wa kimataifa, kisiasa ni kipindi ambacho hali ya dunia bado ni tete, na siasa za kijiografia zinaonekana kuleta mivutano inayojikita kwenye suala la Ukraine, huku nchi za magharibi zikijaribu kuzishinikiza nchi za Afrika kuunga mkono msimamo wao wa kuitenga Russia kidiplomasia.

Alipozungumzia suala hilo, Bw. Qin Gang alisema hakuna nchi yenye haki ya kuzilazimisha nchi za Afrika kuchagua upande, au kuifanya Afrika kuwa uwanja wa mapambano kati ya nchi kubwa. Alisema Afrika inapaswa kuwa uwanja wa kuonyesha nani anatekeleza kihalisi mambo yanayohusu amani na maendeleo kwenye bara hilo, au nani anayeisaidia Afrika kuwa na sauti zaidi katika usimamizi wa dunia.

La muhimu ambalo pia limefuatiliwa kwa karibu, ni kuwa ziara ya Bw. Qin Gang imeonyesha kuwa China inatekeleza kivitendo ahadi inazotoa kwa nchi za Afrika. Alipokuwa ziarani nchini Ethiopia, Waziri Qin Gang alizindua makao makuu ya Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Maradhi cha Afrika (Africa CDC), hii ni moja ya ahadi kubwa zilizotolewa na Rais Xi Jinping kwenye mkutano wa mwaka 2018 wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC). Ahadi hii ilitolewa kabla ya kuibuka kwa janga la COVID-19, lakini katika kipindi chote cha janga, China ilikuwa inaendelea kutekeleza ujenzi wa mradi huo ambao sasa umekabidhiwa rasmi kwa Afrika.

Suala la “mtego wa madeni” ambalo limekuwa likizungumzwa sana na vyombo vya habari vya nchi za magharibi, limejitokeza tena wakati wa ziara ya waziri Qin Gang. Uzuri ni kwamba alipoulizwa na wanahabari alijibu kwa takwimu kwamba, ripoti ya benki ya dunia inaonesha kuwa mashirika ya fedha ya kimataifa na wakopeshaji binafsi ndio wenye robo tatu ya deni la nchi za Afrika, na kwamba wao ndio wanatakiwa kutoa mchango mkubwa zaidi katika kushughulikia suala la kupunguza mzigo wa madeni. Na katika ziara hiyo hiyo China imeendelea kuonyesha iko mbele ya nchi nyingi za magharibi, kwa kutangaza kusamehe baadhi ya madeni ya Ethiopia.

Bwana Qin Gang amemaliza ziara yake kwa mafanikio baada ya kutembelea nchi tano, na pia kwa kuitembelea makao makuu ya Umoja wa Afrika na kukabidhi kituo cha Africa CDC, tunaweza kusema alitembelea Afrika nzima. Katika ziara hiyo pia amesema mlango wa China uko wazi kwa nchi yoyote ya Afrika, iwe ni peke yake au hata kwa kushirikiana na nchi nyingine ya tatu, kufanya ushirikiano unaoweza kuleta maendeleo kwa nchi za Afrika.
 
Back
Top Bottom