Sumaye awaponda viongozi wabinafsi
Imeandikwa na Mwandishi Wetu; Tarehe: 28th January 2011 @ 08:04
MATATIZO ya rushwa, wizi na mauaji yanayoikumba nchi hivi sasa kiini chake ni kuwapo baadhi ya viongozi wabinafsi wasiojali maslahi ya watu wao.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ambaye pia alipongeza kukua kwa uchumi ingawa alisema hata hivyo kunaonekana kukua kwa baadhi ya wachache.
Amesema hilo likiachwa liendelee basi linaweza kuja kuwa hatari zaidi kwani ukuaji wa uchumi unapaswa kujidhihirisha kwa wananchi walio wengi.
Akizungumza jana kwenye mahafali ya kidato cha sita kwenye Shule ya Sekondari ya Pugu Dar es Salaam jana, Sumaye aliwataka viongozi walioko madarakani kuokoa hali ya sasa ya migogoro kwa kuwajibika na kuwatumikia wananchi na si kujifikiria wenyewe.
"Nawaomba vijana mnaohitimu leo mwende mkawe kioo cha jamii huko mwendako, mtambue juhudi za wazazi na walezi wenu, kwani vinginevyo ni sawa na usaliti, nasema hivi kwa sababu siku hizi moyo wa upendo na kujituma kwa ajili ya wenzetu umepungua katika Taifa letu," alisema Sumaye.
Alisema watu masikini wamekuwa hawathaminiwi na kila mtu akiwaachia mzigo huo waubebe wenyewe, hali ambayo ni hatari katika nchi yoyote na ndio maana zimekuwapo kelele za ufisadi, wizi, rushwa na mauaji kila kukicha.
"Kuna usemi kwamba ni vizuri kuwa mtu muhimu lakini ni muhimu zaidi kuwa mtu mzuri, hivyo tatizo la ubinafsi ndilo linasababisha haya yote, nawaomba huko mwendako mtumie elimu yenu kuonesha tofauti," alisema.
"Ukuaji wa uchumi ukiwapo kupitia kwa utajiri wa mtu mmoja au wachache ni hatari kwa nchi yetu iwapo hatua hazitachukuliwa," alisisitiza.
"Si kwamba napiga vita matajiri, la hasha, ila natamani kila mtu awe tajiri na si wachache wenye nacho waendelee kuwa nacho na wengi waendelee kudidimia," alisema.
Awali alisema kutokana na umuhimu wa elimu kwa nchi yoyote inayopigania maendeleo, Serikali haina budi kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa nchini kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu, inazingatia ubora wa viwango vya kimataifa.
Alisema kwa sasa bado mazingira ya elimu nchini hayajaridhisha na kwamba tatizo la wanafunzi kukosa madawati na kukaa chini, upungufu wa vitabu, maabara zisizo na vifaa na uhaba wa walimu, linaanza kurejea hali ambayo inasababisha kiwango cha ubora wa elimu nchini kushuka.
"Elimu ndio msingi wa maendeleo ya nchi yoyote, kama tunataka kuendelea kuwa masikini basi tuendekeze kuwa na elimu duni, kwa sasa kuna Soko la Pamoja la Afrika Mashariki, ni lazima Tanzania ioneshe ushindani kupitia elimu," alisema.
Mhitimu wa kidato cha sita, Francis Dago akisoma risala kwa niaba ya wenzake 239, alisema Shule ya Pugu imekuwa na historia nzuri kwani ndipo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alifundisha, Rais mstaafu Benjamin Mkapa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda walisoma.
Alisema kiwango chake cha elimu kimekuwa kikipanda mwaka hadi mwaka ingawa kuna changamoto ya uchakavu wa mabweni na madarasa na tatizo la mipaka na wakazi wanaoishi jirani na shule hiyo.