Kuanguka kwa CCM: Kutimilika kwa Unabii...

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
32,934
2,000
NA sasa imekuwa, kama ilivyopaswa kuwa; ndivyo ilivyotakiwa kuwa na naam, imekuwa kama ilivyotabiriwa. Na sasa itakuwa kwa kadiri ya unabii. Ndugu zangu, tunashuhudia kutimilika kwa taratibu kwa unabii ambao habari zake niliziandika tarehe 20 Januari, 2007 na kama nilivyoonesha wakati ule unabii hauepukiki kutimilika. Tunaposhuhudia mamia ya wanachama wa CCM wanapoanza kukikimbia chama hicho kimsingi tunashuhudia kuharakishwa kwa kutimilika kwa unabii huo. Wanachama hawa wanakubali alichosema Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kuwa "CCM si mama yangu".

Kwa muda mrefu wamekuwepo Watanzania wengi ambao wanaamini kabisa CCM kwao ni zaidi ya chama tu cha siasa; kwa hawa CCM ni maisha yao, ni uhai wao, ni hatima yao na kwa wengine mapenzi waliyonayo kwa CCM ni kama ya mtoto kwa mzazi wake. Kweli kabisa wapo wengine ambao hata wakizungumza wanazungumza lugha ya mahusiano ya mzazi na mtoto wanaposema: "CCM ni baba ya upinzani" nchini. Wenye mapenzi ya namna hii kwa kweli hawana lolote baya wanaloweza kuliona chini ya CCM na zuri lolote linaloweza kufanywa na CCM litapigiwa mbiu na kufanyiwa sherehe katika hali ya kukitukuza chama.

Mamia haya ya Watanzania hawa waliopofushwa na mapenzi kwa CCM wanajikuta mara zote wakijjisikia kusisimka hadi akili wanapofikiria CCM. Wengine wakiona rangi ya kijani na njano tu fikra zao zote zinapigwa ganzi na lolote litakalosemwa linasuuza mioyo yao. Nimeshuhudia mara kadhaa wakati viongozi wa CCM wanapozungumza na Wana CCM kunakuwa na hali fulani hivi ya kupigwa bumbuwazi la aina fulani kwa wasikilizaji; utaona wengine wanapiga makofi bila sababu, wengine hucheka cheka kwa furaha na wengine hushangilia hata kama kinachosemwa ni kile kile kilichosemwa miaka ishirini iliyopita!

Fikiria kiongozi wa CCM anasimama: "Kuanzia sasa tunataka uwajibikaji" na watu wanashangilia! Ni kana kwamba wamesahau miaka 30 iliyopita walisema hivyo hivyo, miaka ishirini iliyopita walisema hivyo hivyo na miaka mitano iliyopita walisema hivyo hivyo. Leo hii kiongozi wa CCM anasimama na kusema: "Hatutavumilia tena ufujaji wa mali ya umma" na watu wanapiga makofi na kugongesheana; ni kana kwamba wamesahau miaka mitano iliopita viongozi wale wale walisema haya haya na kushangiliwa vile vile!

Sasa, wananchi hawa wengine wameanza kutambua kuwa huwezi kushangilia picha! Wametambua kuwa maji hayafungwi kombe na ya kuwa debe la mende halitwangwi! Wananchi hawa wengi hasa wa vijijini wamefunguliwa; wametambua matumaini waliyokuwa nayo walipoiona "CCM nambari wani" na kuwa "Nyerere yupo Nyerere yupo" yametoweka na kupotelea mbali kama kinda la tetere aliyepotea kiota.

Wamefunguliwa. Kufunguliwa huku kwa kweli ni mafanikio makubwa zaidi ya harakati za mapambano ya kifikra. Nilipoanza kuandika kwa kina zaidi na kusomwa na maelfu ya watu kila Jumatano nilielezea kuwa mabadiliko ya kifikra ndio msingi wa mabadiliko mengine yoyote yale. Huwezi kuwa na mabadiliko ya kiuchumi, kiuongozi au hata kimfumo kama watu bado wanafikra zile zile. Mtumwa mwenye mawazo ya kitumwa huwezi kumpa shamba alime ukamwambie ni lake.

Mara nyingi mtumwa ambaye bado amefungwa kifikra akipewa shamba lake alime atakesha akimuuliza bosi wake nini cha kufanya. Hatojiamini kuwa ni lake na mara zote atakuwa ana wasiwasi kuwa anaweza kunyang'anywa au ataona kama ni mtego fulani hivi. Ndio maana kufunguliwa kwa wafungwa haikuwa tu sala la kuwafungua minyororo yao; kwani mfungwa si lazima awe na minyororo ili atawalike; anahitaji kutawaliwa kifikra tu. Mtu ambaye amezaliwa mtumwa, na kutumikishwa kama mtumwa hata bila minyororo wala mijeledi atajitambua kuwa yeye ni mtumwa. Huyu hahitaji kuvunjiwa makomeo ya malango yake ili awe huru, anahitaji tu kufunguliwa kifikra kujijua yeye ni nani.

Kwa miaka yote iliyopita tangu nitangaze "Kuanguka kwa CCM unabii utatimia" – miaka mitano iliyopita - tumeshuhudia mamia ya kina dada na kaka zetu wakiwekwa huru kifikra. Wakikombolewa na kukumbushwa kuwa wao ndio wenye nguvu kuliko risasi, ndio wenye nguvu kuliko vimulimuli, ndio wenye nguvu kuliko suti na magari yenye bendera. Ndugu zetu ambao walikuwa na mapenzi ya ajabu kwa chama tawala walianza taratibu kukataa CCM kwenye sanduku la kura baada ya kufanikiwa kuikataa kwanza kifikra! Tunakoenda sasa ni kufunguliwa zaidi kwa mamilioni ya wananchi wetu.

Mojawapo ya athari kubwa za ukoloni (colonial legacy) ni kutawaliwa kifikra. Hili ni kweli pia kwenye mfumo wa ubaguzi wa rangi (apartheid) na vile vile ni kweli kwenye mfumo wa ufisadi (corrupt system). Mifumo yote hii ambayo ni kandamizi (oppressive systems) ina madhara ya kwanza kabisa kwenye akili za wanaokandamizwa. Mifumo hii yote athari yake kubwa ni kuwafanya watu wajione duni mbele ya watawala.

Wapo watu ambao hadi leo wanaamini kabisa kuwa wakoloni walikuwa ni watu wema sana na kwa kweli wenye kutupenda kweli kweli; hawa wakimuona Mzungu leo hii wanajisikia kutekenyeka hadi kwenye chembe za mwisho za ubongo wao. Wenye fikra hizi watakataa kwa hasira pendekezo lile lile likitolewa na Mmatumbi mwenzao lakini likitolewa na John Smith watakuwa wa kwanza kulikumbatia tena huku wakitetemeka sauti zao wanaposema "Thank you sir!"

Kwenye ufisadi ni hivyo hivyo, watu wanafika mahali hawaamini kabisa kuwa kuna jambo lolote linaloweza kufanyika likafanikiwa bila vitendo vya rushwa. Nimewahi kusikia simulizi la mwanaharakati mmoja anayepiga vita rushwa ambaye pamoja na kuwa anapiga vita rushwa ilimbidi atoe rushwa aliposimamishwa na polisi ili kuwahi kikao ambacho alikuwa anaenda kuhutubia ubaya wa rushwa katika taasisi za serikali!

Yeye mwenyewe hakuona tatizo hapo kwani kile alichokitoa aliamini ni ‘rushwa ya usumbufu' kwamba angeweza kuwakatalia polisi na kwenda hadi kituoni na kuandikisha maelezo na hilo lingemletea usumbufu mkubwa! Ni kutawaliwa kiakili! Leo hii, ufisadi umekuwa ni mfumo wa kiuchumi ambapo hata watu ambao wanasema wanapiga vita ufisadi wao wenyewe wanajikuta kwa namna moja au nyingine wananufaika na ufisadi huo huo! Watu wanapiga vita vitendo vya ufisadi lakini makampuni yao yanapoomba tenda serikalini ndio hao hao wanajaribu kuandikiana mikataba mibovu na risiti za uongo ili waweze kugawanya ‘kidogo'!

Sasa, haya yote yanaleta mzigo wa kiakili kwa wananchi. Uzuri wa watu wa kijijini kinyume na mjini hawategemei sana serikali kwenye mambo yao. Mtu atalima na kuvuna mazao yake, atayaanika na hatimaye kuyaweka kwenye gunia. Ataenda kuuza kwa bei ambayo ataikuta huko na akirudi zake nyumbani hiyo ni hela yake. Lakini inapotokea anadhulumiwa bei au fedha za malipo mtu huyo anakuwa na uchungu zaidi kuliko mtu wa mjini ambaye amezoea kuishi kwa mitkasi. Ndio tuliyoyaona Tandahima hivi karibuni na tutaendelea kuyaona kwenye vijiji vingi ambavyo wananchi wake wamefunguliwa!

Kufunguliwa huku kwa kiakili kunaiweka CCM kwenye nafasi mbaya zaidi kuliko wakati mwingine wowote wa historia yake. Ikumbukwe kuwa kwa miaka karibu thelathini CCM ndicho chama pekee kilichokuwa mawazoni mwa Watanzania. Hukuweza kuzungumzia Tanzania bila kuzungumzia CCM na hukuweza kuzungumzia CCM bila kuzungumzia Tanzania. CCM ilitawala kila nyanja za maisha lakini utawala wake mkubwa zaidi haukuwa kwenye taasisi mbalimbali bali ulikuwa kwenye akili za watu. Ilifika mahali watu waliogopa CCM kama walivyoogopa Usalama wa Taifa kwani vyote viwili vilifanya kazi vile vile. Ukiitibua CCM, CCM ilikuwa haina simile. Hivyo, utawala wa CCM pia ulijaa hofu dhidi yake.

Masalio ya hofu hii yapo hadi leo lakini pia hofu hii imekaa kinamna nyingine tena. Kuna hofu ya kujulikana kuwa mtu haipendi CCM. Hofu hii huambatana na hisia ya hatia (guilty feeling). Nimewahi kusikia mara hii pale mtu anaposema "wewe utaikataa vipi CCM wakati ndio imekusomesha bure?" Wakati mwingine inaulizwa "CCM ni kama mama yako huwezi kumkataa mama yako pamoja na mabaya yake yote". Na ni kweli kabisa wapo watu ambao wanajisikia vibaya na uchungu wakiona CCM inaasemwa vibaya na wengine wanaweza hata kufanya vitu vibaya kwa wale wanaoisema vibaya CCM! Watu hawa wametawaliwa kifikra per excellence.

Hawa hawawezi kufunguliwa; hawafunguki hata kwa kuombewa au kufukiziwa ubani! Wamekuwa watumwa wa kifikra na minyororo iliyofungwa kwenye fikra zao imejichimba kwenye ngozi za mikono na shingo zao na kuwa sehemu yao. Huwezi kukata minyororo hiyo bila kusababisha kuangamia kwao! Hawa hatuwezi kuwasaidia wafunguke!

Ndiyo maana binafsi siamini kabisa kuwa mabadiliko nchini yataletwa na wasomi hasa wale wenye kufurahia utawala wa CCM! Ni sawasawa na hapa Marekani ambapo historia inatuonesha tofauti ya "watumwa wa nyumbani" na "watumwa wa kondeni".

Watumwa wa nyumbani walikuwa karibu sana na bosi na walipewa mahali pa kula na kulala na walitendewa vizuri zaidi kuliko watumwa wa kondeni. Matokeo yake ni wale watumwa wa kondeni ndio hatimaye waliweza kuwa chachu ya mabadiliko kuliko watumwa wa nyumbani. Maana hawa wanyumbani kuambiwa kuwa kuna uhuru wanajikuta hawaamini; kwamba watoke katika ‘maisha mazuri' na kwenda kwenye ‘uhuru' haiingii akilini. Lakini wengine walipoweza kufunguliwa kiakili waligeuka wapelelezi wazuri sana; lakini wengine walikufa wakiwa wanafurahia kuitwa "mtumwa mzuri kwa bwana wake!"

Ndugu zangu, imekuwa na sasa inatimia; waliokuwa wamefungwa wamevunjwa minyororo yao, na waliokuwa wametawaliwa kiakili wamefunguliwa. Na kama ilivyotarajiwa ni wanakijiji ndio wanaongoza wimbi la mabadiliko. Kuanzia Mbozi hadi Meatu, kuanzia Njombe hadi Geita, kutoka kona za Kigoma hadi kwenye vijiji vya Manyara, maelfu ya wananchi wetu wanazidi kufunguliwa wakitupilia mbali kongwa la utumwa wa kifikra; wamekataa wao na uzao wao kuabudu kwenye altare ya CCM. Wamekataa kuitwa ‘watumwa wa nyumbani'!

Mojawapo ya vitu ambavyo CCM imevifanya na haikujua kuwa imepanda maangamizi yake ni kuanzishwa kwa ‘shule za kata'. Shule hizi zimekuwa ni sehemu ya kupandikiza mbegu ya fikra. Watu ambao hawakupata nafasi ya kusoma sasa wamesoma lakini baada ya kushindwa kuendelea namasomo ya juu vijana wengi waliosoma sekondari wamerundikana vijijini wakiwa na fikra zinazowaka bila kukoma kama taa ya chemli; wanachochewa zaidi na zaidi kwa kusikiliza na kufuatilia mambo kupitia njia mbalimbali.

Ndiyo maana naamini kabisa vita kubwa ambayo inakuja kati yetu na watawala itahusiana na uhuru wa vyombo vya habari na mitandao ya intaneti. Naweza kuona kutoka mbali CCM ikijipanga kuleta sheria au sera ambazo zitajaribu kuzuia vyombo vya habari na hasa mitandao ya kijamii. Siyo mitandao tu bali hata watumiaji wake; sote ambao tumekuwa tunaandika kwa uhuru na kuchochea mabadiliko ya kifikra tutajikuta tunaanza kubanwa kwa ama madai ya ‘usalama wa taifa' au ‘sheria ya vyombo vya habari'. Naweza kuwahakikishia tu kuwa mapambano sasa yanaenda kwenye ngazi tofauti kabisa sasa kwani CCM haiwezi kamwe kuacha twende kwenye uchaguzi mkuu wa 2015 katika mazingira yale yale ya 2010; hawawezi na kwa hakika watalazimisha watu kubadilika!
Naomba kutangaza mapema, mara moja na daima; nilishavunja kongwa la utumwa wa fikra za CCM, sitompigia mwanadamu yoyote magoti na sitoi sadaka ya sifa za uongo kwa mtu yeyote.

Kwa vile unabii utatimia ulivyo, nawasihi wale wote waliofunguliwa kuwa tayari kwa lolote kwani vichaa wamepewa sime sokoni! Tutakiona cha moto! Kama walivyowahi kusema wengine – ni bora kufa kwa heshima kuliko kuishi kwa aibu! Tuendelee kuwaamsha watu wengi zaidi ili kuhakikisha kuwa pigo la kwanza takatifu, pigo lisilo na huruma, pigo lisilo na onyo liangukie CCM kwenye chaguzi zote zinazokuja kuanzia sasa.

Si kwa sababu tunawachukia wana CCM; la hasha! Hawa ni ndugu zetu, ni rafiki zetu, na wengine ni jamaa zetu wa karibu. Bali kwa sababu wengine tumetambua na kuthibitisha kuwa CCM na sera zake imeshindwa, hatima yake ni kukataliwa, na adhabu ya wanaojaribu kuijenga upya ni kutiwa pingu. Ni matumaini yangu uongozi ujao hautawapepesea macho watawala hawa walioshindwa bali wakae wakijua uongozi mpya utakapochukua nchi utafumua kila kitu chao na kuhakikisha wale wote waliofilisi taifa letu na kugongelea misumari ya kongwa kwenye shingo za watu wetu wanasimamishwa kizimbani! Kuanzia aliye mkuu wao hadi aliye mdogo wao.

Kwani unabii utatimia; ndivyo ilivyopaswa kuwa, nayo itakuwa kwani hivyo ndivyo ilitakiwa iwe. NA ITAKUWA.


Nitafute Facebook: "Mimi Mwanakijiji
Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com
 

Matola

JF-Expert Member
Oct 18, 2010
40,094
2,000
Mzee Mwanakijiji fanya editing ya hii makala yako ili kurahisisha usomaji, kikubwa tenganisha paragraph kwa kuruka mstari mmoja ili kuongeza mvuto kwa msomaji.
By the way Makala imetulia sana nitarudi hapa baadaye.
 
Last edited by a moderator:

Dingswayo

JF-Expert Member
May 26, 2009
4,022
2,000
Kuna hadithi ya Abunuwasi alimuona mtu mmoja anakata tawi juu ya mti huku amekalia upande karibu na majani ya tawi na sio upande karibu na shina. Abunuwasi akamwabia yule mtu, 'Kwa namna hivyo uanvyokata hilo tawi, hakika utaanguka'. Yule mtu hakutaka kumsikiliza Abunuwasi, kwani alimuona kuwa yu mjinga, akaendelea kukata lile tawi hadi lilipokatika na yule mtu kudondoka chini!

Yule mtu akaondoka mbio kumkimbilia Abunuwasi, ambaye alikuwa hajafika mbali bado. Alipomkuta akamsimamisha Abunuwasi na kumuuliza huku akitweta, 'Lazima uniambie ni siku gani mimi nitakufa, kwani ulijuaje kuwa mimi nitaanguka pale mtini?'
 

Mzalendo80

JF-Expert Member
Oct 30, 2010
2,508
1,500
Huu uzi nimeusoma Tz Daima, Shukrani mkuu MM kwa kazi yako. Kwa sasa kila mtanzania anajua kuwa CCM ipo ICU inapumulia Machine
 

Kiumbo

JF-Expert Member
Feb 4, 2012
560
0
MM NIMEKUBALI HATA KM NI NDEFU ILA INA MAONO MAZURI SANA. Inafaa sana kwa elimu uraia kwa mabadiliko ya sasa. Ila angalia wasije wakakupa ukuu wa wilaya hata km uko huko maana waandishi wanazibwa mdomo kwa staili nyingine.
 

ngaranumbe

Senior Member
Apr 16, 2012
148
0
Makala imetulia, ila wa Tz hawasomi mambo na kupunguza ulimbukeni; utawaona akina mama wakicheza ngoma na T.shirt za kijani na kurandaranda kila kikao kinakofanyikia wanakula hukox2 na hupewa buku 5 kama mshiko-mbaya zaidi ni pale ngono zinapofanyika.
 

Maganga Mkweli

JF-Expert Member
Jul 14, 2009
2,096
2,000
hii ndio silaha kubwa ya kifo cha CCM naamini ... na mimi ni shuhuda wa haya mabadiliko kwa hichi kipengele na vijana walivyo na hasira kwa kutambua haki zao na wajibu wao tu kupitia CIVICS maana hilo ndio somo kila mwalimu anaweza fundisha hata shule ikiwa na mwalimu mmoja CIVICS lazima ifundishwe
Mojawapo ya vitu ambavyo CCM imevifanya na haikujua kuwa imepanda maangamizi yake ni kuanzishwa kwa ‘shule za kata'. Shule hizi zimekuwa ni sehemu ya kupandikiza mbegu ya fikra. Watu ambao hawakupata nafasi ya kusoma sasa wamesoma lakini baada ya kushindwa kuendelea namasomo ya juu vijana wengi waliosoma sekondari wamerundikana vijijini wakiwa na fikra zinazowaka bila kukoma kama taa ya chemli; wanachochewa zaidi na zaidi kwa kusikiliza na kufuatilia mambo kupitia njia mbalimbali.
unabii utakamilika hakika ccm kifo chenu kipo karibuni... amina
 

Insurgent

JF-Expert Member
Jun 26, 2007
469
0
Ndoto ya Mafisi wanaokesha wakisubiri mkono uanguke. CHADEMA si malaika lakini wanajua kuupepeta mdomo.
Tanzania si kichwa cha mwendawazimu.
 

Mdondoaji

JF-Expert Member
Mar 17, 2009
5,109
1,225
Sheikh Yahaya mwengine well tukuulize umetumwa ? Kila la kheri we shall see mie sina chama ila nadhani CCM kuanguka ni ngumu sana. Zaidi kwasababu Chadema ni chama hakijajipanga kuchukua nchi hata kidogo. Sana sana kutatokea machafuko tu hasa ya kidini mark my words......
 

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
32,934
2,000
Sheikh Yahaya mwengine well tukuulize umetumwa ? Kila la kheri we shall see mie sina chama ila nadhani CCM kuanguka ni ngumu sana. Zaidi kwasababu Chadema ni chama hakijajipanga kuchukua nchi hata kidogo. Sana sana kutatokea machafuko tu hasa ya kidini mark my words......
Point nzuri hiyo
 

dada jane

JF-Expert Member
Dec 8, 2011
565
0
MMM live long life. Mimi ni mwl hatulali tunabukua na somo la civics kwa sasa linagombaniwa sana na walimu kwa sasa.
 

Nkandi

Member
Nov 20, 2010
83
95
Mwanakijiji...uliyosema ndiyo hali halisi. I salute you for this.....Hatutokaa kimya hata siku moja mpaka kufunguliwa kifikra kutakapokuwa kwa watu wote wa taifa hili
 

Mtoboasiri

JF-Expert Member
Aug 6, 2009
5,101
0
Sheikh Yahaya mwengine well tukuulize umetumwa ? Kila la kheri we shall see mie sina chama ila nadhani CCM kuanguka ni ngumu sana. Zaidi kwasababu Chadema ni chama hakijajipanga kuchukua nchi hata kidogo. Sana sana kutatokea machafuko tu hasa ya kidini mark my words......
Hilo la kutokea machafuko limekuwa linatumiwa sana na ccm, kwa bahati mbaya kipindi hiki habari zinapatikana kwa urahisi zaidi hivyo upotoshaji watu eti kwa kisingizio cha kuwepo machafuko upinzani ukipewa madaraka hauna mashiko!
 

Mnama

JF-Expert Member
Oct 13, 2010
1,902
2,000
Kifo cha CCM ni hakika labda utokee muujiza gani sijui ,swala la Chademu kujiandaa au kutojiandaa ni swala la wakati tu muda ukifika tutajua.
 

FredKavishe

Verified Member
Dec 4, 2010
1,090
1,195
Huwa nikisoma makala zako napata moyo zaidi wa kusambaza yote yaliyo mema kwenye makala zako hakika muda ni huu wakati umefika
 
Top Bottom