Kosa langu

plan z

JF-Expert Member
Jun 10, 2019
1,381
1,414
Ilikuwa asubuhi nzuri sana iliyojaa uchangamfu wa aina yake. Hali ya hewa ilikua rafiki kwa kila mtu, mawingu mazito yalitanda anga zima la jiji la Dar es salaam na kulimeza jua lililokua kero kwa wakazi wengi wa jiji hilo sababu ya joto lake kuwatesa wengi.

Kijimvua laini kilinyesha kila mahali na kuiosha miili ya wahangaikaji wengi wa jiji hilo ambao kwao kuoga lilikuwa jambo la bahati nasibu sababu ya kujali muda.

Ilikua ni jumatatu ya kivutia siku ambayo watu wengi walikua wanawahi mihangaikoni kutafuta ridhiki za kila siku.

Mitaani kote watu walitapakaa kila kona, hawakuijali ile hali ya mvua wengi waliifurahia, si barabarani , kivukoni kwenye madaladala kote watu walijaa, msemo wa mjini cha bure salamu ulithibitika hapo.

Mimi na baba yangu Mzee Kamba tulikua miongoini mwa watu walioijaza mitaa.
Tulikua tunaenda chuoni Baltimore key health kufanya usajili ili nianze mwaka wangu wa kwanza wa masomo chuoni hapo.

Tulitumia usafiri binafsi, namshukuru Mungu kwa kiasi fulani maisha ya wazazi wangu yalikua mazuri kiasi chake walikua na nyumba nne magari matatu ya kutembelea na moja kwa ajili ya kazi za shamba.

Ukubwa wa foleni na umuhimu wa watu kuwahi kazini na mihangaikoni siku ya jumatatu ulitukawiza barabarani, baba yangu Mzee Kamba alitumia muda huo kunipa mawaidha, yale yote niliyopewa na mama nyumbani aliona ni kama hayatoshi. Baba yangu alikua anapenda sana mafanikio barabara nzima maongezi yake yalihusu kutengeneza pesa, habari za wanawake hakutaka kuzisikia hata kidogo, muda wote huo alikua akinihusia kua nikitaka kufaulu masomo yangu vizuri na kupata kazi nzuri ni lazima nifunge zipu yangu na kusahau kila kitu kuhusu wanawake mpaka muda sahihi ukifika, na muda sahihi ni pale nitakapokua nimetimiza ndoto zangu zote.

Tulifika chuoni Baltimore key health, uzuri na mpangilio wa majengo na kila kitu chuoni hapo uliungana na mawaidha ya baba yangu Mzee Kamba kuniongezea motisha. Foleni tuliyoikuta ofisi ya msajili ilinipa nafasi ya kutembea na kuzunguka chuo kizima. Kila nilichokiona chuoni hapo kilinivutia, majengo makubwa ya kisasa na bustani nzuri za maua zilipendezesha sana mazingira ya hapo ilikua ni lazima nifanikiwe, ni lazima niwe daktar sikuona kitu chochote cha kunizuia.

Zamu yetu ya kufanya usajili ilifika, baba yangu Mzee Kamba alinilipia ada na michango yote, taratibu zote na kila kitu kilikamilika.

Nilipewa chumba cha kukaa, chuo kilikua kipya, kilimilikiwa na familia ya Baltimore Woodward kutoka nchini Canada, kwa taratibu zao walizojiwekea ilikua ni lazima wanafuzi wote wakae hostel ili kuzuia matabaka kati ya waliokua nacho na wasiokua nacho.

Baada ya kila kitu kukamilika baba yangu alinikabidhi pesa za matumizi kwa ajili ya mambo mengine pamoja na chakula maana tulikua tunanunua kutoka cafeteria za chuo hata nje ya chuo pia tuliruhusiwa kununua sababu kila mtu alipenda kula chakula anachokitaka.

Wiki moja ilipita usajili na kila kitu kilimalizika. Wanafunzi wote waliwasili tayari, Baltimore key health chuoni masomo yalianza yalikua ni magumu mno kuliko sehemu zote nilizopita awali.

Ma lecture wote walikuwa wazungu, lafudhi zao na kingereza chao orijino vilitutesa sana ilihitajika umakini mkubwa sana kuwaelewa.
Tulikuwa wanafunzi wa kwanza chuoni hapo, wote tulikua wapya kabisa asilimia kubwa tulikua tumetokea kidato cha sita wachache sana walitokea diploma.

Hakukua na wa kwanza wala wa mwisho kama sekondari lakini kila mtu alisoma kwa bidii, hakuna hata mmoja aliyetaka kufeli wala ku supp kila mtu alitaka kupata matokeo mazuri kuwafurahisha wazazi wake.

Nilisoma kwa bidii sana, maneno ya baba yangu yalikua kama kimvuli changu kila muda yalijirudia masikioni mwangu.

Sio yeye peke yake sikutaka kuwaangusha wote pamoja na mama yangu. Nilifanya kila nilichoweza kuhakikisha nafanya vizuri.

Darasani nilishirikiana na kila mtu katika mambo yote ya kitaaluma jambo lililofanya nijulikane na watu wote kwa sababu ya ucheshi wangu pamoja na akili nilizokua nazo.

Kila mara jina la Alfred Kamba lilikuwa miongoni mwa wanafunzi waliofaulu vizuri kwa kupata GPA ya juu kabisa kitu kilichofanya niwe mwanafunzi bora karibu katika kila semista.

Jambo hili lilifanya niwe mtu wa furaha mara kwa mara, kupeleka matokeo mazuri nyumbani lilikua jambo la ufahari na la kujivunia kwangu.

Itaendelea.
 
Chapter 2

Furaha hii na salamu za pongezi za kila mara kutoka nyumbani vilidumu kwa semista kadhaa, lakini polepole kama mwendo wa kinyonga mambo yalianza kubadilika ufaulu wangu ulianza kupungua kila mtu aliliona hilo mimi pia nilijiona kua ninafeli lakini sikufanya chochote kwani muda huo akili, mawazo na kila kitu changu kilikua kina muwaza Leyra, msichana nilietokea kumpenda ghafla kwa sababu ya uzuri aliokua nao.

Nimewaona wasichana wengi warembo mitandaoni na kwenye filamu nzuri za mapenzi lakini sijaona msichana kama Leyra.
Leyra alikua msichana mrembo pengine kuliko wote niliowahi kuwaona kwa macho yangu yote mawili tena yakisaidiwa na nguvu miwani yangu ya macho ambayo kutwa nzima haikubanduka machoni mwangu.

Tabasamu lake lilikua ni tiba tosha ya magonjwa mengi pengine kuliko hata madawa tuliyoyasoma hapo chuoni, sio tu tiba bali tabasamu lake lingeweza kumfanya mdaiwa sugu akalipe deni lake, na mkwepa kodi ajipeleke mwenyewe tra.
Jina lake lilisanifu uzuri wake toka lini mtu akaitwa Leyra akawa mmbaya?, ubaya, umbea na ubondia ulikua na majina yake, majina kama Chausiku, Kurusumu, Mwantumu, Asha ngedere, Mwajuma ndala ndefu, chakubimbi na kuendelea.
Sauti yake ilikua tamu kama sauti za vinubi, kama angelikua mwanakwaya nadhani watu wote wangemrudia Mungu mapema maana wasingechoka kumsikiliza.

Nikisema niiongelee sura yake iliyobarikiwa uso mwembamba, pua ndefu, midomo miekundu, macho makubwa ya duara, ngozi nyeupe isiyokua na kovu wala chunusi hata moja bila kusahau nywele zake ndefu alizozifunga kwa nyuma nahisi unaweza ukameza simu yako nikisema niongeze na umbo lake namba nane unaweza ukameza na chaja pia.
Unashindwaje kumpenda mtoto kama huyu labda uwe umelogwa na wachawi wakuu wa kijiji.

Kwa kua sikua nimelogwa, nilijikuta nimekufa na kuoza kwa Leyra, nilimuwaza kila sekunde iendayo kwa Mungu, muda wote moyo wangu uliyalaumu macho yangu kwa kuchelewa kumuona tokea siku ya kwanza tulipowasili hapo chuoni.
Muda mwingi macho yangu yalikua yakitua juu uso wake ni kama yalivutwa na sumaku. Kwenye mawazo yangu nilimvua nguo zote na kulala nae, nilimkunja aina zote nilizozitaka, kama ingekua ni kweli basi naamini ni lazima angelazwa hospitali kwa uchovu au majirani wangekuja kuamua maana kwa uzuri wake hata mwanaume mwenye kibamia angejitutumua kuweka heshima.

Wapo wasichana waliotamani wangekua wanaume ili waufaidi uzuri wake lakini kwa bahati mbaya haikuwezekana.
Lakini pamoja na uzuri wote aliokua nao, Leyra hakua kama wasichana wa uswahilini unakuta msichana sura ngumu kama mkasi wa kupunguzia maua lakini anaringa utasema hatoi kitu cha ushuzi au hakati gogo.
Leyra alikua mtu wa watu kwao walikua matajiri wakubwa lakini hakuchagua marafiki, alicheka na kila mtu si masikini si tajiri kwake watu wote walikua sawa. Tofauti na tabia za kina Cheusi mangala ambao wakipewa tu uzuri inakua kosa.
Leyra kwake ilikua tofauti alijiheshimu kupita kiasi, hakua mtu wa wanaume hata kidogo japo wapo wengi wenye pesa zao waliomtaka lakini wote waliambulia hewa, hewa ambayo huenda ingetosha kujaza mipira yote toka ligi kuu ya Uingereza tokea ikiwa inaanza hadi inaisha kwa muda wa miezi nane.

Sikua nikichoka kumuangalia Leyra nilisikia raha kufanya hivyo, alinishtukia aligundua kua nilikua nikimuangalia sana lakini hakunizuia. Kila mara macho yetu yalikua yakigongana lakini hakunisemesha neno aliishia kutabasamu bila kukasirika jambo lililofanya nizidi kumpenda siku hadi siku.
Kadri siku zilivyosonga mbele ndivyo nilivyozidi kumpenda sikujali tena maneno ya baba yangu wala ratiba yangu ya masomo.
Muda mwingi niliutumia kuuwaza uzuri wake jambo ambalo nilishindwa kujizuia kabisa, kwani kila nilipojaribu kujizuia ni kana kwamba nilikua nikijiumiza mwenyewe.

Hali hii ilidumu kwa muda miezi kadhaa hatimaye kama upepo taarifa zilizagaa kila kona, kila mtu chuoni alijua kua nilikua nikimpenda Leyra hata yeye mwenyewe alijua hilo kwa sababu kila mtu alisema tunapendezana kama tungekua pamoja.

Je nitafanikiwa kua na mtoto Leyra?
Tukutane alhamisi.

...Itaendelea. ..
 
Chapter 3

Ilipoishia..

kila mtu chuoni alijua kua nilikua nikimpenda Leyra hata yeye mwenyewe alijua hilo kwa sababu kila mtu alisema tunapendezana kama tungekua pamoja.

Songa nayo..

Nilitamani sana iwe hivyo lakini nilishindwa, nilikua mgonjwa wa aibu, ujanja na ucheshi wangu kwa watu wote ulikua bure sikua nimewahi kutongoza msichana yoyote toka utoto wangu, wala kua katika uhusiano wowote wa kimapenzi licha ya kutakwa na wanawake kadhaa hapo nyuma. Nilifanya hivyo sio kwa sababu sikua nimekamilika, hapana mimi ni mwanaume rijali niliyekamilika lakini nilifanya hivyo kwa sababu elimu yangu yote ya awali nilisoma seminari maadili na aina ya maisha niliyoishi yalichangia mimi kua hivyo, pia nilifanya hivyo kwa ajili ya masomo, mawaidha ya baba yangu hayakutoka masikioni mwangu hata siku moja pia nilikua nimetoka mbali sana sikutaka kusongwa na mapenzi, lengo langu kubwa lilikua kua daktari bingwa wa magonjwa sugu ya wanawake na watoto pamoja na mifupa ili nimsaidie bibi yangu ambaye toka napata akili sikuwahi kumuona akitembea kwa miguu yake zaidi ya kutumia kiti cha magurudumu.

Mpaka muda huo nakubali kweli nilikua domo zege kwani licha ya kumpenda Leyra sikua nimewahi kumsemesha neno lolote, sikumuogopa bali nilimuonea sana aibu kila nilipo jiringanisha nae niliona mimi sio hadhi yake tabia yake ya kutopenda wanaume ndio ilinimaliza kila nilipowaza kumwambia jibu la kukataliwa lilikuja kichwani kwangu, sikua na jinsi niliishia kukata tamaa na kuumia mwenyewe.Haikua siri tena kila mtu alijua kua nilikua namuogopa Leyra, marafiki zangu wote walijua hata yeye mwenyewe alijua lakini hakufanya kitu chochote nadhani alikua akinicheka kimoyo moyo.
Umaarufu wangu wote ulibadilikia hapo, jina la Alfred Kamba liliacha kusikika tena kwa sababu ya kushuka kwa maendeleo yangu ya kitaaluma. Lakini hii haikunizuia kufahamika kwani kama Yohane mbatizaji nilibatizwa jina la utani Domo Gundi kwa sababu ya kushindwa kumtongoza Leyra.
Jina hili lilikaa mdomoni mwa watu wengi kama sala za asubuhi, lilikaririwa na kila mtu kama orodha za kuzidisha ma lecture tu ndio watu pekee ambao hawakulijua.
Nilikosa raha, akili yangu ilivurugika kiasi cha kupoteza muelekeo wangu mzima wa kitaaluma.

Lucyra Rustin alikua miongoni mwa wasichana warembo sana ambao mwanaume yoyote hawezi kujutia muda wake kua nao. Mvuto wa sura na umbo lake viliuelezea wazi uzuri aliokua nao, kwa wasichana wote Lucyra alifua dafu kasoro kwa Leyra tu ndipo aligonga mwamba nadhani kama sio robo basi aliufikia uzuri wa Leyra kwa theluthi moja.
Lucyra alikua jirani yangu nyumba zetu zilikua pua na mdomo. Tulitoka sehemu moja, tulikua na kucheza pamoja toka utotoni. Wazazi wetu walikua ni marafiki wakubwa sana kwa sababu ya ujirani wetu wa muda mrefu, walisaidiana pamoja kwenye shida na raha, upendo wao ulifanya tuwe kama ndugu.

Toka utotoni Lucyra alitokea kunipenda sana labda kwa sababu wazazi wetu walitutania kwa kutuita mtu na mkewe. Mara kwa mara Lucyra alikua akishinda kwetu, tulicheza michezo yote ya kitoto kwa furaha bila wazazi wetu kutuingilia.
Nilipokua sipo alikua akija nyumbani kuniulizia, muda mwingi alijali kuhusu mimi kuliko hata alivyojijali yeye mwenyewe.
Kila siku Lucyra alikua akiniletea pipi na ice cream za maziwa kutoka dukani kwao, sikujali kama ameiba au amepewa nilikua kama kupe, nilijenga ukaribu mkubwa ili nizidi kuzifaidi zile zawadi zake.
Tulikua watoto lakini nilikua mkatili sana siku ambayo hakuniletea kitu nilinuna maskini ya Mungu mtoto wa watu alikua anatoa machozi kunililia na kuniomba msamaha utasema alikua amenikosea.

Ukaribu wetu ulikua kivutio kwa watu wengi harusi nyingi za mtaani kwetu walitutumia sisi kama baba harusi na bibi harusi wadogo, tulikua kielelezo na maana halisi ya upendo kwa kila mtu, hata wazazi wetu wote walijisikia fahari.
Polepole muda ulianza kututenganisha, nilikua nimemzidi Lucyra miaka miwili. Umri wangu wa kuanza shule ya msingi ulifika, baba yangu Mzee Kamba aliachana na utani wote wa huko nyuma wa kutuita mke na mume, alinipeleka seminari ndogo ya Mtakatifu Don Bosco iliyopo jijini Nairobo nchini Kenya, ambapo nilianza elimu yangu ya msingi, darasa la kwanza.

Nilikua na miaka saba lakini baba yangu hakujali umri wangu wala mimi kua mbali na nyumbani alichojali ni ubora wa elimu na malezi niliyokua ninaenda kuyapata. Nililia sana siku baba yangu aliponiacha seminarini na kurudi Tanzania, sikua nikinyonya lakini nilimkumbuka sana mama yangu kuliko kitu chochote, siku ya kwanza tu niliona ni kama nimekaa huko mwaka mmoja. Seminari nzima darasa la kwanza hadi la saba tulikua watu wanafunzi mia tatu tu. Tulikua wachache sana hivyo huduma zote tulizopata pale zilikua bora kuliko hata huduma za taasisi zingine binafsi.

Ukiacha pipi na ice cream za Lucyra, kitu kingine ninachokikumbuka seminarini hapo tulifundishwa upendo, uaminifu na nidhamu ya juu kabisa, tulikua wadogo lakini mapadri hawakua na masihara hata kidogo lilipokuja suala la nidhamu na uaminifu, kwa macho yangu nilishuhudia mwanafunzi mmoja akifukuzwa kwa kosa la kuokota tunda bustanini na kulila bila kupewa ruhusa.
Tulikua tunaandaliwa kua mapadri wa baadae kama yalivyokua malengo ya seminari zote duniani kote. Hivyo tulifundishwa utii wa hali ya juu mno, mapadri hawakujali umri wala darasa unalosoma, muda wa sala ukifika saa 11 na nusu asubuhi lazima wote muwepo kanisani, muda wa darasani lazima muwepo darasani, muda wa michezo lazima muwepo uwanjani, bila kusahau muda wa kazi lazima wote mshiriki.Tulikua kama siafu kila kitu kilifanyika pamoja kwa ushirikiano, tulioga muda mmoja wote maji ya baridi, tulikula chumba kimoja, tulivaa sare moja hatukuruhusiwa kubeba nguo zozote kutoka nyumbani, kifupi tulikua kama watoto wa mama na baba mmoja.

Hii ndio ilikua aina yangu ya maisha kutoka nikiwa na miaka saba mpaka ninamaliza kitado cha sita nikiwa na miaka karibu kumi na saba hivi. Kwa maisha ya aina hii unaanzaje kuwaza wanawake?, muda wote mtu upo bize, upende usipende kanisani utaenda, utake usitake kuamka utawahi, uwanjani michezo hutashiriki hata kama upendi, kazi utafanya na mwisho wa siku maji ya baridi utaoga.
Eti ndugu zangu kwa hali hii kwanini nisiwe domo geze?, naanzaje kwa mfano ikiwa tu sketi na wasichana unawaona mara 2 kwa mwaka wakati wa likizo kila baada ya miezi sita.

Maisha ya shule ya seminari yalifanya nimsahau Lucyra ilifika hatua hata pipi na ice cream zake nikazisahau, nilikua napambana ili niwepo shuleni hapo kwani mchujo ulianzia darasa la kwanza mpaka kidato cha sita, usipofikisha wastani wa 75 hata uwe mtoto wa raisi wa nchi utarudi kwenu. Nilisahau kila kitu kuhusu Lucyra, marafiki zangu wakubwa walikua ni chakula (ninapenda sana kula), kitabu na maji ya baridi muda wa kuoga.
Lucyra tulionana nae tu wakati wa likizo nilipokua nikirudi nyumbani nchini Tanzania.

Kipindi cha likizo yangu ndio kilikua kipindi cha Lucyra
kunenepa kila aliposikia nimerudi alikua akija nyumbani na kushinda kila siku. Kuonana na kuongea na mimi ndio ilikua furaha yake kubwa kuliko kitu chochote nakumbuka kila muda tuliokua pamoja Lucyra hakuchoka kuniambia kua ananipenda sana, hata tulipokua kua wakubwa hakuchoka kunipenda, nilipomsahau alinikumbuka kwa simu, jumbe nzuri za mapenzi pamoja na email zisizokua na idadi.

.....Itaendelea....
 
Chapter 4

Nilimuhurumia sana Lucyra jinsi alivyokua akiteseka kwa sababu yangu. Kiukweli sikumfanyia makusudi, utotoni sikumkubalia kwa sababu ya masomo na malezi yangu ya kiseminari lakini safari hii sikumpenda kabisa kwa sababu ya Leyra. Sikuogopa ujirani wa familia zetu wala ukaribu wa wazazi wetu nilimueleza Lucyra kila kitu wazi lakini kutokana na kuzidiwa na nguvu ya mapenzi alishindwa kabisa kunielewa tena kumuogopa kwangu Leyra ndio kulimpa moyo na kufanya azidi kusubiri jibu la ndio kutoka kwangu, jambo ambalo kiukweli lilikua haliwezekani.

Ukisema cha nini wenzako wanasema watakipata lini.
Kama ilivyokua kwangu kumuogopa Leyra kulivyompa moyo Lucyra ndivyo kumkataa kwangu Lucyra kulivyompa moyo Daniel, Cr wa darasa letu ambaye alitokea kumpenda sana Lucyra. Daniel na Lucyra walifahamiana tokea sekondari, walisoma darasa moja kidato cha tano na cha sita katika shule ya Mt. Mathias iliyopo jijini Dar es salaam.
Tokea huko Daniel alikua akimtaka Lucyra, alimueleza jinsi anavyompenda lakini mimi nilikua kikwazo, Lucyra alimkataa kwa sababu yangu lakini cha ajabu Daniel hakuacha wala hakuchoka kumpenda.
Mwanzo nilikua mbali na Lucyra nchini Kenya masomoni lakini Daniel alinifahamu sababu Lucyra alimwambia habari zangu. Safari hii nilikua karibu nae chuo kimoja darasa moja, Daniel aliogopa sana alijua wazi kama ningemkubali Lucyra basi huo ndio ungekua mwisho wake. Mimi kumkataa Lucyra aliona haitoshi aliamini asipofanya kitu ipo siku ningeweza kubadilisha mawazo yangu.

Mimi kumpenda Leyra kwa Daniel zilikua ni habari njema lakini kitendo cha kumuogopa ilikua habari mbaya kwake.
Njia sahihi ya kufanya hio izidi kua habari njema kwake ilikua ni mimi na Leyra kua karibu. Daniel alidhamiria kufanya kitu lakini hakujua afanye kitu gani, jambo hilo lilimuumiza kichwa kwa muda wa wiki mbili mpak Dr. Grosse alipokuja Darasani na kutaka Cr atengeneze makundi mbali mbali kwa ajili ya asaimenti alizokua ameziandaa.
Daniel hakutaka kuzubaa aliona hio ndio ilikua fursa pekee ya kuitumia kutengeneza ukaribu wangu na Leyra. Daniel alicheza kama Ronaldo, alinipanga kundi moja na Leyra bila kuogopa naye alijipanga kundi moja na Lucyra.
Lilikua jambo muhimu sana kwetu sote ingawa mwanzo lilinitesa sana kwa sababu ya aibu, kujizuia kubehua na kukohoa mbele ya Leyra. Japo niliteseka mwanzoni lakini mpango wa Daniel ulizaa matunda, polepole kama mwendo wa kobe nilianza kumzoea Leyra na ukaribu wetu mkubwa ukaanzia hapo.

“Hi naitwa Leyra Lacena” Leyra aliniambia baada tu ya kukutana kwenye kundi tulilipongiwa.

“Naitwa Alfred Kamba” kwa mara ya kwanza niliongea nae kama haitoshi tukasalimiana kwa kushikana mikono.

Labda kwa sababu wote tulikua tunapendana, ndani ya muda mfupi ukaribu wangu na Leyra ulikua mkubwa sana, kama mwendo wa saa mbovu lile jina la domogundi lilianza kupotea taratibu.Leyra alikua na kitu fulani cha pekee ndani yake achana na uzuri, tabasamu na uchangamfu aliokua nao. Ndani yake ni kulikua na nguvu fulani ya kutenda miujiza sababu kila sekunde niliyoongea nae nilisikia furaha ya ajabu, tabasamu lake lilitosha kunisahaulisha matatizo yangu yote, nilijiona mwepesi mwili mzima kana kwamba nilikua nimesamehewa dhambi zangu zote.
Wakati Tanzania ikipata uhuru wake mwaka 1961 mimi uhuru wangu niliupata hapo, polepole hali ya kujiamini ilikuja, nilianza kumtania Leyra, nikaanza kumshika kiuno, kumkumbatia na kumuangalia kwa uhuru zaidi bila kuibia kama hapo awali.

“Leyra wewe ni mzuri sana” nilimwambia kila mara tulipokutana, ushuzi ulipata mjambani kama utani na mimi domo zege nikawa nimeula.

Kila nilichofanya na kumwambia Leyra alikua akitabasamu hata siku moja sikuwahi kumuona akiwa amekasirika.
Pamoja na mambo yote hayo kumwambia Leyra kua nampenda nilishindwa, nilitamani kumwambia Leyra kua nampenda sana na naomba awe mpenzi wangu lakini nilishindwa kabisa. Kila nilipotaka kumwambia maradhi yangu ya aibu yalinishika na kufanya niwe mpole kama mkulima aliyepotea shamba.
Leyra alitambua udhaifu wangu kua nilikua mahututi na maradhi ya aibu, aliamua kunipa ushirikiano, kila nilipomsifia kuhusu uzuri wake yeye pia alinisifia, kila nilipokua nikimuangalia nae aliniangalia, nilipotabasamu nae alitabasamu, alishika na kuzichezea ndevu zangu huku akiitekenya pua yangu.
Jamani ndugu zangu naombeni msinicheke kiukweli nakubali kua nilikua fala wa mwisho kabisa duniani kwani licha ya ushirikiano wote huo alionipa Leyra bado nilishindwa kumtamkia Leyra neno nakupenda.
Kwa sababu na yeye pia alikua ananipenda Leyra aliamua kunivumilia aliamini hatua tuliyofikia ilikua ahueni kuliko hapo awali.

Leyra alizidi kuwakataa wanaume wanaojua kueleza hisia zao ambao kutwa nzima walikua wakimsumbua na kumfuata kama kumbikumbi, aliwakataa kwa sababu yangu bila shaka alitamani kuniambia kua ananipenda lakini aliogopa kunianza, aliogopa angeonekana malaya ndio maana akachagua kuvumilia mateso yote kwa sababu yangu mimi.
Jambo hili lilituumiza sote wawili, ukaribu wetu haukua na maana yoyote sababu tulikua tunapendana lakini tulishindwa kuelezana hisia zetu.
‘When a woman love she love for real’ maneno ya wimbo wa msanii maarufu R-Kelly yalithibitika hapa kwani licha madhaifu yangu yote bado Leyra aliendelea kunivumilia, muda wote alikua upande wangu kila tulipokua free darasani au weekend tulishinda wote, tulitoka out kutembea sehemu tofauti tofauti pamoja.

Mambo yote haya yalikua mwiba mkali kwenye moyo wa Lucyra msichana mrembo aliyetokea kunipenda sana pengine kuliko wanawake wote waliowahi kunipenda. Ukaribu wangu na Leyra ulimtesa sana kuliko kitu chochote, muonekano wake dhaifu kila nilipoonana nae uliyathibitisha maumivu yake wazi, nilimuhurumia sana lakini sikuzikubalia hisia zake.
Mpaka wakati huo mpango wa Daniel haukusaidia kitu chochote kwa upande wao sababu ulimuumiza sana Lucyra. Badala ya kupendwa kama alivyodhani hapo awali safari hii Daniel alichukiwa zaidi kwa sababu ya kunipanga kundi moja na Leyra na kufanya tuwe na ukaribu mkubwa ambao ulimuumiza sana Lucyra msichana aliyenipenda toka utoto wetu ambaye maskini ya Mungu alianza kukuonda sababu ya stress na mawazo.
Kila nilipomuona Lucyra nilikumbuka utoto wetu, wema na upendo mkubwa alionionyesha toka utotoni ulinihukumu, maradhi yake ya mapenzi yalinitoa machozi, kudhoofu kwake kulinighutusha sana nilitamani niwe nae hata kwa kumdanganya lakini kutoka seminarini nilifundishwa kutokua muongo hata kidogo. Kwanini niwe na mtu ambaye simpendi ili kumsaidia na kumfurahisha yeye, moyo wangu ulikataa kabisa kulikubali hili jambo.

Kila muomba mboga huombea chungu chake maneno haya ya wahenga yalinipa moyo kuendelea kushikilia msimamo wangu, sikujihesabia haki lakini naamini sikua na kosa lolote mateso yote aliyoyapata Lucyra ilikua ni juu yake mwenyewe.
Pengine labda nilikua na makosa bila kujua ndio maana Mungu aliamua kuniadhibu kwa kunipa maradhi ya aibu na kufanya nishindwe kumuambia Leyra hisia zangu kwani hadi muda huo sikua nimemuambia neno lolote kuhusu mahusiano licha ya jitihada zote alizokua amezifanya.

......... Itaendelea......
 
Chapter 5

Leyra Lacena alikua msichana wa kipekee sana, alikua na uvumilivu wa ajabu hakutaka kunichoka mapema kiasi kile, alipoona jitihada zake hazijazaa matunda aliamua kunipeleka nyumbani kwao, alinitambulisha kwa wazazi wake na ndugu zake wawili wa kike ambao wote kwa pamoja walinipokea kwa uchangamfu mkubwa sana jambo lililozidi kuniaminisha kua hakika Leyra Lacena alikua ni mali yangu licha ya kwamba sikua nimemtamkia neno lolote la nakupenda.
Maisha yao yalikua ya kizungu familia yake ilinifurahia sana, hawakujali kuhusu dini yangu, walikua wakarimu sana bila shaka waliupenda uchangamfu wangu jambo lililofanya niwazoee mapema. Mimi pia nilimpelekea nyumbani kwetu kama alivyofanya yeye hapo awali, wazazi wangu na wadogo zangu walimpokea kwa furaha, wote waliushangaa uzuri wake. Nilimtambulisha Leyra kama rafiki yangu, niliogopa kuharibu mambo sababu kwanza sikua nimemwambia Leyra kua nampenda, pili niliwaogopa sana wazazi wangu hasa baba yangu ambaye siku zote alinisihi niachane na habari za wanawake mpaka muda sahihi utakapofika.

Furaha yote ilidumu kwa muda mfupi kwani baada tu ya kurudi chuo habari za Lucyra ziliwafikia wazazi wangu, waliniita nyumbani, bila hatia yoyote walinigombeza kama mtoto mdogo. Hukumu ya mateso yote ya Lucyra ilikua juu yangu, waliogopa kuvunja ujirani mkubwa wa familia zetu ambao ulikua umedumu kwa muda mrefu. Sikuwafanyia jeuri niliheshimu mawazo yao lakini sikuyaunga mkono, ilikua ni too late tayari, kwangu ilikua ni rahisi kwa Tanzania kuchukua kombe la dunia kuliko mimi kumuacha Leyra.
Wakati maradhi ya aibu yakiendelea kunitesa maradhi ya mapenzi nayo hayakua nyuma kumtesa Lucyra, ilikua afadhali yangu kwa sababu maradhi yake yeye yalizidi kuongezeka siku hadi siku. Kwake hospitali iligeuka kua kama chooni sababu ya kwenda mara kwa mara, kulazwa kwake ilikua ni kama dozi, badala ya saa mipira ya plastiki ilining’inia mikononi mwake, aliongezewa maji mara kwa mara sababu ya kupungua kwake.

Jambo hili liliwaumiza sana wazazi wake, hawakunisemesha neno lakini nyuso zao zilionyesha wazi chuki yao iliyokua juu yangu, waliniona kama msaliti niliyemsaliti binti yao na kumuacha awe mtu wa kuteseka kila siku kwa sababu ya mapenzi. Kutojali kwangu wala kuogopa kitu chochote kulizidi kuwakasirisha, kwa kinyongo na chuki nyingi juu yangu waliamua kuhama Dar es salaam, walihamia Arusha, walimuhamisha na binti yao Lucyra pia hawakutaka anione tena kama ilivyokua kwao.

Kuvuja kwa pakacha nafuu kwa mchukuzi, kuhama chuo kwa Lucyra ilikua ahueni kwangu sababu nilipata uhuru wa kua na Leyra muda wote. Furaha yangu hiyo kwa Daniel ilikua msiba kuhama chuo kwa Lucyra lilikua pigo kubwa sana moyoni mwake, kwake kumuona Lucyra ana kwa ana kila siku ilikua ni furaha tosha licha ya kwamba hakua amekubaliwa.
Katika moja ya nyimbo zake Marehemu Remy Ongala aliwahi kuimba kua kipenda roho hula nyama mbichi, kipenda roho haoni wala hasikii, hivyo ndivyo ilivyotokea kwa Daniel, kwake kukaa mbali na Lucyra ilikua ni mateso makali, wiki moja tu toka Lucyra ahame chuo, Daniel alianza kukonda.
Mapenzi ni kitu cha ajabu sana, yaone tu kwa mwenzako akiteseka, unaweza kumuona kama chizi lakini hujui kile anachokihisi moyoni mwake. Hata uwe gaidi kama Osama na misuli mikubwa kama The Rock mbele ya mapenzi utakua mdogo kama panado za Kenya. Hata anko Magu pamoja na kutumbua kote akifika kwa mama Janeth anakua mpole kama kifaranga cha njiwa.

Hivyo ndivyo ilivyokua kwa Daniel wiki moja bila kumuona Lucyra ilitosha kumtesa, kama mwanzo alijua asipofanya kitu lazima atateseka zaidi kama sio kufa kabisa. Katika mazingira ya kushtukiza Daniel nae alihama chuo bila hata kuaga.
Kuhama kwake kulihashiria uchaguzi, uchaguzi mdogo wa Cr ulifanyika kwa bahati nzuri nilichaguliwa kushika mahala pake. Nilikua Cr mpya, nilijiona kua miongoni mwa vijana wachache wenye bahati, kua Cr ni jambo la kawaida lakini kwangu lilinisaidia sana, ufaulu wangu ulianza kuongezeka sababu kiongozi yoyote lazima uongoze kwa mifano.
Bado naendelea kuyashangaa mapenzi, mapenzi ni kitu cha ajabu sana sababu kuhama kwa chuo kwa Daniel na kumfuata Lucyra alipo bado haikumzuia Lucyra kunikumbuka. Licha ya kwamba nae alihamishwa chuo lakini bado aliendelea kunikumbuka.

Mwanamke akipenda amependa kweli, Lucyra alikua kama kupe hakuchoka kunikumbuka hata mara moja. Mara kwa mara alinitafuta WhatsApp, huko alinitumia picha nyingi za utotoni tulizopiga wote wakati tukikua na kuifurahia michezo yetu ya kitoto pamoja. Kila muda aliomba nimtumie picha zangu.Lucyra hakunichukia alizidi kuniambia kua bado ananipenda sana na kila dakika kila saa hua ananifikiria. Kila siku aliponitafuta aliuliza kuhusu hali yangu pia alinijuza kuhusu maendeleo ya afya yake ambapo kutokana na maelezo yake bado alikua akisumbuliwa na maradhi ya mapenzi juu yangu.

Kadri maradhi ya mapenzi yalivyodhidi kumtafuna Lucyra na kumfanya azidi kudhoofika ndivyo maradhi ya aibu nayo yalivyozidi kunitafuna na mimi. Kuhama kwake chuo hakukunisaidia chochote zaidi ya kunipa ukaribu mkubwa na Leyra ambapo licha ya ukaribu huo bado nilishindwa kumueleza Leyra hisia zangu mpaka muda huo.
Dar es salaam jua lilizidi kua kali, watu wengi mitaani waliendelea kutafuta pesa kwa udi na uvumba. Chuoni nako masomo yalizidi kua magumu kila mwanafunzi alikua bize kusoma kwa bidii kuhakikisha anafaulu mitihani yake yote.
Sekunde, dakika, saa, siku, wiki, mwezi, miezi, mwaka, hatimaye miaka ilikatika, polepole kama mwendo wa kinyonga mjane email, simu na meseji za Lucyra zilianza kupungua. Ilianza kupita siku moja bila kupata simu wala ujumbe wowote kutoka kwake hatimaye wiki hadi miezi ikawa inapita bila kupata simu wala ujumbe wowote kutoka kwake. Kwangu kilikua sawa sikujali chochote kwa sababu sikua nikimpenda.

Tulikua mbioni kumaliza mwaka wa pili, mpaka wakati huo sikua nimemtamkia Leyra neno nakupenda. Tulikua na ukaribu mkubwa sana kila mtu alidhani tulikua wapenzi lakini haikua, kitu pekee nilichoambulia kwa Leyra mpaka wakati huo ilikua ni kuyabusu mashavu yake na kumkumbatia sababu ya ule ukaribu wetu.Muda wa mitihani ulifika, chuoni kila mwanafunzi alikua bize kusoma. Tulikua tunamaliza mwaka wa pili wa masomo. Tulifanya mitihani ya kumaliza semista, mitihani ilikua migumu sana lakini kwa neema za Mungu tulimaliza salama. Baada ya kumaliza mitihani tulifunga chuo na kwend likizo ndefu ya field muda wa miezi mitano.

Muda wa likizo miezi mitano kwangu ilikua ni kama mwaka, kama ilivyokua kwa Daniel mimi pia sikuweza kukaa mbali na Leyra, hali hii ilinitesa sana lakini sikua na jinsi zaidi ya kukabiliana nayo. Nilijitahidi sana mara kwa mara tukawa tunawasiliana, muda mwingi wa likizo ya field tulitumia ku chat na kuongea kwa video call kila siku.
Hali hii ilidumu kwa miezi kadhaa ya mwanzo lakini ghafla ilianza kubadilika polepole. Leyra aliacha kujibu meseji zangu, mwanzo nilidhani bahati mbaya lakini haikua, kila meseji niliyotuma WhatsApp aliisoma lakini hakunijibu, sikutaka kukata tamaa kwa sababu nilikua nampenda, niliendelea kumtafuta lakini cha ajabu hata nilipompigia simu hakupokea tena wakati mwingine alikata kabisa.

......... Itaendelea .........
 
Chapter 6

Ilipoishia...

kila meseji niliyotuma WhatsApp aliisoma lakini hakunijibu, sikutaka kukata tamaa kwa sababu nilikua nampenda, niliendelea kumtafuta lakini cha ajabu hata nilipompigia simu hakupokea tena wakati mwingine alikata kabisa.

Songa nayo..

Kweli dunia duara yote yaliyomkuta Lucyra yalinikuta mimi, tena ilikua afadhali ya Lucyra nilikua nikimjibu meseji na kupokea simu zake, mimi simu zangu kwa Leyra hazikupokelewa na meseji hazikujibiwa kabisa ingawa alikua anazisoma. Ilikua ghafla sana sikutegemea kama Leyra angebadilika kiasi kile, kiukweli niliumia sana. Ni kama Lucyra aliniambukiza, maradhi yake yote ya mapenzi yalihamia kwangu, kwa mara ya kwanza nikaonja maumivu makali aliyokua anayapata Lucyra juu yangu hakika akikua anateseka sana.Nilikua nampenda sana Leyra pengine kuliko kitu chochote kile ukimtoa Mungu na wazazi wangu. Yeye ndie alikua mwanamke wangu wa kwanza kumpenda maishani mwangu, mapendo yote ya kipadri niliyofundishwa seminarini Don Bosco kule nchini Kenya yalikua kwake kwa sababu sikua padri, labda baadae yangehamia kwa wagonjwa lakini nilikua mwanafunzi sikua daktari bado.

Nilitamani kumpigia Leyra simu na kumfokea kwa yale aliyokua ananifanyia lakini hata ningepiga simu isingepokelewa, hata kama ingepokelewa ningemfokea kama nani yake maana hatukua wapenzi, tulikua na ukaribu mkubwa lakini hatukukubaliana kua wapenzi sababu ya udomo zege wangu.Ni kama nilikua kuzimu inayotembea duniani, hali hii ilinitesa sana kuliko kitu chochote. Kila nilipoenda nilimuwaza Leyra, iwe kanisani, uwanja wa taifa kutazama mpira au bichi kupunga upepo bado sura yake ilikatiza kwenye mzunguko wangu wa damu, nilishindwa kabisa kumsahau Leyra.

Ile miezi mitano ya likizo kwangu ilikua ni kama miaka mitano, nilitamani sana kuonana na Leyra niliamini labda ingefanya akumbuke tulivyokua. Nilijuta sana kwanini nilishindwa kumwambia Leyra hisia zangu kua ninampenda, ingawa yeye mwenyewe alilijua hilo. Hakuna marefu yasiyokua na mwisho, likizo yetu ilikua ndefu lakini mwisho wa siku iliisha. Wote tulirudi chuoni kwa furaha, kwanza kuingia mwaka wa tatu na kuanza mwaka mwingine wa masomo, pili kukutana tena na marafiki maana ni muda mrefu kidogo ulikua umepita. Chuoni nilipanga kumueleza Leyra hisia zangu kua ninampenda sana, ingawa ilikua ni kama nimechelewa maana Leyra alikua ameanza kubadilika tabia. Mwaka wa tatu ulianza, masomo yalikua magumu sana kuliko mwaka wa kwanza na wa pili. Bila kupoteza muda nilimtafuta Leyra mapema sana kabla masomo hayajawa magumu zaidi. Sikuamini nilichokiona, safari hii ilikua ni bora kuongea na Leyra kwenye simu kuliko ana kwa ana.

Leyra alikua amebadilika sana, hakupenda kuongea na mimi tena kama zamani, achana na kumshika mkono na kubusu mashavu yake muda huu Leyra hakutaka hata nimguse. Leyra alianza kunichukia ghafla, zile fursa zote adimu za kutoka out na kwenda kutembea pamoja sikuzipata tena, sikua nimemkosea lolote wala sikua nimemkubalia Lucyra lakini nashangaa kwanini alibadilika na kuanza kunichukia.
Mwaka huo wa tatu wa masomo ulikua wa mateso mengi kwangu, achana na ugumu wa masomo darasani, kutotakiwa tena na Leyra ilikua ni kama nipo jela. Nilijuta kusoma hapo chuoni Baltimore key health chuoni sio kwa sababu ni chuo kibaya hapana, ni kwa sababu uwepo wangu hapo ulifanya nikutane na Leyra, na kua mtu wa kuteseka kila siku kwa sababu yake.

Nilitamani kuhama chuoni hapo kama Lucyra ili niwe mbali zaidi na Leyra labda ingeweza kunisaidia lakini kwa bahati mbaya nilikua nimechelewa, haikua rahisi kupata uhamisho mwaka wa tatu. Furaha yote niliyokua nayo mwanzo chuoni hapo iligeuka kua huzuni, kwanini Leyra hanipendi tena?, nilijiuliza lakini sikupata majibu hasa ukizingatia sikua nimemkosea hata mara moja. Nilichanganyikiwa sana.
Ukiacha Mungu pia nina amini sana katika sayansi lakini yaliyonikuta yalifanya kwa mara ya kwanza niamini maneno ya wahenga kua ‘Chelewa chelewa utakuta mwana sio wako’. Nilijilaumu sana, msemo wa ‘Kuku wako manati ya nini’ uliniponza, nilijuta sana kwanini sikumwambia Leyra hisia zangu. Kwa mara nyingine tena niligundua ni jinsi gani Lucyra alikua akiumia juu yangu.

Mwaka wa tatu ulikua mwaka wa mwisho kwa Leyra chuoni hapo, yeye alikua anamaliza mwaka huo tofauti na mimi niliyekua nasoma miaka mitano kwa sababu ya kuchukua magonjwa mawili, magonjwa sugu ya wanawake na watoto pamoja na mifupa, wakati Leyra yeye alichukua ugonjwa mmoja tu wa mifupa.Semista ya kwanza mwaka wa tatu iliisha, ilikua maajabu, sikutaka kuamini kama kweli Leyra alikua mjamzito, niliumia sana pengine kuliko nyakati zote maisha yangu. Ujauzito wake ndio ulikua sababu kubwa ya kunichukia, sababu iliyofanya anisahau na kutojishughulisha tena na mimi wala ule ukaribu wetu. Niliumia sana lakini nilijikaza kiume, nililia kimya kimya kila nilipokua peke yangu kila nilipotoka nje nilificha maumivu yangu kwa tabasamu bandia.

Kwa chuki na hasira nyingi nilimpa pongezi na hongera za kua mjamzito, naye bila wasiwasi wowote alizipokea kwa mikono miwili. Aliniambia angefurahi sana kama angejifungua mtoto wa kiume mzuri kama mimi. Sikumjibu kitu, maumivu makubwa kama upanga mkali yaliuchoma moyo wangu, mimba yake ilinitesa kuliko kitu chochote, nilitamani kummeza lakini kila nilipoangalia kosa lake halikuepo maana mimi ndiye nilieshindwa kumueleza hisia zangu.

... Itaendelea .. .
 
Chapter 7
.

Ghafla kama upepo nilianza kupokea salamu za pongezi kutoka kwa marafiki zangu na watu mbalimbali, kila mtu aliamini kua ujauzito wa Leyra ulikua ni wa kwangu kwa sababu ya ule ukaribu wetu mkubwa tuliokua nao mwishoni mwa mwaka wa pili. Habari za ujauzito wa Leyra zilisambaa kila mahali zilimfikia hadi Lucyra, licha ya kuacha kuwasiliana na mimi Lucyra alinitafuta tena, kwa moyo mweupe alinitumia ujumbe mrefu wa kunipongeza na kuahidi zawadi za nguo za mtoto pamoja na matoi ya kuchezea pindi mtoto atakapozaliwa.

Nilimshukuru Lucyra kwa shingo upande, mimba ya Leyra haikua ya kwangu sikuwahi kulala nae hata mara moja lakini niliona aibu kukataa zile pongezi. Kila salamu ya pongezi niliyopewa niliipokea, safari hii niliogopa kupewa majina mabaya zaidi ya lile la domo gundi nililopewa awali sababu kama ningezikataa zile salamu za pongezi kila mtu angejua kua ujauzito wa Leyra haukua wangu jambo ambalo lingezalisha aibu kubwa sana kwangu.
Kadri siku zilivyoenda ndivyo mimba ya Leyra ilizidi kukua, safari hii haikufichika tumbo lilikua kubwa kabisa, kadri tumbo lake lilivyozidi kuongezeka ndivyo ukaribu wetu nao ulivyozidi kupungua. Siku za mitihani ya kumaliza mwaka wa tatu na wa mwisho kwa Leyra zilikaribia, huo ndio ulikua mwisho wangu nilijua wazi nisingeweza kumpata tena. Jambo hili lilivimeza vyanzo vyote vya furaha yangu, niliumia sana, kwangu furaha ilikua ni kama simulizi maana nilikua nikiisikia kwa watu. Japo sikumjua lakini nilimchukia sana mwanaume aliyempa Leyra ujauzito kwa sababu hakuharibu tu ndoto zangu za kuishi na Leyra bali aliharibu kila kitu kuhusu maisha yangu, kwa uziri aliokua nao Leyra haikua rahisi mwanaume huyo kumuacha Leyra aendelee na maisha yake ni lazima alikua amepanga kumuoa.

Wiki ya mwisho ya kujisomea kabla ya kuingia kwenye chumba cha mtihani ilifika, semista nzima nilishindwa kusoma ningewezaje kusoma wiki moja ya mwisho. Nilijihurumia sana, maneno ya baba yangu yalikua kama mwangwi kila sekunde yalijirudia masikioni mwangu. Nilijaribu kunenepesha ng’ombe siku ya mnada, nilijitahidi sana kusoma, kila diskasheni iliyokua mbele yangu niliihudhuria, maktaba, hosteli kote nilikesha nikisoma lakini wapi, ng’ombe aligoma kunenepa siku ya mnada, vitu vya kusoma vilikua vingi, akili iligoma kabisa kuingiza vitu vipya kichwani.
Nilikata tamaa, niliona wazi aibu nyingine ya kufeli mitihani inasubiri kunitafuna. Nilichanganyikiwa, kufeli mitihani hiyo kulimanisha nisingeweza kuendelea na masomo yangu mwaka unafuata. Sababu kubwa ya yote haya alikua Leyra, nilijuta kwanini sikumuambia mapema toka mwanzo kua nilikua nampenda, kila nilipotafuta kosa lake sikuliona lakini kama alijua nampenda na yeye alikua ananipenda kwanini na asingeniambia.

Wiki nzima ya kujisomea sikua nimefanya kitu chochote cha maana, sikufungua tena notsi zangu, sikuwasha laptop wala simu yangu, nilikata tamaa ya kufaulu kabisa. Nilimpenda sana mama yangu lakini kwa mara ya kwanza katika maisha yangu nilijuta kuzaliwa. Siku moja kabla ya mitihani kuanza nilienda kujipumzisha kwenye bustani za chuo huku nikiugua kwa hofu, sikua nikiogopa mitihani lakini nilijua wazi kua ni lazima nitafeli, niliichukia sana mwaka wangu wa tatu, ukitoa mimba ya Leyra wenyewe ndio ulifuatia kuyaharibu maisha yangu.
Nilivuta vuta miguu yangu iliyokua imeishiwa nguvu kwenye viunga vya bustani hiyo, mwanga mkubwa wa jua uliokua ukipiga kwenye vioo vikubwa vya majengo ya ghorofa pembezoni kwa bustani hiyo ulionekana kunikejeli. Sikua na matumaini ya kufaulu hata kidogo. Nilipotambua ukweli juu ya kufeli kulikokua mbele yangu, nilitambua ukweli mwingine wenye kuumiza na kutisha zaidi, kua kama nitafeli mitihani yangu basi sitaweza kuendelea na masomo ya juu na kuharibu ndoto zangu za muda mrefu za kua daktari na kushindwa kulipa fadhila kwa bibi yangu.

Nilitoka bustanini nikiwa nimekata tamaa ya maisha, niliwaza na kuchagua kazi nyingine ambayo ningefanya endapo kama ningefeli mitihani yangu na kushindwa kuendelea na masomo ya juu. Nilikua kama chizi anaetafuta vyakula vya kuokota mitaani kwani nilitoka bustanini na kuzunguka chuo kizima, kila mtu alikua bize kusoma. Sikujali kitu, niliondoka chuoni na kwenda kanisani, ‘Sala ni silaha ya haraka zaidi kuliko kitu chochote’ maneno haya tuliyofundishwa seminari yalinipa moyo na ndio yalikua tumaini langu la mwisho. Japo waswahili wamasema Mungu na mbio lakini mimi sikujali. Kanisani nilisogea mbele kabisa, nilipiga magoti na kumuomba Mungu atende miujiza kisha nikarudi chuoni kisubiri mitihani.
Siku ya mitihani ilifika, mitihani yote ilifanyika, ilikua ni migumu sana lakini baada ya majuma mawili ilimalizika.

Stress za masomo na mitihani ziliwachanganya watu, wapo walioondoka chuo siku hiyo hiyo baada tu ya kumaliza mitihani. Leyra nae hakutaka kumaliza hata siku moja pale chuoni, siku zake za kujifungua zilikua zimekaribia. Kwa mara ya kwanza baada ya kutojali kuhusu mimi kwa kipindi kirefu, Leyra alinitafuta, tuliongea mambo machache kisha akaniaga na kunitakia kila la heri, nilijua nitafeli kutokana na maandalizi yangu mabovu lakini yeye alinipa moyo, alinihakikishia ni lazima nitafaulu na nitaendelea na masomo ya juu. Nilimshukuru sana, hakika ilikua ni huzuni kubwa, sote tulilia sana tulikua tunapendana lakini kosa dogo tu lilifanya tusiwe pamoja.

Nilimtakia kila ka heri pia maana sikua na jinsi zaidi ya kukubali matokeo kua mwenye kisu kikali ndiye anayekula nyama siku zote. Leyra alinishukuru pia kwa kila kitu, alinishukuru kwa muda wote tuliokua pamoja na mambo yote ya kitaaluma tuliyoyafanya wote. Baada ya hapo aliondoka hakutaka kuongea maneno mengi zaidi, alijua wazi jinsi gani ujauzito wake ulivyokua unaniuumiza, hakupenda niendelee kuumia, aliniaga kisha akaahidi atanipigia simu pindi atakapojifungua na tutaonana tena baada ya miezi mitano pindi atakaporudi tena chuoni kwa ajili ya kuhudhuria graduation yake.

Baada ya miezi mitatu matokeo yakitoka, namshukuru Mungu nilifanya vizuri, nilifaulu vizuri sana, sala zangu dakika za majeruhi zilitenda muujiza. Kila la heri na maneno ya Leyra yalitimia, nilikua naendelea na masomo yangu ya juu kumalizia miaka miwili iliyobaki. Nilikua naendele na masomo yangu ya juu, nilimuahidi Mungu kubadilika. Japo ilikua ngumu lakini nilisahau kila kitu na kuanza kusoma kwa bidii zaidi. Nilianza maisha mapya bila Leyra, sikutaka kuonana nae tena maishani mwangu, nilibadilisha namba zangu zote za simu, ilikua ni lazima nimsahau la sivyo nisingeweza kusoma vizuri.

........ Itaendelea......
 
Chapter 8

Nilimaliza field kisha nikarudi nyumbani kujiandaa na miaka yangu miwili ya mwisho iliyokua imebaki. Sikutaka hata kuhudhuria graduation ya Leyra nilijua kuonana nae tena hakutanisaidia kitu chochote zaidi ya kuniumiza. Niliamini ni lazima angekuja na mwanaume waliyezaa nae pamoja na mtoto wao jambo ambalo lingefichua ukweli uliokua umejificha machoni mwa watu wengi ambao waliamini kua mimba ya Leyra ilikua ni yangu.
Nilirudi chuoni wiki mbili baada ya graduation, kitengo cha mawasiliano chuoni nilipokelewa na barua ya Leyra aliyokua amemuachia mkuu wa kitengo Dr. Dufresne. Niliichukua barua hiyo iliyokua kwenye bahasha kubwa ya pinki, nilitafuta sehemu iliyotulia, niliifungua na kuanza kuisoma kwa umakini na utulivu mkubwa.

Kwako Alfred,

Ni matumaini yangu u mzima wa afya, kuhusu mimi ondoa shaka ni mzima wa afya tele. Nakuandikia barua hii huku bahari kubwa ya machozi ikiyameza macho yangu. Napenda kukujuza kua nimejifungua mtoto wa kiume. Nafahamu kua nilikuumiza sana na ujauzito wake, labda ndio sababu ukabadilisha namba za simu na kutohudhuria graduation yangu. Kiukweli sikudhamiria hata nikisema nikueleze ilivyokua hautaniamini. Fahamu tu kua mimi ni mwanamke niliyekamilika, ilifika hatua nikahitaji mwanaume wa kutimiza hamu zangu hapo ndipo nikapata ujauzito. Siku zote za maisha yangu mpaka naingia kaburini nitasikitika kwa sababu mwanaume huyo haukua wewe.
Kamwe sitajutia mtoto niliyempata, nitajutia tu kwa kua hakua mtoto wako. Najua ulidhani ninakuchukia lakini hapana sikuchukii hata kidogo, ujauzito wangu ndio ulinituma hivyo, wewe ni daktari mtarajiwa naamini utaelewa nini namaanisha. Alfred sitakusahau kamwe sio kwa sababu nakupenda, hapana. Sitakusahau kwa sababu umefanya nizae na mwanaume nisiyempenda hata kidogo, ambaye muda si mrefu nitafunga naye ndoa ili nimlee mwanangu na baba yake wa damu. Najuta kwanini wewe haukua huyo mwanaume, najuta kwanini nilikubali achukue nafasi yako, sikulaumu na wewe pia naomba usinilaumu mimi, najua ni makosa yetu wote maana tulipendana lakini tukashindwa kuelezana hisia zetu. Ni vizuri sana wote tumeyajua makosa yetu ingawa bahati mbaya imekua kwa kuchelewa. Naumia kuishi na mwanaume nisiyempenda, huku kwake upo mwili pekee, akili na moyo wangu wote upo kwako wewe. Nataka ujue kua bado ninakupenda, kila dakika kila saa ninakukumbuka sana kwa sababu wewe ndiye ulitakiwa ulilime shamba langu. Kama ningekua mkristu basi ningempa mwanangu jina lako Alfred kama kumbukumbu, bahati mbaya mimi ni muislamu. Pole kwa maumivu yote niliyokuumiza, mimi pia naumia sana lakini kutokua pamoja ni makosa yetu, ni kosa lako pia ni kosa langu maana haikua lazima wewe unieleze hata mimi pia ilikua wajibu wagu kukueleza hisia zangu. Mwisho kabisa nakutakia kila la heri katika maisha yako mapya, najua utaumia kuoa na kuishi na mwanamke usiyempenda lakini nakuahidi kila siku nitakuombea kwa Mungu akupunguzie maumivu hayo. Ni mimi nikupendae kwa dhati.

Leyra Lacena.

Barua ile ilitosha kunitoa machozi, Mungu pekee ndiye anayejua ni jinsi gani nilivyolia. Hakika ni kosa langu, nililigundua hilo lakini bahati mbaya ilikua kwa kuchelewa, kutokua pamoja na Leyra ilikua ni uzembe ujinga wangu mwenyewe.

Nilimjibu barua yake, nilimshukuru kwa maneno yake na kwa kadi ya mualiko wa harusi yake iliyotarajiwa kufungwa miezi miwili baadae. Japo nilimshukuru kwa kadi lakini sikupanga kuhudhuria harusi yao pia sikutoa mchango maana nilijua kufanya hivyo ni sawa na kuzidi kumuumiza Leyra ambae hakua akimpenda mume wake mtarajiwa hata kidogo ila yaliyotokea hakua na jinsi zaidi ya kukubali.
Nilianza rasmi maisha yangu mapya bila Leyra, lilikua ni jambo gumu sana lenye kuumiza kupita kiasi lakini hakukua na jinsi ilibidi iwe hivyo. Niliendelea na masomo yangu, safari hii nilisoma kwa bidii kuliko huko nyuma. Sikutaka kujua habari za Leyra, hata harusi yake sikuhudhuria, sikumchukia tena, bali niliogopa huenda angechanganyikiwa pindi ambapo angeniona nikimlilia wakati akiwa anaolewa.

Kosa langu kubwa lililoyagharimu maisha yangu lilikwisha tokea, sikutaka kutenda tena kosa lingine, niliogopa kuteseka kama Leyra alivyokua akiishi na mwanaume asiyempenda.Niliamua kumtafuta Lucyra msichana niliyewahi angalau kumpenda utotoni mwangu na kushindwa kumkubalia kwa sababu ya ubize wa masomo yangu. Kuolewa kwa Leyra kulifanya nigundue kua Lucyra alikua miongoni mwa wanawake wachache niliowapenda.

..... Itaendelea ....
 
Chapter 9

Sikutaka tena kuchanganya mapenzi na shule, nilisoma kwa bidii mpaka nilipomaliza masomi yangu na kufaulu vizuri sana. Maisha yaliendelea, baada ya kumaliza chuo niliajiriwa na hospitali ya chuo hicho hicho. Lengo langu la kua daktari lilitimia, nilifanya kazi vizuri kwa moyo wote maana ilikua ndio wito wangu, kila mtu alinipenda, mabosi wangu walinipenda, wagonjwa nao walinipenda mimi pamoja na huduma zetu kitu kilichofanya hospitali ya Baltimore key health hospital izidi kua maarufu Tanzania nzima.

Nilianza kujipanga kimaisha nilijenga nyumba nikanunua gari mbili za kutembelea kisha nikaanza kutafuta mwenzi wa maisha. Hapo ndipo nilipomkubuka Lucyra. Nilianza kumtafuta sana kama sindano ya mkono iliyopotea kwenye mchanga, nilimtafuta Lucyra kwenye simu lakini sikumpata, simu zake zote hazikupatikana, whatsapp akaunti yake ilifutwa, emails nazo kila nilipotuma hakunijibu, nilijihisi kuchanganyikiwa sababu sikujua alipokua.
Niliwashirikisha wazazi wangu suala hili, kwa msaada wao mkubwa nilisafiri kwa ndege mpaka arusha nikafika mpaka nyumbani kwa wazazi wake lakini sikumpata Lucyra, kote huko hakuwepo hata wazazi wake hawakuwepo nyumba yao hiyo waliiuza kwa mhindi ambaye ndiye alinipa hizo taarifa zote na kwa bahati mbaya zaidi hakujua walipohamia maana walipomaliza biashara ya kuuziana nyumba kila mtu alishika hamsini zake.

Kumkosa Lucyra kulifanya nichanganyikiwe, kosa langu lingine la kutomkubali mapema lilianza kunitafuna nilianza kuumia na kuteseka upya. Nilitokea kumpenda Lucyra ghafla, sijui kwanini sikumpenda kutokea awali kwani safari hii mapendo yangu yote kwa Leyra yalihamia kwa Lucyra haraka sijui kwanini mwanzo sikumpenda hivi labda kwa sababu wanaume hatujui kupenda kweli.
Baada ya kuulizia majirani na kumtafuta Lucyra bila mafanikio nilirudi tena Dar es salaam kuendelea na kazi yangu ya utabibu. Kumkosa kwangu Lucyra kulifanya niendelee na kazi, nilifanya kazi kwa bidii sana, niliamua kubaki single bila mpenzi, juhudi na muda wangu mwingi niliweka katika kazi zangu.

Nilifanya kazi miaka miwili bila kujua habari za Lucyra wala Leyra. Kwa Leyra ilikua sawa maana nilishaamua kumsahau lakini kwa Lucyra kutokujua chochote kuhusu yeye bado kuliendelea kuniumiza ndani kwa ndani. Baada ya kufanya kazi Baltimore key health kwa miaka miwili niliacha kazi, niliamua kufanya kazi zangu mwenyewe. Nilifungua hospitali yangu binafsi, haikua kubwa sana lakini ilikua nzuri yenye uwezo wa kutoa huduma nyingi tena nzuri kuliko hata mahospitali makubwa. Hispitali yangu ilijihusisha zaidi na magonjwa ya watoto na wanawake, lakini sana sana ilikua maalumu kwa ajili ya watoto. Siku zote kazi ngumu zina malipo yake polepole hospitali yangu ilianza kuvuma, niliipa jina la AL hospital (A ilikua jina langu Alfred na L ilikua kuwaenzi Leyra na Lucyra), kila mtaani ilikua ni LA hospital, ndani ya muda mchache tulipata watoto wengi wagonjwa wa kuwahudumia.

Niliendelea kupambana na maisha mchana na usiku nilihakikisha hospitali yangu inakua bora machoni mwa watu wengi, kiukweli nilifanikiwa kwani kila aliyepata huduma kwetu alikua balozi wetu. Huduma zetu nzuri zilifanya tuwe maarufu kila kona, wagonjwa walikuja kwetu kila siku wakafanya akaunti ya AL hospital izidi kufulumia pesa kila siku. Ndani ya muda mfupi nilianza kua bilionea hospitali iliniingizia pesa nyingi sana, kama ningekua mtu wa starehe na majivuno nchi nzima ingeujua utajiri wangu.
Kadri pesa zilivyoongezeka ndivyo uhitaji wa huduma zetu ulivyozidi kua mkubwa. Nami bila kuchelewa nilitumia fursa, nilianza kufungua matawi ya AL hospital Tanzania nzima. Niliajiri watu wasomi katika menejimenti yangu hivyo walinishauri njia zote za kupita. Kwa taaluma zao walinishauri kama nataka uwekezaji wangu uwe salama basi nitafute wanasheria na msemaji wa AL hospital.

Niliheshimu mawazo yao, bila kuchelewa nilitumia vyombo vya habari kutangaza tenda hiyo, mshahara wa milioni 3 na nusu kwa mwezi ulifanya maombi yawe mengi kupita kiasi. Kila aliyetima cv zake alikua na sifa ilitupa tabu sana kujua yupi tumchukue na yupi tumuache. Mimi pamoja na timu yangu nzima ya menejimenti tuliamua kuweka intavyuu ili kupata watu sahihi zaidi.

Siku ya intavyuu ilifika, watu walikua wengi kama utitiri. Tulianza kumu intavyuu muombaji mmoja mmoja, ilikua kazi ngumu lakini ilikua ni lazima ifanyike. Siku ya kwanza ilipita, ya pili ya tatu, hatimaye wiki mbili za intavyuu ziliisha. Siku moja kabla ya wiki mbili kumalizika nilishangaa kumuona mtu ambaye sura yake haikua ngeni machoni kwangu. Nilijiuliza nimewahi kumuona wapi lakini sikupata majibu. Nilimuangalia kwa makini naye pia aliniangalia, nikahisi huyu mtu ananifahamu pia maana tabasamu kavu katika uso wake liliashiria kua tumewahi kuonana sehemu pengine na kuongea wote huko nyuma.

...... Itaendelea....
 
Chapter 10

Baada ya kuangaliana kwa dakika kadhaa yule mtu alinifuata na kunisalimia. Alinichangamkia sana kitu amabacho kilinishangaza maana kila nilipo jaribu kumkumbuka nilishindwa kabisa. Tulisalimiana lakini hatukua na muda wa kuongea, tulijali sana muda. Intavyuu iliendelea, zamu ya yule mtu ilifika tulipoanza kumu intavyuu ndipo hapo nikamkumbuka baada ya kujitambulisha majina yake mawili.
Alikua ni Daniel Moses kiongozi wetu wa kwanza kabisa wa darasa wakati tukiwa mwaka wa kwanza. Huyu ndiye Daniel aliyakua anampenda sana Lucyra kipindi kile alikua mwembamba kama kijiti cha fagio, mapenzi yake ya kweli kwa Lucyra yalitaka kimuua kiasi cha kufanya ahame mpaka chuo ili kumfuata Lucyra, ambapo huko alikwenda kusomea sheria.

Safari hii Daniel alikua mnene kama mbwa wa kizungu, kitambi kilimtoka, mashavu nayo yalishirikiana kufanya uso wake upanuke, kifupi Daniel alikua amenenepa mambo yake yalionekana kua safi sema intavyuu aliyokuja kuifanya ilikataa kulithibitisha hilo. Baada ya intavyuu tuliongea mambo mawili matatu kuhusu maisha na kila kitu kwa ujumla, Daniel aliniuliza kuhusu Leyra, nilimshangaa kwa kudhani anafanya makusudi maana kila mtu alijua kilichotokea. Nilimwambia kila kitu kwa ufupi, pole alizonipa na masikitiko yake yalifanya niamini kua kweli hakujua chochote. Nilimuuliza kuhusu Lucyra, Daniel aliniambia ana miaka kadhaa hajawasiliana nae, licha ya kuhama chuo na kumfuata bado Lucyra aliendelea kumkatilia mpaka siku wanamaliza chuo hakua amefanikisha chochote.

Maneno yake yalinipa moyo wa kuendelea kumtafuta Lucyra, lakini nilipoomba namba zake Daniel aliniambia hana na wala hajui ni wapi Lucyra alipokua. Nilikata tamaa ghafla hata maongezi yetu yakabadilika tukaanza kuongea mambo mengine kuhusu maisha na maendeleo kwa ujumla. Baada ya maongezi tuliagana kila mtu akaendelea na hamsini zake.

AL hospital kazi ziliendelea kama kawaida, baada ya vikao kadhaa vya bodi tulianza kutoa mrejesho kuhusu intavyuu iliyofanyika. Daniel aliajiriwa kua mwanasheria mkuu wa hospitali yangu, mbali na matokeo yake mazuri pia urafiki wetu ulichangia kupata nafasi hio, wema mkubwa alionitendea tukiwa chuoni kunipanga kundi moja na Leyra bado niliukumbuka.

Bahati nzuri ikikuchagua unaweza ukapata kila kitu kasoro tu kuokota nyumba. Bahati nzuri ilikua upande wangu. Kila tulichokifanya kilifanikiwa, matawi ya hospitali yangu nayo yalizidi kukua, huduma zetu zilipendwa na kila mtu kiasi cha kupata tuzo ya appreciation kutoka wizara ya afya. Malezi niliyoyapata seminari yalinizuia kijikweza na kuanza majivuno kama vijana wengi wanaopata mafanikio makubwa katika umri mdogo kama wangu, kwani kila wiki tulikua na siku moja ya kuwatibu bure wangonjwa wasioweza kulipa gharama za matibabu.

Ilikua Jumatatu tulivu lakini ndefu kuliko Jumatatu zote toka nianze kazi yangu ya utabibu. Siku hiyo tulikua na kikao kirefu sana, bodi yangu ya hospitali na wizara ya afya tulikua na kikao kujadili sera na jinsi ya kutokomeza ugonjwa wa marelia kwa wakina mama wajawazito na watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano. Tukiwa tunaendelea na kikao ghafla simu ya mezani ukumbi wa mikutano iliita, kama nilivyoipokea ndivyo nami nilivyopokelewa na habari za mshtuko.

“Dokta Alfred, Dharura, dharura, dharura kuna mtoto kaletwa hapa sasa hivi anahitaji uparesheni ya haraka” ilikua simu kutoka mapokezi.

Uhai ni bora kuliko kitu chochote, niliondoka kwenye kikao na kwenda mpaka chumba cha upasuaji huko nako nilipokelewa na timu yangu ya upasuaji ya watu watano. Kitandani nilikutana na mtoto wa miaka mitano au sita akiwa amevunja mguu huku mfupa wa mguu ukiwa umetoka nje ya nyama za miguu.

“Amefanyaje” niliuliza.

“Ameanguka kwenye bembea”

Kilio cha uchungu kutoka kwa yule mtoto na uharaka wa tiba ulinisahaulisha kila kitu kuhusu kukagua faili lake wala kuuliza kuhusu wazazi wake, hata nguo za upasuaji nilizivaa haraka haraka ni kama nilikua nakimbizwa. Ndani ya dakika tano uparesheni nzito ilianza kufanyika. Tulimchoma sindano ya usingizi kisha kwa msaada ya timu yangu nikaanza kuifanya ile upareshi kwa umakini mkubwa sana.
Baada ya masaa manne ya kazi nzito uparesheni ilimalizika. Sikutaka kurudi tena kwenye kikao, nilienda moja kwa moja ofisini kwangu nakuanza kukagua faili ya yule mtoto ambaye mvunjiko wake ulinigusa sana kumsaidia ingawa ilikua wajibu wangu. Kama ilivyokua kwenye intavyuu kuonana na mtu asiye mgeni kwangu, pia jina la mzazi wa mtoto huyu lilinishtua sana.

Jina la mtoto lilikua ngeni kwangu, ila jina la mama yake lililoandikwa sehemu ya mzazi kwenye cheti hapo lilinishtua sana.
Leyra Lacena, Mungu wangu!! Moyo wangu ulipiga paa, mapigo ya moyo yakaongezeka na damu ikaanza kuzunguka haraka haraka mwili mzima niliisikia ikipita. Yule mtoto niliyemfanyia uparesheni muda mchache uliopita kumbe alikua ni mtoto wa Leyra, bila shaka ndiye yule ambaye mimba yake ilifanya mama yake anichukie. Yule ndiye mtoto ambaye mama yake alisema angempa jina langu kama tu angekua mkristu kama mimi, nilishangaa sana labda ndio maana nilitokea kumjali sana.
Ghafla nikiwa katika hali ya kushangaa simu yangu ya mezani iliita, bila kuchelewa niliipokea.

“Dokta Alfred na mruhusu mzazi wa mtoto aje kukuona” sauti ilisikika.

“Sawa”

Haikupita dakika 2 hodi ilisikika mlangoni kwangu, wasiwasi na hofu kidogo vilinishika ghafla bila shaka alikua ni Leyra.


…. Itandelea. ….
 
Chapter 11

Mungu wangu! Nilipatwa na mshangao, alikua ni Leyra Lacena kama nilivyodhani. Nilijitahidi sana kumkwepa mwanamke huyu maisha yangu yote kwa kubadilisha namba yangu ya simu na kukatisha mawasiliano lakini haikuwezekana, kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi hatimaye tulikua tunaonana tena ana kwa ana. Leyra alishangaa sana kuniona, unaanzaje kumsahau mtu unayempenda maisha yako yote?. Leyra alinikumbuka, aliponiona tu mapigo yake ya moyo yalibadilika na kuanza kupiga haraka, pumzi zake nazo zikapanda ni kama mtu aliyetoka kukimbizwa na mbwa wa polisi.

“Alfred Kamba!!” Leyra aliniita kwa mshangao.

Alishindwa kujizuia, nguvu ya mapenzi ilikua kubwa kuliko nguvu yake ya mwili, ilimzidia kiasi cha kumfanya aje anikumbatie na kuyabusu mashavu yangu, kama isingekua pete ya ndoa mkononi mwake bila shaka angeibusu midomo yangu. Sikujua kama nilifurahi kumuona Leyra ama laa, kwangu kila kitu kilikua kawaida, hata alivyonikumbatia sikuona mabadiliko yoyote mwilini kwangu, kila alichokifanya hakikunisisimua kama zamani, labda kwa sababu nilikua nimeanza kumpenda sana Lucyra.

Nilimkaribisha kwenye kiti kisha nikaendelea kuifanya kazi yangu, baada ya kusalimiana nilichukua faili la mtoto wake na kuanza kumueleza kuhusu oparesheni ya mtoto wake na maendeleo yatakavyokua baada ya kumpatia matibabu hayo. Baada ya hapo tuliongea kidogo kisha nikamuomba Leyra anipishe niendelee kuhudumia wagonjwa wengine.
Kesho yake tena Leyra alikuja kumuona mtoto wake, kama kawaida alikuja ofisini kwangu bila hiyana nilimkaribisha. Tuliongea kidogo kisha Leyra akaniomba tutoke, siku hiyo sikua na kazi nyingi nilimkubalia. Alitaka tutumie usafiri wake lakini niligoma nilikua makini sana na ndoa yake. Tulikubaliana kwenda serena hotel kupata chakula cha mchana na kufanya maongezi kidogo hivyo kila mtu aliondoka ma gari lake mpaka hotelini na hapo tukaagiza chakula na kuanza maongezi yetu.

Tuliongea mambo mengi sana, swali la kwanza la Leyra ilikua kuhusu mahusiano yangu, aliniuliza kama nina mtu au nipo mwenyewe. Bila uoga nilimdanganya kua nina familia tayari, mke na watoto wawili. Uso wake ulibadilika kidogo, kwa shingo upande Leyra alinipongeza kama mimi nilivyompongeza wakati wa ujauzito wake kipindi kile chuoni. Ilikua kichekesho kidogo labda alipenda asikie kua nipo singo, lakini hata kama angesikia hivyo bado isingemsaidia chochote maana tayari alikua mke wa mtu.

Tuliongea mambo mengi kuhusu maisha na vitu vingine vingi. Leyra alikua hajui kama ile AL ilikua ni hospitali yangu mpaka wakati ule nilipomwambia. Kwa mshtuko mkubwa Leyra alinipongeza, hakika alijua kutumia fursa alijifagilia na kuponda kule alipokua akifanya kazi. Kwa maongezi mengi yaliyotukumbusha huko nyuma niliamua kumsaidia, nilimwomba afike kesho hospitali na vyeti vyake tuone itakuaje. Leyra alinishukuru sana na baada ya maongezi karibu masaa matatu tuliagana kila mtu akaenda kwake. Kesho yake kama kawaida Leyra aliendelea kuja kumtazama mtoto wake mpaka aliporuhusiwa, katika wakati huo alileta vyeti vyake nami nikaishirikisha menejimenti yangu wote wakaridhika na vyeti vyake hatimaye tukamuajiri kama daktari daraja la kati na naibu mkuu msaidizi idara ya watoto katika hospitali yetu.

Kama kawaida maisha yaliendelea. Leyra na Daniel nao waliendelea kufanya kazi zao katika kutimiza na kufanikisha maendeleo ya AL hospitali. Kila mtu kwa nafasi yake alitimiza wajibu wake bila kukumbushwa wala kuzembea kitu kilichofanya AL hospitali izidi kua gumzo nchi nzima na pembezoni mwa ukanda wa Afrika mashariki na kati. Kibaya chajitembeza lakini kizuri chajiuza, kwa mara nyingine tena tulipata tuzo ya kukubalika kutoka wizara ya afya, baada ya miezi kadhaa shirika la afya duniani nao walitupa tuzo yao ya heshima pamoja na shirika la haki za binadamu ambao wao pia walitupa tuzo ya heshima kuheshimu msaada wetu wa kutenge siku moja kuhudumia wagonjwa wasiojiweza bure kabisa.

Kwetu ilikua ni faraja kubwa sana, si mimi tu kila mfanyakazi wetu alifurahi, kuanzia walinzi getini mpaka ngazi ya juu kwenye bodi na utawala. Ili kujipongeza mwisho wa mwaka tuliamua kufanya sherehe, kwanza kusherekea Happy AL family day sherehe ambayo ilitukutanisha wafanyakazi wote na familia zao kwa lengo la kufahamiana, pili kusherekea tuzo za heshima tulizopewa na kuadhimiaha siku ya kuanzishwa hospitali ya AL ambayo ilikua inatimiza miaka kadhaa.
Kilichotoke siku ya sherehe hiyo kiliniacha mdomo wazi, kwa mara ya kwanza nilimuona mume wa Leyra, waliongozana na mtoto wao niliyemfanyia upasuaji mimi mwenyewe. Hiyo haikunishtua sana maana Leyra nilimuona kama dada yangu wa tumbo moja, sababu sikumpenda tena.

Katika hali ya kutotegemea kwa mara ya kwanza baada ya kuhangaika sana nilionana na Lucyra. Lucyra alikua mke wa Daniel, nilipowaona tu sikuhitaji kujiuliza swali lolote, maana walivaa nguo sare, kitambaa cha shati la kitenge alichovaa Daniel kilafanana na gauni alilovaa Lucyra. Pete vidoleni mwao, kua pamoja muda wote pamoja na ujauzito aliokua nao Lucyra vilieleza wazi. Nilipigwa na butwaa, matumaini yangu yote ya kuja kua na Lucyra yaliishia hapo labda. Kwanini Lucyra hakunijali kama zamani, kila kilichoendelea hapo kilinipa majibu, maana waligandana muda wote walikua pamoja kama kumbikumbi.

Sherehe ilipokwisha wote Daniel na Lucyra walinifuata mezani. Tuliongea mambo mengi, kwa mara ya kwanza baada ya miaka kadhaa nilishikana mkono na Lucyra, tuliongea mambo mengi sana, Daniel alitumia nafasi hiyo kuniomba radhi kua siku nilipomuuliza kuhusu Lucyra alinidanganya kwa sababu aliogopa kuniumiza, pindi angeniambia kua amemuoa huenda ningemnyima hata kazi, ndio maana akaamua kunidanganya. Bila hiyana nilimsamehe maana alifanya yote kwa ajili yangu. Mimi pia nilimuomba msamaha Lucyra kwa yale yote yaliyotokea nyuma, nilimuomba aniombee msamaha kwa wazazi wake pia ili nizidi kuishi kwa amani na baraka tele ziendelee kua upande wangu.

Japo Daniel alijua juu juu niliamua kuwaambia kila kitu kuhusu Leyra, jinsi alivyopata ujauzito mpaka kuolewa na mwanaume kama ambavyo hakuna aliyetegemea. Wote walinionea huruma, Lucyra alilia sana labda kwa sababu aligundua kua zile salamu zake za pongezi zilikua makosa kuzituma maana ujauzito haukua wa kwangu. Tuliongea mengi na kukumbushiana vitu vingi vya nyuma, wote walinicheka na kunitania jinsi nilivyokua domo zege, haikuniumiza chochote maana tulikua tushayasahau yote.
Ghalfa tuliwa katika maongezi, Leyra na familia yake walijiunga katika meza yetu. Tuliongea mambo mengi sana, wote walinipongeza kwa maendeleo niliyoyapata. Nami niliwaambia maana halisi ya AL hospitali kua ni Alfred na Leyra na Lucyra.
Wote walifurahi kusikia hivyo, walinishikuru sana. Muda wote huo mtoto wa Leyra alikua magotini mwangu, nilikua nimempakata, matibabu niliyompa yalifanya tuwe marafiki wakubwa sana kwani kila siku Leyra alikua akinipa salamu zake.

Mume wa Leyra alinishukuru sana kwa huduma niliyompa mtoto wake, aliniambia kua alikua nchini Japan kufuatilia biashara zake za magari ndio maana hakuonekana wakati wote wa kumuuguza mtoto wake. Hakika siku hiyo ilikua siku ya furaha kubwa sana maishani mwangu, kwanza kutimiza ndoto zangu za udaktari na kuwafanya wazazi wangu wawe watu wa furaha muda wote, pili kukutana na wanawake wawili walionipa funzo kubwa katika maisha yangu. Tulikunywa na kuongea kwa furaha mpaka majida ya usiku sana, wote tulikua kama ndugu tayari maana kila mtu aliuona umuhimu wa mwenzake. Baada ya maongezi mengi na vicheko vingi vya furaha, uchovu ulishika nafasi yake. Wote tuliagana na kupeana mawasiliano yetu ya simu, kila mmoja na familia yake aliondola zake, mimi niliondoka zangu mpaka nyumbani kwangu. Baada ya kumkosa Leyra na Lucyra sikutaka kukurupuka tena kufanya makosa yoyote, pesa nilikua nayo lakini kuna muda mwingine pesa sio kila kitu ndio maana nikawa makini sana.

Nilikaa miaka miwili zaidi mpaka kwa msaada wa Leyra ambaye aliamua kunikutanisha na mdogo wake wa damu, ambaye walifanana kila kitu kasoro majina tu huyu aliitwa Leyra yeye aliitwa Saudath. Japo nilianza kumpenda Lucyra lakini nilivyokutana na Saudath nilijiona mtu mpya, nilitokea kumpenda sana, tabasamu lake lilinisahaulisha kila kitu kilichoniumiza maishani mwangu. Baada ya uhusiano wa mwaka mmoja na kidogo niliamua kumuoa Saudath, tulikua dini tofauti lakini habati nzuri wazazi wetu wote walikua waelewa. Baada ya vikao na taratibu zote kukamilika nilimuoa Saudath kwa ndoa ya msemto, tulifunga ndoa kanisani kwetu kisha baada ya hapo kila mtu akaendelea kusali katika dini yake. Safari hii bahati nzuri ilikua upande wangu tena, mwaka wa kwanza tu wa ndoa yetu Saudath alinizalia mtoto wa kiume, nilimshukuru sana mke wangu, maana mtoto wangu akifanana kila kitu na mimi. Nilimpa jina la Baltimore kama kumbukumbu ya maisha yangu na kila kitu kilochotokea chuoni kwetu Baltimore. Nilimlea Baltimore katika misingi yote impendezayo Mungu, huku nikimuombea asije kua domo zege, na kuteseka kama mimi.

Nilichojifunza katika maisha ni kwamba wakati ni lazima mtu ukosee ndipo uweze kujifunza. Unapokosea katika jambo lolote usisikitike wala kujidharau na kujiona kua haufai, bali kua makini na ujiulize maisha yanajaribu kunifundisha nini. Mwanafalsafa maarufu Bibi Katrina Mayer aliwahi kusema kabla maisha hayajakupa furaha ya maisha kwanza ni lazima yakupe mafunzo ya maisha. (Before life gives you its happiness it will offer you its lesson first) pia hao hao wazungu wanasema “Your last mistake is your best teacher” (Kosa lako la mwisho ndio mwalimu wako mzuri) sisemi tukosee makusudi lakini hii ina maana kua tuwe tayari kukosea inapobidi ili tuweze kujifunza, usiogope kufanya jambo fulani kisa unaogopa kufanya makosa au kukosea hapana, fanya kila kitu au fursa iliyopo mbele yako huku ukiwa tayari kujifunza kupitia kila kosa unalolitenda katika maisha yako, mwisho wa siku wote tukumbuke kwamba kutenda kosa sio kosa bali kurudia kosa ndio kosa, na kosa sio kosa mpaka usindwe kujifunza au kulisahihisha.

*Mwisho*
 
Photo
FB_IMG_1572731850050.jpeg
 
Back
Top Bottom