Koki za plastiki zaadimika Kahama

Analogia Malenga

JF-Expert Member
Feb 24, 2012
5,011
9,879
BAADHI ya wafanyabiashara wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamesema koki za plastiki za mabomba zimeadimika wilayani humo, baada ya kulanguliwa kwa wingi na kusafirishwa kwenda Dar es Salaam huku ndoo moja ikiuzwa kwa Sh 30,000.

Ugonjwa wa corona umepandisha mauzo ya koki za plastiki bila kutegemewa, kwani mahitaji zaidi yameibuka ghafla, ukilinganisha na koki za chuma, ambazo bado zipo madukani.

Mfanyabishara mwenye duka la vifaa hivyo mjini Kahama ambaye pia ni Mhasibu wa Kamati ya Maendeleo katika Kanisa la AIC Pastorate ya Nyihogo, Charles Machali amesema wafanyabiashara kutoka Dar es Salaam wamekuwa wakizilangua zote madukani kwa bei ya jumla.

Machali alisema kwa sasa wakazi wa Kahama, wameanza kuhangaika pa kupata koki za plastiki za mabomba, baada ya kulanguliwa kwa wingi na kusafirishwa kwenda Dar es Salaam, huku ndoo moja bado ikiuzwa kwa Sh 30,000 iliyowekewa koki tayari.

Alisema kabla ya kuingia kwa virusi vya corona, koki za plastiki zilikuwa hazina soko, kwani walipokuwa wakichukua mzigo wanasota nao dukani hata mwaka mzima bila kuisha.

“Soko limekuwa kubwa kwa ghafla mahitaji ni mengi kutokana na wananchi kujikinga na virusi vya corona kwa kunawa mikono kwa maji yanayotiririka,” alisema Machali.

Alisema watu mpaka maeneo ya vijijini, wameanza kunawa kila wakati mabwawani kwa kutumia sabuni, hivyo watu wengi wameanza kujenga utamaduni wa kunawa.

Alisema kinachotakiwa waelezwe vyombo vinavyotumika kunawia ili wasizalishe maradhi mengine.

Pia, Machali alisema tangu virusi vya corona vilipotangazwa kuwa vipo nchini, waumini wote waliacha kushikana mikono kwa kutakiana amani ya Bwana, badala yake wamekuwa wakizungumza na waumini kuitikia na hilo limeanza kuwa mazoea sasa.

Wajasiriamali wadogo mjini Kahama, Musa Shayo na Jeneste Kulwa walisema wamekaguliwa na maofisa afya wa halmashauri, ambao wamesisitiza kila mmoja awe ndoo ya kunawia, lakini changamoto wanayopata ni kuadimika kwa bomba za plastiki.

Shayo alisema bomba za plastiki, bei yake ni nafuu, tofauti na za chuma zenye kufungulia hata kwa kiwiko zina gharama kubwa. Pia ndoo moja inauzwa kwa Sh 30,000, hivyo gharama ni kubwa hawawezi kuimudu.
 
Back
Top Bottom