Kliniki za Matibabu ya kibingwa wilayani kutokujumisha Wafamasia Bingwa na Wateknolojia Bingwa wa Maabara za Afya kwenye jopo, Haijakaa sawa

Kliniki za Matibabu ya kibingwa wilayani kutokujumisha Wafamasia Bingwa na Wateknolojia Bingwa wa Maabara za Afya kwenye jopo, Haijakaa sawa

Munamuge

JF-Expert Member
Joined
Sep 22, 2014
Posts
903
Reaction score
896
Salaam, mimi nilie mdogo kati yenu nawasalimu.

Kwanza kabisa napenda kutambua mchango mkubwa na matokeo chanya yatokanayo na kampeni ya huduma za kibingwa katika Hospitali za wilaya na baadhi ya Vituo vya Afya zinazoendelea nchini kote.

Mwezi May mwaka huu, kampeni hizo nadhani zimeanza awamu ya tano, na zipo zinaendelea katika mikoa mbalimbali nchini.

Watanzania wengi ambao hawakua na uwezo wa kusafiri hadi hospitali za mikoa, kanda na hata taifa kwaajili ya uchunguzi, matibabu na ushauri wa kibingwa kuhusu changamoto zao za kiafya wamepata nafasi ya kuonana na mabingwa na wabobezi hao. Changamoto za mifumo ya uzazi kwa akina mama, changamoto za magonjwa ya ndani (ambalo ni janga kubwa zaidi katika nchi yetu), changamoto za vimbe mbalimbali zinazohitaji upasuaji na changamoto za magonjwa ya watoto zimepatiwa ufumbuzi karibu kabisa na wananchi, na kwa gharama nafuu kuliko ambavyo wangelazimika kugharamia kupata huduma hizo katika hospitali za ngazi za juu.

Zaidi ya kutoa huduma kwa wateja, jopo hili ambalo linahusisha Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya wanawake, Upasuaji, Watoto, Koo, pua na masikio, Magonjwa ya ndani, Meno na Utoaji dawa za usingizi na Wauguzi wabobezi (Nurse specialists) limekua likitoa mafunzo kazini na kusimamia wataalam waliopo katika vituo hivyo kutoa huduma za kibobezi zinazowezekana kufanyika na mtaalam wa ngazi ya chini, ama kutoa mafunzo ya namna ya kutoa msaada wa awali kwa mgonjwa anaehitaji huduma za kibingwa kabla ya kumpatia rufaa.

Pamoja na mafanikio hayo, naiona changamoto ya kutoshirikishwa kwa kada nyingine muhimu kama Wafamasia Bingwa/wabobezi na Wateknolojia Bingwa wa maabara, ambao ninaamini mchango wao kwenye jopo hili unahitajika.

Kutokana na ufahamu wangu kuwa na wigo mfinyu, basi nitaelezea sababu chache za umuhimu wa kushirikishwa wafamasia kwenye jopo hili, sitaongelea kundi la wateknolojia maabara kutoka na uelewa wangu kutokua mpana kwenye eneo lao.

Kwanza kabisa: Mfamasia anatakiwa kufanya uchaguzi sahihi wa dawa kwa ajili ya matibabu ya mgonjwa kwa kuzingatia hali ya mgonjwa, mwingiliano wa utendaji kazi kati ya dawa na dawa, dawa na vyakula, dawa na hali yoyote ya vichocheo vya mwili vinavyoweza kutokana na magonjwa ama muundo wa kibayolojia wa mgonjwa (Genetic makeup).
Kutokana na wagonjwa kupewa huduma za kibingwa, basi kuna ulazima wa Mfamasia Bingwa kushiriki pia kwenye kuongoza na kuelekeza wafamasia waliopo katika vituo hivi kufanya uchaguzi na utoaji wa dawa hizi kwa usahihi.

Pili; Utoaji wa dawa kwa dozi sahihi kulingana na hali na hatua ya ugonjwa (Optimization). Ikumbukwe kwenye vitabu vya rejea na mafunzo, matibabu pendekezwa huandikwa kwa kuzingatia kiasi anzia na kiasi ukomo cha dozi (Minimum and Maximum dose), hapa ndipo unaingia umuhimu wa mbobezi kutumia elimu na uzoefu wake kuwasaidia wafamasia wa chini yake katika kufanya maamuzi sahihi kwa mafunzo kazini.

Tatu; Uhitaji wa wafamasia kufanya ufuatiliaji wa huduma za kimatibabu katika hatua zote, hasa kwa wagonjwa waliolazwa. Uwepo wa Mabingwa hawa kwenye kambi hizi za matibabu utasaidia kuwajengea uwezo wafamasia kuanza kutoa huduma hizi na kuboresha mtiririko mzima wa huduma za kimatibabu.
Ikumbukwe huduma hizi hazikua sehemu ya kitita cha mafunzo ya wafamasia katika ngazi za Stashahada ama Shahada (zaidi ya kuelezwa kwenda wodini kwa muda wa majuma mawili bila usimamizi wa Wafamasia tabibu).

Nne; kuongezeka kwa janga la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa za kuua ama kufubaza vimelea (Anti microbial resistance), hasa vimelea kundi la bakteria, ambapo kuna uwezekano miaka michache ijayo tukawa na vifo vitokanavyo na UTI (mfano) kwasababu ya kukosa dawa za kutibu vimelea vya magonjwa kama hayo na kuvifanya vimelea kuendelea kuzaliana mwilini na kuathiri mifumo nyeri ya mwili.
Kuna uhitaji mkubwa wa wabobezi kwenye ufuatiliaji wa matumizi sahihi ya dawa na madhara/maudhi yatokanayo na dawa (Pharmacovigilance Pharmacists) kushirikishwa kwenye huduma hizi ili watoe elimu na mafunzo ya ufuatliaji na udhibiti wa janga hili huko chini.

Hii pia inaendana na ukweli kuwa tuna bomu kubwa linajitengeneza kutokana na matumizi yasiyodhibitiwa ya dawa za asili na tiba mbadala kwa kuchanganya na tiba za kisasa (conventional medicines), tatizo hili linatafuna vizazi vyetu kimya kimya na kuongeza mzigo wa watu wenye magonjwa yasiyoambukiza yanayotokana na mwingiliano wa mifumo ya uchakataji wa kemikali hizi. Elimu kubwa inahitajika huko chini.

Tano; Kutoa hamasa kwa wafamasia waliopo katika halmashauri kwenda kusoma na kujiendeleza ili waweze kuwa Mabingwa pia na kutoa huduma za kibingwa (ukizingatia Muundo mpya wa ajira kwa kada za Afya unaotarajiwa kuanza kutumika mwezi july mwaka huu umeijumuisha na kuitambua kada ya Wafamasia Bingwa).

Kwahiyo ninapenda kuishauri wizara na waratibu wote wa zoezi hili kwakuzingatia kuwa aslimia 95 ya matibabu hukamilika pale tu mgonjwa anapopatiwa dawa, kwahivyo mgonjwa anaweza kuonwa na Daktari Bingwa na akaandikiwa dawa sahihi, lakini kama mfamasia anaetarajiwa kufanya uchaguzi wa dawa hizo na kutoa kulingana na hali ya mgonjwa hajawezeshwa, basi lile kusudio letu halitatimia, basi wizara iwajumuishe Mabingwa hawa ili wakasaidie kubadili mtazamo na mwelekeo wa huduma za kifamasia kwenye hospitali zetu.

Asanteni.
 
Back
Top Bottom