Kitanda cha mpangaji mwenzangu

Kitanda cha mpangaji mwenzangu

Daudi1

JF-Expert Member
Joined
Dec 14, 2013
Posts
15,838
Reaction score
26,244
KITANDA CHA MPANGAJI MWENZANGU-1

“Samahani anti, unaweza kuniazima fagio kama unalo?”
“Sawa anko, ngoja nikuletee.”
Baada ya dakika moja mlangoni…
“Ngoo ngoo ngooo.”

“Ooo, asante anti, nakurudishia sasa hivi.”
Baada ya dakika kumi…
“Anti…anti…antieee…”
“Mama hayupo, kaenda dukani.”“Haya, basi akija mwambie nimerudisha fagio.”

Baada ya dakika tano, mama Tina anarudi ndani, mkononi ameshika kimfuko cha rambo, kwenye korido anapishana na Os Anjelus…
“Anti nashukuru sana kwa fagio.”
“Tayari ee?”

“Tayari, nimempa binti yetu.”
“Sawa anko. Vipi sasa, naona unatoka.”
“Ee anti, nakwenda kwenye ile nyumba niliyokuwa naishi, niliacha vitu vyangu.”
“Haya karibu sana, si tupo,” mama Tina alisema huku akiingia chumbani kwake.
***
Ilikuwa mara yake ya kwanza Os Anjelus kulala kwenye nyumba hiyo ambayo ina wapangaji watatu tu. Yeye alikuwa na chumba kimoja ambacho pia alikitumia kama sebule kwani mlikuwa na masofa.
Mpangaji mwingine ni Halima, yeye anamiliki saluni ya kusuka nywele wanawake, inaitwa Yero Masai. Mara nyingi anakuwa kwenye hiyo saluni na msichana mmoja wa kumsaidia.

Halina hajaolewa, ila rekodi yake kwenye nyumba hiyo ni kubadili wanaume wa kulala naye. Leo akiingia na Abdi, kesho asubuhi anatoka naye, jioni anarudi na Saimon.

Mpangaji wa tatu ni mama Tina. Yeye ana mume, ndiye baba Tina. Ni dereva wa magari ya manispaa. Muda mwingi anakuwa kazini. Mtu anayepatikana nyumbani hapo ni mama Tina tu, Tina naye anakuwaga shuleni, anasoma darasa la kwanza ila siku hiyo ilikuwa Jumamosi kwa hiyo hakwenda shule.

***
Usiku wa siku hiyo, Os Anjelus hakupata usingizi aliouzoea kule alikohama. Ni kawaida, watu wengi hukosa mtiririko mzuri wa usingizi wanapolala eneo geni…
“Iko haja ya kumwita mke wangu sasa. Si nilimpeleka nyumbani ili nitafute chumba kingine? Si nimeshakipata? Sasa nini tena?

“Lakini loh! Yule mama mwenye nyumba kule nilikohama kiboko. Mama mdomo mchana kutwa! Uchafu kidogo wa kuufagia sekunde kumi yeye anafoka nusu saa? Sijawahi kuona mimi.

“Sasa kwa mfano siku ile alipotupa notisi kwa ule uchafu wa kuufagia dakika mbili tu kama nisingemtishia kwenda polisi, si angeongea siku nzima?” aliwaza Os Anjelus huku akihisi kizunguzungu cha ugeni, lakini msisitizo wake mkubwa ndani ya moyo ni kumwita mkewe, Happy.

***
Asubuhi kulikucha, Os Anjelus alikuwa wa pili kutoka nje. Wa kwanza alikuwa mama Tina, baada ya yeye ndiyo akatoka Halima ambapo alimtengea maji ya kuoga mwanaume aliyerudi naye usiku uliopita.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa Halima kuonana uso kwa macho na Os Anjelus kiasi kwamba, mwanzoni Halima alijua ni mgeni wa mama Tina…
“Za leo anko?”

“Nzuri sista, mzima wewe?”
“Mzima, karibu sana.”
“Asante nimekaribia.”

Lakini Halima hakumuuliza Os Anjelus kama yeye ni nani kwenye nyumba ile, aliogopa kuonekana ni ‘mshankupe’ wa mtaa.
Kila mmoja aliendelea na lake, Os Anjelus aliingia chooni, Halima alitenga maji akaenda ndani kumwita jamaa yake, anaitwa Mabange.

***
Halima alitoka na Mabange kwenda kwenye saluni yake, kwenye korido akakutana na mama Tina…
“Za asubuhi mama Tina?”
“Nzuri Halima, umeamkaje?”
“Salama tu,” alisalimia Tina, akapunguza sauti…

“Eti huyu kijana ni nani, mgeni wako?”
“Mgeni wangu?! Aka! Si mpangaji mpya aliletwa na mwenye nyumba juzi.”
“Ooo, kwa sababu sikuwepo. Anafanya kazi wapi?”

“Mi sijui Halima.”
“Ana mke?”
 
KITANDA CHA MPANGAJI MWENZANGU-2

ILIPOISHIA
"Salama tu," alisalimia Tina, akapunguza sauti…
"Eti huyu kijana ni nani, mgeni wako?"

"Mgeni wangu?! Aka! Si mpangaji mpya aliletwa na mwenye nyumba juzi."
"Ooo, kwa sababu sikuwepo. Anafanya kazi wapi?"
"Mi sijui Halima."
"Ana mke?"
JIACHIE MWENYEWE…


"Halima, mimi sijui lolote."
"Ana gari?"
"Halima bwana, mi sitaki," alisema mama Tina huku akiondoka kwa mwendo wake wa madaha.
Halima aligeuka kumwangalia huku akimtamani maana japokuwa ni mwanamke mwenzake lakini moyoni amekuwa akikiri kwamba, mama Tina aliumbika kuliko yeye.

Mama Tina alijaliwa. Kwenye bodi nyuma alikuwa amefungashia, kiuno kilikatika vizuri, japokuwa alishazaa mtoto mmoja lakini bado nido zake zilikuwa zinadai kama za binti aliyeingia ukubwa.
Mviringo wa miguu yake na kuitwa jina la bia lilimfanya azidi kutamanika hata machoni pa wanawake wenzake. Sura yake ilijaliwa duara lenye upole na macho ya kulewa huku midomo ikishibishwa na unene wa rangi nyeusi.

Sauti ya mama Tina ilikuwa na uwezo wa kuwafanya wananchi wenye hasira kali wamsamehe kumchoma moto kibaka aliyemkwapulia simu mzee maarufu wa mtaa.
Siku mojamoja, hasa Jumapili alipokuwa akienda kanisani, aliwaacha hoi watu wa mtaani kutokana na magauni yalivyokuwa yakimkaa.

Umri wake wa miaka 32 ulimtosha kuendelea kuonekana msichana mbichi kutokana na kujitunza na kujaliwa ngozi nzuri na Muumba.

***
Asubuhi iliyofuata, Os Anjelus alitoka chumbani kwake na kukutana na mama Tina kwenye korido…
"Za asubuhi anko?"
"Nzuri anti, umeamkaje?"
"Salama tu. Naona kumekucha?"

"Ee, kumekucha anti, nataka kufua kwanza halafu ndiyo niende kibaruani."
"Pole sana. Ungetafuta mtu wa kukusaidia kazi kama hizo anko."
"Ni kweli, unajua nina mke lakini yupo kwao, nadhani mwisho wa mwezi huu atakuja."
"Hapo itakusaidia."

Mazungumzo yao yalitumia kama dakika moja, kila mmoja akaendelea na mambo yake.
Baba Tina aliondoka kwenda kazini, Os Anjelus alikuwa amemaliza kufua na sasa alikuwa akijiandaa kwa kutoka…
"Ngo…ngo…ngo," mlango wake uligongwa.
"Karibu," alisema kijana huyo huku akifungua mlango…

"Oo anti, karibu."
Mama Tina mkononi alishika sinia lenye chupa ya chai, sukari, kikombe na vitafunwa…
"Karibu chai anko."
"Ooo. Anti mbona unasumbuka jamani?"
"Usijali anko, we kunywa tu."
"Asante sana."

Os Anjelus alipokea sinia hilo na kurudi ndani kwake, akanywa chai na kurudisha vyombo…
"Anti vyombo hivi."
Mama Tina alitokea, akapokea sinia lake huku akishukuru…
"Baadaye basi anti."

"Sawa anko, nilikuwa na wazo moja anko. Ungeacha funguo nikufanyie usafi chapuchapu."
"Hapana nitafanya mwenyewe anti, nisikusumbue."
"Noo, hunisumbui anko, we acha tu."
"Jamani, nitakuchosha anti."
"Wala ndiyo kazi zetu akina mama tukiwa nyumbani."

Os Ajelus aliacha funguo, mama Tina akaipokea na kuifunga kwenye pindo la khanga aliyovaa.
Nusu saa mbele, mama Tina alikuwa ndani ya chumba cha Os Anjelus akifanya usafi. Baadhi ya vitu havikuwa vimepangwa, akapanga yeye alivyoweza huku moyoni akimsifia kijana huyo kwa kuwa na vitu vizuri na vya kisasa.

Alibabaika zaidi kwenye kitanda na mashuka. Ilifika mahali alijitupa kitandani na kunesanesa huku moyoni akisema…
"Kinaonekana kinatoa usingizi mnono."
 
basi siku hiyo usiku mama tina akawa anananii na kijana yule akananii hadi kila mmoja alichoka..kimsingi walisali na kuomba kwa muda mrefu
 
KITANDA CHA MPANGAJI MWENZANGU-4

ILIPOISHIA :
"Nimekuletea chakula anko," mama Tina naye alitumia sauti ya chini.
"Da! Asante sana anti."
Wakati Os Anjelus anapokea, sauti ya Halima mlangoni ilibisha hodi…
"We kaka wa Kingoni."


Ukimya ulitawala kwa muda kwani Os Anjelus alishindwa kuitikia kutokana na uoga kwamba angeingia angemkuta mama Tina…
"Wenyewe humu ndani, hodini," alikomaa Halima.

"Sikia, nenda, fungua mlango lakini usimruhusu aingie ndani hata sekunde moja," mama Tina alimwambia Os Anjelus kwa sauti ya chini sana ili asisikie Halima kule mlangoni.
"Sawa," Os Anjelus alikubali huku akienda kufungua mlango. Mama Tina akijibana kwenye kona ya chumba ili asionekane maana mlangoni hapakuwa na pazia.
"Vipi we Mngoni, mzima?"

"Mzima dada angu, karibu sana."
Mama Tina kule ndani aliposikia karibu sana, alishtuka sana, alijua kijana huyo atamruhusu Halima apite kuingia…
"Mwenzetu ujio wako kufahamiana ni muhimu, ulikuwa ukiishi wapi zamani?"
"Mburahati."
"Una mke?"

"Nina mke na mtoto mmoja."
"Wako wapi sasa?"
"Wako kijijini."
"Watakuja lakini?"
"Mwisho wa mwezi huu watakuwa hapa."

"Sawa, sasa unakula nini maana napika."
"Hapana anti, usijali kuhusu suala la chakula, mi tayari."
"Kwani unapika humu ndani?"
"Nakula gengeni."

"Hivi hiki chumba ni kikubwa kweli?" Hebu nione ndani," Halima alisema akionesha dalili za kutaka kuingia kwa kuinua mguu mmoja na kukanyaga mbele.
"Sista samahani, iko siku utaingia lakini si leo," alisema Os Anjelus huku akiinamia chini kwa aibu.
"Yaani mimi kuingia kwako anko mpaka unipangie siku, unajua ni kwa kiasi gani nimekupenda?" Halima alipasua jipu kwa mara ya kwanza…

"He!" kule ndani mama Tina alijikuta akisema kwa sauti ya mshangao…
"Yaani mwanamke anajitongozesha hivihivi, ama kweli Halima ni malaya sana jamani," alisema mama Tina lakini huku mapigo ya moyo yakimwenda kwa kasi.
"Sista utanipendaje wakati nimekwambia nina mke wangu? Mimi hapa ndani hakuna mwanamke nitakayetembea naye kwa sababu kati ya mambo siyataki ni pamoja na usaliti."
"Ina maana hujawahi kumsaliti mkeo?"

"Na wala sina wazo hilo."
"Basi mwenzetu kumbe ana bahati ya mtende, kuota jangwani."
Mama Tina alimsifia kijana huyo, hasa kwa msimamo wake aliouonesha kwa Halima kwamba hawezi kumsaliti mke wake.

Halima aliondoka, Os Anjelus akafunga mlango kwa funguo na kurudi, akakaa kitandani huku akimwangalia mama Tina kwa macho ya huruma kwa jinsi alivyokuwa amejibanza kwenye kona…
"Pole sana anti."
"Usijali anko, kawaida tu. Unajua huyu msichana ana mdomo sana, angeniona hapa angekwenda kuyatangaza nje."

"Ni kweli kabisa, umetumia busara kushauri usiingie."
"Sasa mi nitatokaje humu?" alihoji mama Tina.
"Ngoja nitoke mimi niangalie hali ya hewa."
"Sawa."
"Mama Tina," aliita Halima kule nje..
"We mama Tina."

Mama Tina aliogopa zaidi, alijua Halima ataingia kwake na atamkuta mtoto. Na ikawa hivyo kweli…
"We Tina mama yuko wapi?"
"Katoka."
"Kaenda wapi?"
"Sijui, aliweka chakula kwenye sufuria akatoka."

Tina alijua hotipoti ni sufuria.
Halima alishtuka kusikia mama Tina aliondoka na sufuria yenye chakula…
"Kaenda nacho wapi? Atakuwa kampelekea yule kijana."
***
Wiki moja tu mbele, siku hiyo mama Tina alikuwa akitoka gengeni, akakutana na mama mmoja jirani yake anaitwa mama Sindilia.

"Nilikuwa nakutafuta sana mama Tina."
"Kuna nini tena mama Sindilia."
"Mwenzangu si umbeya wa mtaani, uhujui?"
"Upi huo mama Sindilia."

"Nasikia unatembea na kijana mpangaji mwenzenu ndani."
"Eti nafanyaje?"
"Nasikia kuna kijana mmoja kahamia kwenu, ndiyo unatoka naye. Nikasema mama Tina huyuhuyu ninayemjua mimi anaweza kufanya upuuzi huo kweli?"
 
KITANDA CHA MPANGAJI MWENZANGU - 5

ILIPOISHIA
"Nasikia kuna kijana mmoja kahamia kwenu, ndiyo unatoka naye. Nikasema mama Tina huyuhuyu ninayemjua mimi anaweza kufanya upuuzi huo kweli?"
JIACHIE NAYO…
"

Ha! Mama Sindilia, unavyoona naweza kufanya upuuzi kama huo kweli, mimi mama Tina? Na ndoa yangu tamu?"
"Ndiyo nikashangaa. We hujasikia?"
"Sijasikia kokote."

"Basi kaa ujue hivyo."
"Wewe nani kakwambia?"
"Mh! Mwenzangu hayo mengine sana, tutaonana siku nyingine," alisema mama Sindilia huku akiondoka zake.

Mama Tina nusura presha impande kwani watu wa mtaa ule anawajua vizuri, si ajabu kumwambia mume wake kuhusu tetesi hizo jambo ambalo litamuweka pabaya.
"Hivi atakuwa nani? Au Halima? Huyu atakuwa Halima tu," alisema moyoni mama Tina wakati akiingia nyumbani kwake.

Licha ya kuwepo kwa madai hayo, mama Tina alitafuta muda wa kuonana na Os Anjelus ili amsimulie habari za mtaani.
Ilikuwa wakati kijana huyo amerudi, kabla hajaingia kwake, mama Tina alimdaka kwenye korido…
"Anko kuna kitu kikubwa sana na cha hatari kinataka kutokea."

"Kinahusu nini anti?"
"Mimi na wewe."
"Nini tena anti?"
"We nenda, usifunge mlango nitakuja kukwambia."
"Poa."

Os Anjelus alizama chumbani mwake, akapumzika kidogo kisha akatoka kwenda kuoga, aliporudi alivaa bukta tu na kujitupa kitandani huku akiwa amefungulia feni kwa spidi ya kawaida.
Mama Tina alimalizana mambo yake, akatembea kuelekea kwa kijana huyo huku akiwa katika hali ya tahadhari. Kabla ya kuingia alimpigia simu Halima akiwa amesimama usawa wa mlango wa chumba chake…

"Halina leo unarudi saa ngapi nataka kukuagiza kitu."
"Mh! Kusema ukweli nitachelewa sana, kuna sehemu nitakwenda kujirusha, labda kwenye saa sita, saba usiku. Ulitaka kuniagiza nini?"
"Sabuni."

"Labda nikununulie nikupe asubuhi."
"Hapana, nitakwenda kununua pale kwenye duka la urembo la kisimani."
"Poa."
Mama Tina akaondoa wasiwasi, maana alidhani Halima angeweza kuingia muda wowote ule. Alizama ndani kwa Os Anjelus.

"Vipi, naona umelala?"
"Nimepumzika tu anti, si unajua tena."
"Ni kweli," alisema mama Tina akikaa pembeni ya kitandani, akashika godoro kulia na kushoto kama anayetaka kuaga kuondoka.

"Mwenzangu, leo nimekutana na mama mmoja jirani, akasema amesikia eti mimi natembea na wewe, he! Nilishangaa sana, mimi sijawahi kupata kashfa kama hiyo hata siku moja katika maisha yangu ya ndoa."
"Mh! Kweli? Yeye huyo mwanamke alisikia wapi?"
"Kagoma kuniambia, lakini mimi nahisi Halima."
"Halima yupi, huyu dada wa chumba cha pili?"
"Huyohuyo."

"He! Mbona anataka kuleta balaa."
"Balaa balaa, tena ni uuaji, maneno kama hayo yakifika kwa mume wangu si ndoa sina!"
"Kabisa anti. Dah! Ni wa kumwonya lakini."

"Mh! Mimi sitamwambia kitu, ila Mungu atanilipia, iko siku yake. Mi najua anakutaka ndiyo maana anafanya hivi, yeye anadhani mimi na wewe ni wapenzi," sasa mama Tina alianza kupunguza sauti. Akaendelea…
"Tena naomba anko, isije ikatokea hata siku moja umekaa naye ukasema ninavyokusaidia kusafisha nyumba au kukupa chakula…"

"Anti, mi si mtoto, siwezi hata siku moja…"
"Unanihakikishia anko?"
"Kweli kabisa."
"Mh! Tushikane mikono tule kiapo."

Os Anjelus akatoa mkono, mama Tina akaupokea, akaubana…
"Ukikiuka itakula kwako."
"Siwezi kukiuka."
"Kweli?"
"Kabisa."

"Siamini," sasa mama Tina alimsogelea usoni kijana huyo…
"We amini."
"Nifanyie kitu chochote niamini," alisema mama Tina.
"Unataka nikufanyie kitu gani?"
"Chochote ambacho mimi nitaamini kweli hutaweza kuanika siri yetu."
 
KITANDA CHA MPANGAJI MWENZANGU - 6

ILIPOISHIA
Os Anjelus akashtuka, akamvutia kwake, mama Tina akatua kwenye kifua cha kijana huyo.
ENDELEA NAYO…


"Jamani, unajua mwenzio nikifanyiwa mautundu kama haya napata tabu," alisema mama Tina kwa sauti yenye aibu.
"Pole sana anti, lakini ikiwa polepole sidhani kama utananihi," alisema kijana huyo ambaye tangu mwanzo alishahisi kwamba mwanamke huyo ana lake jambo…

Sasa mama Tina alikuwa amelala kifuani kwa Os Anjelus, amelegea kama vile ametoka kutundikiwa dripu kwenye zahanati ya mbali na nyumbani kwake.
Alikuwa akihema kwa kasi, mapigo ya moyo yalikuwa si yake. Alipojaribu kufumbua macho yalikataa kwa kujisikia vibaya.

Os Anjelus akajua ni yeye ndiye anayetakiwa kuendesha jahazi la mahaba kwa wakati huo, akamshika na kumtoa kwenye kifua chake, mama Tina akakaa.
"Anti…"
"Be…"
"Uko sawa?"

Mama Tina alitingisha kichwa kuonesha kwamba hayuko sawa…
"Unatakaje?"
Mama Tina kuulizwa unatakaje ikawa kama amechochewa, alimvaa kijana huyo wakaanguka kitandani wote, akaanza kumpapasa sehemu ya kifuani huku akionekana anafanya vile kwa sababu tu ya hali iliyomkumba, la sivyo asingethubutu!

Os Anjelus alishuka chini, mama Tina akabaki kitandani. Alimvuta miguu na kuichanua kila mmoja na upande wake, wa kaskazini ulikwenda huko wa kusini pia ulishika nafasi yake.

Ili kumwonesha mwanamke huyo kwamba yeye ni mahiri kwenye soka la chumbani, Os alipeleka kichwa eneo la wachezaji kukutania ili mpira uanze. Hapo palimchanganya sana mama Tina akaanza kuimba nyimbo za maombolezo ya mahaba huku akijitahidi sauti ya wimbo huo isifike nje wakacheza hata wasioalikwa itakuwa aibu kwake.

Os Anjelus alipoona sauti ya mwimbaji huyo imeanza kukatika, akajua hata mashairi yameanza kumalizika alichotakiwa ni yeye kuingia kucheza ili onesho likamilike.
Alianza kwa staili ya kushambulia upande wa kulia, akaja wa kushoto ili kumchosha mwanamke huyo ambaye hakuonyesha kushambuliwa wala kujikinga ili magoli yasiingie kwenye lango lake.

Dalili za watu kupita nje ya mlango waliokuwemo ndani yake zilikuwa za wazi na mama Tina alimtahadharisha kijana huyo kuwa makini na namna yoyote ya kutoa sauti itakayofika nje kwani itajulikana.
"Poapoa mama," alikubali kijana huyo huku akiendelea na mashambulizi.

Ilifika mahali Os ndiye aliyekuwa akimzuia mama Tina kutoa sauti ya juu kwani alikuwa na dalili zote kwamba hakujali tena lile onyo lake.
"We Tina mama yuko wapi?" sauti ya mpangaji mmoja ilisikika kwa nje, akimuuliza mtoto huyo…
"Sijui," alijibu Tina."
"Basi nenda ndani Tina."

"Mi namngoja mama," alisema Tina na kuanza kulia.
"Ohoooo!" Os Anjelus alihamaki kwa mbali huku akipunguza nguvu za mashambulizi, lakini mama Tina alimhamasisha kwa kumshika mwili na kumwashiria kwamba alichotakiwa kufanya ni kuzidisha kasi ili dakika tisini za mchezo zifike haraka na mambo yaishe.

Lakini dakika hizo kila kijana huyo alipotaka kuzimaliza kwa kuzidisha kasi, mama Tina aligugumia kwa sauti hali iliyomlazimu mwenyeji wake kumziba kinywa ili waliopita nje ya ukumbi wasisikie anavyoimba wakafika getini ili na wao waingie kucheza kama siyo kushuhudia.
Mama Tina alipunguza biti ambapo sasa alikuwa akiimbia ndani ya chumba sauti ambayo alikuwa akiisikia mwenyeji wake tu.

Ilikuwa wakati mama Tina anataka kufika kwenye kilele cha mlima waliokuwa wakiupanda ambapo alitoa uyowe mmoja wa juu kuashiria furaha yake ya kufika akiwa haamini kwa jinsi mlima huo ulivyokuwa na changamoto kibao wakati wa kupanda.

Nje, au kwenye korido yule mpangaji aliyemuuliza mtoto Tina mama yuko wapi alisikia ukelele wa mama Tina, akashtuka na kusimama.
 
KITANDA CHA MPANGAJI MWENZANGU - 7

ILIPOISHIA:
Nje, au kwenye korido yule mpangaji aliyemuuliza mtoto Tina mama yuko wapi alisikia ukelele wa mama Tina, akashtuka na kusimama.
ENDELEA SASA…

Kujua, alikuwa anajua kwamba chumba kile kimeingiliwa na mpangaji mgeni ambaye hamjui jina zaidi ya kumwona, lakini ukelele wa mama Tina kama ulimwingia kichwani japo si kwa ushahidi mkubwa.
"Mh! Huyo si mama Tina kweli?" alijiuliza yule mpangaji huku mapigo ya moyo yakiwa yanampiga kwa mwendo wa mabasi yaendayo mikoani akiwa haamini hata maneno yake ya kumtuhumu mama Tina.

"Eti Tina, umesema mama amekwenda wapi vile?"
"Sijui mimi."
Yule mpangaji akaingia ndani kwake. Akatulia humo huku anatafakari kama alichokisikia ni cha kweli au masikio yake yalikaa vibaya…
"Hivi mama Tina huyu ninayemjua mimi anaweza kufanya hivi?" alijihoji mwenyewe yule mpangaji.
***
"Suka nisubiri dakika tano tu, nachukua kitu nakuja unipeleke nilikokwambia," Halima alimwambia dereva wa bodaboda aliyempeleka nyumbani hapo.
Alikuwa na safari ya kwenda kwingine lakini alilazimika kurudi nyumbani mara moja kwa ajili ya kuchukua kadi ya benki au ATM.
"Poa anti," alikubali dereva wa bodaboda.

***
"We Tina mbona unalia?" Halima alimuuliza mtoto huyo…
"Mama yuko wapi?"
Tina aliendelea kulia. Yule mpangaji mwingine akatoka kuungana na Halima pale kwenye korido ili kumuuliza Tina aliko mama yake.

"Hata mimi nimemuuliza lakini kasema hajui," mpangaji mwingine alisema.
"Sasa na yeye atakuwa amekwenda wapi mpaka anamwacha mtoto kama maskini hapa nyumbani?" alisema Halima huku akiweka simu sikioni na kumpigia mama Tina.

Kule chumbani mama Tina alijisahau, aliingia na simu yake lakini hakuipunguza mlio, akashtukia inaita tena namba ya Halima ambaye alimsikia akiongea nje kwenye korido.
Mlio wa simu ya mama Tina ni wimbo wa Bahati Bukuku wa Dunia Haina Huruma kwa hiyo ulipolia, si Halima wala yule mpangaji aliyeujua, bali hata Tina mwenyewe japokuwa ni mtoto lakini alisema…
"Mama huyo."

Ilikuwa tabu chumbani kwa Os Anjelus, mama Tina ameshajulikana aliko, Halima amejua mwanamke huyo yumo chumbani kwa kijana mpangaji mgeni…
"Ha! We mama Tina, mtoto wako analia huku husikii kwani?" Halima aliulizia akiwa amesimama mlangoni sasa…

"Nakuja Halima," ilibidi mama Tina ajifanye ni jambo la kawaida tu yeye kuingia kwenye chumba cha kijana huyo.
"Sasa mbona hujamuaga mwanao, anaulizwa anasema hajui ulipo."
Mama Tina alijikusanyakusanya kwa kuvaa haraka na kutoka, uso umechoka, macho mekundu ile mbaya. Alikutana uso kwa uso na Halima pembeni yake akiwa yule mpangaji mwingine…

"Nilikuwa naongea na huyu kaka mgeni," alisema mama Tina huku akiwa anajibalaguza kiaina. Aibu ilimkaa. Alitamani siku hiyo iwe haijafika.
"Mama," Tina alisimama akilia na kumfuata mama yake hadi miguuni na kumshika.
"Twende ndani mwanangu."

Halima aliingia ndani kwake, akachukua kama dakika tatu tu kisha akatoka nje. Mama Tina aliamini anaondoka zake baada ya kuiona bodaboda kwa kutumia dirisha lake la sebuleni.
Lakini mpaka dakika kumi zinakatika hakusikia mlio wa bodaboda ikilia kuondoka, akatoka. Akamkuta dereva wa bodaboda amesimama upenuni mwa nyumba, Halima hayupo.

"Yuko wapi huyu msichana?" alimuuliza dereva.
"Ameingia nyumba ile pale."
Mama Tina alishtuka sana kwani nyumba aliyoambiwa ameingia Halima ni ya yule mwanamke aliyemuuliza yeye mama Tina kwamba amesikia anatembea na kijana mpangaji mgeni, akakataa.
 
KITANDA CHA MPANGAJI MWENZANGU - 8

ILIPOISHIA
"Yuko wapi huyu msichana?" alimuuliza dereva.
"Ameingia nyumba ile pale."

Mama Tina alishtuka sana kwani nyumba aliyoambiwa ameingia Halima ni ya yule mwanamke aliyemuuliza yeye mama Tina kwamba amesikia anatembea na kijana mpangaji mgeni, akakataa.
TANUA NAYO…

"Mh!" aliguna mama Tina.
Akiwa ameduwaa nje, mara Halima alitoka akiwa anasindikizwa na mwanamke huyo. Walipokutana macho, mama Tina alishtuka sana…

"Mama Tina hujambo?" yule mwanamke alimsalimia.
"Sijambo za leo?"
"Salama, hawajambo wengine humo ndani kwako?"

Salamu hiyo ilimshtua sana mama Tina, kabla hajamjibu ikawa inajirudia kichwani mwake…
"Salama, hawajambo wengine humo ndani kwako?"
"Hatujambo, Tina hajambo yupo ndani," mama Tina aliiua salamu ya mwanamke huyo kwa staili hiyo.

"Na mpangaji wenu mgeni naye hajambo jamani?" yule mwanamke alisema akiachia tabasamu la msuto kwa mama Tina. Halima naye alicheka akimwangalia mama Tina kwa macho ya kumsuta au kugundua kile alichokifanya chumbani kwa kijana mpangaji mgeni.

"Mh! Na wewe mama nanihii bwana, una maneno mengi," alijibalaguza mama Tina lakini uso wake ulionesha kukasirika kiaina.
Halima alipanda bodaboda na kuondoka huku akimwacha mama Tina bado amesimama nje kwa aibu. Yule mama jirani alishaingia ndani kwake.

Mama Tina baadaye sana aliingia ndani, akapitiliza hadi chumbani kwa Os Anjelus…
"Kimenuka. Huyu malaya amekwenda kumwambia mwanamke mmoja jirani," alisema mama Tina akiwa amesimama.

"Da! Kwa hiyo?" Os Anjelus aliuliza.
"Hata sijui. Ila nitajua cha kufanya. Lakini siwezi kuondoka bila kukupiga busu japo moja tu…mwaaa. Lakini umenifurahisha hata kama tuliingiliwa," alisema mama Tina na kutoka.

***
Usiku wa saa tano, Halima alirejea nyumbani hapo na kukuta nyumba yote kimya! Wapangaji wengine walishalala.
Aliingia ndani kwake, akaweka mkoba na kubadili nguo kwa kuvua alizovaa na kujitupia kanga moja tu iliyokatisha kifuani kwa kuziba nido tu.

apo kwa ndani hata ‘kufuli' hakuwa nayo.
Alifungua mlango akatoka, akaenda kusimama mlangoni kwa Os Anjelus. Alikuwa akiwaza amgongee au la! Aliamini akigonga, wengine watasikia.

Katika kufikiria huko alijikuta akishika kitasa cha mlango, akakizungusha, mlango ukafunguka. Kumbe haukufungwa kwa funguo.
Bila woga, Halima alizama ndani kama mwizi huku akimtupia macho kijana huyo aliyekuwa akiuchapa usingizi.

"Huenda walikubaliana na mama Tina mlango uwe wazi ili aingie muda huu," aliwaza moyoni Halima huku akiwa amesimama mbele ya kijana huyo bila woga wala kujifikiria itakuwaje endapo ataamka.
"We kaka wa Kingoni…we kaka wa Kingoni," alisema Halima akimwamsha mpangaji huyo kwa kumtingisha.

Os alishtuka na kujikuta ana mgeni bila kumtegemea…
"Vipi, mbona ulilala mlango wazi?"
"Khaa! Nilifunga anti, ila sikufunga kwa funguo nilijisahau."
"Mimi nimeukuta upo wazi kabisa, nikahisi wezi wameingia."

"Mh! Kweli?"
Os alifikiri na kuhisi kwamba mama Tina aliingia akamkuta amelala, wakati wa kuondoka akasahau kuurudishia.

"Uwe makini anko, utakuja kuibiwa siku moja," alisema Halima huku akikaa kitandani.
"Vipi, siwezi kulala na wewe kwa usiku wa leo kaka ‘angu?"
"Sasa sista umeshasema kaka‘ako kuna sababu gani ya kulala na mimi?"
"Haya, tufanye si kaka ni watu tu."

"Mh! Ungekwenda kulala kwako tu."
"Hamna bwana, mwenzio najisikia," alisema Halima akimshika kijana huyo na kumvutia kwake.
"Halima unatangaza kwa watu mimi nalala na huyo kijana mbona na wewe upo kwake tena usiku huu?" sauti ya mama Tina ilisema mlango ukiwa wazi.

Wote walishtuka mle chumbani, mama Tina akaganga. Halafu alivyo jasiri akapenyeza mkono na kuwasha taa ya ukutani, tap! Kukawa na mwanga.
 
KITANDA CHA MPANGAJI MWENZANGU - 9

ILIPOISHIA
"Hamna bwana, mwenzio najisikia," alisema Halima akimshikashika kijana huyo na kumvutia kwake.
"Halima unatangaza kwa watu mimi nalala na huyo kijana mbona na wewe upo kwake tena usiku huu?" sauti ya mama Tina ilisema mlango ukiwa wazi.

Wote walishtuka mle chumbani, mama Tina alisimama. Halafu alivyo jasiri alipenyeza mkono wake na kuwasha taa ya ukutani, tap! Kukawa na mwanga mkubwa.
ENDELEA SASA… "

Mi nimekuja tu mara moja," alijitetea Halima…
"Ungekuja mara moja kungekuwa na giza?"
"Hatukutaka kuwasha taa."

"Mmmh! Jamani, muwe wakweli, siyo mnawasingizia wenzenu kumbe na nyie ni mulemule," alisema mama Tina akiondoka kwa hasira.
Hasira zake zilikuwa mara mbili, kwanza Os Anjelus ni ‘mtu' wake, pili Halima ameingilia penzi lake, aliumia sana, basi tu.

Hakwenda chooni, alirudi chumbani kulala huku akiwa anasonya kila wakati…
"Vipi, una nini?" mume wake alimuuliza baada ya kushtuliwa na sonyasonya nyingi.
"Si hao wapangaji, sijui nani kaingia chooni wala hajamwaga maji!"

"Atakuwa nani, labda huyo mpangaji mgeni, maana hiyo tabia sijawahi kuiona wala kuisikia."
"Mm! Yule wala, sidhani kama anaweza kuwa na ustaarabu sifuri kama huo."
"Atakuwa yeye tu, mbona unamtetea au unamjua aliyefanya hivyo?"
"Mimi simjui mume wangu na wala simtetei, ila nasema haoneshi kama ana ustaarabu mbovu kama huo."

Walilala baada ya mazungumzo hayo.
***
Halima aliamka kwake baada ya kutoka kwa Os Anjelus usiku ule hata bila ya kucheza mechi, mama Tina alimtibulia ingawa pia haijulikani kama kijana huyo angemkubalia au la!
Alifikicha macho akiwa uani huku kaaibu kwa mbali kakimtawala usoni.

Mama Tina alichomoka kwake na kutokea uani, hakumsalimia Halima licha ya kwamba alimkuta…
"Za asubuhi mama Tina?"
Kimya…
"Mama Tina nakusalimia."

"Kwani lazima kuitika salamu yako Halima?"
"Khaa! Mke wangu kwani kuna nini? Mtu anakusalimia unasema kwani lazima? Mna ugomvi? Eti Halima kuna ugomvi?"

"Hatuna ugomvi," alijibu kwa haraka mama Tina. Aliamini kwamba kama angechelewa kusema lolote, Halima angeweza kufichua yaliyofichika ambapo yeye asingetaka mambo yafikie huko…

"Sasa kwa nini unakataa salamu yake? Eti Halima kuna ugomvi?" baba Tina alirudia tena kumuuliza Halima maana awali alimuuliza akajibu mke wake…

"Muulize mkeo, si anajua mimi niko singo sijaolewa, yeye kaolewa, muulize sasa," alisema Halima kauli iliyojaa utata wa kutosha kumfanya baba Tina ahisi kuna jambo hasa kwa kauli hii…
"…si anajua mimi niko singo sijaolewa, yeye kaolewa…"
"Mama Tina kuna nini?"

"Hakuna kitu mume wangu, amesema tu. Salama Halima mdogo wangu jamani, umeamkaje?"
"Mimi sijambo."

Baba Tina ambaye alikuwa akienda kazini alifungua mlango mkubwa na kutoka, lakini akili ikakumbuka mazungumzo yake na mkewe usiku uliotangulia kuhusu chooni…
"Si hao wapangaji, sijui nani kaingia chooni wala hajamwaga maji!"

"Atakuwa nani, labda huyo mpangaji mgeni, maana hiyo tabia sijawahi kuiona wala kuisikia."
"Mm! Yule wala, sidhani kama anaweza kuwa na ustaarabu sifuri kama huo."
"Atakuwa yeye tu, mbona unamtetea au unamjua aliyefanya hivyo?"
"Mimi simjui mume wangu na wala simtetei, ila nasema haoneshi kama ana ustaarabu mbovu kama huo."

"Hili suala la leo asubuhi lina jambo zito ndani yake, Halima na mke wangu sijawahi hata kuwasikia wako kwenye mgogoro wowote, ni nini kipya kimetokea?

"Halafu kwa nini Halima amekimbilia mambo ya kuolewa na kutoolewa, ina maana msingi wa mzozo wao ni huo?" alijiuliza mwanaume huyo hata alipokuwa amefika kazini…

"Lazima nianze ufuatiliaji, hapa penye ndoa na usingo pana kitu, mimi ni mtu mzima na ule ni ujumbe nilipewa kwa akili," alisema moyoni baba Tina.
Akiwa katika harakati za kazi, simu ya baba Tina iliita, namba ngeni…
"Halooo," alipokea baba Tina.
"Halo, wewe ni baba Tina?"
 
KITANDA CHA MPANGAJI MWENZANGU- 10

ILIPOISHIA
"Bee!"
"Hebu njoo mara moja."
Halima alitoka akiwa anajifunga kanga vizuri, akasimama kumsikiliza mama Tina…
"Ulisema hospitali anaumwa nani?"
"Mjomba angu. Kwani vipi?"
"Una uhakika Halima?" Endeleaa......

"Khaa! Nitashindwaje kuwa na uhakika wakati anayeumwa ni mjomba?"
"Mbona kuna mtu kaniambia baba Tina amelazwa hapohapo Palestina, ana presha?"
"Mimi sijamwona baba Tina."
"Mh! Haya poa."
"Poa ndiyo."

Mama Tina aliingia ndani, akajikusanya na kukimbilia hospitali ambapo kweli alimkuta mumewe amelazwa.
"Mwenzetu imekuwaje tena?" alimuuliza mumewe kwa sauti ya upole.
"Presha ilipanda."
"Kisa nini?"

"Sijui."
"Sasa mbona hukuniambia?"
"Sikuwa na uwezo hata wa kuongea."
"Umeletwa na nani?"

"Wafanyakazi wenzangu."
"Kha! Sasa mimi kanipigia simu mama Kanisia, kasema amekuona lakini we hujamuona."
"Ni kweli sijamuona."

Mama Tina akatupia macho chini akiamini anaweza kuona mabaki ya chakula, kweli akaona masalio ya mchuzi na ndizi…
"Sasa umekula nini?"
"Sijala kitu."
"Mh!" aliguna…

"Sasa nikakutengenezee chakula gani cha haraka?"
"Hapana, nimeshiba sana."
"Mh!"

Mama Tina alikuwa katika wakati wenye maswali mengi kuhusu mumewe na Halima…
"Eti kuna wodi nyingine ya wanaume hapa Palestina?" alimuuliza mumewe.
"Sina uhakika."

Alisimama na kutoka nje. Akakutana na muuguzi mmoja…
"Samahani sana, eti kuna wodi nyingine ya wanaume hapa Muhimbili?"
"Ile pale, nyingine ingia kwenye mlango ule, ukaulizie."

Mama Tina alikwenda kote, akawaangalia wagonjwa wanaume na kila mmoja alimuuliza tatizo lake. Hakuna aliyesema ana presha ya kupanda wala kushuka.
Akaenda mapokezi…

"Samahanini jamani, eti kuna mgonjwa kaletwa hapa kwa tatizo la presha?" alimuuliza mtu wa mapokezi.
"Nenda kwa daktari wa zamu."
Mama Tina akaenda kwa daktari wa zamu…
"Samahani dokta, kuna mgonjwa wa presha ameletwa leo?"
"Yeah! Yupo mmoja."

"Siyo wawili?"
"Hapana. Kwa nini unataka wawe wawili?"
"Nina sababu zangu."
"Kama zipi?"

"Aaa! Kuna mtu kaniambia kaja kumwangalia mjomba ‘ake ana presha lakini nahisi alikuja kumwangalia mume wangu maana ndiyo mwenye presha, kuna kitu nimekitilia shaka."
"Huyo mtu ni mwanamke?"
"Ndiyo."

"Ni jirani yako?"
"Tunakaa nyumba moja."
"Sasa mtu mkikaa naye nyumba moja ni tatizo kuja kumjulia hali mume wako? Au kwa sababu ni mwanamke?"

"Dokta haiko hivyo unavyofikiri wewe."
"Basi kumbe mna mambo yenu. Hapa mwanaume mwenye presha ni mmoja tu. Aliletwa na wafanyakazi wenzake."

Mama Tina hakukubali, akatoka nje na kumpigia simu Halima...
"Eti huyo mjomba ‘ako amelazwa wodi gani na anaitwa nani? Nataka kumpa pole maana nimekuja kumwangalia baba Tina."

Itaendelea hapa hapa baada ya muda mfupi
 
Back
Top Bottom