Kitabu moto chenye simulizi za ukweli: Mateka mpakani

Kitabu moto chenye simulizi za ukweli: Mateka mpakani

macho_mdiliko

Platinum Member
Joined
Mar 10, 2008
Posts
29,223
Reaction score
60,290
Wakuu habari. Kwa wale wenye hamu ya kuelewa kwa undani vita vya Tanzania na Uganda basi kaeni mkao wa kula. Kachero wa Tanzania aliyetekwa na askari wa Uganda akiwa yeye na wenzake wawili (ambao waliuawa na yeye kunusurika kimiujiza) ameamua kuweka yote hadharani. Amesimuliwa yote kuanzia walivyotekwa, mateso waliopitia, wenzake walivyouawa na yeye alivyotoroka. Ni kitabu ambacho ukinza kukisoma hutakiweka chini. Japokuwa bado hakijachapishwa lakini simulizi zake za mwamnzoni kama zilivyochapishwa na gazeti la Raia Mwema zimewakuna wengi: Hii hapa sehemu ya mfululizo wa simulizi zake.

Kitabu cha ukachero wa kachero wa Tanzania – 2

………………………….

WIKI iliyopita tulianza kuchapisha sehemu ya kwanza ya uchambuzi wa kitabu kipya “Mateka Mpakani” kilichoandikwa na kachero wa Tanzania, Frowin Kagauka, kumuenzi mwenzake aliyeuawa mpakani mwa Tanzania na Uganda. Leo tunaendelea na sehemu ya pili.

…………………….

“AMESEMAJE wakati mlipomuuliza juu ya bastola hiyo? Amekubali ni yake lakini amekataa katakata kuwa yeye ni askari wa Idi Amin,” alinijibu Sajin Mkuu wa Kituo.

“OK. Sajin Binda wajulishe Bukoba ili waje kumhoji.” Niliamuru haraka. Sajini Binda alinipigia saluti nami nikaijibu kwa kubana mikono kwa vile sikuvaa sare za kijeshi na baadaye akaondoka haraka.

“Msimtoe humu mahabusu mpaka wakubwa zangu wafike kutoka Bukoba, sawa?” niliagiza. “Sawa afande,” alijibu Sajini ambaye ndiye mkuu wa kituo hicho kidogo cha polisi hapo kijijini Murongo.

Niliondoka hapo kituoni na ilipofika saa sita na nusu mchana nikijua wakubwa zangu watakuwa wanakaribia kufika hapo kituo cha polisi lakini hawakutokea mpaka saa nane na dakika kumi. Walifika kwa gari aina ya Landrover na wote walivalia sare za kijeshi isipokuwa dereva na mtu mwingine mmoja ndiyo walivaa kiraia.

Hao watatu waliovaa kijeshi mmoja alikuwa luteni na wawili makapteni. Waliovaa kiraia niliambiwa ni Luteni Emir wa Idara ya Usalama wa Jeshi ambaye ndiye aliyeendesha gari hiyo na Meja Stephen kutoka Idara ya Usalama wa Taifa mkoani Kagera. Wakuu hao waliamuru Kafumba atolewe mahabusu na alipotolewa wakamchukua na bastola yake kwenda naye Bukoba.

Sikumuona rafiki yangu Kafumba kwa zaidi ya wiki mbili ndipo siku moja bila ya kutarajia nikakutana naye sokoni hapo Murongo akizungumza na yule mpenzi wake.

“Ah! Rafiki wewe ni mbaya, umenipeleka polisi ili nifungwe bila kosa,” alilalamika. “Siyo hivyo, mimi nilishangaa kuona rafiki tangu una bastola na wewe ni bwana shamba. Naogopa sana askari ndiyo niliipeleka bastola yako polisi. Sasa wamekwambiaje?”

“Walinipeleka Bukoba nikaingizwa kwenye nyumba moja sijui ya nani, nikaulizwa maswali mengi ya Uganda na watu wawili ambao hawakuvaa kiaskari. Lakini watu wale walikuwa wema sana hawakunipiga wala kunisumbua na waliporidhika waliniachia nirudi lakini bastola yangu wamebaki nayo,” alinieleza huku akinikazia macho.

“Sawa bwana, basi tutaonana siku nyingine au leo kama bado upo hapa kwetu” nilimjibu kwa unyonge baada ya kuhisi yeye ni jasusi wa Idi Amin na ameweza kuwahadaa wakubwa zangu hadi wakaridhika kumuachia.

Wiki moja baadaye nikaletewa mwaliko kutoka kwa mzee niliyekuwa namheshimu sana, mzee Idris wa Green Hotel nikahudhurie sherehe yake aliyopanga ifanyike Jumamosi kuanzia saa tano asubuhi hapo hapo Green Hotel. Nikamjulisha Koplo Sudi na Sajin Binda juu ya mwaliko huo, kwa hiyo tukaondoka Murongo hadi Kivukoni. Tulipofika Kivukoni kama kawaida tukapanda boti na kuvuka mto Kagera ambao maji yake yanakwenda kasi sana kiasi cha kuwafanya wenyeji kushindwa kuvuka kwa kuogolea.

Baada ya boti kutuvusha tukatembea kwa miguu kilomita mbili na nusu hivi tukafika kijiji cha Kikagati ambacho kwa kweli ni kizuri kidogo kuliko kijiji chetu cha Murongo. Hapo Kikagati kuna kituo kidogo cha polisi ambacho kimejengewa badi tupu chini hadi juu, wengine huita mtindo huo ‘full suit’, vile vile kuna nyumba ya mkuu wa wilaya ambaye wenyewe walimwita DC na jengo moja kubwa la kampuni ya uchimbaji madini inayoitwa BMC.

Ilipotimia saa tano na dakika tano tulikwenda hapo Green Hotel huku tukiwa tumejaa shauku ya kunywa bia na kuvunja mifupa ya nyama ya kuku na mbuzi ya kuchoma. Kwa mshangao hapo Green Hotel hatukuona dalili yoyote ya sherehe na wala hakukuwa an watu wanaokula au kunywa kama ilivyokuwa kawaida. Kkilichonishangaza zaidi ni kutowaona hata watoto wake wakicheza nje ya hoteli hiyo ambayo mwenyewe mzee Idris anaishi humo humo kwenye vyumba vya uwani.

Kabla hajaamua kuuliza alifika mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa kati ya miaka sita na nane ambaye alituambia ameagizwa na mzee Idris atukaribishe ndani tumsubiri. Bila ya hofu tuliongozana na kijana huyo hadi kwenye sebule yam zee Idris ambayo kwa kweli hata siku moja hakuwahi kunikaribisha. Mtoto huyo alitutolea bia tatu za baridi kutoka kwenye hokofu, akatuwekea glasi kisha akaondoka. Dakika kama tano baadaye mzee Idris alifika na kutusalimu lakini hakukaa alituambia ana shughuli itakayochukua kama robo saa hivi lakini alitupa uhuru wa kujichukulia vinywaji kwenye jokofu. Wakati tunaanza kunywa bia huku bado nikitafakari jinsi ya sherehe hiyo tuliyoitiwa ilivyo, ghafla tukasikia mlio wa gari kubwa likisimama nje ya nyumba hiyo, bila shaka wote tulielewa huo ulikuwa ni mlio wa gari la kijeshi maana tulitazamana kwa mshangao.

Kabla hatujahamaki nini kinafanyika tukasikia vishindo vya hatua nzito za viatu vya kijeshi vikiizunguka hoteli hiyo. Tulipotazamana tena bila ya kusema lolote mlango ulifunguliwa na askari sita waliovalia kivita wakiwa na bunduki aina ya AK47 kila mmoja, wakatuzunguka. Moyo ulinilipuka, mate yakanikauka kinywani, bia yote niliiona chungu na balaa tupu.

“Simama juu.” Aliamuru mmoja wa askari hao ambaye alikuwa na cheo cha Sajini. Wote tulisimama huku mikono yetu ikiwa juu kuomba amani. “Songa mbele haraka.” Aliamuru tena. Tulitoka nje ambako tulikuta askari wengine wanane waliovalia kivita wakiwa na bunduki mikononii wameizunguka hoteli hiyo. Raia wa kijiji hicho au niseme kimji hicho walisimama kwa mbali sana wakishuhudia tunavyokuwa MATEKA MPAKANI.

Tuliingizwa katika lori moja la kijeshi aina ya Liaz na safari ya kwenda tusikokujua ikaanza. Tulipofika njia panda ya kwenda Kabale ambayo ipo upande wa kushoto na Mbarara ambayo ipo upande wa kulia, lori hilo lilitimua vumbi kuelekea kushoto yaani Kabale.

Baada ya mwendo wa kama kilomita nne hivi kutoka hapo Kikagati tukaingia katika kambi ndogo ya jeshi inayoitwa Kabiyanda. Tuliteremshwa katika kambi hiyo ndogo na kuingizwa katika kijumba cha mabati matupu ambapo ndani hakukuwa na lolote mbali ya joto na hewa nzito kwa vile hakukuwa na dirisha bali vitundu vidogo vipatavyo sita tu.

“Tunakuwa mateka mpakani, sijui watatufanyaje. Nahisi hizi ni njama za Kafumba, Kafumba lazima ni jasusi, alikuwa anatupeleleza. Sijui Idi Amini ana nia gani na sisi au nchi yetu…niliwaeleza wenzangu huku nikitetemeka. “Ni dhahiri Kafumba amelipiza kisasi. Lakini nahisi mpango huu ulikuwa ni wa muda mrefu,” alijibu Koplo Sudi.

Saa tisa tulitolewa humo kwenye kijumba na kukalishwa chini kwenye uwanja niliohisi ni wa kufanyia kwata. Koplo Sudi na Sajini Binda walikuwa wananitazama mara kwa mara kama vile wananiulaumu kwa kuwaingiza katika janga hili, lakini sio kosa langu bali ni tamaa yetu ya kunywa bia na kumuheshimu mzee Idris.

“Nani mkubwa kati yenu?” aliuliza Luteni mmoja mweusi mwenye sura mbaya. Hakuna aliyejibu hivyo akaona tumemdharau kaamua kumwita koplo mmoja aliyekuwa amesimama kwa mbali akituangalia.

“Funsa adabu hawa” alimwamuru koplo huyo aliyevalia kivita kwa Kiswahili kibaya kisha akaondoka zake kwa hasira.

“Ah! Mnataka ‘kufunswa’ heshima, hebu simameni.” Tuliinuka kwa hofu huku tukimwangalia nini anachodhamiria kutufanyia. “Nyinyi ni askari?” “Hakuna askari hapa kati yetu” nilimjibu haraka kwa hasira. “Eh! Wewe ndiyo mkubwa enh!” “Mkubwa wa nini?” nilimjibu na kumfanya acheke kidogo.

“O.K nyinyi mnajua Kiswahili kingi sana, hebu chuchumaeni chini huku mkishika masikio yenu.” “Tuonyeshe mfano,” nilimwambia bila hofu.

“Eh! Nyinyi jeuri sana, hebu laleni chini kifudifudi niwachape kidogo fimbo,” alitamka huku akitabasamu. Wakati tunalala kifudifudi ghafla alikuja askari mmoja asiye na cheo na kumwambia mwenzake kwamba tunatakiwa tuingie ndani ya gari tupelekwe katika kambi ya Mbarara. Tuliingizwa ndani ya Landrover moja ya jeshi la Idi Amin huku tukilindwa na askari sita waliovalia kivita wakiwa na bunduki aian ya AK 47 mikononi. Landrover ikapigwa moto na safari ya Mbarara ikaanza. Ilibidi turudi tena mpakani Kikagati kisha tufuate barabara inayoelekea Mbarara ni kama kilomita 150. Tulipofika Mbarara giza lilikuwa limekwishaingia, dereva akasimamisha gari nje ya lango kuu la kambi kubwa ya jehsi ambayo baadaye niliitambua inaitwa Simba Battalion. Taa kubwa ya usalama ikawashwa na kuzimwa kama ilivyo kawaida katika kambi nyingi za jeshi kisha sauti kali ilitaka utambulisho.

“Tumeleta mateka kutoka Kabale” alijibu askari mmoja aliyekaa mbele. Taa iliwashwa tena na kuzimwa halafu mlango ukafunguliwa. Niliona sanamu mbili za samba zilizokuwa upande wa kulia na kushoto mwa lango hilo ambazo zilinifanya nielewe maana ya kambi hiyo kuitwa Simba. Gari iliingia na kuegeshwa nje ya jengo dogo ambalo hata mtu asiyekuwa askari angegundua ni mahabusu.

Tuliamriwa kuteremka na mlango wa mahabusu ukafunguliwa, tukaingizwa. Mahabusu hiyo ilikuwa karibu na lundo la kuni na kwa mbele kidogo kulikuwa na msikiti mdogo. Ndani ya mahabusu hiyo hakukuwa na taa kwa hiyo ilibidi tutulie kimya bila kuongea wala kutembea.

Ulikuwa usiku mgumu sana kwetu hasa kwa mimi kiongozi kwa vile wenzangu walionyesha wamekata tamaa kabisa. Kama kawaida ya usiku ni lazima uche hata kama unapata taabu au raha ni lazima asubuhi ifike. Asubuhi ilipofika tulitolewa nje na kupelekwa katika ukumbi mmoja mdogo ambapo tulikalishwa chini. Dakika kama kumi baadaye waliingia wanajeshi wanne, watatu wakiwa na cheo cha meja na mmoja alikuwa kanali. Kwa jinsi walivyoonekana, walikuja kutuhoji.

“O.K Watanzania, tunaanza na wewe, inuka ujibu maswali yetu.” Alitamka kanali huyo huku akimuonyesha kidole Koplo Sudi. Koplo Sudi aliinuka wima huku akigwaya. “Unacho kitambulisho chochote hapo ulipo?” aliuliza meja mmoja ambaye ni mrefu zaidi ya wenzake. “Sina kitambulisho.” “Sawa, vua shati na suruali yako,” aliamuru kanali huyo.

Koplo Sudi akavua suruali na shati lake na kuviweka mbele yake. “Wewe unafanya kazi gani pale Murongo?” aliuliza meja mwingine ambaye ndiye aliyekuwa akinukuu maelezo yetu.

“Nafanya biashara ya kuuza vitabu sokoni,” alijibu Koplo Sudi huku akigwaya.

Ukisema kweli utapona, lakini ukitudanganya ujue hutaiona tena Murongo,” alitamka kanali huyo kwa Kiswahili kizuri. “Kwani sisi tumewakosea nini? Kosa letu ni nini mpaka mnataka kutuhukumu?” “Hamjafanya kosa lolote, lakini tunataka majibu y kweli,” alisisitiza kanali huyo.

“Unajua sisi tunawaelewa nyinyi vizuri sana, na kuonya tena. Usiseme uongo” alifoka kanali. “Sisemi uongo,” alisisitiza Koplo Sudi. “Jina lako nani?” aliuliza kanali huyo mweusi tii. “Abdallah Salum,” alidanganya. “Hatuna jina la Abdallah katika orodha tuliyoletewa.” “Kama mnayo orodha ya majina yetu kwa nini mnaniuliza jina?”

“Nyinyi wote ni wanajeshi, hiyo tunajua kwa hakika, sasa wewe unajifanya mfanyabiashara. Nakwambia mara ya mwisho, sema ukweli wako vinginevyo huwezi kurudi kwenu. Hatupo hapa kufanya mchezo,” alifoka kanali huyo.

“Umeelewa sasa, yajibu maswali yetu kwa ukweli” aliongeza meja anayeandika.

“Jina lako nani na unafanya kazi gani pale Murongo?” aliuliza meja huyo. Swali hilo lilimfanya Koplo Sudi aanze kutoa mchozi ambao uliniumiza sana moyo.

“Unalia kabla hujateswa, sasa ukiteswa si utakufa kabisa” alitamba meja. Maneno hayo hayakupunguza kasi ya machozi ya Koplo Sudi, kwa hiyo kanali akamwambia arudi aka echini.

“Zamu yako wewe, inuka kuja hapa” alitamka kanali huku akinielekezea kidole. Niliinuka nikapiga hatua tatu na kusimama. “Wewe ujibu maswali yetu kwa ukweli, hatutaki uwongo wala kilio hapa.”

“Sawa,” nilijibu kisha nikakohoa kidogo ili kusafisha koo. “Jina lako nani,” aliuliza kanali. “Nelson,” nilijibu. “Jina lako lingine” “Njata, Nelson Njata. “Yah! Jina la Njata lipo hapa” alidakia meja aliyekuwa anaandika. “Unafanya kazi gani pale Murongo?” aliuliza kanali. “Mimi ni bwana shamba.”

“Tunajua ni bwana shamba, lakini una kazi nyingine pale?” alidakia meja mwingine. “Kazi gani nyingine?” niliwauliza bila wasiwasi. “Unamjua Dan Kafumba?” aliuliza kanali na kunifanya nishtuke. “Namjua ni Mganda na pia ni rafiki yangu.” “Nani alimfikisha polisi?” aliuliza kanali huku akinikazia macho.

“Alijipeleka mwenyewe baada ya kupoteza bastola yake.” “Unaonyesha wewe ni mtu jasiri na mjuba, bila shaka wewe ni mwanajeshi, tena mwenye cheo kikubwa au sivyo? Alidakia meja anayeandika.

“Sivyo, mimi ni bwana shamba, hata Kafumba angekuwapo hapa angenisaidia kuwathibitishia.” “Pale Murongo kuna kituo chochote cha jeshi?” aliniuliza kanali. “Mimi sijui na wala sioni umuhimu wa kujua mambo ya jeshi.”

“Naona wewe nmi mwerevu sana kwa hiyo itabidi uhojiwe kwa nguvu, nenda ukakae,” alitamka kanali kwa ukali.

Nilirudi nyuma polepole na kukaa chini. Sasa ilifia zamu ya Sajini Binda kusimama, lakini maofisa hao walinong’ona kidogo kisha ghafla waliinuka na kuondoka zao. Kwa jinsi walivyoonekana walivyokuwa, kwa vyovyote ni maofisa wa Idara ya Ujasusi wa Kijeshi au ni maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa. Kama nusu saa baada ya maofisa hao kuondoka mlango ulifunguliwa na askari mmoja asiye na cheo akiwa amebeba chano iliyokuwa na bakuli tatu zilizokuwa na uji, akatugawia kila mmoja bakuli lake, tukaanza kunywa huku akituangalia.

Uji huo wa unga wa mahindi ulikuwa wa moto sana na haukuwa na sukari, hata hivyo hiyo haikutuzuia kunywa kutokana na njaa tuliyokuwa nayo. Baada ya kama robo saa hivi tulishamaliza kunywa uji huo na askari huyo akachukua bakuli zake na kuondoka.

“Sijui wanataka nini kwetu?” aliuliza Koplo Sudi kwa unyonge. “Hii yote ni kazi ya yule rafiki yangu Kafumba ni lazima ni jasusi wa Idara ya Usalama wa Taifa ya nchi hii yaani State Research Bureau” lakini kwa vyovyote itakavyokuwa asitokee mtu kati yetu akavunja kiapo chetu” nilitamka huku nikiwakazia macho.

Wakati Koplo Sudi anavaa nguo zake alizokuwa amezivua, mlango ulifunguliwa na askari mmoja aliyekuwa na bunduki aina ya AK 47 mgongoni, akatuamuru tutoke nje. Tulipotoka nje tulikuta askari zaidi ya kumi wenye silaha wakitusubiri. Tulipekuliwa kama tuna silaha na walipoona hatuna walitunyang’anya saa zetu na viatu. Baadaye wakatuamuru tuingie katika lori moja aina ya Benz lililoegeshwa mita kama kumi kutoka hapo. Humo ndani ya lori tulifungwa kamba mikononi na miguuni na safari ya tusikokujua ikaanza lakini njiani askari mmoja aliripoka kwa mwenzake kwamba tutafika katika kambi ya Makindye saa kumi na mbili jioni.

Kambi ya Makindye niliwahi kuisikia kutokana na sifa zake za utesaji na uuaji na ni maalumu kwa kutesea mateka wa vita au askari waasi. Kambi hii niliambiwa ni ya Polisi jeshi tupu (Military Police).

Itaendelea wiki ijayo
 
Daaaah huyu jamaa mbona anapoteza uhondo tena khaaa
 
Kitabu cha ukachero wa kachero wa Tanzania – 3

KATIKA wiki mbili zilizopita tumechapisha sehemu mbili za uchambuzi wa wa kitabu kipya kinachoitwa MATEKA MPAKANI kilichoandikwa na kachero wa Tanzania, Frown Kageuka (pichani) kumuenzi mwenzake aliyeuawa mpakani mwa Tanzania na Uganda na majasusi wa aliyekuwa Rais wa Uganda, Idi Amin. Leo tunaendelea na sehemu ya tatu ya mfululizo wa uchambuzi wa kitabu hicho.

……………

TULIFIKA Makindye usiku, eneo hilo lilifanana sana na Manzese ya Dar es Salaam. Kwa hakika safari yetu ilikuwa ndefu sana kwa hiyo nilihisi tumeingia ndani sana ya nchi ya Uganda na labda tulikuwa karibu na Kampala.

Tuliteremshwa ‘kikuku’ na kuingizwa katika nyumba moja ambayo nilihisi ni mahabusu. Tuliachwa humo tukiwa bado na kamba miguuni na mikononi hadi alfajiri. Usiku wote hatukuweza kuongea lakini asubuhi nilijua tupo wote pamoja baada ya Koplo Sudi kumwambia Sajini Binda kwamba ana njaa sana. Kwa kweli hata mimi nilikuwa na njaa sana lakini hatukuwa na la kufanya. Jua lilipoanza kuonesha makali yake tulifunguliwa kamba tulizofungwa na askari mmoja mwenye cheo cha Sajin.

“Mnataka chai au uji? Aliuliza Sajini huyo ambaye alionyesha ni katili sana. “Chochote unachoona tunastahili,” nilijib kwa upole. “Mimi nawapa uchaguzi nyinyi wafungwa,” alijibu Sajin huyo na kuondoka.

Dakika kama tano hivi baadaye mlango ulifunguliwa na Sajini yule yule aliyekuwapo awali, akaingia ndani akifuatiwa na askari mmoja asiye na cheo ambaye amebeba birika na vikombe vitatu vya bati.

“Haya punguzeni njaa kwa mlo huu nyie wafungwa” alitamka Sajin huyo kwa kebehi huku mwenzake akiweka birika na vikombe karibu yetu na kuondoka.

“Kwani sisi ni wafungwa?” niliuliza kwa upole huku nikimkazia macho. “Eh! Kumbe nyinyi ni kina nani?” alijibu Sajenti huyo huku akinitolea macho. “Sisi sio wafungwa bwana. Tunashangaa jinsi mlivyotukamata na kutuleta hapa.” “Hayo mimi sijui, ninachokijua nyingi ni askati mateka kutoka Tanzania kwa hiyo ni wafungwa.”

“Sisi sio askari bwana, kama mmeambiwa hivyo mmedanganywa kabisa. Mmeshindwa kuwapata askari halisi mkatukamata sisi raia na kutuita askari. Huo ni uonevu mkubwa,” nilimwambia kwa upole.

“Nyinyi watu wa Tanzania Kiswahili kirefu sana, kama siyo askari mmmefikaje hapa Makindye?” aliuliza kwa mshangao huku akituthitibishia hapo tulipo ni Makindye.

“Lakini kama sisi ni wanajeshi kama mnavyotaka tuwe, basi inabidi mtupe huduma sawa na mkataba wa Geneva unaohusu wafungwa wa kivita.” “Wewe mbona unaongea sana? Au ndiyo mkubwa?” aliniuliza kwa ukali na kuondoka zake.

“Inaonyesha hawa wanampango mbaya na sisi, hapa walipotuleta ni ndani kabisa ya nchi yao, ni maili chache tu kufika mjini Kampala. Sijui kama tutarudi salama. Iddi Amin hajawahi kuachia mtu salama na hasa waliokamatwa kimya kimya kama sisi. Ni lazima tufanye kitu ili tujiokoe” niliwaeleza wenzangu kwa sauti ya chini lakini kabla hawajanijibu mlango ulifunguliwa. Askari mmoja aliyevalia rasmi kipolisi jeshi (Military Police) alituamuru tutoke nje haraka. Hapo nje tuliwakuta askari wengine sita waliokuwa na bunduki aina ya AK 47 kila mmoja.

Tulifungwa pingu mikononi na kuongozwa hadi kwenye uwanja ambao bila ya kuamiwa nilijua ni sehemu ya kuulia watu kwa kupigwa risasi. Tulifungwa katika miti iliyokuwa mbele ya magunia mengi ya mchanga ambayo nilijua ni maalumu kwa kuzuia risasi isiende mbali ya hapo.

Baada ya kufungwa kamba kuzunguka mti nilijiona nimeshakuwa mfu. Koplo Sudi na Sajini Binda walianza kulia kama watoto wadogo. Niliogopa sana hali hiyo, kwa vile nilijua Waganda hao watagundua mimi ni kiongozi wao kutokana na ujasiri wa kutoogopa kifo na pia hiyo ilinithibitishia kwamba wenzangu sasa watakuwa tayari kutoa siri zetu zote. Dakika kama mbili baadaye askari jeshi watatu walisimama hatua kama tano mbele yetu na kutulenga kwa bunduki zao.

Wakati nikianza kumuomba Mungu anisamehe makosa yangu niliyomkosea ili anipokee huko mbinguni, ghafla ilifika gari moja aina ya Jeep ikiwa na askari mmoja mwenye cheo cha kanali na mwingine aliyevaa Kaunda suti ya rangi ya kijivu ambaye nilimuhisi ni afisa wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Iddi Amin inayoitwa SRB. Maofisa hao waliteremka kwenye gari na kutusogelea.

“Naona nyinyi ni vijana wadogo sana, kwa hiyo najua hampendi kufa au siyo?” aliuliza kanali huyo huku akitukazia macho. Wote tulikaa kimya bila kutoa jibu lolote wala kukohoa.

“Nani mkubwa kati yenu kwa cheo? Aliuliza ofisa aliyevaa kiraia lakini naye hakupata jibu.

“Nataka kuwahakikishieni kitu kimoja, atakayekuwa mkweli hatutamuua na kwa kuwa tutamhoji kila mtu peke yake inabidi hapa tuwafunge mmoja mmoja. Mtu mjeuri hapa ndio utakuwa mwisho wake” alitamka kanali huyo kwa ukali. “O.K fungua hawa wawili abakie huyu,” aliamuru aliyevaa kiraia.

Mimi na Koplo Sudi tulifunguliwa na kurudishwa mahabusu, Sajini Binda tukamwacha akiwa bado amefungwa. “Hata kama ukisema ukweli haiwezi kuwazuia kutuua. Kumbuka kiapo chako usiwe mwoga.” Nilimkumbusha Koplo Sudi. “Lakini, lakini afande….” “Shii, kumbuka kiapo , usiwe mwoga, kama ni kifo acha tukikabili.” Nilisisitiza.

Kabla ya Koplo Sudi hajaendelea kutamka neno linguine tukasikia mlio wa risasi tatu ambazo zilitufanya tupate kiwewe cha ghafla.

“Wameshamuua, wameshamuua.” Alilalamika Koplo Sudi. Mimi sikumjibu lolote bali nilimkazia macho tu, alipoona hivyo aliinuka haraka alipokaa na kuniangukia miguuni kwangu huku akilia.

“Watatuua wote afande,” alilalamika. “Wacha tufe lakini kumbuka kiapo, usiwe mwoga,” nilimjibu huku na mimi nikitoa mchozi wa chuki.

“Nisaidie afande, naogopa sana.” Alizidi kulalamika. “Nyamaza!” nilimwamuru kwa ukali, akanyamaza. Punde kidogo mlango ulifunguliwa na polisi jeshi mmoja. “Nani ndiye Koplo Sudi?” aliuliza askari huyo akiwa amesimama mlangoni. Koplo Sudi hakujibu bali aliongeza kasi ya kulia na kumfanya askari huyo aje juu.

“Nauliza nani ndiye Koplo Sudi sitaki kusikia kilio.” Alifoka. “Ni mimi, ni mimi.” Hatimaye alijibu. “Kuja hapa haraka.” Aliamuru kwa ukali. Koplo Sudi aliinuka na kumfuata.

Alipotoka mlango ukafungwa, nikabaki ndani peke yangu. Sasa nikajua siri zimeanza kutoka, kama wamemjua Koplo Sudi bila shaka Sajini Binda amekwishawaeleza mengi. Hofu ikazidi kuniingia, nikajua sasa watanishughulikia mimi kikamilifu wapate siri. Niliwaza sana bila kupata jibu lolote, tama ya kujiokoa ikaanza kujengeka polepole akilini mwangu.

“Wakishajua mimi ndiye kiongozi hasira zao zote zitaniangukia mimi.” Nilijisemea peke yangu kama mwehu. Dakika kama ishiriki baadaye nikasikia mlio wa risasi mbili nikajua Koplo Sudi naye ameshauawa. Hofu ikanizidi, nikajua zamu yangu ya kutolewa roho imekaribia. Nilimkumbuka Mungu, nikamwomba aniokoe na kifo hicho, nikalia sana, lakini sikulia kwa hofu ya kifo bali nilimlilia Mungu aniepushie balaa hilo. Kilio change kilikatizwa ghafla na sauti ya polisi jeshi aliyekuwa mlangoni.

“Unalia huku umepiga magoti na mikono juu unamwomba Mungu eee! Alitamka askari huyo kunigutua. Haraka nilifuta machozi yangu, kwa kweli nilipata nguvu mpya, hofu ya kifo ilinitoka kabisa, nilihisi ni sababu ya kilio changu kwa Mungu.

“Wewe ndiyo Luteni, siyo?” aliniuliza huku akitabasamu. “Umetumwa unite au uniulize swali?” nilijibu kwa upole huku nikitabasamu.

“Haya unaitwa,” alitamka huku akiendelea kutabasamu. Niliinuka haraka tukaongozana hadi kule kwenye uwanja wa mauaji ambako nilipaita machinjioni. Nilipofika hapo nikafungwa kamba kama awali kisha askari wanne wenye silaha wakajipanga mbele yangu wakingoja amri ya kunifyatulia risasi. Baada ya kufungwa kamba nikaoiona tena ile gari aina ya Jeep ikija na baadaye ikasimama palepale iliposimama mwanzoni. Yule kanali na mwenzake aliyevaa kiraia ambaye nilimuhisi ni afisa usalama wa taifa kutoka SRB, walinisogelea tena kama walivyofanya mwanzoni. Muda wote huo nilikuwa naichunguza ile miti kuona kama ina damu ili nipate uhakika kama wenzangu kweli wameuawa.

Hata hivyo sikuona damu yoyote katika miti hiyo kwa hiyo nikahisi umetumika ujanja wa kututisha lakini kama wametumia mbinu hiyo basi wamesahau kupata miti hiyo japo rangi inayofanana na damu.

“Wewe ndiyo Luteni Njata au siyo?” aliniuliza huyo aliyevaa kiraia. “Unaniambia au unaniuliza?” nilimjibu bila hofu. “Wenzako wote wamekubali kushirikiana nasi na wamejibu vizuri lakini tumewaua kwa ujeuri wao.” Alieleza kanali huyo.

Maneno haya niliyatafakari na kugundua wenzangu hawajauawa bali wamenigeresha mimi kwa milio ya risasi tu. “Sasa jibu maswali yetu vizuri na kwa usahihi, udanganyifu wowote utakaofanya utasababisha uwafuate wenzako huko ahera, umenielewa?” alitamka.

“Nimekuelewa bwana.” Nilijibu kwa upole. “Wewe tumeambiwa ndiyo kiongozi wa wenzako na cheo chako ni luteni, kweli?”. “Kweli” nilijibu kwa upole huku nikimkazia macho. “Unaongoza askari wangapi pale Murongo?” ofisa aliyevaa kiraia aliniuliza.

“Nawaongoza hao hao wawili waliowaambia mimi ni kiongozi wao.” “Yaani wewe ni kiongozi wa askari wawili tu, kambi gani hiyo ya watu wawili?” aliuliza kanali. “Kwani wameaambia tupo wangapi?” “Ah? Yaani wewe badala ya kutujibu maswali yetu, unatuuliza sisi maswali tukujibu?” alifoka huyo aliyevaa kiraia.

“Siyo hivyo wakubwa, maswali yenu mengine najua majibu mnayo wenyewe, sasa mimi nashangaa mkiniuliza. Mnanichelewesha bure kunipiga risasi, niuweni roho zenu zitulie.” Nilijibu kwa utulivu mkubwa uliowafanya wanishangae. “Wewe huogopi kufa?” aliniuliza kanali huku akinikazia macho.

“Kila mtu atakufa hapa duniani hata kama utamtanguliza mwenzio kufa ujue iko siku na wewe utamfuata.” Nilijibu na kuwafanya wazidi kunishangaa. “O.k. sawa bwana, sasa pale Murongo kuna kambi ya jeshi?” aliuliza kanali. “Hakuna” nilijibu kwa mkato.

“Kumbe nyinyi ni askari mnaofanya nini pale kijijini?” alifoka aliyevaa kiraia. “Tunataka kufundisha askari raia yaani mgambo.” “Mmeshaanza kuwafundisha?” alizidi kuuliza. “Bado labda mwezi ujao tutaanza.” “Kitu gani kinachowafanya muanze kufundisha mwezi ujao?” ofisa huyo aliuliza. “Bado hatujakamilisha mipango ya kupata vifaa na watu wa kuwafundisha.” “Unaona unavyojibu vizuri? Wewe sasa utakuwa rafiki yetu hatuwezi kukuua.” Alitamka kanali huku akitabasamu.

“Pale Murongo kuna redio ya mawasiliano?” alizidi kuuliza ofisa huyo huku akiandika. “Ipo.” Nilijibu nikijua wenzangu wameshaeleza yote. “Ipo sehemu gani pale Murongo?” aliuliza kanali.

“Kwa kweli ni vigumu, labda twendeni nikawaonyeshe huko huko,” nilijibu kwa upole na kuwafanya wacheke sana. “Wewe mjanja sana, kweli wewe ni ofisa wa jeshi,” alisifu ofisa huyo aliyevaa kiraia.

“Hebu mfungueni kamba, huyu sasa ni rafiki yetu, ameonesha ushirikiano, tutawarudishia Murongo,” aliamuru kanali kisha wakaingia kwenye gari yao na kuondoka. Polisi jeshi mmoja alinifungua kamba na baadaye wakanirudisha mahabusu ambako niliwakuta Sajini Binda na Koplo Sudi wakinywa uji. Sikuwasemesha kitu nilikaa kwa huzuni huku nikiwakazia macho.

“Mmewaeleza mambo mengi sana mkifirikia ni njia ya kujinusuru katika mikono yao, siyo?” niliwauliza kwa upole lakini sikupata jibu. “Tuone sasa kama kweli wataturudisha Murongo baada ya kuwapa wanachokitaka,” nilizidi kueleza.

“Nani kati yenu aliulizwa juu ya masafa (frequency) ya redio yetu ya mawasiliano?” niliwauliza lakini hakuna aliyenijibu.

Hali hiyo ilinithibitishia kwamba wameeleza mambo mengi sana na sasa wanaona aibu hata kuongea na mimi. “Ndiyo maana hawakuniuliza maswali mengi kwa kuwa mengi wamekwishaelezwa na hawa.” Niliwaza.

Jioni ilipofika tulitolewa humo mahabusu tukiwa tumefungwa vitambaa vyeusi usoni na pingu mikononi, tukaingizwa ndani ya lori moja. Dakika chache baadaye lori hilo liliondoka kuelekea tusipopafahamu lakini tulitumia muda wa dakika kama ishirini au ishirini na tano hivi ndipo lori hilo liliposimama. Tuliteremshwa na kuongozwa hadi kwenye ngazi fulani ambako tuliteremka chini hadi kwenye chumba kimoja chenye hewa nzito na harufu mbaya ya mikojo na damu.

Humo tulifunguliwa vitambaa tulivyofungwa lakini ikawa sawa na tulivyofungwa kutokana na giza la humo ndani. Hali ya mahabusu ile ya Makindye ilikuwa ni afadhali kuliko hii inayotisha. Tulitulia kimya sakafuni bila kusemezana kitu kutokana na utisho wa humo ndani. Hata hivyo kwa kawaida maongezi yananoga unapoongea na mtu huku unamuona, sasa hii giza imevunja hata hamu ya kuongea.

Tulikaa humo ndani bila kufahamu kama ni jioni, usiku au asubuhi imefika. Kwa kadiri nilivyotafakari jinsi tulivyokamatwa na tulivyofanyiwa ni dhahifi kifo kilikuwa bado kinatuandama. Uchovu na njaa ndiyo vitu vya kwanza kutishia maisha yetu hasa mimi ambaye nilikuwa sijaonja kitu chochote kwa siku mbili. Wakati tukiwa bado hatujui la kufanya tulisikia sauti kutoka kwenye kipaza sauti kidogo kilichokuwa humo ndani.

“Luteni Njata na Sajini Binda kuja nje haraka.” Sauti hiyo iliamuru na wakati huo huo mlango mzito wa chuma ulijifungua tukaona mwanga kidogo mbele yetu. Mimi na Sajini Binda tuliinuka na kuuendea mlango huo lakini Koplo Sudi alimshika Sajini Binda huku akilia sana akimuomba asimuache. Nilishangaa sana kwa nini amshikilie Sajini binda badala ya mimi mkubwa wao. Hata hivyo baadaye nilihisi labda kwa vile mimi amekwishaniudhi kwa kusaliti kiapo cha jeshi letu. Sajini Binda alipoona Koplo Sudi hamuachi, akaamua kutoka naye. Tulitokea kwenye ukumbi mrefu ambako tuliwakuta vijana wawili waliovalia Kaunda suti zao maridadi wakitusibiri.

“Mmeitwa wawili mnakuja watatu, nyinyi watu vipi?” alifoka mmoja wao ambaye ni mfupi kidogo kuliko mwenzake. “Huyu mwenzetu anaogopa kubaki peke yake” alijibu Sajini Binda.

“O.K. njooni huku.” Alitamka huku akitangulia mbele. Kwa kweli humo ndani kulionesha wazi ni sehemu ya mauaji. Tuliongozana na maofisa hao katika ukumbi huo mrefu uliokuwa unawake taa hadi kwenye mlango mwingine wa chuma uliokuwa upande wa kushoto. Ofisa huyo aliugonga mlango huo kwa kutumia chuma cha kufungia nje na baada ya sekunde chache ukafunguliwa.

Bila kuongea na aliyeufungua mlango huo, akatuonyesha ishara tuingie ndani. Sajini Binda na Koplo Sudi walitangulia kuingia wakifuatiwa na mimi. Maofisa waliotuleta wakafunga mlango huo kwa nje na kuondoka zao. Humo ndani tulikuta ukumbi mrefu kidogo uliojaa harufu mbaya zaidi kuliko kule tulipowekwa mwanzo. Kulikuwa na nyororo nyingi zilizofungwa ukutani ambazo zilinijulisha ni za kufungia watu. Mbele kidogo ya ukumbi tulikuta watu wanne wamefungwa nyororo mikononi wakiwa wamesimama wima lakini vichwa vyao upande wa sura wameangushia vifuani mwao huku damu zikiwatoka mdomoni, puani na masikioni. Walionesha uhai umekwishawatoka. Kuona hivyo, Koplo Sudi alianza kutapika hatimaye akazirai.

Wakati tunamhudumia Koplo Sudi kwa kumpepea kwa mashati yetu tuliyoyavua, mlango uliokuwa juu ya ngazi mbele yetu ukafunguliwa. Wanaume sita vipande vya baba wakaingia na kusimama mbele yetu. Miamba hiyo ya watu ilikuwa vidari wazi na walivaa chupi tupu. Hakika unaweza kuzimia kabla hawajakugusa. Jinsi maumbile yao yalivyo na sura zao mbaya za kutisha ni dhahiri wamewekwa maalumu kwa ajili ya utesaji hadi kuua. Moyoni nilijua wazi tupo katika jengo maalumu la Idara ya Ujasusi ya Iddi Amin (SRB) la kuhojia watu. Tukaamriwa tuvue nguo zetu zote tubaki kama tulivyozaliwa. Baadaye watu hao wakaanza kutupiga mgongoni kwa kutumia waya fulani bila ya kutusemesha kitu. Ulikuwa ni muda wa adha kubwa ambayo tangu nizaliwe sijawahi kuipata. Koplo Sudi alizimia tena akifuatiwa na Sajini Binda lakini wauaji hao waliendelea kuwapiga hadi mimi nikaona niwaokoe.

Itaendelea Jumatano ijayo
 
Kitabu cha ukachero wa kachero wa Tanzania – 4

Siku ya hukumu yetu mbele ya majasusi wa Idi Amin’

KWA wiki ya tatu sasa tumekuwa tukiendelea kuchapisha mfululizo wa makala zinazotokana na rasimu ya kitabu cha Jasusi wa Tanzania anavyoeleza yaliyowasibu yeye na wenzake baada ya kutekwa na Majasusi wa Idara ya Ujasusi wa Idi Amin. Ili kufahamu zaidi endelea kusoma simulizi hizi ambazo zitapatikana katika kitabu kiitwacho Mateka Mpakani, kilichoandikwa na Frown Kagauka (pichani).

SAJINi Binda alipoona Koplo Sudi hamuachii, akaamua kutoka naye. Tulitokea kwenye ukumbi mrefu ambako tuliwakuta vijana wawili waliovalia Kaunda suti zao maridadi wakitusubiri.

“Mmeitwa wawili mnakuja watatu, nyinyi watu vipi?” alifoka mmoja wao ambaye ni mfupi kidogo kuliko mwenzake. “Huyu mwenzetu anaogopa kubaki peke yake,” alijibu Sajini Binda. “O.k njooni huku” alitamka huku akitangulia mbele. Kwa kweli humo ndani kulionesha wazi ni sehemu ya mauaji. Tuliongozana na maofisa hao katika ukumbi huo mrefu uliokuwa unawaka taa hadi kwenye mlango mwingine wa chuma uliokuwa upande wa kushoto. Ofisa huyo aliugonga mlango huo kwa kutumia chuma cha kufungia nje na baada ya sekunde chache ukafunguliwa.

Bila kuongea na aliyeufungua mlango huo, akatuonyesha ishara tuingine ndani. Sajini Binda na Koplo Sudi walitangulia kuingia wakifuatiwa na mimi. Maofisa waliotuleta wakafunga mlango huo kwa nje na kuondoka zao. Humo ndani tulikuta ukumbi mrefu kidogo uliojaa harufu mbaya zaidi kuliko kule tulipowekwa mwanzo. Kulikuwa na nyororo nyingi zilizofungwa ukutani ambazo zilinijulisha ni za kufungia watu. Mbele kidogo ya ukumbi tulikuta watu wanne wamefungwa nyororo mikononi wakiwa wamesimama wima lakini vichwa vyao upande wa sura wameangushia vifuani mwao huku damu zikiwatoka midomoni, puani na masikioni. Walionesha uhai umekwishawatoka. Kuona hivyo, Koplo Sudi alianza kutapika hatimaye akazirai.

Wakati tunamhudumia Koplo Sudi kwa kumpepea kwa mashati yetu tuliyoyavua, mlango uliokuwa juu ya ngazi mbele yetu ukafunguliwa. Wanaume sita vipande vya baba wakaingia na kusimama mbele yetu. Miamba hiyo ya watu ilikuwa vidari wazi na walivaa chupi tupu. Hakika unaweza kuzimia kabla hawajakugusa. Jinsi maumbile yao yalivyo na sura zao mbaya za kutisha dhahiri wamewekwa maalumu kwa ajili ya utesaji hadi kuua. Moyoni nilijua wazi tupo katika jengo maalumu la Idara ya Ujasusi ya Idi Amin (SRB) la kuhojia watu. Tukaamriwa tuvue nguo zetu zote tubaki kama tulivyozaliwa.

Baadaye watu hao wakaanza kutupiga mgongoni kwa kutumia waya fulani bila kutusemesha kitu. Ulikuwa ni muda wa adha kubwa ambayo tangu nizaliwe sijawahi kuipata. Koplo Sudi alizimia tena akifuatiwa na Sajini Binda lakini wauaji hao waliendelea kuwapiga hadi mimi nikaona niwaokoe.

“Ebu waacheni hao mimi ndiye mkubwa, nitawaeleza yote na kama kuteswa mimi ndiyo ninayestahili siyo hawa.” Nilitamka kwa taabu sana huku nikiona giza usoni.

“Usiposema utakuwa mwisho wako katika mto wa mamba,” alijibu mmoja wao. “Nitaeleza yote, kweli yote, mwiteni mkuu wa Idara ya SRB niongee naye,” nilitamka kisha fahamu zikanipotea.

Nilipozinduka nikajiona nipo sakafuni nimelala, nikainuka haraka na kuangaza macho huku na huku nikajiona bado tupo kwenye ukumbi huo huo wa kutisha. Sajini Binda na Koplo Sudi walikuwa wamelala mbele yangu huku damu zikiendelea kuwavuja mgongoni na mdomoni. Hata mimi pia nilikuwa natokwa damu kinywani na mgongoni ambako kulijaa mipasuko ya kuchapwa. Nilipoangaza kwenye mlango wa juu ya ngazi nikaona pamefungwa nikajua ile mipande ya watu imerudi ndani. Kabla sijawaza zaidi, mlango tulioingilia ulifunguliwa na kijana mmoja aliyevaa Kaunda suti ya rangi ya kijivu.

“Waamshe wenzako mje huku” alitamka kijana huyo ambaye alionyesha ni wa kabila la Kinubi ambalo limejaa katika Idara ya Usalama wa Taifa ya Idi Amin Dada. Niliinuka haraka na kuwaamsha wenzangu ambao walikuwa hoi kabisa. Mimi niliona ni nafuu tuondoke humo ndani ingawa sikujua ya huko tunakokwenda. Nilitumia karibu dakika kumi kuwazindua Sajini Binda na Koplo Sudi. Tulipojikongoja kwa maumivu makali huku tukiongozwa na kijana huyo hadi kwenye chumba kingine ambacho tuliambiwa tuvae nguo zilizomo. Kwa kweli hazikuwa nguo za kuvaa labda niite makoti ya kaki ambayo yalitusitiri kwa kuwa hatukuwa tumevaa nguo.

Baada ya kuvaa kaki hizo akatupeleka katika chumba kisafi kidogo ambamo kulikuwa na meza moja na viti vitatu. Ofisa huyo alituambia tukae sakafuni tusubiri kisha yeye akaondoka zake. Dakika kama tano hivi baadaye ofisa mwingine aliingia akatuangalia bila kutusemesha kitu kisha akaondoka zake.

Ndipo baadaye walipoingia watu wanne waliovalia Kaunda suti zao nzuri sana na walionesha dhahiri kuwa vyeo vyao ni vikubwa. Watatu walikaa kwenye viti na mmoja alibaki amesimama wima. “Nani kati yenu anayetaka kuongea na mkuu wa SRB?” aliuliza kijana aliyesimama kando ya hao walioketi vitini. “Ni mimi,” nilimjibu haraka.

“Sawa, mkuu wetu ni huyu nakaa katikati naitwa Kanali Farouk Minowa, kwa hiyo eleza yale nasema tamweleza,” alitamka kijana huyo aliyesimama ambaye alionesha dhahiri anafanya mazoezi ya judo au karate na weusi wake ulidhihirisha ni Mnubi. Nilimkazia macho huyo bosi wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Idi Amin nikaamini yale niliyoambiwa kwamba Idi Amin amegawa madaraka mengi kwa watu wa kabila la Wanubi na Wakakwa ambalo ni kabila lake. Huyo Kanali Farouk alionesha wazi ni Mnubi. “Sikiliza bwana mkubwa,” nilianza kumwambia huku nikiwa nimesimama. “Mimi na hawa wenzangu tulikamatwa pale mpakani katika kijiji cha Kikagati wakati tunakunywa pombe katika Green Hotel nashangaa tunaambiwa sisi ni askari wa Jeshi la Tanzania, naomba bwana mkubwa uingilie kati jambo hili. Fanya uchunguzi ili tusiteswe bure.” Nilimwambia kwa upole.

“Nyamaza, kaa chini haraka,” aliamuru kijana aliyesimama. “Wewe ulisema nahitaji bosi yetu ili umueleze upumbavu wako? Unafikiri tunafanya mchezo? Hujui kwamba tunazo habari zenu zote zilizo sahihi?” alifoka kijana huyo huku akinisogelea.

“Nilichosema mimi ndicho ninachojua ni sahihi, sasa iwapo nyinyi mnajua zaidi kuliko tunavyojijua sisi wenyewe tupo radhi kuwasikiliza nyinyi.” Nilimjibu kwa upole bila kuogopa weusi wake kama mkaa na macho yake mekundu kama damu.

“Yaani wewe kijana nasumbua sisi, tumeacha shughuli zetu muhimu kuja sikiliza wewe kumbe huna lolote la kutuelesa sasa hii ndiyo takuwa mahakama yenu. Hatutaki Kiswahili yenu murefu ya kuzungukazunguka. Anza mashitaka kapteni.” Alifoka mtu aliyekaa kushoto kwa Farouk.

Kijana aliyesimama ambaye cheo chake kumbe ni kapteni alisogea hapo mezani na kuchukua jalada lililokuwapo.

“Luteni Njata, Sajini Binda na Koplo Sudi nyinyi ni askari wa Jeshi la Tanzania. Mnashitakiwa kwa kuvuka mpaka wa nchi yetu bila ya kibali, hilo ni kosa la kwanza na kosa lenu la pili ni kuingia Uganda na kufanya ujasusi. Je, mnalo la kujitetea kabla hamjahukumiwa?” alitamka kapteni huyo kijana.

“Tuanze na wewe kiongozi wao, Luteni Njata ebu tetea.” Aliongeza kapteni huyo. “Siwezi kujitetea kwa kosa ambalo sikulifanya. Iwapo nia yenu ni askari wa Tanzania, basi mmedanganywa, sisi siyo askari wa Jeshi la Tanzania,” nilijibu kwa ujasiri.

“O.k hamna cha kujitetea kwa hiyo mnahukumiwa adhabu ya sanamu ya kireno kwa siku tatu kisha mtaachiwa huru kwa mlango wa bustanini.” Alieleza kapteni huyo na kufunga jalada.

Kwa kweli ilikuwa ni kesi ya kuchekesha lakini ndivyo ilivyokuwa. Mwendesha mashitaka ni huyo huyo na hakimu ni huyo huyo. Baadaye wote wakaondoka, wakatuacha sisi hatujui la kufanya wala kuelewa maana ya “sanamu ya kireno’ na wala “mlango wa bustani.”

Itaendelea Jumatano ijayo
 
Kitabu cha ukachero wa kachero wa Tanzania – 8

MAWIO yalipokaribia ndege nao wakaanza kuimba kwa sauti zao nzuri kuashiria kwamba mwanga sasa unataka kuchukua nafasi ya giza. Pamoja na dalili hiyo ya mapambazuko mimi sikutoka nje mpaka nilipoona kumepambazuka kabisa. Nikafunga mlango polepole na kuchungulia nje kama kuna mtu yeyote lakini hakukuwa na mtu bali magari yaliyokuwa yameegeshwa.

Nikatoka na kuliendelea bomba la maji lililokuwa mita chache kutoka katika chumba hicho ambako nilipiga mswaki na kunawa uso. Baadaye nikarudi kwenye chumba hicho kuweka vitu vyangu sawa na kuondoka zangu kuelekea kwenye mlango mkubwa wa kuingilia katika eneo hilo la kanisa.

“Habari za asubuhi” aliniuliza mlinzi wa hapo mlangoni. “Nzuri, naondoka,” nilimjibu haraka kmlangoni kuepusha maswali zaidi.

“Ngoja nikufungulie, naona una haraka sana,” alitamka huku akiuendea mlango na kuufungua bila kunihoji zaidi labda alishajulishwa na wenyewe. “Asante, kwa heri,” nilitamka na kuondoka zangu.

Hatua chache tu kutoka hapo mlangoni kuna barabara inayoitwa Cathedral, nikaifuata barabara hiyo kuelekea upande wa kulia. Nikaipita hospitali iitwayo Mengo na kuendelea mbele hadi nikatokea katika barabara iitwayo Natete. Wakati huo maeneo yote hayo yalikuwa tulivu bila pilikapilika za watu au magari.

Kutoka Natete nikajikuta nipo katika barabara iitwayo Namirembe ambayo niliifuata mpaka kutokea viwanja vya michezo. Kwa kweli mpaka muda huo nilikuwa najiendea tu bila ya kujua wapi naelekea lakini nilijivunia uzoefu wangu katika Jiji la Dar es Salaam. Ukiwa mzoefu wa jiji kama la Nairobi na ukaja Dar e s Salaam kwa mara ya kwanza ukaachwa mahali kama Manzese au Buguruni kwa vyovyote utajua ufuate njia ipi ili ufike katikati ya jiji.

Kwa hiyo na mimi ilikuwa hivyo hivyo, kadiri nilivyoona nikienda mbele idadi fulani ya watu na magari inaongezeka nikajua huko ndiko mjini. Nilikatiza katika uwanja mmoja wa michezo na kutokea mahali panapoitwa ngome kongwe ya Kampala (Kampala Old Fort) na baadaye nikapita kwenye njia ndogo ya miguu nikatokea barabara inayoitwa Martin.

Nikapita kando ya msikiti mmoja mkubwa ambao kando yake kuna hospitali na kujikuta nimetokea barabara ya Mackai ambayo nilipoifuata nikajikuta nimetokea kwenye kituo cha mabasi kilichopo karibu na uwanja maarufu wa mpira wa miguu uitwao Nakivubo.

Hapo katika kituo cha mabasi kulikuwa na mabasi mengi yaliyokuwa yakielekea sehemu mbalimbali. Kilichonishangaza ni kuona kwamba mabaso hayo yalikuwa hayajazi abiria kama yalivyo mabasi ya nyumbani Tanzania.

Aidha nilishangaa kuona wanafunzi wa shule hawakubughudhiwa walipokuwa wakiingia kwenye mabasi hayo, tofauti sana na nyumbani Tanzania ambako wanafunzi huonekana kama maadui wa wenye mabasi, hasa ya daladala.

Nilizubaa hapo kwenye stendi ya mabasi nikiangalia watu wanavyopanda na kuteremka kutoka kwenye mabasi, nikagundua kuna tofauti kubwa sana na utaratibu wa kupanda mabasi wa nyumbani Tanzania. Abiria walipanda mabasi bila kusukumana na wanafunzi walikaa kwenye viti vya mabasi bila bughudha yoyote. Mbali na hilo nikagundua mji wa Kampala ni msafi kuliko Dar es Salaam, hakukuwa na taka zilizotupwa hovyo hovyo wala taka zilizotelekezwa, hali ambayo ilisababisha hata inzi waonekane kwa nadra.

Baada ya kushangaa shangaa hapo stendi kwa karibu saa moja nzima nilimsogelea kijana mmoja ambaye nilimuomba anielekeze mahali penye nyumba ya kulala wageni ya karibu na yenye bei nafuu. Kijana huyo bila ya kinyongo alinijibu kwa kiingereza kizuri kama ilivyo kwa wananchi wengi wa Uganda, kwamba nyumba za kulala wageni zipo daraja tofauti kutegemea uzuri na ubora wake. Alisema zipo nyumba za hali ya chini sana, hali ya kati na hali ya juu ambayo inakaribia hadhi ya hoteli.

“Nielekeze ilipo ya hali ya kati,” nilimwambia haraka. “Unalijua soko la Owino?” “Mimi ni mgeni, sijui,” nilimjibu. “Ukipita ule uwanja wa mpira wa Nakivubo utafuata barabara ya Nakivubo Palace wa mwendo wa kama kilomita mbili halafu tazama upande wa kushoto utaliona soko kubwa liitwalo Owino.” “Enhee! Baada ya kulikuta soko la Owino?” “Baada ya kulikuta soko hilo kwa mbele kidogo utakuta Owino Guest House na mbele ake kuna hoteli ya Kisenyi.” “Asante sana,” nilijibu na kuondoka zangu.

Nilitembea kwa miguu kwa zaidi ya dakika kumi hivi nikajikuta nimefika katika soko la Owino ambalo kwa kweli linafanana sana na soko kuu la mjini Morogoro. Mbele ya soko hilo nikaikuta nyumba ya kulala wageni iitwayo Owino na mbele kidogo nikaiona hoteli ya Kisenyi.

Niliingia katika hoteli ya Kisenyi kuulizia malipo yake kwa siku, nikaona siyo ghali lakini walinitaka nionyeshe pasipoti kabla ya kupangishwa kitu ambacho sikufikiria kabisa, kwa hiyo nikaiacha hoteli hiyo licha ya uzuri wake nikaendelea nyumba ya kulala wageni ya Owino. Nilipofika Owino nilipokelewa kwa shauku na kinadada watatu ambao walikuwa wamekaa nje ya nyumba hiyo wakiwa wanakunywa supu.

“Unakaribishwa” alitamka mmoja wao ambaye ni mnene zaidi kuliko wenzake. “Ahsante” nilijibu na kuingia ndani hadi sehemu ya mapokezi ambako nilimkuta kijana mmoja wa kiume. Kijana huyo alinieleza masharti na malipo ya kupanga chumba, nami nikaridhika kwamba patanifaa. Hata hivyo wasiwasi wangu ulikuwa juu ya wanawake wale watatu mashangingi ambao nilihisi wanaweza kutumiwa kunichunguza au kunimaliza fedha zangu chache nilizokuwa nazo.

“Usalama wake ukoje hapa? Hakuna wizi?” nilimuuliza kijana huyo. “Nyumba hii ina usalama mkubwa, lakini usipende kuingiza wanawake chumbani mwako,” alinieleza kijana huyo kwa kiingiereza murua. Wananchi wengi nchini Uganda wanaongea kiingereza vizuri kwa sababu ni moja ya rasmi za nchi hiyo. Lugha nyingine rasmi ni kinyankole na kiswahili. Hata redio Uganda hutumia lugha zote hizo tatu katika matangazo yake. Wananchi wa Tanzania huzungumza sana Kiswahili na ndiyo lugha rasmi.

Nipoafikiana na kijana huyo nikapanga chumba kwa siku mbili kwa hiyo nikalipia kabisa fedha zote ili kama nikikurupushwa niondoke bila ya deni. Baada ya kulipia chumba hicho nikapewa fomu kujaza majina yangu, uraia, ninakotoka na niendako. Tofauti na kule katika hoteli ya Kisenyi hapa sikudaiwa pasipoti wala kuulizwa.

Nilionyeshwa chumba change namba tisa ambacho kilikuwa na meza ndogo moja, feni ya mezani, kitanda cha futi tatu na nusu chenye chandarua, kiti kimoja na chini kulikuwa na zulia lililoanza kuchakaa. Humo chumbani nilipumzika katika kiti kwa dakika kama kumi hivi na baadaye nikavua nyuo zangu na kuvaa taulo la humo chumbani ambalo halikuwa zuri ingawa lilionekana limefuliwa. Baadaye nikatoka kwenda kwenye vyoo ambavyo vilikuwa nje ya vyumba, nikaoga haraka kisha nikarudi chumbani kwangu na kujilaza kitandani kupata buraha.

Mara nyingi nyumba za kulala wageni zenye vyoo vya nje hutokea sana matukio ya wizi na hasa wakati mpangaji anapotoka kwenda chooni, hata kama umefunga chumba chako kwa funguo. Nililala kwa starehe mpaka karibu saa sita hivi nipo nilipoamka na kutoka nje kwenda kutembetembea maeneo ya jirani ambako nilijikuta nimefika katika uwanja wa mpira wa Nakivubo ambako kulikuwa na watu wengi wakisubiri kuingia ndani ya uwanja. Nilihisi kulikuwa na mechi kubwa jioni bdiyo maana wapenzi wanaingia mapema ndani ya uwanja.

Baadaya kupita hapo Nakivubo nikajikuta nimetokea kwenye mzunguko uliopo karibu na kituo cha mabasi na teksi ambapo nikaufuata mtaa wa Luwum na kulikuta kanisa zuri la katoliki liitwalo “Christ the King”. Ndani ya uwa wa kanisa hilo niliona nyumba nzuri za mapadre na masista. Mbele ya kanisa hilo nikaona Kampala Casino ambayo wakati huo ilikuwa imefungwa vinginevyo ningeingia ndani nicheze kamari.

Kutoka hapo Kampala Casino nikarudi nilikotoka na kuifikia hoteli iitwayo Royal ambayo kwa kwlei inapendeza sana kutokana na mandhari yake nzuri. Nikaingia kwenye hoteli hiyo ili nile chakula cha mchana lakini nilipozisoma bei za vyakula ziliniogopesha, kwa hiyo nikanywa kahawa na keki mbili tu.

Nilipomaliza kufungua kinywa muda huo ambao ni muda wa kula chakula cha mchana niliendelea kukaa kwneye hoteli hiyo ambayo wakati huo ilikuwa ikipiga muziki mzuri aina ya fanki ya polepole. Hata hivyo niliamua kuendelea kukaa mahali hapo zaidi kwa kuwa nilifikiri huenda ningemuona mtu yeyote ninayemfahamu kutoka nyumbani Tanzania.

Wazo langu hili liligonga ukuta baada ya kukaa hapo hotelini kwa saa nzima bila ya kuona sura hata moja ninayoifahamu au japo kuifananisha tu. Nilijiona mjinga, nikaamua kurudi ili kujipumzisha.

Nilipofika nikauchapa usingizi mpaka niliposhtuka jioni sana. Nafikiri uchovu niliokuwa nao ndio ulionifanya nilale foofofoo. Baada ya kuamka nikaenda tena kuoga na baadaye nikala mikate na nyama iliyokuwa kwenye kopo na kisha nikarudi tena kule kwenye hoteliu ya Royal ambako miziki ilinivutia sana. Nilipofika sikuamini macho yangu, watu walikuwa wengi hotelini hapo na palichangamka sana. Taa za rangi zilizokuwa zinawaka kwa kupokezana na miziki mizuri iliyokuwa ikipigwa ilipafanya mahali hapo paonekane pa kuvutia sana.

Nilitafuta nafasi ya kukaa lakini kila meza ilikuwa na watu wanne au sita wakila nyama za kuchoma na kunywa bia na waragi. Hii waragi ni pombe inayopendwa sana huko Kampala ambayo ni sawa sawa na konyagi ya Tanzania. Zunguka zukunka yangu ya kutafuta mahali pa kukaa nikajikuta nimekaa kwenye kiti cha meza ya peke yangu.

Hatua chache au niseme umbali wa kama mita mbili hivi kulikuwa na meza nyingine iliyokuwa na mtu mmoja ambaye macho yangu yaliganda kwake kama macho ya kinyonga anapotaka kumnasa mdudu amle.

Mtu huyo alikuwa mwanamke na alionekana kama vile anamsubiri mtu kwa sababu mara kwa mara alikuwa akiitazama saa yake nzuri iliyokuwa inang’ara ambayo nilihisi ni ya dhahabu. Mwanamke huyo mrefu kidogo mwenye unene wa wanawake wa Kihaya, Kinyakyusa au Kinyamwezi alikuwa amevaa vitenge maridadi ambavyo kwa kweli vilimpendeza sana.

Kichwani alikuwa amejifunga kilemba ambacho kililingana rangi na vitenge alivyovaa. Masikioni, shingoni na vidoleni alijipamba kwa dhahabu tupu. Hakika alionekana ni mwanamke mwenye uwezo kifedha. Wengi walimtazama lakini mimi nilitia for a.

Baada ya pilikapilika za ‘unywaji’ hatimaye nilifanikiwa kukaa pamoja na mwanamke huyo ambaye alijitambulisha kwangu kuwa ni Elizabeth Byarugaba. “Mbona jina la baba yako ni kama la watu wa mkoa wa Kagera nchini Tanzania, umewahi kuishi huko au ni mzaliwa wa huko?”

“Ni kweli kuna kina Byarugaba wengi mkoani Kagera lakini mimi siyo wa huko na wala sijafika huko. Hata hivyo Wahaya wengi wameingiliana na Waganda ndiyo maana desturi zetu, vyakula, maumbile, majina na hata lugha zinafanana kidogo.”

Baada ya maongezi na vinywaji, nilifanikiwa kuondoka hadi nyumbani kwa Elizabeth ambapo tuliendelea na vinywaji sambamba na mazungumzo ya hapa na pale, huku nikibaini viashiria kuwa Elizabeth ni mtumishi wa serikali, hasa kwa sababu eneo analoishi ujenzi wa nyumba zake ni mithili ya watumishi wa umma.

“Ni vyema ukaoge tukalale,” aliniambia. Niliingia maliwatoni na kujitumbukiza kwenye dishi maalumu la kuogea lakini wakati huo nikamsikia Elizabeth akipiga simu.

Itaendelea
 
Kitabu cha ukachero wa kachero wa Tanzania – 9

WIKI iliyopita tuliona namna kachero wa Tanzania alivyokaribishwa nyumbani kwa mwanadada Elizabeth. Tuliona pia wakati kachero huyo anakwenda kuoga, akasikia mwanadada huyo akipiga simu na kunyata karibu yake ili kumsikiliza, akihisi alikuwa akiwasiliana na majasusi wa shirika la ujasusi la aliyekuwa Rais wa Uganda, Idi Amin, (State Research Bureau- SRB). Endelea

……………

HARAKA nikatoka kwenye dishi hilo la kuogea nikanyata kuusogelea mlango ambao niliusindikiza huku moyo wangu ukienda kasi kutokana na kuhisi kwamba ananichongea. Hapo nyuma ya mlango nilitulia kama vile mamba anasubiri mawindo ndani ya maji, nikimsikia Elizabeth akieleza habari zangu, moyo wangu ukazidi kulipuka na mate yakanikauka.

Baada ya kugundua hivyo nikarudi haraka kwenye dishi la kuogea, nikaoga haraka haraka lakini ghafla Elizabeth alifungua mlango. “Hujamaliza kuoga tu? Njoo bwana tulale.” Aliniambia huku akitabasamu. “Nakuja sasa hivi,” nilimjibu huku nikitoka kwenye dishi.

Moyoni nilikwishamtilia shaka Elizabeth kwamba ni mfanyakazi wa serikali mwenye cheo cha juu na pia amepewa nyumba nzuri ya kuishi inayofanana na nyumba za serikali za Oysterbay (Dar es Salaam). Wakati nilipotoka chooni nilimkuta Elizabeth amekwishajilaza kwenye kitanda chake cha futi sita ambacho kwa kweli ni kitanda cha gharama kubwa.

Mapigo ya moyo yakaongezeka kwa kasi lakini siyo kwa ajili ya hofu bali kwa ajili ya tamaa ya ukware. Mwili ulinisisimka na mishipa kutanuka, nikajitupa katika kitanda hicho bila kukumbuka kwamba amekwishanichongea.

“Karibu” alitamka Elizabeth kwa sauti nyororo yenye kuonesha kwamba tayari akili zake zimekwishaingia katika dimbwi la mapenzi. Alinikumbatia na kunigeuza nikawa juu yake… lakini kabla sijachukua hatua yoyote simu ikaita. Eliza akakurupuka kitandani na kuinua mkono wa simu iliyokuwa juu ya meza ndogo nzuri ya vioo tupu.

“Hello, hello” aliita Elizabeht huku akiinua simu hiyo na kwenda nayo sebuleni ili nisisikie anayotaka kuongea. “Yes, yes, o.k” alisikika akiitikia. Aliporudi alionyesha ni mwenye wasiwasi kidogo kwa hiyo sikusita kumuuliza. “Kuna nini?” “Hakuna wasiwasi ni rafiki yangu amenipigia simu,” alijibu kunitoa hofu. “Mbona hizi nyumba kama za serikali?” lilinitoka swali bila kutegemea. “Kwa nini unauliza hivyo?” “Naona zinafanana na nyumba za serikali za Tanzania na hata zile za Kenya. Si unajua Waingereza walitutawala kwa hiyo vitu vingi vinafanana.” Nilitamka na kumfanya Elizabeth anikazie macho.

“Wewe uliwahi kufanya kazi serikalini?” aliniuliza lakini kabla sijajibu nikasikia kengele ya mlango inagonga. “Vipi nani tena usiku huu?” nilitamka huku nikibabaika. “Sijui ngoja nikaone,” alijibu huku naye akitweta kwa hofu.

Wakati Eliza anakwenda kufungua mlango, haraka haraka nikachukua nguo zangu na viatu nikavaa na baadaye nikamfuata mlangoni. Aliponiona nimemfuata mlangoni huku nikiwa nimekwishavaa nguo zangu alibabaika sana kuufungua mlango wa pili ambao ni wa grill. “Ah! Imekuwaje?” aliniuliza lakini sikumjibu kitu, wakati huo huo nikasikia mlio wa gari kwa nje nilioutambua ni wa Landrover ikisimama nje ya nyumba hiyo.

Kwa kweli niliogopa sana nikajua sasa nimepatikana. Hata hivyo kwa kutumia uaskari wangu nikapata mbinu ya haraka ya kujiokoa. Haraka haraka Elizabeth akafungua mlango huku mimi nikiwa nimejibanza nyuma ya mlango wa ndani karibu naye.

Wanaume wanne waliovaa suti nyeusi waliingia ndani kama umeme huku wakiwa wameshika bastola mikononi lakini kabla hawajatahamaki mimi nikazima taa na kuwapiga kikumbo.

Wawili walianguka ndani na mmoja aliyekuwa karibu na mlango aliangukia nje pamoja na Elizabeth na mwingine akabaki ameduwaa. Hapo nje nikaikuta gari aina ya Landrover ya rangi ya bluu iliyochanganyika na nyeusi kidogo, nikaigundua ni gari ya State Research Bureau (SRB).

Dereva wa gari hiyo alipoona kizaazaa hicho cha wenzake kuanguka chini na mimi natoka akahamanika, akafungua mlango wa gari akitaka kuniwahi lakini hakuweza.

Nilikimbia kama swala anayemkimbia simba huku milio ya risasi ikivuma nyuma yangu. Sikusimama wala kugeuka nyuma niliongeza kasi mpaka nilipofika kwenye uwanja mkubwa ambao niligundua ni wa mpira wa miguu.

Huku nikiwa natweta kwa nguvu nilikaa chini nikaangaza macho huku na huku kuthibitisha usalama wangu. Hakukuwa na kitu chochote cha kutilia shaka, usiku ulikuwa tulivu lakini wa kutisha sana kwa sababu kulikuwa kimya sana na hakukuwa na mtu yeyote anayetembea barabarani mbali na magari ya jeshi yaliyokuwa yakipita mara kwa mara. Nilihisi magari hayo yalikuwa katika harakati za vita si kunitafuta mimi.

Nilijilaza chali huku nikijaribu kuwaza namna nilivyoponyoka kwa maofisa wale wa Usalama wa Taifa wa Uganda lakini sikupata jibu ulikuwa ni muujiza wa Mungu tu. Hali ya hapo kiwanjani ilikuwa ya baridi sana lakini sikushangaa kwa sababu najua mstari wa Ikweta umepita Uganda na Kenya, kwa hiyo hali hiyo ni ya kawaida.

Joto huwa joto na baridi huwa baridi. Labda kilichonifariji kidogo ni kutokuwapo mbu katika eneo hilo kwa hiyo nikajigeuza na kulala kifudifudi ili kuizuia baridi isinishambulie hadi kuamsha ule ugonjwa wa pwani, ngiri. Kwa kweli usingizi wangu ulikuwa wa mang’amung’amu.

Hata hivyo, pamoja na adha yote niliyoipata mahali hapo usiku haukuchelewa. Sauti za jogoo zilizosikika kwa mbali zilinisaidia kunijulisha kwamba mawio yanakaribia. Baadaye kidogo sauti ya adhana na za ndege zikasikika vizuri masikioni mwangu nikajua siku mpya imeanza.

Wazo la kuufuata mzigo wangu kule katika nyumba ya kulala wageni ya Owino lilinijia lakini nikalipuuza kwa vile nilihisi nikiendelea kuzubaa hapa mjini wanaweza kunitia mbaroni. Nikajipapasa mfukoni kuthibitisha kama dola zangu za Kimarekani alizonipa Padre Franz zipo na nilipothibitisha zipo nikafikicha macho na kuangaza huku na huku ili kuthibitisha kama nipo salama.

Baada ya kuthibitisha nipo salama nikainuka na kujinyoosha mgongo kisha nikaondoka eneo hilo bila kuwa na uhakika hasa wapi ninakoelekea ingawa azma yangu ni kuondoka katika jiji hilo siku hiyo. Nilitembea njiani bila kukutana na askari yeyote na hata watu wachache niliopishana nao hawakuwa na habari na mimi. Kwa kweli nilishukuru sana Mungu.

Katika tembea yangu hiyo ghafla nikajikuta nimetokea katika barabara iliyokuwa na kibao kilichoandikwa Naguru. Nikaifuata barabara hiyo na kujikuta napita karibu na uwanja mzuri wa michezo ulioandikwa K.C.C Sports Ground wa eneo hilo linaloitwa Lugogo ambao ulikuwa upande wa kulia na upande wa kushoto kulikuwa na nyumba zilizojengwa vizuri kwa mpangilio kama za Shirika la Nyumba (NHC).

Baadaye nikaiacha barabara hiyo inayoenda katika eneo la viwanda na kukatiza hadi kwenye stendi ya mabasi iliyopo karibu na soko linaloitwa Nakawa ambalo lipo karibu na barabara kuu ya Jinja. Hapo stendi nikakuta hekaheka kubwa utafikiri ni mchana. Watu walikuwa wanapanda mabasi, wengine walikuwa wanashusha mizigo na wengine kupandisha mizigo ili mradi mahali hapo palionekana kumekucha.

Muda mrefu baadaye nikajitumbukiza katika mgahawa mmoja ulioandikwa Super K Tea Room ambao kwa kweli nilipoingia ndani sikuamini macho yangu kama kweli mgahawa huo unastahili kuitwa super kwa jinsi ulivyokuwa shaghalabaghala sana kwa sababu kwa kawaida migahawa mingi inayozunguka eneo la soko na stendi ya mabasi mara nyingi inakuwa michafu kutokana na idadi kubwa ya wateja wanaoingia ambao wengi wao wanakuwa na haraka.

Nilipomaliza kufungua kinywa nikanunua mswaki na dawa ya meno aina ya Signal kisha nikanunua maji ya chupa ambayo niliyatumia kupigia mswaki na kunywa. Baadaye nikasimama kidogo hapo stendi ya mabasi nikishangaa jinsi watu wanavyoingia na kuteremka katika mabasi bila kugombea ingawa idadi yao ilikuwa kubwa ukilinganisha na ile ya mabasi. Ghafla macho yangu yakatua katika basi moja aina ya Isuzu lililoandikwa Mengo Jinja Express ambalo lilikuwa linaelekea Jinja hadi Tororo. Bila kufanya ajizi nikajitumbukiza katika basi hilo kwa nia ya kuondoka Uganda kupitia Kenya.

Tororo ni mji wa mpakani kati ya Uganda na Kenya lakini upo upande wa Uganda. Humo ndani ya basi zilibaki nafasi kama sita tu ili basi lijae. Nikakaa katika kiti cha pili kabla ya kufikia nyuma kabisa. Abiria watatu wanaume waliokuwa wameketi kiti cha mbele yangu walikwua wakizungumzia vita iliyoanza katika mpaka wa Tanzania na Uganda. Basi lilipoondoka hapo Nakawa tulipita Mukono, Seta, Namataba na Lugazi ambayo ni miji midogo inayofanana sana na miji ya Tanzania kama Muleba na Biharamulo.

Humo ndani ya basi maelezo ya vita yalishamiri sana kiasi cha kunitia hofu. Baadhi ya Waganda waliokuwa wakiongea niliwasikia wakisema majeshi ya Amin yanakaribia kuuteka mkoa mzima wa Kagera na kuufanya uwe sehemu ya Uganda. Maneno hayo yalinikera sana lakini sikuwa na la kufanya bali kushughulikia namna nitakavyotoka aslama katika nchi hiyo.

Baada ya mwendo wa takriban saa nne tukafika Jinja ambapo baadhi ya abiria waliteremka na wengine wakaingia. Mji wa Jinja ni mkubwa kidogo, unafanana sana na mji wa Morogoro na hata jinsi viwanda vilivyozunguka kando ya mji huo vinafanya ufanane zaidi na Morogoro ingawa kwa kweli Jinja ina viwanda ni vingi zaidi na pia ni maarufu duniani kutokana na maporomoko ya Owen ambayo hutoa umeme mwingi.

Hekaheka za hapo stendi ya basi ya Jinja zilikuwa kubwa kuliko zile nilizoziona katika stendi ya basi iliyokuwa karibu na soko la Nakawa jijini Kampala. Labda kwa sababu mji wa Jinja una sifa ya kuwa na viwanda vingi vikubwa, hoteli nyingi nzuri na watalii wengi ambao hufika katika mji huo kuangalia chanzo cha mto Nile. Mto Nile huanzia Jinja hadi katika Bahari ya Mediterania.

Mbali ya mabasi mengi hapo stendi kulikuwa na pikipiki kubwa nyingi ambazo abiria tuliyekaa naye kiti kimoja aliniambia kwamba pikipiki hizo ni za kukodi ziendazo Tororo na Kampala. Aidha, aliniambia pikipiki hizo ambazo hukodishwa na watu wenye safari za haraka zinajulikana sana nchini humo kwa jina la bodaboda. Abiria huyo ambaye alikuwa akiongea kwa ufasaha Kiingereza aliniambia mbali ya kuwepo hizo bodaboda pia kuna teksi ambazo huziita special hire zinazotumiwa sana na watu wenye uwezo kifedha.

Tuliondoka Jinja saa sita kamili mchana na baada ya kutoka mjini tukaanza kupita maeneo yenye viwanda mbalimbali na mashamba makubwa ya miwa utafikiri Kilombero. Mbali na mashamba hayo ya miwa, tuliyapita mashamba mazuri ya pamba ambayo kwa kweli yalivutia macho sana.

Baadaye tukaingia mji mdogo unaoitwa Iganga ambao naweza kuufananisha na mji wa Korogwe wa mkoani Tanga. Hapo tulisimama kwa dakika kama kumi hivi na baadaye safari ya Tororo mji wa mpakani ikaanza. Kabla ya kufika Tororo tulivuka daraja kubwa kama lile la Wami katika barabara ya Chalinze hadi Segera.

Daraja hilo niliambiwa ni la mkono wa tano wa mto mkubwa unaoitwa Kyoga. Kilomita chache baada ya kuvuka daraja hilo niliona kwa mbali mbele yetu milima mkubwa niliambiwa inaitwa Elgon, iliyopo nchini Kenya.

Moyoni shauku ya kufika Tororo iliongezeka sana, lakini tulipofika karibu na bao kubwa lililoandikwa “Tororo welcomes you” lenye kuonesha tunaingia Tororo tukasimamishwa na askari wa jeshi la Idi Amin Dada ambao walitisha sana kutokana na jinsi walivyovaa kivita huku kila mmoja akiwa na bunduki.

Askari hao waliokuwa kama 18 au 20 hivi walionesha hawana mchezo hata kidogo. Kando ya barabara kulikuwa na magari mawili ya dereva, lori moja aina ya Tata na Landrover mbili. Kiongozi wa askari hao aliyekuwa na cheo cha luteni kanali aliamuru abiria wote tuteremke na basi lipekuliwe.

Tukiwa nje ya basi hilo kila mmoja wetu alitakiwa aoneshe kitambulisho au hati ya kusafiria. Hali hiyo ilinifanya nijisikie kutaka kujisaidia haja ndogo na tumbo la kuharisha ghafla. Mate yalinikauka na mwili ukaanza kufa ganzi. Nilifikiria nitimue mbio lakini nilijua haitanisaidia kitu kwa sababu bunduki zote za askari hao zitaelekezwa kwangu, kwa hiyo nitapoteza maisha.

Ilipofikia zamu yangu kujieleza nikajipa moyo na kueleza kwamba mimi ni Mtanzania ninayeishi nchini Kenya, nilikuja Uganda kufanya biashara ya mitumba ya nguo lakini nilipokuwa Jinja niliibiwa begi langu ambalo lilikuwa na hati zangu mbalimbali na pasipoti.

“Wewe huna kitambulisho chochote?” aliuliza kwa ukali luteni aliyenihoji. “Umetoka wapi? Uliingia lini Uganda?” alizidi kuniuliza luteni huyo lakini kabla sijajibu nilivutwa na askari mwingine mwenye cheo cha kapteni aliyekuwa amesimama kando akisimamia utekelezaji wa ukaguzi huo. “Tumbukiza kwenye gari” alitoa amri kapteni huyo kwa askari wa chini yake. Nilichukuliwa kikuku na kuingizwa kwenye lori aina ya Tata ambamo niliwakuta watu kama 10 hivi ndani ya lori hilo.

Ndugu wasomaji wa gazeti la Raia Mwema na kwa kweli uwasilishaji huu wa kitabu cha MATEKA MPAKANI kilichoandikwa na kachero Frowin Kagaueka, kuwaenzi wenzake wawili waliouawa na majasusi wa State Research Bureau (SRB) chini ya utawala wa Idi Amin wa Uganda, tunaishia hapa kuhusu yaliyomo kwenye kitabu hicho ambacho kitachapwa na kusambazwa kwa ajili ya kuuzwa hivi karibuni. Tunamshukuru Frowin Kageuka kwa kuruhusu wasomaji wa Raia Mwema kusoma sehemu ya kitabu hicho kupitia gazeti hili kabla ya kitabu husika kuchapwa na kusambazwa. Kwa maswali na mawasiliano zaidi kuhusu kitabu hicho mnaweza kuwasiliana moja kwa moja na mtunzi kwa namba ya simu 0715 411113 – Mhariri
 
Tunweza kupataje hicho kitabu?
 
Tunweza kupataje hicho kitabu?
Ndugu wasomaji wa gazeti la Raia Mwema na kwa kweli uwasilishaji huu wa kitabu cha MATEKA MPAKANI kilichoandikwa na kachero Frowin Kagaueka, kuwaenzi wenzake wawili waliouawa na majasusi wa State Research Bureau (SRB) chini ya utawala wa Idi Amin wa Uganda, tunaishia hapa kuhusu yaliyomo kwenye kitabu hicho ambacho kitachapwa na kusambazwa kwa ajili ya kuuzwa hivi karibuni. Tunamshukuru Frowin Kageuka kwa kuruhusu wasomaji wa Raia Mwema kusoma sehemu ya kitabu hicho kupitia gazeti hili kabla ya kitabu husika kuchapwa na kusambazwa. Kwa maswali na mawasiliano zaidi kuhusu kitabu hicho mnaweza kuwasiliana moja kwa moja na mtunzi kwa namba ya simu 0715 411113
 
Raiamwema ya wiki hii hakuna mwendelezo wa makala ya Jasusi Kagauka sijui kwanini gazeti limeamua kutuacha hewani.
 
Wakuu habari. Kwa wale wenye hamu ya kuelewa kwa undani vita vya Tanzania na Uganda basi kaeni mkao wa kula. Kachero wa Tanzania aliyetekwa na askari wa Uganda akiwa yeye na wenzake wawili (ambao waliuawa na yeye kunusurika kimiujiza) ameamua kuweka yote hadharani. Amesimuliwa yote kuanzia walivyotekwa, mateso waliopitia, wenzake walivyouawa na yeye alivyotoroka. Ni kitabu ambacho ukinza kukisoma hutakiweka chini. Japokuwa bado hakijachapishwa lakini simulizi zake za mwamnzoni kama zilivyochapishwa na gazeti la Raia Mwema zimewakuna wengi: Hii hapa sehemu ya mfululizo wa simulizi zake.

Kitabu cha ukachero wa kachero wa Tanzania – 2

………………………….

WIKI iliyopita tulianza kuchapisha sehemu ya kwanza ya uchambuzi wa kitabu kipya “Mateka Mpakani” kilichoandikwa na kachero wa Tanzania, Frowin Kagauka, kumuenzi mwenzake aliyeuawa mpakani mwa Tanzania na Uganda. Leo tunaendelea na sehemu ya pili.

…………………….

“AMESEMAJE wakati mlipomuuliza juu ya bastola hiyo? Amekubali ni yake lakini amekataa katakata kuwa yeye ni askari wa Idi Amin,” alinijibu Sajin Mkuu wa Kituo.

“OK. Sajin Binda wajulishe Bukoba ili waje kumhoji.” Niliamuru haraka. Sajini Binda alinipigia saluti nami nikaijibu kwa kubana mikono kwa vile sikuvaa sare za kijeshi na baadaye akaondoka haraka.

“Msimtoe humu mahabusu mpaka wakubwa zangu wafike kutoka Bukoba, sawa?” niliagiza. “Sawa afande,” alijibu Sajini ambaye ndiye mkuu wa kituo hicho kidogo cha polisi hapo kijijini Murongo.

Niliondoka hapo kituoni na ilipofika saa sita na nusu mchana nikijua wakubwa zangu watakuwa wanakaribia kufika hapo kituo cha polisi lakini hawakutokea mpaka saa nane na dakika kumi. Walifika kwa gari aina ya Landrover na wote walivalia sare za kijeshi isipokuwa dereva na mtu mwingine mmoja ndiyo walivaa kiraia.

Hao watatu waliovaa kijeshi mmoja alikuwa luteni na wawili makapteni. Waliovaa kiraia niliambiwa ni Luteni Emir wa Idara ya Usalama wa Jeshi ambaye ndiye aliyeendesha gari hiyo na Meja Stephen kutoka Idara ya Usalama wa Taifa mkoani Kagera. Wakuu hao waliamuru Kafumba atolewe mahabusu na alipotolewa wakamchukua na bastola yake kwenda naye Bukoba.

Sikumuona rafiki yangu Kafumba kwa zaidi ya wiki mbili ndipo siku moja bila ya kutarajia nikakutana naye sokoni hapo Murongo akizungumza na yule mpenzi wake.

“Ah! Rafiki wewe ni mbaya, umenipeleka polisi ili nifungwe bila kosa,” alilalamika. “Siyo hivyo, mimi nilishangaa kuona rafiki tangu una bastola na wewe ni bwana shamba. Naogopa sana askari ndiyo niliipeleka bastola yako polisi. Sasa wamekwambiaje?”

“Walinipeleka Bukoba nikaingizwa kwenye nyumba moja sijui ya nani, nikaulizwa maswali mengi ya Uganda na watu wawili ambao hawakuvaa kiaskari. Lakini watu wale walikuwa wema sana hawakunipiga wala kunisumbua na waliporidhika waliniachia nirudi lakini bastola yangu wamebaki nayo,” alinieleza huku akinikazia macho.

“Sawa bwana, basi tutaonana siku nyingine au leo kama bado upo hapa kwetu” nilimjibu kwa unyonge baada ya kuhisi yeye ni jasusi wa Idi Amin na ameweza kuwahadaa wakubwa zangu hadi wakaridhika kumuachia.

Wiki moja baadaye nikaletewa mwaliko kutoka kwa mzee niliyekuwa namheshimu sana, mzee Idris wa Green Hotel nikahudhurie sherehe yake aliyopanga ifanyike Jumamosi kuanzia saa tano asubuhi hapo hapo Green Hotel. Nikamjulisha Koplo Sudi na Sajin Binda juu ya mwaliko huo, kwa hiyo tukaondoka Murongo hadi Kivukoni. Tulipofika Kivukoni kama kawaida tukapanda boti na kuvuka mto Kagera ambao maji yake yanakwenda kasi sana kiasi cha kuwafanya wenyeji kushindwa kuvuka kwa kuogolea.

Baada ya boti kutuvusha tukatembea kwa miguu kilomita mbili na nusu hivi tukafika kijiji cha Kikagati ambacho kwa kweli ni kizuri kidogo kuliko kijiji chetu cha Murongo. Hapo Kikagati kuna kituo kidogo cha polisi ambacho kimejengewa badi tupu chini hadi juu, wengine huita mtindo huo ‘full suit’, vile vile kuna nyumba ya mkuu wa wilaya ambaye wenyewe walimwita DC na jengo moja kubwa la kampuni ya uchimbaji madini inayoitwa BMC.

Ilipotimia saa tano na dakika tano tulikwenda hapo Green Hotel huku tukiwa tumejaa shauku ya kunywa bia na kuvunja mifupa ya nyama ya kuku na mbuzi ya kuchoma. Kwa mshangao hapo Green Hotel hatukuona dalili yoyote ya sherehe na wala hakukuwa an watu wanaokula au kunywa kama ilivyokuwa kawaida. Kkilichonishangaza zaidi ni kutowaona hata watoto wake wakicheza nje ya hoteli hiyo ambayo mwenyewe mzee Idris anaishi humo humo kwenye vyumba vya uwani.

Kabla hajaamua kuuliza alifika mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa kati ya miaka sita na nane ambaye alituambia ameagizwa na mzee Idris atukaribishe ndani tumsubiri. Bila ya hofu tuliongozana na kijana huyo hadi kwenye sebule yam zee Idris ambayo kwa kweli hata siku moja hakuwahi kunikaribisha. Mtoto huyo alitutolea bia tatu za baridi kutoka kwenye hokofu, akatuwekea glasi kisha akaondoka. Dakika kama tano baadaye mzee Idris alifika na kutusalimu lakini hakukaa alituambia ana shughuli itakayochukua kama robo saa hivi lakini alitupa uhuru wa kujichukulia vinywaji kwenye jokofu. Wakati tunaanza kunywa bia huku bado nikitafakari jinsi ya sherehe hiyo tuliyoitiwa ilivyo, ghafla tukasikia mlio wa gari kubwa likisimama nje ya nyumba hiyo, bila shaka wote tulielewa huo ulikuwa ni mlio wa gari la kijeshi maana tulitazamana kwa mshangao.

Kabla hatujahamaki nini kinafanyika tukasikia vishindo vya hatua nzito za viatu vya kijeshi vikiizunguka hoteli hiyo. Tulipotazamana tena bila ya kusema lolote mlango ulifunguliwa na askari sita waliovalia kivita wakiwa na bunduki aina ya AK47 kila mmoja, wakatuzunguka. Moyo ulinilipuka, mate yakanikauka kinywani, bia yote niliiona chungu na balaa tupu.

“Simama juu.” Aliamuru mmoja wa askari hao ambaye alikuwa na cheo cha Sajini. Wote tulisimama huku mikono yetu ikiwa juu kuomba amani. “Songa mbele haraka.” Aliamuru tena. Tulitoka nje ambako tulikuta askari wengine wanane waliovalia kivita wakiwa na bunduki mikononii wameizunguka hoteli hiyo. Raia wa kijiji hicho au niseme kimji hicho walisimama kwa mbali sana wakishuhudia tunavyokuwa MATEKA MPAKANI.

Tuliingizwa katika lori moja la kijeshi aina ya Liaz na safari ya kwenda tusikokujua ikaanza. Tulipofika njia panda ya kwenda Kabale ambayo ipo upande wa kushoto na Mbarara ambayo ipo upande wa kulia, lori hilo lilitimua vumbi kuelekea kushoto yaani Kabale.

Baada ya mwendo wa kama kilomita nne hivi kutoka hapo Kikagati tukaingia katika kambi ndogo ya jeshi inayoitwa Kabiyanda. Tuliteremshwa katika kambi hiyo ndogo na kuingizwa katika kijumba cha mabati matupu ambapo ndani hakukuwa na lolote mbali ya joto na hewa nzito kwa vile hakukuwa na dirisha bali vitundu vidogo vipatavyo sita tu.

“Tunakuwa mateka mpakani, sijui watatufanyaje. Nahisi hizi ni njama za Kafumba, Kafumba lazima ni jasusi, alikuwa anatupeleleza. Sijui Idi Amini ana nia gani na sisi au nchi yetu…niliwaeleza wenzangu huku nikitetemeka. “Ni dhahiri Kafumba amelipiza kisasi. Lakini nahisi mpango huu ulikuwa ni wa muda mrefu,” alijibu Koplo Sudi.

Saa tisa tulitolewa humo kwenye kijumba na kukalishwa chini kwenye uwanja niliohisi ni wa kufanyia kwata. Koplo Sudi na Sajini Binda walikuwa wananitazama mara kwa mara kama vile wananiulaumu kwa kuwaingiza katika janga hili, lakini sio kosa langu bali ni tamaa yetu ya kunywa bia na kumuheshimu mzee Idris.

“Nani mkubwa kati yenu?” aliuliza Luteni mmoja mweusi mwenye sura mbaya. Hakuna aliyejibu hivyo akaona tumemdharau kaamua kumwita koplo mmoja aliyekuwa amesimama kwa mbali akituangalia.

“Funsa adabu hawa” alimwamuru koplo huyo aliyevalia kivita kwa Kiswahili kibaya kisha akaondoka zake kwa hasira.

“Ah! Mnataka ‘kufunswa’ heshima, hebu simameni.” Tuliinuka kwa hofu huku tukimwangalia nini anachodhamiria kutufanyia. “Nyinyi ni askari?” “Hakuna askari hapa kati yetu” nilimjibu haraka kwa hasira. “Eh! Wewe ndiyo mkubwa enh!” “Mkubwa wa nini?” nilimjibu na kumfanya acheke kidogo.

“O.K nyinyi mnajua Kiswahili kingi sana, hebu chuchumaeni chini huku mkishika masikio yenu.” “Tuonyeshe mfano,” nilimwambia bila hofu.

“Eh! Nyinyi jeuri sana, hebu laleni chini kifudifudi niwachape kidogo fimbo,” alitamka huku akitabasamu. Wakati tunalala kifudifudi ghafla alikuja askari mmoja asiye na cheo na kumwambia mwenzake kwamba tunatakiwa tuingie ndani ya gari tupelekwe katika kambi ya Mbarara. Tuliingizwa ndani ya Landrover moja ya jeshi la Idi Amin huku tukilindwa na askari sita waliovalia kivita wakiwa na bunduki aian ya AK 47 mikononi. Landrover ikapigwa moto na safari ya Mbarara ikaanza. Ilibidi turudi tena mpakani Kikagati kisha tufuate barabara inayoelekea Mbarara ni kama kilomita 150. Tulipofika Mbarara giza lilikuwa limekwishaingia, dereva akasimamisha gari nje ya lango kuu la kambi kubwa ya jehsi ambayo baadaye niliitambua inaitwa Simba Battalion. Taa kubwa ya usalama ikawashwa na kuzimwa kama ilivyo kawaida katika kambi nyingi za jeshi kisha sauti kali ilitaka utambulisho.

“Tumeleta mateka kutoka Kabale” alijibu askari mmoja aliyekaa mbele. Taa iliwashwa tena na kuzimwa halafu mlango ukafunguliwa. Niliona sanamu mbili za samba zilizokuwa upande wa kulia na kushoto mwa lango hilo ambazo zilinifanya nielewe maana ya kambi hiyo kuitwa Simba. Gari iliingia na kuegeshwa nje ya jengo dogo ambalo hata mtu asiyekuwa askari angegundua ni mahabusu.

Tuliamriwa kuteremka na mlango wa mahabusu ukafunguliwa, tukaingizwa. Mahabusu hiyo ilikuwa karibu na lundo la kuni na kwa mbele kidogo kulikuwa na msikiti mdogo. Ndani ya mahabusu hiyo hakukuwa na taa kwa hiyo ilibidi tutulie kimya bila kuongea wala kutembea.

Ulikuwa usiku mgumu sana kwetu hasa kwa mimi kiongozi kwa vile wenzangu walionyesha wamekata tamaa kabisa. Kama kawaida ya usiku ni lazima uche hata kama unapata taabu au raha ni lazima asubuhi ifike. Asubuhi ilipofika tulitolewa nje na kupelekwa katika ukumbi mmoja mdogo ambapo tulikalishwa chini. Dakika kama kumi baadaye waliingia wanajeshi wanne, watatu wakiwa na cheo cha meja na mmoja alikuwa kanali. Kwa jinsi walivyoonekana, walikuja kutuhoji.

“O.K Watanzania, tunaanza na wewe, inuka ujibu maswali yetu.” Alitamka kanali huyo huku akimuonyesha kidole Koplo Sudi. Koplo Sudi aliinuka wima huku akigwaya. “Unacho kitambulisho chochote hapo ulipo?” aliuliza meja mmoja ambaye ni mrefu zaidi ya wenzake. “Sina kitambulisho.” “Sawa, vua shati na suruali yako,” aliamuru kanali huyo.

Koplo Sudi akavua suruali na shati lake na kuviweka mbele yake. “Wewe unafanya kazi gani pale Murongo?” aliuliza meja mwingine ambaye ndiye aliyekuwa akinukuu maelezo yetu.

“Nafanya biashara ya kuuza vitabu sokoni,” alijibu Koplo Sudi huku akigwaya.

Ukisema kweli utapona, lakini ukitudanganya ujue hutaiona tena Murongo,” alitamka kanali huyo kwa Kiswahili kizuri. “Kwani sisi tumewakosea nini? Kosa letu ni nini mpaka mnataka kutuhukumu?” “Hamjafanya kosa lolote, lakini tunataka majibu y kweli,” alisisitiza kanali huyo.

“Unajua sisi tunawaelewa nyinyi vizuri sana, na kuonya tena. Usiseme uongo” alifoka kanali. “Sisemi uongo,” alisisitiza Koplo Sudi. “Jina lako nani?” aliuliza kanali huyo mweusi tii. “Abdallah Salum,” alidanganya. “Hatuna jina la Abdallah katika orodha tuliyoletewa.” “Kama mnayo orodha ya majina yetu kwa nini mnaniuliza jina?”

“Nyinyi wote ni wanajeshi, hiyo tunajua kwa hakika, sasa wewe unajifanya mfanyabiashara. Nakwambia mara ya mwisho, sema ukweli wako vinginevyo huwezi kurudi kwenu. Hatupo hapa kufanya mchezo,” alifoka kanali huyo.

“Umeelewa sasa, yajibu maswali yetu kwa ukweli” aliongeza meja anayeandika.

“Jina lako nani na unafanya kazi gani pale Murongo?” aliuliza meja huyo. Swali hilo lilimfanya Koplo Sudi aanze kutoa mchozi ambao uliniumiza sana moyo.

“Unalia kabla hujateswa, sasa ukiteswa si utakufa kabisa” alitamba meja. Maneno hayo hayakupunguza kasi ya machozi ya Koplo Sudi, kwa hiyo kanali akamwambia arudi aka echini.

“Zamu yako wewe, inuka kuja hapa” alitamka kanali huku akinielekezea kidole. Niliinuka nikapiga hatua tatu na kusimama. “Wewe ujibu maswali yetu kwa ukweli, hatutaki uwongo wala kilio hapa.”

“Sawa,” nilijibu kisha nikakohoa kidogo ili kusafisha koo. “Jina lako nani,” aliuliza kanali. “Nelson,” nilijibu. “Jina lako lingine” “Njata, Nelson Njata. “Yah! Jina la Njata lipo hapa” alidakia meja aliyekuwa anaandika. “Unafanya kazi gani pale Murongo?” aliuliza kanali. “Mimi ni bwana shamba.”

“Tunajua ni bwana shamba, lakini una kazi nyingine pale?” alidakia meja mwingine. “Kazi gani nyingine?” niliwauliza bila wasiwasi. “Unamjua Dan Kafumba?” aliuliza kanali na kunifanya nishtuke. “Namjua ni Mganda na pia ni rafiki yangu.” “Nani alimfikisha polisi?” aliuliza kanali huku akinikazia macho.

“Alijipeleka mwenyewe baada ya kupoteza bastola yake.” “Unaonyesha wewe ni mtu jasiri na mjuba, bila shaka wewe ni mwanajeshi, tena mwenye cheo kikubwa au sivyo? Alidakia meja anayeandika.

“Sivyo, mimi ni bwana shamba, hata Kafumba angekuwapo hapa angenisaidia kuwathibitishia.” “Pale Murongo kuna kituo chochote cha jeshi?” aliniuliza kanali. “Mimi sijui na wala sioni umuhimu wa kujua mambo ya jeshi.”

“Naona wewe nmi mwerevu sana kwa hiyo itabidi uhojiwe kwa nguvu, nenda ukakae,” alitamka kanali kwa ukali.

Nilirudi nyuma polepole na kukaa chini. Sasa ilifia zamu ya Sajini Binda kusimama, lakini maofisa hao walinong’ona kidogo kisha ghafla waliinuka na kuondoka zao. Kwa jinsi walivyoonekana walivyokuwa, kwa vyovyote ni maofisa wa Idara ya Ujasusi wa Kijeshi au ni maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa. Kama nusu saa baada ya maofisa hao kuondoka mlango ulifunguliwa na askari mmoja asiye na cheo akiwa amebeba chano iliyokuwa na bakuli tatu zilizokuwa na uji, akatugawia kila mmoja bakuli lake, tukaanza kunywa huku akituangalia.

Uji huo wa unga wa mahindi ulikuwa wa moto sana na haukuwa na sukari, hata hivyo hiyo haikutuzuia kunywa kutokana na njaa tuliyokuwa nayo. Baada ya kama robo saa hivi tulishamaliza kunywa uji huo na askari huyo akachukua bakuli zake na kuondoka.

“Sijui wanataka nini kwetu?” aliuliza Koplo Sudi kwa unyonge. “Hii yote ni kazi ya yule rafiki yangu Kafumba ni lazima ni jasusi wa Idara ya Usalama wa Taifa ya nchi hii yaani State Research Bureau” lakini kwa vyovyote itakavyokuwa asitokee mtu kati yetu akavunja kiapo chetu” nilitamka huku nikiwakazia macho.

Wakati Koplo Sudi anavaa nguo zake alizokuwa amezivua, mlango ulifunguliwa na askari mmoja aliyekuwa na bunduki aina ya AK 47 mgongoni, akatuamuru tutoke nje. Tulipotoka nje tulikuta askari zaidi ya kumi wenye silaha wakitusubiri. Tulipekuliwa kama tuna silaha na walipoona hatuna walitunyang’anya saa zetu na viatu. Baadaye wakatuamuru tuingie katika lori moja aina ya Benz lililoegeshwa mita kama kumi kutoka hapo. Humo ndani ya lori tulifungwa kamba mikononi na miguuni na safari ya tusikokujua ikaanza lakini njiani askari mmoja aliripoka kwa mwenzake kwamba tutafika katika kambi ya Makindye saa kumi na mbili jioni.

Kambi ya Makindye niliwahi kuisikia kutokana na sifa zake za utesaji na uuaji na ni maalumu kwa kutesea mateka wa vita au askari waasi. Kambi hii niliambiwa ni ya Polisi jeshi tupu (Military Police).

Itaendelea wiki ijayo
Simulizi za huyu jamaa zilinisisimua sana. Tatizo kwenye Gazeti la Raia mwema tuliambiwa hawataendelea tena kutoa simulizi hizo. Tuliambiwa tukinunue na namba ya simu kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa jinsi ya kukipata tuliwekewa but kila nikipiga hiyo namba haipatikani. Msaada wa aliyeweza kupata ufafanuzi wa jinsi kukipata Wakuu.
 
Mkuu Mawembasa1979 ulifanikiwa kupata Kitabu? Nimejaribu kupiga simu na kutuma ujumbe mfupi kwa mhusika wa Dar lakini hakuna majibu yoyote.
 
Mkuu Mawembasa1979 ulifanikiwa kupata Kitabu? Nimejaribu kupiga simu na kutuma ujumbe mfupi kwa mhusika wa Dar lakini hakuna majibu yoyote.
Mwambesa1979 yaani mkuu una quote uzi mzima ili iweje sasa kwani ukiandika bila kuquote hawezi kuona mbona tunakuwa wavivu wa kuelewa Kila siku tuambiwa kitu kile kile!???
 
Niliambiwa niende Ubungo Plaza ndio kuna ofisi za Raia Mwema na Kitabu kinapatikana hapo hapo.

Nimefanikiwa kupata kitabu, Ofisi za Raia Mwema ziko Kinondoni though sio Ubungo Plaza.
a9057ec538f205c7322ed54865cb95a1.jpg
 
Back
Top Bottom