KITABU: Kamlete, akibisha mlipue by Hammie Rajab

Sura ya Tano​

KAPTENI SHAIBU aliusukuma mlango wa ofisi ya sekretari wa Meja Jenerali Kaswiza, akaingia.

Mama Pius, sekretari wa Meja Jenerali alipomtupia jicho tu moyo wa Shaibu ulinyong’onyea zaidi. Yalielekea kumweleza kwa kifupi yote atakayokumbana nayo huko ndani kwa Mzee Kaswiza. Na hayakuwa mema.

“Karibu, Kapteni” Mama Pius alimkaribisha, tabasamu dogo la wasiwasi likionekana usoni mwake.

“Asante.” Shaibu alibahatisha tabasamu.

‘‘Ingia unasubiriwa.” Akamuambia bila kumuangalia usoni.

Bila ya kugonga mlango, aliusukuma akaingia.

Meja Jenerali Kaswiza aliketi nyuma ya meza kubwa ya ofisi yake, upande wa pili wa meza hiyo, katika viti vilivyokuwa upande wa kushoto, waliketi watu wawili waliovaa sare ya suti nyeusi. Kisha mtu wa tatu aliyekuwa ni kama alijificha akisubiri Shaibu aingie alijitokeza na kwenda kukaa mlangoni akiwa mikono ameiweka kiunoni penye silaha yake iliyofichwa.

Watu wote watatu waliinua macho kwa pamoja wakamtazama. Kwa ukakamavu wa kujilazimisha, Kapteni huyo akampigia saluti mkuu wake.

Uso wake ukiwa umejaa mikunjo ya hasira, Meja Jenerali Kaswiza aliipokea saluti hiyo kwa kubetua kichwa tu. Kisha akamwelekeza Shaibu kwa mkono aketi kwenye kiti kimojawapo kati ya vitatu vilivyokuwa upande wa kulia mbele ya meza yake.

“Kapteni Shaibu,” Mzee huyo alimwita mara tu alipoketi. “Uko chini ya ulinzi wa serikali.” Alitamka neno moja moja huku akiuma meno.

Moyo wa Shaibu ulipiga mshindo mkubwa, akahisi pengine wenzake waliusikia. Aliachia kinywa nusu wazi, akayageuza macho haraka kuwatazama watu wawili waliokuwa wamejituliza nje katika dirisha la ofisi hiyo wakiwa na silaha mkononi kama kujitayarisha kumkabili iwapo kama ataamua kuleta rabsha.

Akayarudisha macho kwa mkuu wake. “Kwa kosa gani, mzee?” Akaamua kujitetea.

“Kwa kushiriki katika mipango ya kutaka kumuua kiongozi wa nchi na kuleta mapinduzi ya kumwaga damu.”

Kapteni Shaibu alipitisha nukta kadhaa akijilamba midomo kabla ya kusema kwa sauti iliyojaa kitetemeshi, “Sina habari hizo kabisa, mzee.”

“Sikiliza, Shaibu. Hawa mabwana unaowaona hapa wametoka Ikulu.’’ Akasema kwa hasira za wazi. ‘’Ni watu wa kitengo cha usalama wa taifa. Wana ushahidi kamili.” Alisita kidogo. Kisha akaendelea, “Sijakukabidhi kwao kwasababu nataka nijue je kuna vijana wengie katika mpango huu? Vijana wote kumi wa hapa jeshini mliowashirikisha, walikamatwa kwa siri hapa hapa leo asubuhi. Baadhi yao, raia, walikamatwa tangu jana usiku. Ulibaki wewe, Luteni Maige na Mwasia mmoja anayeitwa Sadrudin Visram. Kwanza, yuko wapi Maige? Tumepiga simu kila mahali hawajui alipo. Kwa vyovyote wewe unajua. Yuko wapi?”

Shaibu alihisi sakafu ikipasuka, na yeye akizama haraka na kiti chake. Bora ingekuwa hivyo. Angejua mwenyewe la kufanya huko ardhini. Pengine angekwepa kifo na kifungo cha maisha kizuizini. Alitambua fika kuwa hapana msamaha katika njama kama hizo.

“Sikiliza, Bwana Shaibu,” mmoja kati ya wale watu wawili alisema alipoona Shaibu ameduwaa. "

‘’Shabaha yetu kubwa, ni kumpata Maige. Tukimshika, huenda mambo yakawa si mabaya sana upande wako. Yuko wapi Luteni Maige?”

‘‘Kwa kweli sina hakika,” Shaibu alisema bila ya kusita. “Sijui.”

“Hujui?” mtu mwingine aliuliza huku akifinya macho.

“Leo hamkuonana?”

“Tulionana kama saa sita”

“Hapa hapa au nje?”

“Alikuja ofisini kwangu, lakini hakukaa sana. Akaondoka.”

‘‘Alisema anakwenda wapi?”

“Sikumuuliza. Kama hayupo hapa huenda yuko mjini.” Akasema huku akijua wazi kwamba ni lazima aseme kweli la sivyo angekutana na mateso kuanzia hapo hapo alipo.

“Unadhani yuko sehemu gani huko mjini ambako tunaweza kumpata haraka?”

“Sina hakika. Hakuniambia anakokwenda.” Pakazuka kimya cha nukta mbili tatu hivi.

“Mzee Kaswiza,” yule wa kwanza alisema hatimaye. “Hatuna budi kumchukua Kapteni Shaibu kwa kumhoji zaidi. Tafadhali iarifu familia yake.” Alinyamaza kidogo. Kisha akaendelea. “Hivi sasa kesi hii iko chini ya Meja Mwita, huko Makao Makuu ya Upelelezi. Pengine leo hii au kesho, mmoja wa wapelelezi wa huko atafika hapa kwa kutaka kujua zaidi juu ya Luteni Maige. Kama si Ray Sibanda mwenyewe, basi atakuja msaidizi wake, Jack Solomon.”

“Sawa,” Mzee Kaswiza alisema. Akamgeukia Kapteni Shaibu. “Umejitafutia balaa, Kapteni. Kushawishiwa kufanya jambo baya kama hili na askari uliyemzidi umri na cheo ni kulifedhehesha jeshi zima, Nakutakia mateso mengi.”

Shaibu alikuwa wa kwanza kusimama, akafuatiwa haraka na mmoja wa wale watu watatu, mikono yote ya mtu huyo ikiwa imezama mifukoni mwa koti lake alipohifadhi bastola ndogo.

Alipokuwa akiongozwa nje, hakutaka hata kumtazama Mama Pius.

***

Taarifa ya Habari ya saa kumi siku ile haikuficha kitu. Mtangazaji, kwa sauti tulivu, alisoma vichwa vya habari, kisha akaanza kusoma habari kamili iliyo muhimu.

Dar es Salaam: Safari ya kiongozi wa nchi, iliyotazamiwa iwepo keshokutwa akielekea Ethiopia kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi huru za Afrika, imeahirishwa.

Kuahirishwa kwa safari hiyo kumetokana na kugundulika kwa njama iliyopangwa ya kutaka kumuua kiongozi huyo hapa hapa nchini, endapo angesafiri siku hiyo. Wanajeshi wawili, Kapteni Shaibu na Luteni Maige, wanasadikiwa kuhusika moja kwa moja na njama hiyo. Mmoja wa wanajeshi hao, Kapteni Shaibu, leo hii ametiwa mbaroni na yuko chini ya ulinzi wa serikali kwa kuhojiwa. Juhudi zinaendelea za kumsaka Luteni Maige ambaye, hadi hivi sasa, hajulikani aliko.

Wanajeshi wengine kumi wa ngazi za chini pia walikamatwa leo hii asubuhi huko Makao Makuu ya Jeshi ili kuisaidia serikali katika upelelezi wa njama hiyo.

Jana usiku, raia watatu, akiwemo Mwenyeketi wa wafanyabiashara Mkoani wa Dar Es Salaam ndugu Mohsin Hilal na jambazi lililopevuka, Big Ben, pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Polisi mstaafu, Paskali Nyirenda, walikamatwa kwa kushukiwa kuhusika katika njama hiyo. Raia mwingine, Sadrudin Visram, Mwasia, ambaye pia anasadikiwa kuhusika katika njama hiyo, hajulikani aliko. Hivi sasa juhudi za kila hali zinafanywa ili kuwakamata Luteni Mige na Visram. Hali ya nchi ni tulivu, na wananchi wanaombwa waendelee na shughuli zao kama kawaida.

***

Siku iliyofuatia, Alhamisi, Meja Mwita alifika kazini mapema zaidi kuliko ilivyo kawaida yake.

Alipoingia tu ofisini mwake na kuketi kitini, aliinua simu akazungusha nambari ya sekretari wake.

“Habari ya asubuhi, Matilda?” Meja Mwita alimsalimia.

“Nzuri, mzee. Shikamoo.”

“Marahaba. Ray yupo?”

“Hajafika. "

“Solomon je?”

“Bado.”

“Okay. Yeyote kati yao atakayefika mwanzo, mwambie aje ofisini. Tafadhali.”

‘‘Sawa, mzee.”

Akakata simu. Akawasha sigara, akaisoma kwa mara ya tano taarifa ya Ikulu iliyomwamuru atume vijana wake wafanye upelelezi juu ya njama iliyokusudiwa, na muhusika mkuu, Luteni Maige, atiwe mbaroni haraka iwezekanavyo.

Wakati Meja Mwita akisoma taarifa hiyo, sekretari wake alikuwa akipiga simu nyumbani kwa Ray.

Mary, msichana wake, ndiye aliyeipokea.

“Nyumbani kwa Bwana Sibanda. Nani mwenzangu?”

“Mary, Matilda hapa. Namuhitaji Ray tafadhali.” Akasema kwa sauti nzito yenye msisitizo.

“Hallo, Mati!” Ray aliita alipoichukua simu.

“Habari za asubuhi, bosi?”

“Nzuri. Vipi?”

“Mzee anakuhitaji haraka sana.”

“Mwambie niko njiani. Jack ameshafika?”

‘‘Bado, bosi. Mzee ameagiza yeyote kati yenu atakayetangulia kufika, aripoti ofisini kwake.”

“Okay. Nitafika baada ya dakika ishirini. Nitayarishie kahawa.”

“Sawa, bosi.”

***

Wafanyakazi wawili-watatu walishaanza kuingia ofisini. Alipomaliza kutia maji katika birika la kahawa na kuuchomeka waya wa birika hilo katika swichi, Matilda alimwona Jack Solomon akiingia. Jack pia alimwona Matilda.

“Aisee, ongeza maji” Jack alisema huku akiachia tabasamu pana. “Ni chai au kahawa”

‘‘Kahawa.”

“Nitakunywa. Mzee ameshafika?”

“Zamani,” Matilda alijibu. “Alikuwa akiwahitaji nyote wawili. Wewe na Ray. Kasema, yeyote kati yenu atakayetangulia kufika akamwone. Kwa hiyo Unatakiwa ofisni kwa mzee haraka iwezekanavyo.”

Mwisho wa sura ya tano​
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom