Kiswahili ni lugha na tunu ya taifa.

philosophy

Senior Member
Nov 11, 2012
104
42
KISWAHILI NI LUGHA NA TUNU YA TAIFA.
Nani kasema Kiswahili si lugha imara? Nani anasema Kiswahili si lugha mashuhuri? Na nani ansema kuwa Kiswahili si lugha ya kisomi? Ni jukumu la kila mzalendo kuitangaza zaidi na kuitukuza lugha imara,mashuhuri na lugha mama ya waswahili. Haya ni baadhi ya maswali na mawazo yanayoibuka baada ya watumwa wa tamaduni zao, hasa wazawa wa Afrika ya Mashariki, wakiwemo wasomi: kuidharau na kuitweza lugha nzuri na kipenzi cha watu wa mashariki mwa Afrika. Baadhi ya watu, wakiwemo wazawa wa Afrika ya Mashariki, hasa wasomi wanaonekana kutweza ya kwao, na kuwa watumwa wa kutukuza ya wengine. Ni wazi na ni ukweli kuwa, baadhi ya wasomi, hasa wa elimu ya juu pamoja na viongozi wa serikali wanabeza juhudi zinazofanywa ili kuifanya lugha ya kiswahli kuwa lugha rasmi na lugha ya kufundishia kuanzia ngazi ya elumu ya awali hadi vyuoni. Watu hawa, ambao ni maadui wakubwa wa maendeleo ya Kiswahili, wanaamini na kusisitiza kuwa lugha ya Kiswahili ni changa na ni bado sana kutumika katika ngazi zote za elimu. Kwa uhakika ukiyaangalia kwa undani na kuchunguza mawazo haya, hakika haipingiki kuwa haya ni mawazo yasiyo na hoja yoyote ya mashiko. Pengine twaweza kuyaita mawazo ya kibwenyenye. Ni mawazo au hoja za kuagizwa na baadhi ya watu kuwa, “nendeni mkaongee hivvyo”. Hakika sisi tunaoona faida ya lugha hii hatuwezi kuyafumbia macho mawazo kama haya, yenye kulenga kudharirisha Kiswahili. Hoja kama hizi na nyingine zenyekufanana na hizi, zaweza kujibiwa kwa hoja zifutazo: madhalani, hoja ya kuwa Kiswahili ni lugha isiyokuwa na misamiati ya kutosha, ni kauli na hoja inayosimamiwa bila uchunguzi wa kutosha. Kwani, ni misamiati mingapi katika lugha yenye idadi rasmi ya kuthibitisha kuwa lugha hii inatosha kuitwa lugha iliyo na misamiati kamili? Pili, watu hao wanaosimamia hoja hii, wanaifahamu na kuijua misamiati yote ya lugha ya Kiswahili? Kwa kuweza kujibu hoja hizi, basi wanaweza kusimamia hoja hiyo ya uchache wa misamiati. Lakini kabla ya kuendelea kutetea hoja zao, ambazo kimsingi hazina mashiko; ni vema watu hawa wanaobeza Kiswahili, watambue sifa za lugha, kuwa miongoni mwa sifa hizo ni kuwa, lugha yoyote ile, huzaliwa, hukua, na kufa pia lugha zote za watu ni lugha sawa na hakuna lugha iliyobora kuliko lugha nyingine, sambamba na hayo, lugha yoyote ile inajitoshereza aidha, kimaana, kiutamaduni na kimsamiati: nakuweza kutumika katika shughuli zozote zile za kiuchumi, kiutamaduni, kisiasa na hata kielimu kulingana na matakwa na makubaliano ya watu wa eneo husika. Hivyo basi, Kiswahili nacho ni lugha iliyobora na yenyekutumika katika nyanja mbalimbali za kimaisha ikiwemo elimu, kama wazawa wa lugha hii tutaamua kuifanya hivyo, ila sio kuidharau na kutukuza lugha za wengine. Kama haitoshi, lugha ya Kiswahili, ilizaliwa tangu watu wa Afrika mashariki walipoanza kuzungumza lugha hii, na kuitumia katika masuala yao ya kimaisha. Ndipo lugha hii imekuwa ikikua na bado inaendelea kukua kusambaa kwani wazungumzaji wake wanazidi kuongezeka na kuwa wingi kulinganisha na awali. Misamiati ya Kiswahili inazidi kuongezeka na watu wanaitumia kwa ufasha na kiufanisi zaidi. Maneno mapya yanazidi kusanifishwa kila kukicha. Lugha ya Kiswahili haijafa, na bado itaendelea kuishi na kuishi milele - kizazi na kizazi (ama vizazi vijavyo). Maana wazungumzaji wa lugha hii wanazidi kuzaliwa na kuongezeka. Lugha ya Kiswahili imekuwa lugha lulu kwani ni miongoni mwa lugha zilizo na wataalamu wengi duniani. Tunao wasomi waliobobea katika taaluma hii, wasomi wa vyuo vikuu wanaojikita katika taaluma ya Kiswahili, maprofesa na madakitari waliobobea katika taaluma ya Kiswahili. Ipo misamiati mingi sana inayofaa kutumika katika elimu; kigezo cha mabadiliko ya sayansi na teknolojia sio sababu toshelevu ya kuchelea kutumia Kiswahili katika elimu ya juu. Hata hivyo, lugha hizo zinazopigiwa chapuo kuwa ndizo bora kutumika kufundushia elimu ya juu, nazo hazikuumbiwa kuwa na misamiati (istilahi) hizo, bali visawe vya istilahi hizo vilitafutwa. Mfano, lugha ya kiingereza imekopa baadhi kama sio mingi, kutoka lugha za kilatini na lugha ya kigiriki. Kwa mfano, neno “kisimbuzi” ni kisawe halisi katika Kiswahili kinachowakilisha neno la kingereza yaani “decoder” ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakikosea kusema na kukiita king’amuzi,neno ambalo lina maana kinyume na maana halisi. Pia neno “talakilishi” kisawe cha neno “computer”-katika kiingereza, “talakilishi mpakato”, kisawe cha neno “laptop”-katika kiingereza. Ikumbukwe kuwa, kabla suala la elimu halijazagaa sana ulimwenguni kote, miaka ya kabla ya kuja kwa Kristo, wagiriki walikuwa watu wa kwanza kujiingiza katika ugunduzi mbalimbali wa kielimu na Ugiriki ndiko sayansi ilianzia. Maneno mengi ya kielimu na kisayansi yalikuwa ni ya lugha ya kigiriki, kwani wao walikuwa watu wa mwanzo kujiingiza katik elimu na ugunduzi mbalimbali. Lakini hii haikuifanya lugha kama, kilatini, kiingereza,kifaransa, kijerumani,kirusi na nyinginezo, kutotumika katika elimu hasa pale jamii zao zilipojiingiza katika suala zima la elimu na ugunduzi kwa ujumla. Na ndio maana lugha hizo zimeonekana kubobea sana katika masuala ya kielimu na gunduzi mbalimbali. Waliona ni bora kabisa kutumika katika kufundishia tangu elimu ya awali hadi elimu ya juu, ndio sababu, hata leo hii mtu amabye sio mwelewa wa lugha hizi, akienda kupata elimu katika mataifa hayo, ni sharti ajifunze lugha hizo kabla ya kuendelea na masomo. Kwa mantiki hiyo, hoja ya kwamba Kiswahili bado ni lugha changa na haina istilahi na misamiti ya kutosha, sio hoja za msingi, na ni hoja za kuikosea heshima lugha hii tukufu. Twaweza kusema kuwa, ni hoja zisizo na mashiko yoyote. Leo hii kamusi na vitabu vingi vya Kiswahili, vimeandikwa vyenye misamiati na istilahi pamoja na visawe vya kutosha katika kuhakikisha kuwa lugha ya Kiswahili inajitoshereza. Mathalani vitabu kama, Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Kamusi ya Falsafa na Visawe , pamoja na vitabu vingine vingi vilivyotungwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), na Baraza la Kiwahili Tanzania (BAKITA). Vipo vitabu vingi vya fasihi, na isimu ya lugha vimeandikwa kwa wingi na wataalamu wetu. Tatizo ni pale ambapo watanzania pamoja na watumiaji wa Kiswahili, kutopenda kuvisoma vitabu hivyo na kuona msamiati, istilahi na visawe halisi vilivyotumika katika kufikisha dhana zilizokusudiwa. Na hapo bila uchunguzi huo, wanaibuka baadhi ya watu na kusema Kiswahili hakina msamiati wa kutosha, istilahi na visawe vya kuweza kufasiri taaluma na dhana za kisayansi. Hii sio kweli, bali ni upotoshaji mkubwa. Hivyo, watanzania na watu wa Afrika ya Mashariki, tusikubali kudharirishiwa lugha yetu, na kupoteza utambulisho wetu. Kwani hoja zote hizo za kuibeza lugha ya Kiswahili ni juhudi haramu za ajinabi ambao kwao ni kutaka kupuuza kila kilicho akhiyari ya waafrika. Kiswahili sio lugha yatima. Bali ni lugha adhama. Lugha ya Kiswahili, inastahili kabisa bila ubishi kufundishia hata elimu ya juu kwani, inayo misamiati na istilahi za kutosha katika kuendesha shughuli ya ufundishaji na ujifunzji; mathalani, istilahi kama: halula-laweza kutumika katika taaluma ya utabibu na akfani, pamoja agronomia-hutumika katika taaluma ya viumbe na mimea, akiolojia na mengineyo mengi. Pia zaidi ya akthari 150 ya wazungumzao kiswahili kote duniani, inatosha kuipa hadhi kubwa lugha ya Kiswahili kutumika katika taaluma mbalimbali na kufundishia katika elimu ya juu. Kati ya hao, milioni 90 ni wakazi wa Tanzania na Kenya, milioni 25 ni watu wa jamuhuri ya watu wa Kongo, Rwanda ni milioni 8, Burundi ni milioni 10 na milioni 8, ni watu kutoka sehemu zingine za ulimwengu. Kama lugha hii inazungumzwa na watu zaidi ya milioni 150, kutoka sehemu zote dunia, kuna kizuizi gani cha kutoitumia katika ugunduzi na vyuo mbalimbali vya elimu ya juu. Ni jambo la kushangaza, na pia kusikitisha, hasa kuona kuwa baadhi ya majirani, wanaheshimu na kuihusudu lugha ya Kiswahili, ambayo kwao ni akrama. Ni ushahidi tosha kutufanya sisi wazawa tuipende na kujivunia Kiswahili, pia ni sababu tosha kwetu sisi kuamua iwe lugha rasmi katika mataifa yetu, pamoja na kuitumia katika ugunduzi mbalimbali na kuifundishia katika elimu ya juu. Ni jambo la kudhoofisha mioyoni mwetu sisi watumiaji wa Kiswahili, kuona wapo baadhi ya wataalamu wanaandika vitabu na majarida mbalimbali kwa kuwanufaisha zaidi watu wa nje kwa kukuza lugha zao: kama kiiingereza, badala kuinufaisha jamii ya waswahili kwa kualifu vitabu vyao kwa lugha ya utambulisho wetu. Ijapokuwa zipo mbinu chafu za kuathiri lugha yetu pamoja na watumiaji wake, tusisite kuwaadia wale watu ajwadi kwa kuifnanya lugha ya Kiswahili izidi kuwa akhiyari, kwa kuandika vitabu vya tamthiliya, riwaya, ushairi na adithi pamoja na vitabu vya taaluma nyingine vilivyoandikwa kwa Kiswahili japo waandishi hao ni akali. Wanastahili pongezi za dhati watu kama: S.Robert, F.M.K.Senkoro, S.A.Shafi, C.Momanyi, P.Mhando, Massamba, S.A.Mohamed, Mohammed S.A, E.Kezilahabi, Kahigi, Sengo na Kiango, Kiimbira, Mulokozi, Balisidya, Wamitila, na wengineo wengi. Hakika wamechangia sana kuifanya lugha ya kiswahli iwe adhimu miongoni mwa lugha za ulimwengu. Lakini pia pongezi za pekee zimwendee mwanafalsafa mashuhuri hapa nchini Tanzania,mheshimiwa Dk. Mihanjo, kwa kuamua kueneza elimu ya falsafa kwa kutumia lugha tukufu ya Kiswahili. Katika kutambua umuhimu wa Kiswahili,ameamua kuandika vitabu vyake kwa lugha ya Kiswahili: miongoni mwa vitabu vyake ni pamoja na kitabuchake cha ‘Usanifu wa hoja toka Wayunani hadi Waafrika(Watanzania)’. Pamoja na na wataalamu hawa, pia hatuwezi kuyaacha nyuma mashirika, mabaraza na vyama mbalimbali vinayochangia kukuza na kuendeleza Kiswahili kama Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), Kamati ya lugha ya Afrika Mashariki, na mashirika mengine mengi sana. Kwa hiyo, ni jukumu la kila mzawa wa Afrika ya mashariki, kupigania na kulinda lugha ya Kiswahili kwa kuipa hadhi ya kuwa lugha ya kitaalamu na lugha yenye uwezo wa kutumika katika taaluma za kisayansi, sanaa, biashara na kufundishia katika elimu ya juu. Jambo hili litafanikiwa, kwa wahusika wenyewe, kuithamini na kuipenda lugha hii pasi na aya yoyote. Itaonekana zaidi ni lugha yenye thamani, kwa kutoruhusu kutamka maneno yasiyo ya Kiswahili, kutochanganya Kiswahili na lugha nyingine kwa wakati mmoja katika maongezi, kufuata kaida na misingi ya Kiswahili, sarufi ya Kiswahili ni muhimu sana kuifuata katiaka kuimarisha lugha hii tukufu na adimu sana ulimwenguni. Kwa kuhitimisha, na washukuru wale wadau wote ambao wanaguswa na jambo hili la kupuuza Kiswahili na kuamua kupigana kurudisha na kulinda hadhi ya Kiswahili. Lakini pia niwatahadharishe wale wote wanaodhani Kiswahili ni lugha isiyo na wenyewe; kuwa, wasijaribu tena kuwa na mawazo potofu kama hayo tena. Na kwa kufanya hivyo, wanakuwa wamepotoka, abadani hakuna atakaye wafumbia macho kwa maovu hayo. Hivyo basi, watuunge mkono kwa juhudi zetu mathubuti za kuiendeleza lugha ya Kiswahili, ili na sisi kwa pamoja kama wana wa Kiswahili, tuweze kuwa na utambulisho maalumu duniani kwa kupitia lugha ya Kiswahili na kuutangaza utamaduni wetu kama watu wengine duniani. Ahsanteni sana!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom