SoC01 Kisa cha Aisha

Stories of Change - 2021 Competition

Glory Tausi

New Member
Mar 8, 2012
2
6
AISHA

Aisha anajitizama kwa chati kwenye kioo kidogo kilichoko chumbani kwake, anashusha pumzi hafifu kwa anachokiona mbele yake.

"Kweli nimechunda Aisha mimi," Anakiri kimyakimya.

Tayari uso ulikuwa umekomaa mithili yaajuza aliyemaliza miongo kadhaa ilhali umri wake ni miaka 24 tu. Binti mdogo kabisa, lakini amechakaa kiasi anajihurumia yeye mwenyewe. Bila shaka anakijua kilichomchosha. Hana mashaka nacho. Hata angeamshwa usingizini, angekitambua kilichomchakaza namna ile. Ni ngono za mfulululizo zisizochagua kitanda wala mlalaji wa kitanda hicho.

"Hakika natumika Aisha miye…loh!" anajisimanga kimoyomoyo.

Akiwa anajitafakari, anaisikia sauti nyingine ndani ya kichwa chake ikimuasa:Badilika Aisha. Acha biashara ya kujiuza. Tumia hivyo vijipesa ulivyojipatia kufanya biashara hata ya kuchoma vitumbua.

Wakati wazo hilo likimpitikia kichwani, alijitazama namna mkorogo ulivyombabua uso na kumuunguza mwili. Akajisemea, “Yaani niunguzwe na mkorogo na makaa ya moto pia? Aah wapi! Siwezi.”

Pamoja na changamoto nyingi za kazi yake hiyo ya kujiuza, bado kuna muda anaifurahia hiyo, haswa akutanapo na mteja mwenye pochi nene na asiye na mkono wa birika, halafu awe mnywaji. Wateja wa namna hiyo ni rahisi mno kuwaibia. Wakishalewa tu basi simu na wallet si vitu muhimu tena kwao. Kitu pekee wakiwazacho ni ngono tu. Na hapo ndipo Aisha hutumia nafasi hiyo kuwaibia na kutokomea kusikojulikana pasi kuuchosha mwili wake.

Kuwaibia wateja walevi si kazi rahisi moja kwa moja. Mara kadhaa hukumbana na nakama. Aisha anaikumbuka vema siku moja alipokuwa na mteja wake mlevi, wakitokea bar mpaka kwenye moja kati ya gesti bubu za maeneo ya Sinza Kumekucha. Baada ya mchakato wa kuchojoana nguo na kufuatiwa na mtanange wa kuyatesa vilivyo magodoro ya gesti ile, bwana yule akaanza kukoroma kama mtu anayekata roho. Kama kawaida yake, Aisha akaamua kuitumia fursa. Akajiinua kitandani na kwenda maliwatonikujiswafi mwili, kisha akatoka na kuanza kuvaa upesi upesi.Alipomaliza kuvaa akanyatia nguo za mteja wake, akatoa walletili kujichotea kiasi chake. Cha ajabu, hakukuta pesa. Akiwa anaangaza huku na kule akitafakari, mara ghafla akahisi kuna kitu hakiko sawa, mkoromaji aliacha kukoroma.alipoelekeza uso kitandani, wakagongana uso kwa uso…macho kwa macho. Mshituko alioupata Aisha, laiti kama angelikuwa na moyo mbovu basi siku hiyo nduguze wangeliweka msiba. Macho yalimtoka pima, mithili ya mtu aliyeona joka lenye vichwa saba.

Yule bwana aliinuka kitandani na kumkamata Aisha shingoni kama kitoto cha paka. Alimpiga almanusra ya kumuua. Alikuja kuokolewa na wahudumu wa gesti akiwa ameshapoteza fahamu. Kitokea cha hapo, alikaa wiki tatu akijiuguza majeraha. Isingelikuwa akiba anayoweka kila siku basi angelikufa kwa njaa na kukosa matibabu. Aliapa kuacha umalaya. Akaanza kutafuta kazi nyingine. Kwa bahati, anacho cheti alichosomea u-sekretari, kozi aliyosomeshwa kwa jasho la Bi Khadija; mama yake mzazi aliyekuwa mchoma chapati tu.

Kutafuta kibarua kukageuka kibarua kingine. Kila alipopeleka cheti, aliulizwa pia kuhusu ujuzi na uzoefu kazini, ambao hakuwa nao. Hakupata kazi. Akaishia kupata kibarua cha kufua kwa Wahindi Kariakoo. Kazi aliyofanya kwa siku tatu tu. Wahindi licha ya kubadili nguo kila kukicha pia walikuwa wachafu haswa. Nguo za ndani za Baba mwenye nyumba zilitosha kumueleza wazi namna ambavyo hakuwa mwaminifu kwa mkewe. Lakini hayo hayakumuhusu, kule kufua tu kulimchosha. Baada ya hizo siku tatu, hakurudi tena.

Akaamua kurudi Tabata kutafuta bar mpyaili aanze kufanya kazi rasmi. Alibadili vijiwe mara kwa mara ili asije kukutana na wateja aliowaibia.

Anagutuka kutoka kwenye lindi la mawazo. Akakumbuka anatakiwa akamtumie mama yake pesa ya dawa. Hali ya Bi Khadija ili taabani dhooful hali. Anajisogeza kibanda cha tiGoPesa kilichoko karibu. Anampatia mhudumu shilingi elfu 32 na kuanza kumtajia namba za simu huku akimsisitiza mhudumu,“Esta, nataka atoe elfu 30 kamilli.”

“Uko dunia gani Aisha? Gharama zimepanda mpenzi,” Mhudumu anamjibu.
“Unasema? Zimepanda kiasi gani?” Aisha anahoji kwa wahka.
“Tazama bango hapo…niongezee buku tu lakini.”
“Duh. Esta, naomba umtumie tu, ntakupitishia buku lako baadaye, sikuwa najua kama gharama zimepanda,” Aisha anamrai Esta kwa upole na taadhima. “Serikali ingetufikiria kina Aisha na mama zetu wachoma chapatti jamani…hiyo buku iliyozidi si ingenisaidia hata nauli mpaka Segerea mie?”
“Ndo hivyo mdogo wangu, tumeshikwa pabaya haswaa. Na hivi vibanda tutafunga tu sasa, watu waaanze kuficha pesa ndani ilikukwepa haya magharama ya kutuma na kutoa pesa,” Esta alijibu kwa huzuni.

BI KHADIJA

Bi Khadija alizijua vyema tabia za binti yake, lakini angefanya nini, umaskini ulikuwa umewagubika kila kona ya maisha yao.Hakuweza kumkanya bintiye kuuachana na biashara ile haramu, alichoambulia ni kumkumbusha mara kwa mara umuhimu wakutumia kinga kila akutanapo na mwanaume. Alimsisitiza ubaya wa kushika mimba angali mdogo. Si kwamba Bi Khadija hakupenda wajukuu, lakini alijua fika haya si mazingira ya kulea mtoto. Chumba chao kimoja cha mbavu za mbwa walichopanga maeneo ya Tandale Mahakama ya Simu, hata wao wawili hakikuwatosha, kuongeza mtu wa tatu ingekua mateso ya kujitakia tu.

Lakini pia aliyawaza maradhi, hakutaka binti yake apitie adha za kumeza vidonge ‘vya kuongeza siku’ kila siku kama apitiavyo yeye.

Bi Khadija mwenyewe alikuwa amechoka kwelikweli. Umri ulimtupa mkono na maradhi yalizidi kumchujisha. Naye, kama ilivyo kwa binti yake, ukimwona utasema ana miaka 60, kumbe ndo kwanza ametimiza miaka 44. Alimpata Aisha akiwa na miaka 20 tu, na tangu hapo, umaskini ukawa ni wimbo wa taifa kwao.

Bi Khadija hakumbuki hata aliyempa mimba ya Aisha ni nani. Anachokumbuka ni namna alivyokuwa akidemka demka pale kijijini na vijana wawili watatu, mpaka alipojigundua kuwa yu-mjamzito.

Kufuatia ujauzito huo, baba yake mzazi, Ustadh Khamis, alimtimua na bakora kama panya aliyekunya kwenye unga wa ugali. Akatimkia kwa mama yake mdogo, huko Mlali, ambapo alipoishi mpaka Aisha alipozaliwa, akiuza matunda ili kujipata chochote. Pamoja na kuambulia kipato kidogo mno, kisichokidhi hata nusu ya mahitaji yake, bado alilazimika kugawana na mama yake mdogo ili tu asionekane mzigo na tumbo lake…..kila alipoyakumbuka hayo, Bi Khadija hakutaka kabisa Aisha ayapitie.

Aisha alipofikisha umri wa miaka mine, ndipo Bi Khadija alipopata wazo la kwenda Dar Es Salaam kutafuta kibarua. Aliamini jiji kubwa kama Dar es Salaam, lingewezakumpatia kazi ya kufanya itakayomwingizia pesa nyingi aachane na umaskini.

Mambo hayakuwa kama alivyowaza. Maisha yakawa magumu kupindukia. Kazi zilikua za shida, hata pesa ya kumlisha Aisha alikosa. Hata mtu aliyekuwa amewahifadhinyumbani kwake, ambaye alikuwa alikuwa ni ndugu yao wa mbali sana, naye aliwachoka. Hapo ndipo Bi Khadija akajiingiza rasmi kwenye biashara ya ukahaba. Akafanilkiwa kupanga chumba chake mwenyewe. Hakuwa na muda wa kutosha kukaa na Aisha, hivyo,Aisha alikuwa kwa kulelewa na majirani mama akiangaika kutafuta rizki. Baadaye, Bi Khadija aliamua kuchoma Chapati baada ya kuona Aisha anakua sana–na hawezi tena kuwa anawaingiza wanaume ndani huku Aisha akiona.

Maisha ya kuchoma chapati yalikuwa magumu zaidi ya yale ya ukahaba. Lakini kwakuwa alidhamiria kuachana na ukahaba, kwa hivyo akakomaa kuunguza viganja na vigoko vya miguu. Miezi michache mbele akaanza kusumbuliwa na tumbo la kuharisha na hali ya kukosa hamu ya kula.

Mwanzoni Bi Khadija aliihusisha hali ile na Imani za kishirikina. Akaanza kuhangaika kwa waganga wa kienyeji. Alipoteza pesa chungu tele na nafuu asiipate. Siku moja,shoga yake, aitwaye mama Havijawa, akamshauri aende Hospitali, iliyokuwa maeneo ya Sinza Palestina, ili kwenda kucheki shida nini. Akaafiki, japo kishingo upande.

“Dokta ninaumwa sana. Nimezunguka bara na visiwani kutafuta tiba bila mafanikio, mpaka sasa naelekea kukata tamaa!”
Daktari alimsikiliza Bi Khadija kwa kina. Kisha baada ya kumwuliza maswali mawili matatu, alimwandikia vipimo.

Majibu ya vipimo yalipotoka, ilibidi daktari atumie takribani saa nzima kuzungumza naye kabla ya kumpatia majibu. Vipimo vilionesha ana virusi vya UKIMWI.Majibu yalimshitua sana na kummaliza nguvu, lakiniu ushauri na nasaha kutoka kwa daktari vilimsaidia.

Ilimchukua muda Bi Khadija kukubaliana na matokeo. Lakini kwakuwa maisha yalipaswa kuendelea, alijivika ujasiri na kuendelea kupambana na maisha, ili kumhudumia Aisha. Miaka ikaenda akitumia dawa za kufubaza makali ya virusi. Aisha alikua kwa shida na dhiki kubwa, lakini alifanikiwa kuhitimu elimu yake ya kidato cha nne. Baada ya kidato cha nne, Aisha Alisoma kozi fupi ya usekretari, kisha aliingia mtaani kuanza maisha mapya ya kutafuta.

Bi Khadija alipoona mambo yamezidi kuwa mabaya, akaamua kurudi zake kijijini kwao Bunduki, Mgeta, Mkoa wa Morogoro, ambapo walikuwa na nyumba ndogo ya udongo. Aisha alibaki mjini, akimwahidi kumtumia pesa kidogo za kujikimu. Lengo kuu lilikuwa ni kumwachia nafasi kwenye kijichumba chao kidogo mithili ya banda la kuku.

Pamoja na ukweli kwamba, Aisha anamkumbuka mama yake, na kumjali kwa hali na mali. Na pamoja na ukweli kwamba, Bi Khadija hataki Aisha apitiye adha na madhila makubwa yaliyomfika yeye, lakini bado hatari ya kukabiliwa na umasikini na maradhi makubwa inamkabili Aisha. Asipopata mwongozo sahihi na msaada wa jamii au Serikali yake, anaweza kuja kukumbuka shuka ilhali kumeshakucha, kama ambavyo Bi Khadija aliamua kuachana biashara ya ukahaba akiwa tayari amekwisha athirika na UKIMWI bila kujijua.

UJUMBE

1. Aisha na mama yake wanawakilisha asilimia kubwa ya wanawake ambao wanatumia ngono kama sehemu ya kujipatia kipato illi kuweza kujikimu na hali ngumu ya UCHUMI inayowakabili wananchi wengi wa hali ya chini.

2. Aisha na mama yake wanatukumbusha pia kuwa uzuri si kitu cha kudumu. Na ugumu wa Maisha unachangia watu wengi kuwa na hali duni za kiafya.

3. Bi Khadija anatukumbusha jinsi gani hali ngumu ya uchumi inaweza kupelekea mtu kujiingiza kwenye tabia zisizofaa hata kupelekea kupata magonjwa hatarishi yasiyo na tiba.

4. Ukosefu wa AJIRA, Bado unaendelea kuwa mwiba mchungu kwa jamii, huku uhitaji wa watu wenye ujuzi wa miaka kadhaa kwenye chanja fulani ukiwa ni moja ya chanzo kikubwa cha wengi kufanya kazi yoyote ile ili kujiongezea kipato na wengine kujiingiza kwenye tabia zisizofaa hata kupelekea kuhatarisha AFYA zao.

5. Maisha ya wawili hawa yanatuonyesha jinsi gani Serikali imeshindwa kufikiria matabaka fulani kwenye jamii wakati wafanyapo marekebisho mbalimbali yahusuyo mifumo ya kifedha na athari zake kwa jamii husika.

6. Aisha pia ametuonyesha jinsi gani kuna ugumu kuachana na tabia Fulani uliyoizoea hata kama ni mbaya. Aisha anathibitisha ama kwa hakika mazoea ujenga tabia.

HITIMISHO

Wakati mwingine tunatamani kuenenda katika mienendo sahihi lakini Mazoea, Hali ngumu za Maisha zinazochangiwa na Uchumi mbovu, na Elimu Duni kutufanya tuishi Maisha yasiyopendeza Machoni mwa Jamii inayotuzunguka na Machoni kwetu wenyewe.

Huku serikali ikizidisha uchungu wa Maisha kwa namna moja au nyingine.
 
Very painful story. Sio kwamba walipenda wamejikuta wametumbukia katika hili shimo.

Mungu Baba turehemu hatuna namna ya kufanya.
 
Back
Top Bottom